Sunday, September 3, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 29


ILIPOISHIA:
“Kuna kazi nimepewa ya kuhakikisha namzuia baba yake Shenaiza hicho anachokifanya, na ni lazima nitimize.”
“Kazi? Nani aliyekupa hiyo kazi? Halafu umzuie kwani anafanya nini na wewe umejuaje?” Raya alinibana kwa maswali, nikawa nashindwa hata namna ya kumjibu.
SASA ENDELEA...
“Si naongea na wewe Jamal!”
“Aah! Unajua ni stori ndefu kidogo na... na... ni...” nilijikuta nikishikwa na kigugumizi, Raya alikuwa akinitazama huku amenikazia macho. Nadhani kuna mambo alianza kuhisi kama hayaendi sawa.
Nilichokifanya ilikuwa ni kumzugazuga na kubadilisha mada, nikamhakikishia kwamba nitakapokaa na kutulia nitamueleza kwa kirefu kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Bado Raya alionesha kutoridhishwa na maelezo yangu na kikubwa kilichokuwa kikimsumbua ilikuwa ni wivu.
Kwa sababu kihistoria alishajenga mawazo akilini mwake kwamba mimi simpendi isipokuwa yeye ndiyo analazimisha mapenzi, alikuwa akiteseka sana ndani ya moyo wake akiamini kwamba akitokea mwanamke ambaye nitampenda, kama alivyokuwa akihisi kwa Shenaiza, nitamuacha jumla, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea.
“Halafu kuna mambo yananichanganya sana kichwa changu, sijui ni ndoto, maruweruwe au uchawi hata sielewi. Mbona nakumbuka kama mimi na wewe kuna sehemu tulikutana halafu tukaongea mambo mengi tu? Na kubwa zaidi mbona nakumbuka kama na mimi nilikufa?” kauli aliyoitoa Shenaiza muda mfupi uliopita ilijirudia ndani ya kichwa changu, nikawa natazama juu darini nikitafuta majibu ya maswali yangu.
Alichokisema Shenaiza ndicho kilichokuwa ndani ya akili yangu, ni kweli mimi na yeye kuna sehemu tulikutana na tukaongea mambo mengi tu, akanieleza kwamba ameamua kujiua kwa kujiovadozi madawa ya kulevya, akanihakikishia na mimi kwamba nilikuwa nimekufa lakini nikawa nambishia.

Shauku ya kutaka kufahamu zaidi kuhusu kilichotokea, ilinisukuma kuweka nadhiri ndani ya moyo wangu kwamba lazima nimtafute tena Shenaiza ili tuzungumze kwa kina, huenda mwenzangu alikuwa anaelewa kilichotokea kwa ufasaha zaidi.
Raya aliendelea kunisemesha mambo mengi lakini nikiri kwamba akili yangu haikuwa pale wodini, nilikuwa nikimfikiria Shenaiza na yote yaliyotokea. Naomba nieleweke kwamba hiyo haikumaanisha kwamba sikuwa nampenda Raya, nilishaamua kuwa naye baada ya kugundua kuwa ananipenda sana lakini kila nilipomfikiria Shenaiza, nilijikuta mwili wangu ukisisimka mno.
Bado kuna swali kubwa halikuwa limepata majibu akilini mwangu, haya yote yaliyokuwa yakitokea kwenye maisha yangu, kuanzia Shenaiza kunipigia simu na baadaye kunieleza kwamba amekosea namba, akaniganda kwamba hata kama amekosea anaomba nimsaidie na yote yaliyofuatia mpaka muda huo niliokuwa wodini.
“Hivi kama Mungu angeamua kuyachukua maisha yangu jumla, ningekufa nikiwa gizani kabisa, nikiwa sielewi chochote kilichosababisha mpaka nikafikwa na mauti? Mimi ni mtu wa ajabu eeh!” nilijikuta nikimuuliza Raya swali hilo, akashusha pumzi ndefu na kunitazama.
“Kwa hiyo kumbe muda wote nilikuwa naongea peke yangu?” alisema Raya huku akionesha kukasirishwa na kitendo cha mimi kuzungumza kitu ambacho hakikuwa na uhusiano wowote na kile alichokuwa akiniongelesha.
Niligundua kwamba nimekosea na kwa kuwa sikutaka kumuudhi Raya, ilibidi nimdanganye kwamba tangu nimerejewa na fahamu zangu, nahisi kichwa changu hakipo sawa kwa hiyo asinielewe vibaya, nikamuona akishusha tena pumzi na kunisogelea, akanibusu na kuninong’oneza:
“Nakupenda sana mpenzi wangu, nakuombea upone kabisa ili tuendelee na maisha yetu,” akanibusu na lipsi zake laini kwenye midomo yangu, akanibusu tena kwenye paji la uso kisha akaniambia kwamba anaenda kuniandalia chakula.
Alipofungua mlango na kutoka, ndugu na marafiki zangu waliokuwa wakisubiri nje, waliingia wodini na kukaa pembeni yangu, tukaendelea na stori za hapa na pale, wengi wakinipa pole kwa kilichotokea. Japokuwa hali yangu ilikuwa ikizidi kuimarika kwa kasi, lakini niliwaona watu wote wakiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua nini hasa kilichotokea.
Sikuwa tayari kueleza kila kitu, nikawa nafupisha tu kwamba nilivamiwa na majambazi walionijeruhi vibaya na kunifanya ninuse kaburi. Nilikuwa na sababu maalum za kutoeleza kila kitu kilichotokea, bado nilikuwa na kazi kubwa ya kuifanya.
Muda wa kuona wagonjwa ulipoisha, watu wote waliondoka na kuniacha nikiwa na nesi aliyekuwa akinihudumia tu, huku nikiendelea kumsubiri Raya ambaye aliahidi kwamba ndiyo atakayeniuguza mpaka nipone na kuruhusiwa kutoka wodini.
Kwa kuwa ndiyo kwanza alikuwa ametoka na kwenda kuniandalia chakula kama mwenyewe alivyosema, niliona huo ndiyo muda muafaka wa kumtafuta Shenaiza ili anieleze ukweli wa mambo mengi niliyokuwa nahitaji kuyajua.
“Nesi samahani naomba nikuulize,” nilimuuliza yule nesi mchangamfu aliyekuwa akipenda kunitania.
“Niulize tu honey wangu, nakupenda lakini mume mwenyewe una wanawake kibao, hujui najisikia wivu?” alisema huku akinisogelea, nikajikuta nikicheka kwa sauti. Nilimuuliza kuhusu Shenaiza kama anafahamu wodi aliyolazwa.
Alinipa majibu ambayo yalinishangaza sana, aliniambia kwamba msichana huyo alikuwa amelazwa kwenye wodi ya wagonjwa wa akili na kwamba kuna muda ilikuwa ni lazima wamfunge kamba kwa jinsi alivyokuwa akiwasumbua madaktari na wagonjwa wenzake.
Kiukweli nilishangazwa sana na maelezo hayo kwa sababu muda mfupi uliopita, nilikuwa nimezungumza naye na hakuonesha dalili zozote za kuchanganyikiwa mpaka alipokuja kuchukuliwa kwa nguvu na wale manesi.
Nilimuomba anielekeze vizuri wodi aliyokuwa amelazwa kwa sababu nilikuwa na mazungumzo muhimu naye, akaniambia kwamba utaratibu wa hospitalini hapo hauruhusu. Ilibidi niendelee kumbembeleza ambapo aliniambia atanisaidia kwa sababu ananipenda, akanisaidia kuinuka pale kitandani, tukaongozana kuelekea kwa Shenaiza kama nilivyomuomba.
Njia nzima yule nesi alikuwa akiendelea kunitania kuhusu mambo ya kimapenzi mpaka ikafika kipindi nikawa na wasiwasi kama kile alichokuwa anakisema ni utani au ananifikishia ujumbe kwa njia ya utani! Ukarimu na ucheshi wake, achilia mbali uzuri wa kipekee wa sura na umbo aliojaliwa, vilinifanya nimzoee haraka.
Alinipeleka mpaka kwenye wodi hiyo lakini kutokana na mazingira ya mle ndani, aliniambia nimsubiri hapohapo nje, akaingia na kwenda kuzungumza na manesi wenzake na muda mfupi baadaye, alitoka akiwa na Shenaiza ambaye aliponiona tu, alinikimbilia na kunikumbatia.
“Eti wameamua kunipakazia kwamba mimi ni mgonjwa wa akili. Jamal, eti mimi naongea kama mtu aliyechanganyikiwa?” aliniuliza Shenaiza huku akilia kwa uchungu, nikamuomba yule nesi atuache kidogo ili tuzungumze wawili tu, akanitazama kwa macho yake mazuri ya kurembua kisha akatingisha kichwa kuonesha kukubaliana na nilichomwambia.
“Nakupa dakika tano tu, nakusubiri pale pembeni,” alisema, nikamshukuru na kumshika mkono Shenaiza, tukakaa kwenye benchi lililokuwa pembeni.
“Akina nani wanaokupakazia kwamba wewe ni mgonjwa wa akili?”
“Baba na watu wake, wanataka kuniziba mdomo maana nimetishia kwamba nitaueleza ulimwengu wote ukweli wa wanachokifanya, naomba unisaidie,” alisema Shenaiza huku akilia, akanikumbatia kwa nguvu huku machozi mengi yakinichirizikia mwilini.
Kitu ambacho lazima nikikiri hapa, japokuwa nilikuwa nimeamua kumchagua Raya kuwa mke wangu mtarajiwa, nilipokuwa nikimtazama Shenaiza au kukaa naye karibu, moyo wangu ulikuwa ukisuuzika mno. Nadhani hata yeye alikuwa analijua hilo ndiyo maana kila tunapokaa pamoja, ilikuwa ni lazima anishike mkono, aniegamie au anikumbatie.
“Sasa nakusaidiaje Shenaiza mbona unazidi kuniweka kwenye wakati mgumu?”
“Unataka kuwajua watu waliokuwa nyuma ya tukio lako la kunusurika kuuawa?”
“Ndiyo, hata sasa hivi nataka kuwajua. Bado nina maswali mengi kichwani ambayo hayana majibu.”
“Najua, majibu ya maswali yako yote ninayo na kwa hali ilipofikia, nipo tayari kukueleza kila kitu kabla hawa mashetani hawajaniharibu kumbukumbu zangu maana najua haya madawa ya wagonjwa wa akili wanayolazimisha nichomwe, huwa yanaenda kuvuruga kabisa ubongo,” alisema Shenaiza kisha akanibusu kwenye paji la uso.
“Nenda Kisutu, Mtaa wa Mama Zayumba, nyumba namba 203, muulize mtu anaitwa Firyaal, ni mdogo wangu wa kuzaliwa na nilishampa maelekezo, kuna bahasha atakupa na hiyo ndiyo yenye majibu ya maswali unayoyahitaji,” alisema Shenaiza huku akinitazama kwa macho ya upole.
“Narudia tena kukuomba msamaha kwa yote yaliyotokea Jamal, naomba unisamehe. Nahitaji ukaribu wako na msaada wako katika kipindi hiki kigumu ninachopitia,” alisema Shenaiza huku macho yake yakiwa yamebeba ujumbe mzito zaidi, tukatazamana kama sekunde tano mfululizo, nikamuona akiachia tabasamu hafifu lililofanya uzuri wake wa asili uonekane vizuri.
“Ukikamilisha kazi nitakupa zawadi ya ushindi,” alisema Shenaiza huku akinifinyia kijicho kimoja, nilishaelewa alimaanisha nini. Nikasimama na kumshukuru, nikambusu kwenye paji la uso wake na kugeuka nyuma ili nirudi kule wodini kwangu.
Sijui Raya alikuwa amefika muda gani eneo hilo kwani nilipogeuka tu, macho yangu na yake yaligongana, japokuwa alikuwa umbali wa mita kadhaa, niliweza kuona hali aliyokuwa nayo. Ilionesha hata kitendo cha mimi kumbusu Shenaiza alikiona kwa macho yake, nikamuona akianza kububujikwa na machozi.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...