Tuesday, September 12, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 37


ILIPOISHIA:
Niliendelea ‘kuperuzi’ yake mafaili, moja baada ya jingine. Kama nilivyokuwa nimeona awali, yalikuwa yamejaa taarifa za watu mbalimbali, wakubwa kwa wadogo, yakiwa na taarifa kuhusu hali zao za kiafya na viungo mbalimbali kwenye mwili, bado nikawa sielewi. Niliendelea kuchimba kwa undani, taratibu nikaanza kugundua mambo ambayo ama kwa hakika yalinishangaza sana.
SASA ENDELEA...
Kwa jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na mtandao mpana sana wa watu kutoka hapa nyumbani Tanzania, India, Marekani, Uingereza na nchi za Kiarabu ambao ulikuwa ukihusisha hospitali kubwakubwa duniani ambao walikuwa wakifanya biashara ambayo nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuijua.
Nilipoendelea kufuatilia kwenye mafaili yake, niligundua kuwa kulikuwa na namba za mawasiliano za kila mtu ambaye taarifa zake zilikuwa zimeandikwa na kama hiyo haitoshi, pia kulikuwa na taarifa za mtu wa karibu (next of keen), nikawa nimepata pa kuanzia.
“Naomba ukaninunulie kalamu na daftari dogo kule nje ya hospitali,” nilimwambia Raya lakini akanikatalia na kuja juu.
“Ina maana unaona afya yako siyo muhimu kuliko hicho unachokifanya? Siendi popote mpaka ule kwanza,” alisema huku akinisogezea chakula, nikashusha pumzi ndefu na kuiweka laptop pembeni, nikanyoosha mikono nikiashiria aninawishe, nikaanza kula.
“Unaonekana kuwa na pilikapilika nyingi, kwa nini hujionei huruma mpenzi wangu? Inabidi upone kwanza, afya yako ni muhimu kuliko kitu kingine chochote,” Raya alisema kwa upole huku akinibembeleza nile, nikawa nakula huku mara kwa mara macho yangu yakigongana na ya nesi Shamila.

“Sawa nimekuelewa mpenzi wangu,” nilisema kwa upole. Jambo jingine ambalo sikuwa najua linatokea kwa sababu gani, ninapokuwa na Raya nilikuwa na kawaida ya kutulia sana, jambo ambalo hata Shamila alilitambua.
Kwa kawaida, unapokaa jirani na mtu mwenye tabia fulani kwa muda mrefu, kuna mambo mawili, wewe umbadilishe au yeye akubadilishe! Raya alikuwa na hulka ya upole na utulivu, nahisi kwa sababu ya kukaa naye karibu muda mwingi, na mimi alikuwa ameniambukiza tabia hizo ndiyo maana ninapokuwa karibu naye, nilikuwa nikitulia sana.
Tofauti na Raya, Shamila alikuwa mcheshi sana, anayependa masihara na mchangamfu, ambaye naye kila nilipokuwa nikipata muda wa kuwa naye karibu, nilikuwa nikibadilika na kuendana naye.
Nilikula harakaharaka, ili kumfurahisha Raya nilimaliza chakula chote, akanimiminia na juisi, nikaifuta yote, nikamuona akitabasamu, akaja kunibusu kwenye paji la uso wangu na kunishukuru kwa kula vizuri, na mimi nikamshukuru kwa kuniandalia chakula kizuri.
Akakusanya vyombo vyake na kuviweka kwenye kikapu, akataka kutoka kwenda kuninunulia vile nilivyomuagiza lakini kabla hajatoka, Shamila aliniletea karatasi kadhaa nyeupe zilizokuwa zimebanwa pamoja vizuri na kalamu, akanikabidhi. Nilimuona Raya akimtazama kwa jicho kali kama anayesema ‘mbona unajipendekeza sana’?
Sikuwa na muda wa kupoteza, harakaharaka nilichukua tena laptop na kuanza kuzinakili namba za simu za wale watu wote pamoja na watu wao wa karibu. Namba zilikuwa nyingi mno lakini kwa kuanzia, niliandika namba hamsini, yaani za wahusika 25 na ndugu zao wa karibu 25.
“Kama unahitaji msaada wangu niambie mpenzi wangu, nipo kwa ajili yako,” alisema Raya, nikamwambia naomba akaninunulie vocha ya shilingi elfu kumi. Kabla Raya hajainuka, Shamila aliingilia kati:
“Kama unataka vocha usijali mgonjwa wangu, mimi nina pesa kwenye simu naweza kukuunganisha.”
“Tunashukuru kwa msaada wako, tukihitaji tutakwambia. Ngoja nikakununulie mume wangu,” alisema Raya kwa nyodo za kike, akanibusu tena kwenye paji la uso na kutoka huku akitembea kwa maringo, nikabaki kutingisha tu kichwa.
Kwa jinsi upepo ulivyokuwa ukielekea, nilijua kama nisipokuwa mkali kwa Shamila, muda si mrefu watavaana na Raya na kuleta picha mbaya kwani walishaanza kuchokozana.
“Kwa nini unafanya hivyo Shamila? Si tumekubaliana kwamba uhusiano wetu uwe wa siri kwanza? Kwa nini mnafanya mambo ya kitoto?” nilimwambia Shamila nikiwa nimevaa uso wa ‘usiriasi’.
“Hata kama... ndiyo awe anakubusubusu mbele yangu, na mimi nina moyo ujue, sina chuma. Asipoacha na mimi sitaacha,” alisema Shamila huku akionesha dhahiri alivyokuwa akiumia moyoni kwa sababu ya wivu. Japokuwa ndiyo kwanza tulikuwa tumeanza mapenzi yetu, Shamila alionesha ‘kukolea’ sana.
Muda mfupi baadaye, Raya alirudi akiwa na vocha, akakwangua mwenyewe na kuweka kwenye simu yake kisha akanipa. Nikamshukuru.
“Naombeni mnipe muda wa kuwa peke yangu kwa dakika kadhaa, kuna simu za muhimu nataka kuzungumza nazo,” niliwaambia, nikawaona wanatazamana kisha Raya akabeba kikapu chake na kuniaga kwamba atarudi baadaye.
“Sasa kuhusu simu yako?”
“Baki nayo tu mpenzi wangu, nitaichukua baadaye nikirudi, mtu yeyote akipiga pokea,” alisema Raya, nikaelewa kwa sababu gani amesema vile, akamtazama Shamila kuanzia juu mpaka chini kwa yale macho ambayo wenyewe wanaita ‘kunyali’, akatoka na kikapu chake na kuniacha mle wodini nikiwa na Shamila.
Ili kumfanya Raya awe na amani, nilimwambia Shamila naye atoke, kwa bahati nzuri alinitii, akamfuata Raya nje, sijui walienda kuzungumza nini huko nje, nikabaki peke yangu. Harakaharaka nilianza kupiga namba za simu za wale watu nilizozichukua.
Cha ajabu, katika namba zote ishirini na tano, hakuna hata moja iliyokuwa ikipatikana, ikabidi nianze kujaribu upande wa pili; namba za watu wao wa karibu. Nilipoanza ya kwanza tu, iliita, nikaiweka sikioni huku nikiwa makini kutaka kusikia nani atapokea.
“Haloo!”
“Haloo, habari yako dada.”
“Nzuri, nani?”
“Samahani mimi naitwa Jamal, najua hunijui lakini nilikuwa na shida na Simon Nyimbi, unamfahamu?”
“Ndiyo, ni mchumba wangu.”
“Ok, nampigia simu yake simpati, naweza kuzungumza naye?” nilimuuliza swali la mtego, akaingia mzimamzima kwenye ‘target’ yangu.
“Simon alisafiri kwenda kusoma India, huu ni mwezi wa kumi sasa tangu aondoke.”
“Ameenda kusomea nini na amedhaminiwa na serikali au nani?”
“Ameenda kusomea teknolojia ya mawasiliano (IT), alipata udhamini wa shirika moja liitwalo Black Heart.”
“Tangu aondoke umewahi kuwasiliana naye?”
“Hapana, sijawahi kuwasiliana naye hata mara moja ila kuna siku kuna mwanaume alinipigia simu na kunieleza kuwa yeye ni mwakilishi wa shirika la Black Heart nchini India, akaniambia nisiwe na wasiwasi mume wangu mtarajiwa yuko bize na masomo na atarudi baada ya miaka miwili kupita,” alisema yule msichana niliyekuwa nazungumza naye kwenye simu.
Kabla sijakata simu, nilimuuliza anaishi wapi ambapo aliniambia kwamba anaishi Kibaha, Pwani, nikamshukuru kwa ushirikiano kisha nikakata simu.
Maelezo yake yalitosha kunipa mwanga wa kilichokuwa kinaendelea, harakaharaka nikachukua laptop yangu na kuingia kwenye mtandao, ‘nika-google’ shirika liitwalo Black Heart, mtandao ukafunguka, nikaanza kusoma kuhusu shirika hilo.
Kwa maelezo yaliyokuwa yameandikwa mtandaoni, shirika hilo lilikuwa likiwasaidia vijana weusi kuwalipia gharama za masomo nje ya nchi au kuwasaidia maskini wenye maradhi mbalimbali kwenda kutibiwa nje ya nchi. Nikachukua mawasiliano yao na kuyaandika pembeni, nikaendelea na ile kazi.
“Nilipiga namba ya pili, akapokea mwanaume. Nilijitambulisha kwa upole, nikamueleza yule mwanaume ambaye kwa jinsi alivyokuwa akizungumza alionesha kuwa ni mtu wa makamo, kwamba naitwa Jamal na nilikuwa namuulizia mtu aitwaye Tusekile Mwankenja, nikamdanganya kwamba tulisoma wote shule ya msingi.
“Mimi ni baba yake. Yupo nchini India kwa matibabu, alikuwa anasumbuliwa na matatizo ya figo kwa muda mrefu, kwa bahati nzuri tukapata mdhamini ambaye alimgharamia kila kitu, hivi tunavyoongea yupo Apollo Hospital, Mumbai akiendelea kupatiwa matibabu.”
“Ooh! Poleni sana, alisafiri na nani kwa upande wa wanafamilia na mara ya mwisho mlizungumza naye lini?”    
“Aliondoka peke yake kwa sababu tuliambiwa hilo shirika la wadhamini lina uwezo wa kumlipia mgonjwa pekee, kama tunataka mtu wa kwenda naye sisi familia ndiyo tumlipie kila kitu lakini tukashindwa kutokana na umaskini.”
“Mara ya mwisho mlizungumza naye lini?”
“Kiukweli tangu aondoke hatujawahi kuzungumza naye, wanasema hospitalini hawaruhusu kutumia simu,” alijibu mwanaume huyo, nikashusha pumzi ndefu.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.


No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...