ILIPOISHIA:
Nilifungua zipu kisha nikaanza kufanya
kama vile nilivyoelekezwa. Nikiwa naendelea na kitendo kile cha aibu na cha
aina yake, nilisikia watu wote waliokuwa sebuleni wakishtuka, nadhani waliniona
nilichokuwa nakifanya, sikuwajali, nikaendelea kuumwaga, mara kilisikika
kishindo kikubwa ambacho kilinifanya nishindwe kuendelea kufumba macho,
nikayafumbua.
“Mungu wangu!” nilisema kwa sauti ya
juu.
SASA ENDELEA...
Kile kilichokuwa kikinitoka, hakikuwa
haja ndogo kama mwenyewe nilivyokuwa nadhani, ilikuwa ni damu, tena nzito
kabisa yenye wekundu uliokolea kisawasawa, na kile kishindo kilichosikika,
kilikuwa ni cha dude kubwa lililoanguka kutoka angani.
Sijui niliiteje dude hilo kwa sababu
kwanza lilikuwa na miiba kama nungunungu, lakini pia lilikuwa na mabawa yenye
kucha kama popo, ukubwa wake ulikuwa kama ng’ombe mdogo.
Usoni lilikuwa na pembe zilizojikunja na
sehemu ya macho, kulikuwa kumezibwa kabisa, kwa kifupi halikuwa na macho. Ile
damu iliendelea kunitoka, hata pale nilipotaka kuikata haja ndogo, iliendelea
kunitoka kwa wingi utafikiri inavutwa na bomba.
Lile dude la ajabu, lilijiburuta chini
na kusogea mpaka pale nilipokuwa natolea haja ndogo, kwenye vizingiti vya
milango, likafumbua mdomo kidogo na kutoa ulimi mrefu uliokuwa umegawanyika
katikati kama wa nyoka, likaanza kulamba kile nilichokuwa nakitoa.
Naomba nieleze vizuri kilichotokea na
ambacho huwa kinatokea pale mtu anapokumbwa na nguvu za uchawi. Yaani tukio
unaliona, na ile hatari iliyopo mbele yako unaiona kabisa lakini mwili unakufa ganzi,
unakuwa huwezi kufanya chochote zaidi ya kile ambacho unakuwa umeshaanza
kukifanya na akili zako zinakosa maamuzi, kwa kifupi unakuwa siyo wewe.
Hicho ndicho kilichotokea, sikuwa na
uwezo wa kuikatisha ile haja ndogo ya damu, sikuwa na uwezo wa kwenda mbele,
wala sikuwa na uwezo wa kurudi nyuma, nilitamani kupiga kelele za kuomba msaada
lakini pia sikuweza kufanya hivyo, nikabaki nimeduwaa tu.
Lile dude lililamba ile damu yote pale
mlangoni, likaona haitoshi, likafumbua mdomo wake ambao ulikuwa na meno mengi
na kukinga ile iliyokuwa ikiendelea kunitoka kupitia haja ndogo, nikasikia kitu
kama ganzi ikinipata kwenye maeneo yangu nyeti kisha ile damu ikakata.
Lile dude ambalo ama kwa hakika lilikuwa
linatisha, likajilamba na kugeuka, likajikung’uta kwa nguvu kwenye mabawa yake
yenye kucha kubwa na kali, likawa kama linataka kuruka kwani lilipigapiga mbawa
zake, kufumba na kufumbua, likayeyuka na kupotea.
Lilipopotea tu, nilihisi kichwa kikiwa
kizito, nikaanza kuona giza machoni mwangu, nikawa nasikia sauti za ajabuajabu
masikioni, nikadondoka chini kama mzigo. Sikuelewa tena kilichoendelea.
***
Nilipokuja kuzinduka, nilijikuta
nimelala chini kwenye majani, mwili wangu ukiwa unahisi baridi kali kuliko
kawaida. Kilichonizindua zilikuwa ni kelele za ngoma na manyanga na sauti za
ajabuajabu za watu wakiimba nyimbo kwa lugha ambayo sikuwa naielewa.
Nilifumbua macho, huku mapigo yangu ya
moyo yakiwa yananienda mbio kuliko kawaida, macho yangu yalitazama juu moja kwa
moja. Nikawa naziona nyotanyota kwa mbali kuashiria kwamba ni usiku sana,
lakini pia upande wangu wa kushoto, kulikuwa kumewashwa moto mkubwa ambao
ulipafanya pale nilipolala, pawe na mwanga.
Niligeuza shingo kutazama pale ni wapi,
nilishtuka kugundua kwamba kumbe nilikuwa katikati ya duara, watu wengi
waliokuwa hawana kitu mwilini zaidi ya kujiziba kidogo na nguo nyeusi au
nyekundu kwenye maeneo nyeti walikuwa wamenizunguka. Wengine ambao ni wanawake,
walikuwa wamejiziba pia vifuani mwao.
Walikuwa wakiimba na kucheza kwa
kuzunguka duara ambalo ndani yake nilikuwa nimelazwa mimi na pia kulikuwa na
moto mkubwa jirani kidogo na pale nilipokuwa nimelala. Walikuwa wakiimba na
kucheza, huku kila mmoja akionesha kuwa na furaha kubwa.
Nilishtuka mno, nikawa sielewi pale ni
wapi na nimefikaje, nilijaribu kuwatazama watu hao kwenye nyuso zao kama kuna
yeyote ninayeweza kumtambua lakini macho yangu hayakuwa na nguvu za kutosha
kuona. Nilitaka kusimama lakini nilishtuka zaidi kugundua kwamba kumbe nilikuwa
nimefungwa mikono na miguu kwa kamba za miti.
Zile purukushani zangu, ziliwafanya wale
watu waache kila walichokuwa wanakifanya, wote wakawa wananitazama. Niligeuka
huku na kule, wote walikuwa wamenikazia macho. Kilichozidi kunitisha, macho yao
yalikuwa yakiwaka kama wanyama wakali wa porini.
Nikamsikia mmoja kati yao akizungumza
kwa lugha ambayo sikuwa naielewa, watu wote wakainua mikono juu kisha taratibu
wakaishusha chini, wakati wakishusha mikono, nao walishuka mpaka wakapiga
magoti, wakapeleka vichwa vyao mpaka chini kisha wakainuka na kusimama kama
mwanzo.
Yule mwanaume ambaye sikuwa najua yupo
upande gani, aliyarudia tena maneno yale, wakafanya hivyo tena mpaka chini, wakarudia
mara tatu kisha wote wakakaa chini na kukunja miguu.
Kizee kimoja kilichokuwa kimepinda
mgongo, kiliibuka kutoka kusikojulikana, kikiwa kinatembelea mkongojo. Kikawa
kinajikongoja kuja pale nilipokuwa nimefungwa, kadiri kilivyokuwa kinanikaribia
ndivyo mapigo ya moyo wangu yalivyokuwa yakizidi kuongezeka.
Sikujua kinataka kunifanya nini,
kilisogea mpaka pale nilipokuwa nimefungwa, nikakiona kikitoa kisu kikali,
kikaniinamia huku kikiyumbayumba, nikajua nimekwisha. Nimewahi kusikia kwamba
wachawi wana mchezo wa kuchinja watu na kuwala nyama, nikajua na mimi ndiyo
siku yangu ya kuliwa imewadia.
Tofauti na nilivyotegemea, wala
hakunidhuru mwilini, badala yake alikitumia kile kisu kukata kamba nilizofungwa
mikononi na miguuni. Kilichonishangaza zaidi, kumbe alikuwa akinijua mpaka jina
langu kamili.
“Togolai!”
“Naam, shikamoo babu,” niliitikia kwa
kutetemeka. Hakujibu salamu yangu, badala yake alinionesha sehemu ya kukaa,
akaniambia kwa ishara nikunje miguu kama watu wengine wote walivyokuwa wamekaa.
Nilitii agizo hilo haraka.
Kumbe pembeni ya pale nilipokuwa
nimelazwa, kulikuwa na vifaa mbalimbali, nikamuona akichukua kibuyu kimoja,
akakitingisha kisha akanipa na kunionesha kwa ishara kwamba ninywe kilichomo
ndani.
Huku nikitetemeka, nilikishika kibuyu
hicho, nikawa nakipeleka mdomoni huku nikimtazama kwa kina mzee huyo, pamoja na
watu wengine waliokuwa wamenizunguka kwa mbali.
“Nwa, ulogoleza shoni, nwa!” aliongea
kwa kilugha ambacho sikuwa nakielewa lakini kwa jinsi matamshi yake
yalivyokuwa, nilihisi ananiambia, ‘kunywa, unaogopa nini, kunywa’.
Nilipokisogeza kibuyu hicho karibu na
pua, nilikumbana na harufu kali kwelikweli, ikabidi nizibe pua, nikanywa huku
nikiwa nimefumba macho. Kabla sijameza, nilisikia vitu vikinitembea mdomoni,
nilipotazama vizuri kile kibuyu, pale kwenye mdomo wa kunywea, sikuyaamini
macho yangu, nikataka kutema lakini tayari nilishachelewa, vitu vyote vilikimbilia
tumboni vyenyewe.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu
kwenye Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment