ILIPOISHIA:
“Hapana! Hapanaaa,” nilisema kwa sauti
ya juu, ikabidi baba anizibe mdomo maana alihisi naweza kuropoka mambo mengine
na kuwafanya wasiohusika wajue.
“Huna haja ya kuogopa, zipo njia za
kutimiza hicho ulichoambiwa bila kuonekana kama wewe ndiyo umefanya moja kwa
moja, mbona sisi huwa tunafanya sana tu,” alisema baba, macho yakanitoka.
SASA ENDELEA...
Aliondoa mkono wake mdomoni mwangu,
akaniambia wameniamini ndiyo maana wameniunganisha kwenye jamii yao, akaniambia
faida nitakazozipata ni nyingi na kubwa sana kwa hiyo sina sababu ya kuogopa
kutimiza sharti lile dogo nililopewa.
“Sijawahi kuua mtu hata siku moja,
nitaanzaje,” nilisema, baba akatabasamu na kumgeukia baba yake Rahma, wakacheka
na kugongesheana mikono. Sikuelewa kwa nini wao wacheke wakati mimi nilikuwa
kwenye hali mbaya kiasi hicho, hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye moyo wangu.
“Unatakiwa ujue namna ya kudhibiti hofu
yako, ukiwa mwoga hivi huwezi kufanya chochote,” alisema baba, baba yake Rahma
akamuunga mkono, wakawa wananieleza kwamba mtihani niliopewa ni mdogo sana na
endapo nitashindwa nitakuwa nimewaangusha sana na kila mtu atanicheka.
“Utathibitisha kwamba kauli yangu
niliyoitoa juu yako ni sahihi.”
“Kwamba wewe bado una akili za kitoto,”
baba alisema. Hakuna kitu nilichokuwa sikipendi kama kusikia kauli za namna
hiyo kutoka kwa baba, nikajikuta morali fulani ukinipanda ndani kwa ndani,
nikajisemea kwamba nitamuonesha kwa vitendo kama mimi siyo mtoto.
“Endelea kupumzika mpaka mwili upate
nguvu, tutakuja baadaye kukuelekeza nini cha kufanya,” alisema baba, wakatoka
na kuniacha nimelala palepale kitandani. Kwa nje nilisikia wakifunga mlango kwa
funguo, nikabaki nashangaa kwa nini wananifungia?
Sikuwaza sana kuhusu hilo la mlango,
bado nilikuwa na mawazo mengi juu ya hatma yangu na ile kazi niliyokuwa
nimepewa. Sikuwahi kudhani hata siku kwamba eti na mimi naweza kuwemo kwenye
orodha ya wachawi, tena wanaoua na kula nyama za watu wasio na hatia.
Ni kweli kuna kipindi nilikuwa nikitamani
kuwa na nguvu kama za baba lakini nilichokuwa nikikijua ni kwamba nguvu zake
zilikuwa ni za kutibu watu na kufanya yale yasiyowezekana tu, sikujua kuwa
gharama zake ni kubwa kiasi hicho.
Sikupata jibu mtihani mkubwa uliokuwa
mbele yangu ningeuvuka vipi, sikujua ni kwa kiasi gani moyo wangu utakuwa na
hatia kwa kuyakatisha maisha ya mtu asiye na hatia. Kuna wakati nilikuwa
nikitamani kama nitoroke na kuelekea kusikojulikana lakini kila nilipokuwa
nikifikiria vile vitisho nilivyokuwa napewa, nilijikuta nikikosa ujanja.
Nilipokumbuka na kauli za baba za
kunidharau, nilijikuta nikizidi kuchanganyikiwa, sikuelewa nini itakuwa hatma
yangu. Basi niliendelea kuwaza na kuwazua pale kitandani, mwili ukaanza kupata
nguvu taratibu, saa zikawa zinazidi kuyoyoma.
Mida ya jioni baba alikuja tena,
akafungua mlango na kuingia akiwa na bakuli lililokuwa na supu ya kuku wa
kienyeji. Akaniwekea vizuri na kuniambia niinuke mwenyewe pale kitandani. Kwa
kuwa safari hii nilikuwa na nguvu, niliinuka mwenyewe na kukaa kitako.
Akanisogezea lile bakuli na kunipa.
Nililipokea huku mikono ikitetemeka, nikaanza kuinywa supu ile kwa pupa. Muda
mfupi tu baadaye, bakuli lilikuwa tupu. Ile njaa niliyokuwa nayo sasa ilikuwa
imepungua na nilijihisi kuwa na nguvu kama zamani.
“Hebu jaribu kusimama mwenyewe,” baba
aliniambia wakati akikusanya mifupa na kuiweka kwenye lile bakuli,
nikajishikilia kwenye kingo za kitanda na kusimama. Bado miguu haikuwa na nguvu
vizuri lakini niliweza kusimama, akaniambia nizunguke mle ndani, kweli
nikaweza.
“Safi sana, sasa umekuwa mwanaume
kamili,” aliniambia huku akinielekeza kuendelea kupumzika mpaka usiku. Nilirudi
kitandani na kujilaza, kidogo nikawa najisikia vizuri, baba akatoka na kufunga
tena mlango kwa ndani.
Kiukweli nilikuwa nimemkumbuka sana
Rahma, sikujua anawaza nini juu yangu maana siyo kawaida tukae wote nyumba moja
halafu tusionane siku nzima. Nilitamani japo nipate muda mfupi wa kuonana naye,
nimweleze kinachonitokea maishani mwangu maana angeweza kuhisi kama labda
simpendi tena na ndiyo maana nimebadilika.
Muda ulizidi kuyoyoma na hatimaye giza
likaingia, mara nikasikia mlango ukifunguliwa. Walikua ni baba na baba yake
Rahma, waliingia na kuwasha taa, wakanisogelea mpaka pale kitandani.
“Vipi unaendeleaje?”
“Naendelea vizuri.”
“Safi, sasa inatakiwa tuondoke kuna
mahali tunaenda kukuonesha sehemu tunapochimba dawa zetu za kufanyia kazi,”
baba aliniambia, nikainuka na kukaa vizuri.
“Kwa mfano hiyo kazi uliyopewa, huwezi
kuifanikisha kwa urahisi mpaka uwe na dawa na inabidi dawa hizo ukachimbe wewe
mwenyewe, kwa hiyo sisi tunachokifanya ni kukuelekeza tu, mambo mengine
utafanya mwenyewe ikiwa ni pamoja na kujifunza kwa vitendo,” alisema baba.
Sikuwa na cha kujibu zaidi ya kuinuka,
nikataka kwenda kuoga lakini baba alinikataza, akasema sitakiwi kuoga kwa muda
wa siku saba, nikashangaa sana. Aliniambia nivae nguo zangu tuondoke haraka
maana tulikokuwa tukienda ni mbali.
Ilibidi nifanye kama walivyoniambia,
nilivaa nguo zangu vizuri, baba akafungua mlango na kutangulia, kabla hajatoka
aliniambia kwamba kila tunakoenda, sitakiwi kutangulia mbele wala kubaki nyuma,
muda wote niwe katikati yao.
Sikuelewa maana ya maelekezo yake hayo
ila nilitii, akatangulia, nikafuata halafu baba Rahma akafuatia nyuma. Nikiri
kwamba baada ya yale yote yaliyotokea, nilikuwa nikiwatazama baba na baba yake
Rahma kwa jicho tofauti kabisa. Hata sijui nieleze vipi lakini kwa kifupi
nilikuwa nikiwatazama kwa jicho la tofauti.
Tulitoka moja kwa moja mpaka nje na
nadhani hakuna mtu yeyote aliyetuona, tulitoka mpaka pale nje kabisa palipokuwa
na maegesho ya Bajaj na bodaboda.
“Yule jamaa aliyekamatwa kwa mauaji
ameachiwa? Sijui kama tutapona mtaa huu,” nilimsikia dereva bodaboda mmoja
akiwaambia wenzake, akimaanisha mimi. Nilijua kwamba ananizungumzia mimi maana
hata siku ile nilipokuja kuchukuliwa na polisi pale nyumbani, yeye ndiyo
alikuwa kiherehere wa kuwasimulia wenzake kwamba eti mimi nimemuua mtu gesti.
Nilijikuta nimepandwa na jazba,
nikatamani kama nimrukie na kumtandika makofi kwa hasira. Hakuna kitu ambacho
huwa sikipendi kama dharau. Kumbe wakati nikifikiria nini cha kufanya, baba na
baba yake Rahma walishajua ninachowaza.
“Hutakiwi kuwa na hasira zisizo na
msingi, muache afurahishe mdomo wake,” alisema baba yake Rahma huku
akinipigapiga begani. Nilishusha pumzi ndefu, baba akazungumza na dereva mmoja
wa Bajaj, tukaingia na mimi nikakaa katikati.
“Tupeleke Ubungo,” alisema baba, safari
ikaanza. Ubungo hapakuwa pageni kwangu kwani ndiyo sehemu ya kwanza kukanyaga
tuliposhuka kwenye basi tukitokea Chunya. Basi tulienda mpaka Ubungo,
tulipofika baba alimlipa dereva, tukavuka kwenye mataa ya kuongozea magari na
kwenda upande wa pili mpaka kwenye stendi ya daladala.
Tulipanda kwenye gari moja, hata sijui
linaelekea wapi, tukaenda kukaa siti ya nyuma kabisa, mimi nikiwa katikati.
“Kwani tunaenda wapi?”
“Tunaenda Kibaha,” alisema baba,
nikashindwa kumhoji chochote maana hata huko kibaha kwenyewe sikuwa nakujua.
Baadaye gari liliondoka, ikiwa ni majira
ya kama saa tatu za usiku, tukaenda mpaka tulipofika Kibaha, tukashuka na kuanza
kutembea kwa miguu. Tulivuka barabara, nikaona kuna kibao kimeandikwa Tumbi
Hospital, nimewahi sana kuisikia hii hospitali kwani mara nyingi ajali nyingi
zinazotokea mkoa wa Pwani majeruhi au maiti huwa zinapelekwa Tumbi.
Basi tulianza kutembea kuifuata barabara
hiyo, giza nalo likawa linazidi kuwa nene, tukatembea umbali mrefu, tulipofika
kule juu kabisa, tuliiacha barabara ya lami na kuingia vichakani, nako
tukatembea umbali mrefu sana, hatimaye tukatokezea kwenye eneo lililokuwa na
vichana vifupivifupi.
Kwa kutumia tochi aliyokuwa nayo, baba
alianza kumulika kwenye vile vichaka kama anayetafuta kitu, mimi na baba yake
Rahma tukawa tunamfuata kwa nyumanyuma maana kama nilivyosema, mimi sikutakiwa
kutangulia mbele wala kubaki nyuma kwa hiyo ilikuwa ni lazima tutembee
watatuwatatu.
“Unauona huu mti, unaitwa mtunguja, huu
ndiyo hutumika sana kutengeneza ajali za kichawi na unapatikana kwa wingi eneo
hili na ndiyo maana huku kila siku unasikia ajali mbayambaya zinatokea maana
wanafunzi kama wewe, huku ndiyo eneo la kujifunza kwa vitendo,” alisema baba
huku akianza kufukua kwenye shina la mti huo mdogo.
“Sifa yake moja, huu mtu huwa unatoa
damu,” alisema baba, akatoa kisu na kubandua sehemu ndogo ya ganda lake,
nikashangaa kweli mti ukitoa vitu vilivyokuwa vikifanana kabisa na damu.
“Niangalie vizuri namna ya kuchimba
maana tukitoka hapa inabidi na wewe ukafanye majaribio kama wenzako,” alisema
baba. Muda huo ulikuwa ni kama saa sita hivi za usiku, giza nene likiwa
limetanda kila sehemu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment