ILIPOISHIA:
Harakaharaka tukatoka na kuingia ndani
ya teksi, safari ya kurudi hospitalini ikaanza huku muda wote Shamila akiwa na
furaha ya ajabu, akawa ananimwagia mvua ya mabusu. Dakika kadhaa baadaye,
tuliwasili hospitalini lakini mazingira ya pale yalinishtua mno, hofu kubwa
ikaukumba moyo wangu tulipofika kwenye maegesho ya magari.
SASA ENDELEA...
Gari jeusi lililokuwa na vioo vya rangi
nyeusi (tinted), Isuzu Bighorn lilikuwa limepaki kwenye maegesho hayo huku
milango ya upande mmoja ikiwa wazi. Kumbukumbu zangu zilionesha kwamba hiyo
haikuwa mara ya kwanza kuliona gari hilo machoni mwangu, nikawa najaribu
kukumbuka ni wapi?
Shamila alimlipa dereva teksi na kutaka
kushuka lakini nikamzuia, akabaki anashangaa. Niliendelea kulitazama lile gari
na kwa makini, ghafla kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu baada ya
kumuona mmoja kati ya watu waliokuwa ndani ya gari hilo.
Alikuwa ni kijana mmoja mwenye asili ya
Bara la Asia, ambaye rangi ya ngozi yake ilikuwa ikifanana sana na ya Shenaiza
pamoja na mdogo wake, kuonesha kwamba walikuwa na aina fulani ya unasaba kati
yao. Nilipozidi kumtazama, nilimkumbuka kwamba mimi na yeye tulikutana kwenye
matukio mawili tofauti, tena yote ya hatari yakimhusisha Shenaiza.
Tukio la kwanza lilikuwa ni siku
nilipokuwa najaribu kumtorosha Shenaiza hospitalini, kipindi hicho wakati ndiyo
kwanza tumeanza kufahamiana. Tukio la pili, ambalo liliyafanya mapigo ya moyo
wangu yaniende kasi kuliko kawaida.
Lilikuwa ni tukio ambalo almanusra
liukatishe uhai wangu baada ya kuvamiwa na watu nisiowafahamu kwenye foleni,
maeneo ya Magomeni Mataa ambao walinishambulia vikali na kunijeruhi vibaya na
kitu chenye ncha kali kifuani.
“Ni yeye! Ni mwenyewe...” nilijikuta
nikitamka kwa nguvu, Shamila na yule dereva teksi wakabaki kunishangaa, wakiwa
hawaelewi nilichokuwa namaanisha.
“Upo sawa kweli? Kama kuna tatizo si
uniambie mpenzi?” alisema Shamila huku na yeye akiwa makini kutazama kule
nilikokuwa naangalia, ghafla nikamuona amekazia macho pale kwenye lile gari,
naye akawa ni kama ameona kitu.
Kwa bahati nzuri, ile teksi tuliyopanda
ilikuwa pia na vioo vyenye tinted kwa hiyo haikuwa rahisi kwa watu waliokuwa
nje kutuona. Tulitulia kwa dakika kadhaa, wote tukiwa tunawatazama wale vijana
ambao walionekana kama wanajadiliana kitu huku macho yao yote yakiwa upande
zilipokuwepo wodi, hasa ile niliyokuwa nimelazwa mimi.
“Unawafahamu?”
“Ndiyo, wana ukaribu na Shenaiza na
ndiyo waliohusika kwenye jaribio la kutaka kuyakatisha maisha yangu.”
“Sasa hapa watakuwa wamefuata nini?”
“Kuna mawili, wanaweza kuwa wamemfuata
Shenaiza au wamenifuata mimi.”
“Wakufuate wewe? Kwa kipi hasa?”
“Nimeshakwambia kuwa ni hawa ndiyo
walioshiriki kwenye jaribio la kutaka kuyakatisha maisha yangu, yule mmoja
namkumbuka vizuri kabisa.”
“Basi kama ni hivyo kwa nini tusiwapigie
simu walinzi wa hospitali wawasiliane na polisi na kuwakamata? Mimi nina namba
za mlinzi wetu wa kule getini,” alisema Shamila huku akitoa simu yake lakini
nikamzuia.
Yule dereva teksi aliendelea kutulia
kama haelewi chochote kinachoendelea, tukaendelea kujadiliana mle ndani ya
teksi kwa muda mrefu huku nikiwa nimekosa kabisa amani.
Hakuna kitu kibaya maishani kama kuwaona
wabaya wako lakini ukawa huna namna ya kulipa kisasi, nikaamua kufuata ule
usemi maarufu ambao Waingereza hupenda kuutumia; ‘dont hunt what you can’t kill’
wakimaanisha usiwinde usichoweza kukiua!
Tukiwa bado tumetulia pale kwenye gari,
ghafla kwa mbali tulimuona mtu aliyekuwa amevalia mavazi ya kidaktari akitoka
kwenye wodi niliyokuwa nimelazwa, akatazama huku na kule kama anayetafuta kitu
kisha akatembea harakaharaka mpaka pale kwenye lile gari, akawa anazungumza na
wale watu waliokuwa mle ndani ya lile gari huku mara kwa mara wakigeuka
kutazama kama kuna mtu aliyekuwa akiwatazama.
“Mungu wangu, nini kinachoendelea hapa?
Mbona huyu aliyevaa kama daktari siyo mfanyakazi hapa hospitalini?”
“Siyo daktari? Kivipi? Na kama siyo
daktari mbona amevaa nguo za kidaktari na ameingia hadi wodini?”
“Niamini ninachokwambia, madaktari wote
wa hapa nawafahamu, huyu siyo mfanyakazi,” alisema Shamila kwa kujiamini,
nikaiona hatari kubwa iliyokuwa mbele yangu. Kwa tafsiri nyepesi, mtu huyo
alikuwa akishirikiana na wale watu waliokuwa ndani ya gari.
Kilichozidi kunishangaza, aliwezaje
kuingia mpaka ndani ya wodi niliyokuwa nimelazwa bila kugunduliwa na walinzi wa
hospitali hiyo? Kama angekuwa na nia ya kunidhuru ingekuwaje?” nilijikuta
kijasho chembamba kikinitoka.
Waliendelea kujadiliana pale kwenye gari
kisha tukamuona yule aliyejifanya daktari akivua koti lake jeupe na kuliweka
kwenye siti za nyuma za gari, akaingia kwenye gari, milango ikafungwa na gari
hilo ambalo muda wote lilikuwa likinguruma taratibu bila kuzimwa (silencer),
likaanza kurudi nyuma likitafuta upenyo wa kutoka kwenye maegesho hayo.
Muda mfupi baadaye, liliondoka kwa kasi
kubwa huku likitimua vumbi bila kujali kwamba eneo hilo lilikuwa ni hospitali
na kulikuwa na wagonjwa waliokuwa wakihitaji utulivu, nikashusha pumzi ndefu na
kuegamia kwenye siti niliyokuwa nimekaa, Shamila naye akafanya hivyohivyo.
“Sasa itakuwaje?”
“Sipo tayari kuendelea kulazwa kwenye
hii hospitali, ni bora nikafie mbele ya safari, hapa si sehemu salama tena,”
nilimjibu Shamila, akawa anatingisha kichwa kuonesha kuniunga mkono kwa kile
nilichokuwa nakisema.
Tukiwa bado ndani ya teksi ile,
nilishtuka sana baada ya kumuona Raya akifungua mlango na kutoka kwenye ile
wodi niliyokuwa nimelazwa, mkononi akiwa amebeba kikapu kilichokuwa na chakula,
akionesha kuwa na huzuni kubwa ndani ya moyo wake.
Baada ya kutoka wodini, alikaa kwenye
benchi lililokuwa pale nje na kuweka kikapu chake chini, akawa anatazama huku
na kule huku akionesha kuwa na wasiwasi mkubwa ndani ya moyo wake. Kwa
kumtazama tu, japo nilikuwa kwa mbali, nilielewa kilichokuwa kikipita ndani ya
kichwa chake, nikajikuta nikimuonea huruma sana.
Kumbe wakati nikimtazama Raya kwa
huruma, Shamila naye alikuwa akinitazama usoni! Haya mambo ya mapenzi hatari
sana, akashikwa na wivu mkali, akanizindua kwa kunigeuza kule nilikokuwa
natazama na kunigeuzia kwake.
“Uko sawa?” aliniuliza huku hisia kali
za wivu zikijionesha waziwazi kwenye uso wake.
“Nitakuwaje sawa katika mazingira kama
haya? Naomba unisaidie jambo, kamuulize Raya yule daktari feki alipoingia
wodini amesemaje?” nilimwambia Shamila, akaendelea kunitazama machoni huku
akionesha dhahiri kwamba kuna jambo alikuwa anataka kuniambia.
Kwa shingo upande alishuka na kutuacha
mimi na dereva teksi ndani ya ile teksi, aliposhuka tu, nilimwambia dereva
aloki milango, tukawa tunamtazama Shamila anavyotembea kwa maringo kuelekea
kule nje ya wodi alikokuwa amekaa Raya.
“Vipi kaka ndiyo unakaa hapa nini?”
aliniuliza yule dereva teksi kwa lugha za vijana, akimaanisha kama mimi ndiye
niliyekuwa nikitoka kimapenzi na Shamila, nikashindwa cha kumjibu kwani kwa
muda huo akili yangu ilikuwa ikienda ‘resi’ sana, akaendelea:
“Duh! Si mchezo, utakuwa unafaidi sana,
bonge la kifaa, ningekuwa mimi ningetangaza ndoa kabisa!”
Alikuwa na haki ya kusema hivyo kwa
sababu kama nilivyoeleza awali, Shamila alikuwa mwanamke aliyejaaliwa uzuri wa
kipekee mno, ukichanganya na umbile lake lililojazia kwa nyuma, hakuna mwanaume
ambaye amekamilika angeweza kupishana naye bila kugeuka mara mbilimbili.
Japokuwa alikuwa amevaa nguo zake za
kazini, uzuri wake haukuweza kujificha, nikajikuta kwenye wakati mgumu kwani
Raya nilikuwa nampenda na alikuwa na mapenzi ya dhati kwangu, ukichanganya pia
kwamba mimi ndiye niliyekuwa mwanaume wake wa kwanza maishani, nilijihisi kuwa
sehemu ya maisha yake!
Niliendelea kutulia mle ndani ya teksi,
Shamila akaenda mpaka pale Raya alipokuwa amekaa huku amejiinamia, alipomuona
Shamila tu, harakaharaka alisimama na kumsogelea, akawa anamuuliza jambo ambalo
japokuwa sikuwa nasikia, nilitambua kwamba ananiulizia mahali nilipokuwa mimi
‘mgonjwa wake’.
Tofauti kabisa na tulivyokubaliana,
nilishangaa Shamila akimuonesha kwa kidole kwenye ile teksi niliyokuwemo,
nikamuona Raya akiacha kila kitu palepale na kuanza kutimua mbio kuja kwenye
ile teksi, Shamila akawa amesimama akimtazama. Nilijua wazi kwamba amefanya
hivyo kwa sababu ya wivu.
Ghafla akiwa anakuja mbio, lile gari
lilitokeza tena na kuja kwa kasi pale lilipokuwa limepaki awali, nikashtuka
kugundua kuwa kumbe wale watu hawakuwa wameondoka, nikajua lazima watashtukia
mahali nilipo kutokana na jinsi Raya alivyokuwa anakuja kwa kasi.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu
kwenye Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment