ILIPOISHIA:
“Ukikamilisha
kazi nitakupa zawadi ya ushindi,” alisema Shenaiza huku akinifinyia kijicho
kimoja, nilishaelewa alimaanisha nini. Nikasimama na kumshukuru, nikambusu
kwenye paji la uso wake na kugeuka nyuma ili nirudi kule wodini kwangu.
SASA
ENDELEA...
Sijui
Raya alikuwa amefika muda gani eneo hilo kwani nilipogeuka tu, macho yangu na
yake yaligongana, japokuwa alikuwa umbali wa mita kadhaa, niliweza kuona hali
aliyokuwa nayo. Ilionesha hata kitendo cha mimi kumbusu Shenaiza alikiona kwa
macho yake, nikamuona akianza kububujikwa na machozi.
Nilijikuta
mwili wangu ukipigwa na ganzi, nikabaki nimesimama nikihisi hata miguu ilikuwa
mizito kuinyanyua. Raya alipoona nimemuona, aligeuka na kuanza kutembea
harakaharaka huku akiendelea kulia. Niljihisi kuwa na hatia kubwa sana ndani ya
moyo wangu.
Japokuwa
mimi na Shenaiza hatukuwa tumebusiana kwa nia mbaya, nilijaribu kujiweka kwenye
nafasi ya Raya na kuhisi maumivu ambayo alikuwa anayahisi kwa wakati huo. Kwa
wale ambao wamewahi kupitia maumivu ya mapenzi watakuwa wanaelewa vizuri
ninachomaanisha!
Ukimpenda
mtu halafu ukasikia au ukahisi mtu mwingine pia anampenda, ukiwaona pamoja
lazima moyo uume sana, na hapo ni ukiwaona kawaida tu, iwe wameongozana
barabarani au wamekaa sehemu! Raya alishajua kwamba kuna kitu kipo kati yangu
na Shenaiza na kama hakipo basi kinakuja lakini kibaya zaidi, alikuwa amenifuma
laivu nikimbusu msichana huyo!
Uso
wangu ulinishuka kwa haya, sikujua nitatumia maneno gani kumlainisha Raya,
nikawa nazidi kuongeza mwendo kumfuata lakini ghafla nikahisi kitu kikinipasua
pale kwenye jeraha langu kifuani ambalo japokuwa nilikuwa na nafuu kubwa, bado
halikuwa limepona kabisa.
Licha
ya maumivu niliyoyasikia, sikutaka kurudi nyuma, nilijikaza kisabuni na
kuendelea kujikokota kumfuata Raya ambaye naye alizidi kuongeza mwendo, akiwa
hataki hata kugeuka nyuma kunitazama. Nilivuka kwenye mlango wa kuingia kwenye
ile wodi niliyokuwa nimelazwa, nikawa naendelea kumfuatilia Raya aliyekuwa
akielekea kwenye geti la kutokea kwa kasi.
Hatua
chache mbele nilishindwa kuendelea kumfuatilia baada ya kuhisi maumivu yakizidi
pale kifuani kwenye jeraha, nikainama kidogo ule upande wenye jeraha, katika
hali ambayo sikuitegemea, nilishtuka mno kugundua kuwa kumbe damu zilikuwa
zikinitoka pale kwenye jeraha kiasi cha kulowanisha shati nililokuwa nimevaa.
Nilipogeuka
nyuma, niliona michirizi sakafuni kuonesha kuwa kumbe damu ilianza kunitoka
pale nilipohisi kitu kikinipasua kifuani, hofu kubwa ikatanda moyoni mwangu.
Nikawa nahaha kutaka kujifuta damu na kuzifuta sakafuni kabla mtu yeyote
hajaona maana ningeonekana mzembe nisiyejijali afya yangu na huenda madaktari
wangenifokea sana lakini sikuwa na nguvu ya kufanya hivyo.
Niligeuka
huku na kule kutazama kama kuna mtu alikuwa akiniangalia, pande zote hakukuwa
na mtu yeyote zaidi ya Raya aliyekuwa akiishia kwa mbali, lakini nilipotazama
kwenye mlango wa ile wodi niliyokuwa nimelazwa, macho yangu yaligongana na ya
yule nesi ambaye kumbe muda wote alikuwa akitazama kila kilichokuwa
kikiendelea, akiwa ametulia tuli.
Nilishindwa
cha kujibu zaidi ya kuendelea kuhaha huku na kule, yule nesi aliendelea
kunitazama huku akitingisha kichwa kwa masikitiko. Maumivu yalinizidi, ikabidi
niegemee kweye ukuta wa korido huku nikipumua kwa shida.
Harakaharaka
yule nesi alikuja mpaka pale nilipokuwa nimeegemea ukuta lakini tofauti na
nyakati zote, safari hii hakuwa akicheka wala kutabasamu, kwa mara ya kwanza
nilimuona akiwa ‘serious’.
“Help
me please!” (Nisaidie tafadhali) nilisema huku nikiendelea kupumua kwa shida,
hakunijibu kitu zaidi ya kunipa ishara kwamba nimshike begani, nikafanya hivyo,
akapitisha mkono wake mmoja kiunoni kwangu, wa kwangu nikaupitisha kwenye bega
lake, akanisaidia kutembea kuelekea wodini huku damu zikiendelea kunitoka.
Yule
nesi alinipeleka mpaka kitandani kwangu, akanisaidia kupanda na harakaharaka
akanivua lile shati nililokuwa nimevaa, akatoka mbiombio na muda mfupi baadaye
alirejea akiwa na kisinia kilichokuwa na vifaa vingi vya tiba.
Kimyakimya
akaanza kunisafisha pale kweye jeraha, akanifungua bandeji iliyokuwa imeachia,
akanipaka dawa ya kuzuia damu kutoka, akanifunga plasta na bandeji nyingine
kisha akanipa dawa za kutuliza maumivu. Akachukua lile shati lililokuwa limeloa
kwa damu na kutoka nalo.
Muda
mfupi baadaye alirudi akiwa na fulana nyeupe, akanipa nivae huku pia akiwa na vifaa
vya kupigia deki, wakati navaa ile fulana kwa umakini ili nisijiumize tena,
yeye alikuwa akifuta damu harakaharaka pale chini ya kitanda changu, akaendelea
kufuta mpaka kule koridoni nilikokuwa nimechafua.
Yaani
hata kama ulikuwa unaumwa vipi, ukikutana na nesi wa namna hii, lazima upone,
nilijihisi kuwa na bahati ya kipekee kuhudumiwa naye. Ile fulana aliyonipa
nivae ambayo hata sikujua ameipata wapi, ilikuwa imepuliziwa manukato mazuri
yaliyofanana na yale aliyokuwa amejipulizia mwilini mwake, nikajisikia raha
fulani ndani ya moyo wangu, nikabaki sina la kusema zaidi ya kumshukuru ingawa
mwenyewe wala hakunijibu chochote.
Aliendelea
kusafisha mpaka nje, aliporudi wodini, niligundua kwamba kumbe wakati
akinisaidia kuniingiza wodini, nilimchafua gauni lake jeupe kwa damu, nikazidi
kujihisi kua na hatia kubwa. Kumbe na yeye alishagundua kwamba nimemchafua,
bila kuzungumza chochote alienda mpaka kwenye chumba cha manesi na kubadilisha
gauni, akarudi akiwa amevaa gauni jingine safi.
Kama
ilivyokuwa mwanzo, hakutabasamu wala kucheka, hata yale masihara yake
hayakuwepo tena, nikahisi nimemkwaza sana kwa nilichokifanya. Alinisogelea pale
kitandani, akanipima joto la mwili wangu kisha nikamsikia akishusha pumzi
ndefu.
Bila
kuzungumza chochote, alienda kukaa kwenye meza iliyokuwa inatazamana na mlango,
nikamuona akifunua mafaili mengi, akawa anajaza vitu ambavyo sikujua ni nini,
nilihisi ni katika kutimiza majukumu yake ya kazi. Aliendelea kuwa kimya huku
mara kwa mara akinitazama kwa kunikazia macho, nikimtazama anakwepesha macho
yake na kujifanya hakuwa ananitazama, na mimi nikawa najifanya kama simuoni.
Japokuwa
alikuwa ameamua ‘kunichunia’, moyoni nilishukuru kwa msaada alionipa kwani muda
mfupi baadaye, yale maumivu yalitoweka kabisa na zile damu nazo zikaacha
kutoka, moyoni nikajiapiza kwamba sitainuka tena kitandani mpaka kidonda
kikauke kabisa.
Nikiwa
pale kitandani, nilizama kwenye dimbwi la mawazo kuhusu mfululizo wa matukio
yale yaliyonitokea maishani mwangu mpaka wakati huo, nilikuwa na shauku kubwa
ya kupona haraka ili niende kule nilikoelekezwa na Shenaiza kwamba nitakutana na
mdogo wake atakayenipa bahasha yenye maelezo ya nilichokuwa nakitafuta.
Hata
hivyo, niliamua kujipa muda kidogo ili nipone kidogo na mwili wangu upate
nguvu, mawazo mengi yakawa yanaendelea kukizunguka kichwa changu. Niliendelea
kujiuliza maswali mengi kuhusu ule ulimwengu mwingine niliouona na maajabu
yake, pia jinsi nilivyokuwa naweza kutoka kwenye mwili wangu halisi na kukaa
pembeni kisha nikaanza kujitazama mwenyewe.
Ndani
ya kipindi kifupi tu nilikuwa nimetokewa na matukio mengi ya kutisha na
kustaajabisha ambayo hakuna ambaye angeweza kuniamini endapo ningemsimulia na
ndiyo maana mwenyewe niliamua kubaki nayo moyoni, mtu pekee ambaye nilitaka
nipate muda wa kutosha kuzungumza naye, alikuwa ni Shenaiza ambaye naye
alionesha kutokewa na hali kama na iliyokuwa nayo mimi.
“Umefahamiana
vipi na yule dada aliyelazwa kwenye wodi ya vichaa?” aliniuliza swali yule nesi
lililonizindua kutoka kwenye lindi la mawazo, nilipogeuka na kumtazama,
alionekana kuwa bize na simu yake ya kisasa, nikashusha pumzi ndefu na
kuendelea kumtazama.
“Si
naongea na wewe Jamal?” alisema, nikashtuka zaidi alipolitaja jina langu kwa
ufasaha mno, kama vile linavyotakiwa kuitwa, tofauti na watu wengi waliokuwa
wakilikosea.
“Ni
rafiki yangu tu.”
“Baba
yake unamjua?” aliniuliza swali lingine ambalo liliufanya moyo wangu ulipuke
paah! Tayari alikuwa amesimama na kunisogelea pale kitandani, ule ‘u-serious’
wake ukawa umepungua kiasi. Alionesha kama kuna jambo muhimu anataka kuniambia
kuhusu Shenaiza na baba yake ingawa sikujua ni jambo gani.
“Ha..pa...na!
Hapana!” nilijibu kwa kubabaika huku nikiwa makini kutaka kusikia ataniambia
nini.
Je,
nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment