ILIPOISHIA:
Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza
alikuwa akifahamu kinachofanywa na baba yake na kwa sababu ilifika hatua akawa
amechoshwa na ukatili huo, alimtishia baba yake kuwa atatoa siri, jambo
lililosababisha ateswe sana, ikawa mtu yeyote akionekana kuwa karibu naye, baba
yake anahisi anaweza kupewa siri hiyo hivyo anauawa haraka kabla hajafumbua
mdomo wake.
“Kumbe ndiyo maana na mimi wananiwinda
kutaka kuniua?” nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa.
SASA ENDELEA...
“Na bado wataendelea kukuwinda mpaka
watakapoyakatisha maisha yako, unapaswa kuwa makini sana mpenzi wangu,” alisema
Shamila lakini alichokisema ni kama hakikuingia akilini mwangu.
Akili yangu ilianza kunienda mbio kuliko
kawaida, nikawa naunganisha matukio, kuanzia siku Shenaiza aliponipigia simu na
kuniambia kwamba ana tatizo kubwa na anahitaji nimsaidie, baada ya awali kuwa
amekosea namba.
“Lazima nikazungumze na Shenaiza,
atakuwa anajua mambo mengi zaidi,” nilisema huku nikijaribu kuinuka, Shamila
akanizuia na kuniuliza kama ninakumbuka kilichotokea muda mfupi uliopita kwenye
maegesho ya magari.
Japokuwa nilikuwa na shauku ya kwenda
kuonana na Shenaiza, maneno hayo ya Shamila yalinivunja nguvu kabisa.
Nilikumbuka jinsi wale wanaume wenye asili kama ya Shenaiza walivyokuwa wakiniwinda
kwa udi na uvumba.
“Kama usingepata akili ya kuingia kwenye
wa ile teksi unafikiri nini kingetokea?” alisema Shamila huku akinibusu kwenye
paji langu la uso.
Kitu ambacho ningependa kukieleza hapa,
ndani ya muda mfupi tu tangu nifahamiane na Shamila na kujikuta nikianguka naye
dhambini, dada huyo mrembo alionesha kuchanganyikiwa kabisa na penzi langu.
Kila mara alikuwa anapenda kunibusubusu,
mara anishike hapa, mara anisafishe kucha, mara anidekeze basi ilimradi roho
yake ifurahi! Moyoni nilikuwa najisikia raha sana kwa sababu siyo siri, sikuwa
mzoefu wa mambo hayo ya kikubwa.
Unajua kwa nini wanaume wengine huwa
wanafikia hatua ya kutelekeza familia zao? Unakuta katika maisha yako, hujawahi
kukutana na mwanamke anayejua kukupetipeti kama ilivyokuwa kwa Shamila. Sasa
ukishaangukia kwenye mikono yake, na wewe ni mgeni wa mambo hayo, lazima
utelekeze mke na watoto na kuhamia kwake.
“Kwani Shamila wewe ni mtu wa wapi?”
“Mbona unaniuliza swali ambalo
haliendani kabisa na mada tunayozungumza?” aliniuliza Shamila huku akinitazama
kwa yale macho yake ambayo muda wote yapo kama yana usingizi!
Nikachekacheka pale na kupotezea mada,
akaendelea kunisisitiza kwamba huo haukuwa muda muafaka wa mimi kutoka na
kwenda kwenye wodi aliyokuwa amelazwa Shenaiza, wala kuzungukazunguka kwa
sababu ya usalama wangu.
“Lakini Shamila, kuna kazi ambayo ni
lazima niikamilishe haraka iwezekanavyo, au wewe unaridhishwa na kinachofanywa
na huyu mzee pamoja na kundi lake?”
“Siyo kwamba naridhishwa mpenzi wangu,
Wazungu wanasema ‘dont hurt what you cant kill’ (usiwinde kitu ambacho hutaweza
kukiua), hata ukifuatilia na kuujua ukweli, utafanya nini?”
Shamila alikuwa amenizidi kwa hoja,
ikabidi nitulie tu wodini huku nikiendelea kutafakari nini cha kufanya kwa
sababu ile hoja ya kwamba niache kufuatilia suala lile kwa sababu sikuwa na cha
kufanya, sikuliona kama ni sahihi kwangu.
Baadaye, nilijifanya kama nimepitiwa na
usingizi, lengo lilikuwa ni kumpumbaza Shamila, kweli aliponiona nimelala
alikuja nakunifunika vizuri kisha akatoka na kwenda kuendelea na shughuli zake.
Nilisubiri kwa dakika kadhaa, nilipoona
kumetulia kabisa, niliamka na kuvaa viatu, nikatazama huku na kule,
niliporidhika kwamba Shamila hakuwepo, nilinyata hadi kwenye chumba cha manesi,
nikachukua koti la kidaktari lililokuwa limetundikwa ukutani, nikalivaa na
kusogea kwenye kioo kilichokuwa pembeni, nikajirekebisha vizuri.
Kama ungenitazama haraka, ungeweza
kudhani na mimi ni muuguzi hospitalini hapo, niliamini hiyo ndiyo itakuwa njia
nyepesi ya kwenda kuonana na Shenaiza kule wodini kwake bila kushtukiwa na mtu
yeyote.
Harakaharaka nilitoka huku nikiwa makini
jeraha langu la kifuani lisije kufumuka tena, nikaingia kwenye lifti na kushuka
hadi ghorofa ya chini, nikashuka na kuanza kutembea harakaharaka kuelekea kule
kwenye wodi ya wagonjwa wa akili, wanawake alikokuwa amelazwa Shenaiza.
Nilifanikiwa kufika kwenye wodi ya
wagonjwa wa akili, kama ilivyokuwa kawaida ya wodi hiyo, nilipokelewa na vurugu
na kelele za kila aina kutoka kwa wagonjwa, nikawa nawapita mmoja baada ya mwingine
mpaka nilipofika kwenye kitanda cha Shenaiza.
Tofauti na nilivyotegemea kumkuta
Shenaiza akiwa amekaa kitandani kwake akilalamika, nilishangaa kumkuta akiwa
amelala tuli, akionesha kabisa kwamba hakuwa kwenye hali ya kawaida.
Nilisimama kwa sekunde kadhaa na kuanza
kumtazama, kwa zile saa chache tu nilizokaa mbali naye, alikuwa amebadilika
kabisa. Ngozi ya mwili wake, iliyokuwa na weupe wa kung’aa, ilikuwa imebadilika
na kuwa na rangi kama ya kijivu hivi, macho yalikuwa yamefumbwa nusu na nusu
yapo wazi, mdomo pia haukuwa umefumbwa, nikajikuta nikishindwa kujizuia kutokwa
na machozi.
“Shenaiza! Shenaiza!” nilimuita lakini
hakuitika, nilijaribu kumtingisha lakini hakutingishika, nikabaki nikihaha huku
na kule, nikiwa sijui cha kufanya. Nilipotazama pembeni ya kitanda chake,
kulikuwa na kichupa kidogo juu ya droo ya kitanda chake, kilichokuwa na
maandishi yaliyosomeka Benzodiazepam.
Harakaharaka nilikichukua kichupa kile
na kukiweka kwenye mfuko wa koti, nikatazama huku na kule kujaribu kuangalia
kamakuna mtyu aliyekuwa akinitazama. Katika hali ambayo sikuitegemea, miongoni
mwa wale wagonjwa wengi wa akili waliokuwa ndan ya wodi hiyo, kuna mmoja
alikuwa ametulia, muda wote akinikodolea macho.
Kwa kumtazama tu, hakuonesha kwamba ni
mwendawazimu kama wale wenzake kwa sababu macho yangu na yake yalipogongana tu,
harakaharaka alikwepesha macho pembeni na kuvunga kama hakuwa akinitazama.
Kitendo hicho tu kilitosha kunifanya niamini kwamba hakuwa mgonjwa kama wale
wengine.
Niliendelea kumkazia macho, akawa ananitazama
kwa wiziwizi, nikamsogelea pale kwenye kitanda alichokuwa amelala juu yake,
nikashtuka kumuona akiwa na simu kubwa ya kisasa ambayo harakaharaka aliificha
kwenye shuka.
“Wewe ni nani?” nilimuuliza kwa sauti ya
chinichini, akanigeukia, tukatazamana.
“Kwani unataka nini?” naye aliniuliza
kwa sauti iliyoonesha dhahiri kwamba ni mwanamke mjeuri sana na alikuwepo pale
kwa kazi maalum.
“Naomba kuzungumza na wewe, unamfahamu
Shenaiza?” nilimuuliza lakini badala ya kunijibu, alinitazama kuanzia juu mpaka
chini kisha akageukia pembeni. Kengele ya hatari ililia ndani ya kichwa changu,
harakaharaka nikageuka na kuanza kutembea kuelekea kwenye mlango wa kutokea.
“Unahatarisha maisha yako, achana na
mambo yasiyokuhusu,” alisema yule msichana, nikageuka na kumtazama, naye akawa
ananitazama. Sikuelewa kwa sababu gani amezungumza maneno yale, nikaendelea
kutembea harakaharaka na kutoka.
“Mungu wangu, mbona sielewi
kinachoendelea?” nilisema huku nikiendelea kutembea kwa haraka, nikaenda mpaka
kwenye lifti na kupanda, nikabonyeza namba ya ghorofa ilipokuwa wodi ya
‘private’ niliyokuwa nimelazwa, lifti ikaanza kupanda.
“Unatoka wapi?” Shamila aliniuliza
nilipofungua mlango tu, kumbe alikuwa amerejea muda mrefu na akawa anahangaika
kunitafuta.
“Nilitoka mara moja,” nilijitetea huku
nikijisikia aibu ndani ya moyo wangu.
“Kwa nini hujihurumii mpenzi wangu? Mimi
sitakwambia tena kuhusu suala la kuzingatia usalama wako,” alisema huku
akinisaidia kuvua lile koti la kidaktari huku akiendelea kunitazama kwa macho
ya mshangao.
“Samahani, eti hii ni dawa gani?”
nilisema huku nikitoa kile kichupa nilichokichukua kwenye kitanda cha Shenaiza.
Akakishika na kukitazama.
“Umekipata wapi?”
“Nimekikuta kwenye kitanda cha Shenaiza,
na anaonekana kama hana fahamu, rangi ya ngozi yake imebadilika na kuwa ya
kijivu,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment