ILIPOISHIA:
Safari hii maneno hayakuwa mengi,
tuliendelea kupasha miili yetu, tayari kwa ngwe ya pili ya pambano letu la
kirafiki. Safari hii yeye ndiye aliyekuwa akiniongoza nini cha kufanya, nami
nikawanafuatisha kwa utii mkubwa, haikuchukua muda, kipyenga kikalia kuashiria
kuanza kwa ngwe ya pili, huku safari hii akionesha kupania kuwa nyota wa
mchezo.
SASA ENDELEA…
Mikikimikiki iliendelea, kwa mud
nilisahau kama nilikuwa mgonjwa ambaye haukuwa umepita muda mrefu tangu
nizinduke kutoka kwenye usingizi wa kifo, wala usingeweza kuamini kwamba ndiye
mimi ambaye nilifikishwa hospitalini kila mmoja akiamini kwamba siwezi kurejewa
na fahamu zangu.
“Jamal! Jamaa..aa..al!” Shamila alipiga
ukelele na kunikumbatia kwa nguvu kifuani kwangu kuonesha kwamba tayari
alishasalimu amri, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida,
huku kila kiungo cha mwili wake kikiwa kimelegea kama mlenda.
Akaangukia pembeni, na mimi nikaangukia
upande mwingine, huku kijasho chembamba kikinitoka. Ni hapo ndipo nilipogundua
kwamba kuna majimaji yalikuwa yakinitoka pale kwenye jeraha langu, nikahisi
huenda ni jasho.
Nilipopeleka mkono na kujishika kisha
nikausogeza mkono machoni, nilishtuka kupita kiasi baada ya kugundua kuwa
zilikuwa ni damu znanitoka pale kwenye jeraha langu.
“M ungu wangu,” nilisema huku nikiinuka
harakaharaka na kusogea kwenye kioo cha dressing table ya kisasa iliyokuwa
ndani ya chumba hicho cha Shamila. Bandeji yote ilikuwa imelowa kwa damu
kuashiria kwamba kumbe zilikuwa zimeanza kunitoka muda mrefu uliopita.
Kumbe zile purukushani na Shamila
zilikuwa zimenitonesha lakini cha ajabu, wala sikusikia maumivu yoyote mpaka
muda huo. Nadhani utamu wa pambano letu la kirafiki ulifanya kazi kama sindano
ya ganzi, kweli waliosema mapenzi yana nguvu ya ajabu hawakukosea.
Cha ajabu, eti tayari Shamila alikuwa
akikoroma kwa uchovu, ikabidi nimtingishe kwa nguvu huku nikiliita jina lake.
Alionekana kuwa mzito sana, akafumbua macho kivivu na kunitazama.
“Amka, angalia mwenzio kilichonitokea,”
nilimwambia huku nikimuonesha kifua change, nikamuona jinsi alivyoshtuka,
japokuwa mwili wake haukuwa na nguvu, alkijikongoja na kuamka, akawa anashangaa
nini kimetokea.
Harakaharaka alichukua upande mmoja wa
khanga na kujifunga akainuka na kunisogelea, akionesha kuwa na hofu kubwa ndani
ya moyo wake.
“Pole Jamal, ooh! Mimi ndiyo
nimekusababishia,” alisema na kunibusu, harakaharaka akatoka huku akikimbia,
macho yangu yakawa yanamsindikiza kwa nyuma, japokuwa nilikuwa kwenye hali
mbaya, nilijikuta nikitabasamu kwani kilichotokea ilikuwa sawa na nzi kufia
kwenye kidonda, umbile lake likaacha mtikisiko adhimu na kunifanya nitingishe
kichwa changu.
Muda mfupi baadaye, alirejea akiwa na
kiboksi kidogo cha huduma ya kwanza kilichokuwa na alama ya msalaba mwekundu,
akanilaza kitandani na kuanza kunihudumia. Cha ajabu zaidi, safari hii wala
sikuhisi kabisa maumivu, nikawa muda wote namtazama Shamila usoni.
Waliosema mapenzi hayajaribiwi
hawakukosea, japokuwa mwenyewe nilikuwa najiona kama namzuga Shamila, kwa yale
‘maujanja’ aliyonionesha, nilijikuta akianza kuugusa moyo taratibu, nikawa
naendelea kumtazama wakati mwenyewe akinihudumia kwa unyenyekevu wa hali ya
juu.
“Mbona unaniangalia usoni, mi nasikia
aibu bwana,” alisema huku akinitazama kwa macho yake yaliyoonesha dhahiri jinsi
alivyokuwa amechoka, wote tukatabasamu.
“Haya inuka nimalizie kukufunga
bandeji,” alisema, ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kumbe tayari alishamaliza
kunifungua ile bandeji iliyokuwa imelowa damu na kunifunga nyingine, nikainuka
kwa umakini kwani hii ilikuwa mara ya pili kujitonesha, akamalizia kunifunga,
akarudia kunipa pole na kunibusu kwenye paji la uso wangu.
Akaanza kubadilisha lile shuka pale
kitandani kwake ambalo nilikuwa nimelichafua, huku akiendelea kuniomba radhi
kwa kunitonesha, nikawa nachekacheka tu.
“Muda umeenda sana, watakuwa
wanakutafuta hospitali, inabidi nikurudishe haraka,” alisema, nikaangalia saa
ya ukutani na kugundua kuwa tulikuwa tumetumia muda mrefu sana nje ya
hospitali, kinyume na utaratibu kwani ikumbukwe kwamba nilikuwa nimelazwa wodini
ila njama zangu na Shamila ndiyo zilizowezesha mimi kutoka.
“Naomba unisaidie kitu kimoja,”
nilimwambia Shamila wakati akiandaa mazingira ya sisi kwenda kuoga, baada ya
kuwa nimeshakunywa dawa za kutuliza maumivu alizonipa baada ya kumaliza
kunifunga jeraha langu.
“Jambo gani mpenzi wangu wa moyo,”
alisema Shamila huku akiniegamia kwa kudeka, nikamwambia naomba aniazime simu
yake nihamishe baadhi ya mafaili kutoka kwenye kompyuta ili nikaendelee
kuyapitia nikiwa wodini.
“Kwani ni mafaili gani? Halafu kwa nini
uyakopi kwenye simu wakati nina laptop?” alisema, jambo lililonifurahisha sana
kwani alikuwa amenirahisishia sana kazi, nikamzugazuga pale, akatoka na kwenda
kwenye chumba cha pili, aliporudi alikuwa na laptop ndogo mkononi, akanipa huku
tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.
Nilimshukuru sana, harakaharaka nikaenda
pale sebuleni, nikaiunganisha laptop na ile kompyuita ya mezani na kuanza
kukopi mafaili yote yaliyokuwa kwenye ile hard disk niliyopewa na Firyaal,
mdogo wake Shenaiza. Wakati mafaili yakiendelea kukopi, nilirudi chumbani kwa
Shamila ambaye alikuwa amejilaza akinisubiri.
“Ahsante kwa yote uliyonifanyia Jamal,
unajua mwanzo nilikuwa siamini kama kweli unanipenda, nilihisi kama mimi ndiyo
nakulazimisha lakini kwa haya uliyonifanyia leo, hata sijui nikwambie nini, kwa
kifupi elewa kwamba nakupenda sana na haijawahi kutokea mimi nikampenda mtu
kama ilivyotokea kwako,” alisema Shamila kwa sauti yenye uwezo wa kumtoa nyoka
pangoni, nikawa nachekacheka tu.
Aliinuka pale kitandani kichovu,
tukaelekea bafuni ambapo aliniogesha kama mtoto mdogo huku akiwa makini maji
yasiguse kidonda changu, alipomaliza, na yeye alioga kisha tukarudi chumbani
ambapo harakaharaka tulivaa, tukatoka sebuleni ambapo nilienda kuchungulia pale
kwenye kompyuta, nikakuta haijafika hata nusu kukopi.
“Inabidi nikukaangie mayai ule
harakaharaka tuondoke,” alisema Shamila huku akimalizia kuvaa vizuri nguo zake
za kazini, nikakosa cha kumjibu kwa sababu kiukweli nilihitaji muda zaidi ili
nikopi yale mafaili yote.
Aliwasha jiko la gesi, akanikaangia
mayai na dakika tatu tu baadaye, tayari yalikuwa tayari, akaniandalia mezani na
juisi, nikaanza kula taratibu ili angalau nivutevute muda, akampigia simu
dereva teksi na kumuelekeza atufuate.
Cha ajabu, wala hakuonesha kutaka kujua
nilikuwa nikihangaika na nini kwenye kompyuta, akaendelea kujiandaa kwa
kujipodoa kama ilivyo kawaida ya wanawake muda mfupi baadaye honi za gari
zikasikika nje kuonesha kuwa tayari ile teksi aliyoiita ilishafika. Bado
kompyuta haikuwa imefikisha hata asilimia ishirini na tano za kukopi, nikawa
sina ujanja zaidi ya ‘ku-cancel’ palepale ilipoishia, nikiamini lazima kuna
mambo mengi tu yalishaingia kwenye ile laptop.
“Wala usiwe na wasiwasi, hapa ni kama
kwako, kama hujamaliza kazi zako nitakuandalia utaratibu mwingine tuje tena,”
alisema Shamila, nikakualiana naye. Nikaichomoa ile laptop na kuzima kompyuta
huku ile hard disc ikia ndani yake. Nilijua nafanya makosa lakini nikaamini
Shamila hawezi kuiwasha hiyo kompyuta kwa sababu kwanza hakuwa akiijua password.
Harakaharaka tukatoka na kuingia ndani
ya teksi, safari ya kurudi hospitalini ikaanza huku muda wote Shamila akiwa na
furaha ya ajabu, akawa ananimwagia mvua ya mabusu.
Dakika kadhaa baadaye, tuliwasili
hospitalini lakini mazingira ya pale yalinishtua mno, hofu kubwa ikaukumba moyo
wangu tulipofika kwenye maegesho ya magari.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment