ILIPOISHIA:
“Nimekikuta kwenye kitanda cha Shenaiza,
na anaonekana kama hana fahamu, rangi ya ngozi yake imebadilika na kuwa ya
kijivu,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
SASA ENDELEA...
“Benzodiazepam,” Shamila alisema kwa
sauti ya juu, akitamka maneno yaliyokuwa yameandikwa kwenye kile kichupa
nilichokikuta pembeni ya kitanda cha Shenaiza.
“Kwani ni dawa gani?”
“Mungu wangu! Wameamua kummalizia kabisa
mdada wa watu. Hii ni dawa ya usingizi ambayo hairuhusiwi kutumika bila
uangalizi wa kutosha wa daktari. Mtu anapotumia dozi kubwa, husababisha muda
wote awe analala tu na kama hali hii ikiendelea kwa muda, husababisha mgonjwa
kupoteza kumbukumbu na kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.”
“Haa! Na siyo kwamba dawa hii hutumika
kuwatibu wagonjwa wa akili?”
“Hapana Jamal, hii hutumika tu
kuwatuliza watu wenye msongo mkali wa mawazo au stress kiasi kwamba wanakosa
usingizi. Wakitumia dawa hii chini ya uangalizi wa daktari, huwasaidia kupata
usingizi na kuwapunguzia msongo mkali au ‘stress’, lakini narudia tena, ni
lazima itumiwe chini ya uangalizi mkali wa daktari.”
“Sasa kwa nini wanampa Shenaiza?”
“Jibu ni moja tu, wanataka watu wote
waamini kwamba kweli amechanganyikiwa. Kama kwa siku chache tu alizokaa hapa
hospitalini kichupa kimeshaisha, maana yake ni kwamba anapewa dozi kubwa sana
ambayo ndani ya muda mfupi tu, itamfanya apoteze kumbukumbu na kuwa
mwendawazimu.”
“Shamilaa! Cant we help her?” (Shamilaa!
Hatuwezi kumsaidia?)
“Its none of our business Jamal.” (Hilo
halituhusu Jamal)
“Kwa nini unasema hivyo?”
“Nikukumbushe tu kwamba mambo yote hayo
yanafanywa kwa maagizo ya baba yake mzazi. Unataka kusema wewe una uchungu na
Shenaiza kuliko baba yake?” alisema Shamila na kunifanya nikose cha kujibu,
nikajiinamia huku nikijisikia uchungu mkali sana ndani ya moyo wangu.
Ni hapo ndipo nilipoanza kuelewa kwa
nini Shenaiza alikuwa akihitaji sana msaada kutoka kwangu. Ni hapo pia ndipo
nilipoelewa kwa nini alikuwa anashindwa kunieleza moja kwa moja ni msaada gani
aliokuwa anauhitaji na alikuwa akisumbuliwa na tatizo gani. Nilishusha pumzi
ndefu na kukaa vizuri pale kitandani.
“Utakapojaribu kutoka tena wodini na
kwenda unakokujua mwenyewe, kitakachokupata mimi sitahusika maana naona
hunielewi,” alisema Shamila huku akionesha kukasirishwa na kitendo changu cha
kutoka wodini bila ruhusa yake, wakati nikijua kwamba nilikuwa nikisakwa na
watu wenye nia ovu.
“Nisamehe Shamila, lakini muda mwingine
nakuwa sina namna zaidi ya kuvunja sheria zako,” nilisema kwa upole,
akanisogelea, tukawa tunatazama, nikambusu kwenye paji lake la uso.
“Kwa nini unaonekana kuguswa sana na
matatizo ya Shenaiza?” Shamila aliniuliza huku akikaa vizuri, nikashusha tena
pumzi ndefu nikitafakari nianzie wapi kumueleza. Kwa jinsi hali ilivyokuwa,
kumsaidia Shenaiza peke yangu lilionekana kuwa suala gumu, ilikuwa ni lazima
nimueleze Shenaiza ukweli ili kwa pamoja tujue namna ya kumsaidia.
Ilibidi nianze kumsimulia Shamila kila
kitu kuhusu mimi na Shenaiza. Nilimueleza kilichotokea kuanzia siku ya kwanza
msichana huyo alipopiga simu yangu na baadaye kuniambia kwamba alikuwa amekosea
namba. Nilimueleza alivyoendelea kunisumbua akidai kwamba hata kama amekosea
namba, anaamini mimi naweza kumsaidia kumtoa kwenye matatizo makubwa yaliyokuwa
yanamkabili.
“Nilimueleza Shamila jinsi
nilivyoendelea kuwasiliana na msichana huyo, jinsi tulivyoenda kukutana na
kumkuta akiwa na hali mbaya hospitalini baada ya kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya.
Sikumficha kitu, niliendelea kumueleza jinsi alivyonishawishi nimtoroshe
hospitali na yote yaliyotokea baada ya hapo.
Shamila alikuwa kimya kabisa
akinisikiliza, kadiri nilivyokuwa naendelea kumsimulia kuhusu sakata hilo la
Shenaiza, taratibu nilianza kumuona na yeye akiguswa, nilimfafanulia kila kitu
isipokuwa kilichotokea baada ya mimi kushambuliwa na kunusurika kufa, na
kujikuta nikizinduka nikiwa kwenye ulimwengu mwingine.
Nilimficha kuhusu kipengele hicho kwa
sababu maalum kwani nilijua hata nimueleze kwa lugha gani, hawezi kunielewa,
sanasana atahisi labda na mimi nimeanza kuchanganyikiwa.
Nashukuru Mungu kwamba maelezo yangu
kuhusu Shenaiza yalimuingia sana moyoni mwake, naye akaguswa kama nilivyokuwa
nimeguswa mimi lakini kabla ya yote akanitahadharisha.
“Mara kwa mara nimemsikia Raya
akilalamika kwamba wewe una uhusiano wa kimapenzi na Shenaiza,” alisema Shamila, kauli ambayo
ilinishtua sana. Nikajua kwamba kumbe hata kabla sijaanzisha uhusiano naye wa
siri, Shamila alikuwa akinifuatilia kwa karibu sana na tayari alikuwa anajua
mambo yangu kadhaa.
Akaendelea: “Sasa isije kuwa mi
nakusaidia kumuokoa Shamila kumbe nakurahisishia mpango wako wa kumuokoa mpenzi
wako, nikija kujua kwamba ni kweli mna uhusiano naye wa kimapenzi nitafanya
jambo hilo ambalo hutakuja kulisahau maishani mwako.”
“Siyo hivyo Shamila, wala sina uhusiano
naye wa kimapenzi, ni kama nilivyokueleza na hakuna chochote zaidi ya hayo
niliyokwambia.
“Ndiyo nimeshakwambia hivyo, kwa jinsi
ninavyokupenda sitaki kuona mtu mwingine akikusogelea, hata huyo Raya naandaa
mpango wa kumtoa kwenye maisha yako, nataka nibaki peke yangu, wewe ndiyo mume
wangu mtarajiwa,” alisema Shamila na kunibusu na lipsi zake laini, mkondo wa
raha za kipekee ukapita kwa kasi kwenye mishipa yangu ya damu, nikajikuta
nikisisimka mno hasa nilipokumbuka asali aliyonilambisha.
“Nakuhakikishia, suala kama hilo
haliwezi kutokea,” nilisema kwa kumnong’oneza sikioni, akaruka kidogo kwa msisimko
na kunibusu tena, akaniambia kwamba ananipenda sana na anaamini mimi ndiyo baba
mtarajiwa wa wanaye.
“Kwa hiyo utanisaidia kuhusu suala la
Shenaiza,” nilimchombeza, akanihakikishia kwamba yupo tayari kunisaidia kwa
chochote ambacho nakihitaji, hata kama kitayagharimu maisha yake.
Nilifurahishwa mno na majibu yake kwani
kiukweli, naomba Mungu anisamehe! Hilo ndiyo lilikuwa lengo langu kubwa la
kuanzisha naye uhusiano wa kimapenzi, nilitaka nimtumie kukamilisha baadhi ya
mambo yangu!
Siyo jambo zuri hata kidogo kucheza na
hisia za mtu anayekupenda, nawashauri watu wenye tabia hii waache mara moja kwa
sababu mapenzi huwa hayajaribiwi, kama ambavyo ilitokea kwangu na Shamila, Raya
na Shenaiza. Nitafafanua kwa kina baadaye jinsi ujanja wangu wa kucheza na
hisia za wote watatu kwa wakati mmoja zilivyonigharimu.
Tulichokubaliana na Shamila ilikuwa ni
kufanya kila kinachowezekana kwanza kumjua daktari aliyekuwa akisimamia
matibabu yake, na ikiwezekana kumbadilishia dawa bila mwenyewe kujua, kwamba
badala ya kuendelea kumpa sumu Shenaiza, ampe dawa zitakazomsaidia mwili wake
kurudiwa na nguvu zake upya na akipata nafuu tu, tufanye utaratibu wa
kumtorosha.
Tulijadiliana pia kwa kina juu ya nini
cha kufanya baada ya kugundua mchezo haramu uliokuwa ukifanywa na baba yake
Shenaiza kwa kutumia Shirika la Black Heart, wa kuwasafirisha watu na kwenda
kuwauza kisha kuwaua na kuwatoa viungo muhimu miilini mwao, kwa kivuli cha
kujifanya wanaenda kuwasomesha, kuwapatia matibabu au kuwatafutia kazi.
Kutokana na upana wa mtandao wa baba
yake Shenaiza, Shamila alinishauri kwamba kwa sababu tayari nilikuwa
nimeshapata pa kuanzia, niendelee kukusanya taarifa kimyakimya kisha
nikishapata nafuu na kuruhusiwa kutoka hospitalini, ndiyo tukae tena na kuamua
nini cha kufanya kuhakikisha tunamuangusha baba yake Shenaiza na kuokoa maisha
ya watu wengi waliokuwa wakienda kutolewa kafara bila wenyewe kujua chochote.
“Lakini sitakiwi kuendelea kukaa hapa
hospitalini zaidi, wanaweza kuja hata huku na kunichukua kiulaini, wakaenda
kuniua au kunifanya chochote wanachotaka ili kuniziba mdomo,” nilimwambia
Shamila, akaniondoa wasiwasi kwamba naye analijua hilo lakini hatutakiwi
kufanya mambo kwa kukurupuka. Akanihakikishia kwamba kila kitu kitaenda vizuri,
nimuachie yeye.
Wakati tukiendelea kuzungumza, Raya
alifungua mlango na kuingia akiwa na kikapu cha chakula, mazungumzo yakakatika
ghafla, Shamila akajifanya yuko bize kwenye meza ya dawa, akipangapanga vitu.
“Habari za saizi nesi,” Raya alimsalimia
Shamila kwa unyenyekevu, jambo ambalo hakuwahi kulifanya kabla. Shamila naye akajibu
kwa uchangamfu, nikabaki njia panda. Sikujua walizungumza nini muda ule mpaka
wakamaliza tofauti zao. Raya akaja mpaka pale kitandani na kunibusu mdomoni,
Shamila akageuka na kulishuhudia tukio hilo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment