ILIPOISHIA:
Nilipokisogeza kibuyu hicho karibu na
pua, nilikumbana na harufu kali kwelikweli, ikabidi nizibe pua, nikanywa huku
nikiwa nimefumba macho. Kabla sijameza, nilisikia vitu vikinitembea mdomoni,
nilipotazama vizuri kile kibuyu, pale kwenye mdomo wa kunywea, sikuyaamini
macho yangu, nikataka kutema lakini tayari nilishachelewa, vitu vyote
vilikimbilia tumboni vyenyewe.
SASA ENDELEA...
Pale kwenye sehemu ya kunywea, ndipo
paliponipa picha kwamba nilichokunywa kilikuwa ni kitu gani. Minyoo mingi ya
rangi mbalimbali, ilikuwa imechanganywa na maji machungu yenye harufu mbaya
mno. Jambo lile, la kugundua kwamba nilikuwa nimekunywa minyoo, lilinifanya
nisisimke sana, nilijaribu kujitapisha lakini ilikuwa sawa mna kazi bure.
Kwa jinsi minyoo yenyewe ilivyokuwa
imechangamka, muda mfupi tu baadaye, nilisikia tumbo likianza kutibuka, hofu
kubwa ikanitanda ndani ya moyo wangu. Sikujua nini itakuwa hatma yangu.
Yule babu alikichukuaa kibuyo na
kukifunga, akakirudisha pale chini, nikamuona akichaguachagua na muda mfupi
baadaye, alichukua kibuyu kingine lakini hiki kilikuwa kidogo kuliko kile cha
awali. Akawatazama wale watu wengine waliokuwa wamekaa pembeni na kutulia kisha
akawapa ishara fulani, nikaona wanaume wawili wakiinuka.
Wakatembea harakaharaka kusogea mpaka
pale nilipokuwa nimekalishwa. Sikutaka kuyaamini macho yangu, ilibidi
nijifikiche macho nikidhani labda nipo ndotoni.
Haikuwa ndoto, ilikuwa ni kweli
kabisa. Mbele yangu walikuwa wamesimama baba na baba yake Rahma. Niliwatazama
mmoja baada ya mwingine, bado nikawa siamini. Nao walikuwa wamevaa kama wale
watu wengine, walijistiri kidogo tu lakini sehemu kubwa ya miili yao ilikuwa
wazi.
Ni hapo ndipo nilipoielewa kauli ya baba
yake Rahma aliyoitoa muda mfupi kabla ya yale mauzauza hayajanitokea, kwamba
eti utii ni jambo muhimu sana na la lazima kwa jamii yao. Kumbe urafiki au
ukaribu wa baba na baba yake rahma ulikuwa zaidi ya vile kila mmoja alivyokuwa
akiamini.
Yule mzee alimtazama baba, baba naye
akamtazama kisha kichwa chake akakiinamisha kwa utii, yule babu akawa anaongea
kwa lugha ambayo hata sikuwa naielewa, baba naye akawa anamfuatisha
anachokisema, muda mfupi baadaye baba yake Rahma naye alikuwa akifuatisha
walichokuwa wanakisema.
Muda mfupi baadaye, walinizunguka na kutengeneza
kama duara jingine hivi, wakawa wanaendelea kuzungumza yale maneno kwa sauti ya
juu, muda mfupi baadaye wale watu wengine nao walidakia, wakawa wanawafuatisha.
Ilivyoonesha, wote walikuwa wakiielewa vizuri lugha ile maana hakuna aliyekuwa
akibabaika.
Baadaye, yule mzee alitoa ishara, watu
wote wakanyamaza, akaanza kuzungumza lakini safari hii, alikuwa akiongea
Kiswahili japo ilionesha hakuwa akikielewa vizuri. Akawaambia watu wote kwamba
anayo furaha kubwa kukutana nao usiku huo na furaha yake iliongezwa zaidi na
tukio lililokuwa likifanyika usiku huo.
Aliwaambia watu wote kwamba kulikuwa na
utambulisho wa mwanachama mpya, akanitaka nisimame. Nilishtuka sana, mwanachama
mpya? Wa nini? Ina maana kile ni chama? Kinahusika na nini? Sikuwa na majibu.
Nilimgeukia baba, naye akanigeukia, akanipa ishara kwamba nitulie.
Yule babu alimkabidhi baba kile kibuyu,
nikamuona akirudi tena pale palipokuwa na vifaa vingine, akachaguachagua kisha
nikamuona akichukua kitambaa cheusi, au wengine wanapenda kuita kaniki. Alimpa
baba, akainamisha kichwa chake kama ishara ya utii, kisha yule babu akaendelea
kuzungumza na kila mtu.
Alisema hatua ya kwanza natakiwa
kukabidhiwa vifaa kwa ajili ya kazi kisha baada ya hapo, nitatawazwa rasmi kuwa
mwanachama kamili, watu wote wakalipuka kwa shangwe za kila namna. Zilikuwa ni
kelele kubwa sana, kila mtu akionesha kuwa na furaha sana.
Baba aliniinamia, akaongea kwa sauti ya
chini akiniambia nivue suruali niliyokuwa nimevaa maana mpaka muda huo nilikuwa
kifua wazi. Niliona kama ni jambo lisilowezekana, yaani nivue nguo wakati watu
wote wananitazama? Macho yakanitoka.
Ni kama baba alinielewa, alinipa na ile
kaniki, akanionesha kwa ishara kwamba nijifunge juu ya suruali kisha ndiyo
niiteremshe. Nilifanya hivyo, muda mfupi baadaye, nilikuwa nimeshaivua na
kujifunga kaniki. Sasa na mimi nilikuwa nikifanana na wale watu isipokuwa mimi
nilijifunga kaniki ndefu wakati wengine wote walikuwa wamejifunika kwa vipande
vidogo.
Nilikalishwa chini, yule babu akampa
ishara baba, akanisogelea na kupiga magoti, akanikabidhi kile kibuyu
kilichokuwa kimevalishwa shanga, kisha akaongea kwa sauti ya chini akinitaka
nisiogope chochote na nimthibitishie kwamba kweli nimekuwa mtu mzima na si
mtoto kama alivyokuwa akiamini. Nilitingisha kichwa, japokuwa hakuwa ameniambia
chochote, tayari nilishaelewa kilichokuwa kinaendelea.
Nilipokabidhiwa kile kibuyu, baba na
baba yake Rahma waliondoka na kurudi kwenye sehemu zao, yule babu akaniambia
nishike kibuyu hicho kwa mikono miwili kisha nikiinue mbele ya uso wangu.
Nilifanya kama alivyoniambia, nikamuona
akichukua karai la chuma lenye maji meusi ndani yake, akanimwagia kichwani
kisha kwa kutumia kisu kikali, alianza kuninyoa nywele. Sikuwahi kuona mtu
akinyolewa nywele kwa siku, hata kule kijijini kwetu ambako saluni zilikuwa
chache, tulikuwa tukinyolewa kwa wembe au mkasi.
Kwa kawaida nywele zangu huwa ni nguvu
na wakati wa kunyoa huwa ni shughuli kwelikweli lakini huwezi kuamini, yule
babu alipitisha mara kadhaa tu, kichwa kikawa cheupe kabisa. Alichukua dawa
kutoka kwenye kichupa kimoja kisha akanisogelea, akarudia kunisisitiza kwamba
sitakiwi kuachia kibuyu hicho kwani ndiyo maisha yangu.
Alichokifanya, kwa kutumia kilekile
kisu, alianza kunichanja chake, kuanzia kichwani, akaja shingoni upande wa
nyuma, akashuka mgongoni mpaka miguuni. Kiukweli maumivu niliyokuwa nayasikia
yalikuwa makali sana, yote tisa, kumi ni pale alipoanza kunisugua sehemu
alizonichanja kwa kutumia ile dawa iliyokuwa kwenye kile kichupa.
Maumivu ya kuchanjwa ukijumlisha na
ukali wa ile dawa, nilishindwa kujizuia, nikawa nalia kwa maumivu.
“Kumbe hujakuwa mrume wewe,” alisema
yule babu kwa Kiswahili kibovu lakini ambacho kilinifanya nimuelewe.
Alimaanisha kwamba eti bado nilikuwa mtoto ndiyo maana nilikuwa nalia. Hakuna kitu
ambacho nilikuwa nakichukia kama kuitwa mtoto. Japokuwa nilikuwa nikijisikia
maumivu makali, ilibidi nijikaze, akaendelea kunisugua na ile dawa huku
nikigugumia kwa maumivu.
Damu nyingi ilikuwa ikinitoka kwenye
majeraha yangu lakini safari hii sikujali, sikutaka kuonekana mtoto, yule babu
akaendelea mpaka alipomaliza. Baada ya kumaliza, alinishika mkono na
kunisimamisha, akanisogeza kwenye ule moto.
Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe
pale kulikuwa na nyama nyingi ya kutosha imewekwa pembeni ya moto. Yule babu
aliinama pale kwenye nyama, akatoka na kipande kimoja, akanifuata na kunipa.
Kwa akili yangu nilielewa kwamba ananipa
ili niichome kwenye moto ikiiva ndiyo niile, nikashangaa ananiambia eti niile
vilevile ikiwa mbichi. Nilishtuka sana maana ilikuwa bado na damudamu kabisa.
Nilitamani kumuuliza kwanza ile ni nyama
ya nini lakini nilikumbuka kauli ya baba yake rahma na aliyoniambia baba muda
mfupi uliopita kwamba natakiwa kuwa mtiifu, ikabidi nifumbe macho, nikaitia
mdomoni na kutaka kuimeza bila kutafuna lakini ilikuwa kubwa, ikabidi nipige
moyo konde, nikaanza kuitafuna kisha harakaharaka nikameza.
“Twive umile,” alisema yule mzee huku
akinionesha kwa ishara kwamba nifumbue mdomo. Sijui kile ni kilugha alichokuwa
akizungumza, nilifanya kama alivyoniambia, nikafumbua mdomo. Nadhani alitaka
kuhakikisha kama nimemeza, alipohakikisha, alinishika mkono na kuuinua juu kama
wanavyofanya waamuzi wa mapambano ya ndondi wanapomtangaza msshi ulingoni.
Watu wote walishangilia kwa nguvu,
wengine nikawaona wakirukaruka kwa furaha, ikabidi na mimi nifurahi ingawa bado
nilikuwa gizani. Yule mzee aliniachia mkono na kuanza kuzungumza na wale watu,
akiwataka wanipe ushirikiano na kunifundisha yale nisiyoyajua.
Wakati anaongea hayo, sijui nini
kilinituma nitazame pale zilipokuwepo zile nyama, nikashtuka kuliko kawaida
kuona kuna viungo vya binadamu, viganja vya mikono na miguu. Ile nyama
aliyonipa aliichukua palepale, kwa hiyo alikuwa amenipa nyama ya mtu? Macho
yalinitoka nikiwa siamini macho yangu.
Nikiwa bado nashangaa, mwili ukiwa
unatetemeka kwa hofu, nilishtukia wale watu wakikimbilia pale kwenye moto na
kujipanga foleni, yule babu akasogea kwenye zile nyama, akawa anagawa, kila
mmoja anapita na kupewa kipande chake kisha anatafuta sehemu ya kwenda kukaa na
kuanza kula. Nilihisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo.
“Hongera, umekuwa sasa,” alisema baba
huku akinikumbatia, akanishika mkono na kunipeleka kwenye foleni, akaniingiza
kwenye foleni.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment