ILIPOISHIA:
“Niangalie
vizuri namna ya kuchimba maana tukitoka hapa inabidi na wewe ukafanye majaribio
kama wenzako,” alisema baba. Muda huo ulikuwa ni kama saa sita hivi za usiku,
giza nene likiwa limetanda kila sehemu.
SASA
ENDELEA...
Huku nikitetemeka, nilianza kumtazama
vizuri baba alivyokuwa akichimba, alikuwa akifukua shina la ule mti huku
akiuzunguka, akitamka maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa. Baada ya
kuuzunguka karibu mara saba, tayari alishakuwa ameifikia mizizi, akatoa kisu na
kuanza kuichambua na kuikata mmoja baada ya mwingine.
“Hutakiwi kukata mizizi zaidi ya saba
kwenye mti mmoja, na hutakiwi kuchimba mti ambao unaonekana tayari
umeshachimbwa katika siku za hivi karibuni,” alisema baba, nikawa natingisha
kichwa kumkubalia. Baada ya kumaliza, alinikabidhi tochi, akaniambia niutazame
vizuri ule mti, nikaumulika vizuri.
“Sasa na wewe unatakiwa kutafuta mti
kama huuhuu, ipo mingi lakini lazima uwe makini kutafuta wa kuchimba dawa,”
aliniambia baba, basi nikaanza kumulika huku na kule, baba akiwa upande wa
kushoto na baba yake Rahma upande wa kulia.
Muda mfupi baadaye, kweli nilifanikiwa
kuupata lakini ulikuwa umezongwa na miiba mingi, baba akaniambia ni lazima
niitoe kwanza miiba yote ndiyo nianze kuchimba, nilifanya hivyo na baada ya
muda, nilikuwa nimepasafisha pale kwenye shina la mti huo.
Nikaanza kuchimba huku baba akinielekeza
hatua kwa hatua, akaniambia kwa kuwa ndiyo kwanza naanza hakuna umuhimu wa
kunuiza maneno kama alivyokuwa akifanya yeye bali natakiwa kuweka nia moyoni
kwamba nahitaji damu kwa ajili ya kafara.
Nilifanya hivyo, nikawa naufukua ule mti
na nilipozunguka mara ya saba, tayari mizizi ilikuwa ikionekana, baba akanipa
kisu na kuniambia kwamba natakiwa kuchagua mizizi ya katikati, yaani isiwe
mikubwa sana wala midogo sana na isizidi saba.
Nikakata wa kwanza, pale nilipokata
pakawa panatoka yale majimaji kama damu, nikakata wa pili, wa tatu mpaka saba
ilipotimia, shina lote likawa limelowa na yale majimaji ya ule mti kama damu.
“Haya fukia lakini hakikisha hiyo mizizi
hauiweki chini, ishike vizuri,” aliniambia na kunielekeza kwamba wakati wa
kufukia, natakiwa kwenda kinyume na vile nilivyokuwa nafukua, yaani kama wakati
wa kufukua nilikuwa nauzunguka mti kwa kuelekea upande wa kulia, ninapofukia
natakiwa kuanzia upande wa kushoto na hivyo ndivyo nilivyofanya.
Baada ya kumaliza, baba alisema
tunapaswa kwenda kuziosha dawa zetu mtoni na kuzitengeneza vizuri. Sikuwa
mwenyeji wa Kibaha na hata sikuwa najua kama kuna mto, nikawa kama bendera
fuata upepo.
Tulitembea tukikatiza vichaka na mapori,
hatimaye tukatokezea mahali palipokuwa na kama chemchemi hivi, pembeni kukiwa
na bustani za mbogamboga nyingi, baba akatangulia mpaka pale kwenye chemchemi,
kabla ya yote, alitoa kisu chake na kukata jani kubwa la mgomba, akalikata
vipande vitatu, kimoja akanipa, kingine akampa baba Rahma na kingine akabaki
nacho yeye.
Alitoa ile mizizi aliyoichimba,
akaniambia nimtazame kwa makini anachokifanya, ilikuwa imebadilika rangi na
kuwa nyekundu kama damu, akaanza kuiosha ikiwa juu ya jani la mgomba, akafanya
hivyo kwa dakika kadhaa mpaka ilipobadilika rangi na kurejea kwenye rangi yake
halisi ambayo ni kama kahawia fulani hivi.
Ilifika zamu yangu, na mimi nikafanya
vilevile, nikaitoa mfukoni na kuiosha vizuri, kisha ikafika zamu ya baba yake
Rahma ambapo baba alimtolea na kumpa mizizi yake, akaiosha kwa uzoefu wa hali
ya juu kisha tukaondoka eneo hilo.
Hapakuwa mbali sana na barabara kwani
hata kelele za magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi kubwa tuliweza kuzisikia.
Kadiri tulivyokuwa tukisonga mbele ndivyo hofu ilivyozidi kutanda kwenye moyo
wangu.
Tulikatiza vichaka, mapori na mashamba
ya watu na hatimaye tukawa tumetokezea barabara ya lami. Sikujua eneo lile
linaitwaje lakini kwa mzunguko tulioupiga, kuanzia pale tuliposhuka kwenye
gari, tulivyoelekea njia ya Tumbi na baadaye kuingia porini kisha kurudi
barabarani, nilijua kwamba si mbali sana na pale tuliposhukia.
“Mtu yeyote akikusemesha hutakiwi kujibu
chochote, eneo hili lina watu kutoka jamii mbalimbali ambao huwa wanapenda
kupimana nguvu, umenielewa?” baba aliniambia, nikatingisha kichwa kuonesha
kumkubalia.
“Leo ni zamu yako, kwa hiyo inatakiwa
unisikilize kwa makini,” baba aliniambia, akasema kati ya ile mizizi saba,
mmoja natakiwa kwenda kuufunga kwenye mti au jani lolote upande wa pili wa
barabara, mwingine natakiwa kuuweka katikati ya barabara, mwingine natakiwa
kuufunga upande ule tuliokuwepo, mmoja natakiwa kuutafuna na kuumeza na miwili
natakiwa kubaki nayo mwilini, mmoja niweke kwenye mfuko wa kushoto wa suruali
na mwingine niubane kwenye kwapa langu la kushoto kama kipima joto.
Yalikuwa ni maelezo marefu lakini
nilijitahidi kuwa mwelewa maana nilikuwa na shauku kubwa ya kuona nini
kitatokea. Kweli baada ya hali kutulia, kwa maana kukiwa hakuna gari kutoka upande
wowote, nilivuka barabara kinyumenyume mpaka upande wa pili.
Kwa kutumia uzi mweusi alionipa baba,
niliufunga ule mzizi kwenye tawi moja la mti mdogo uliokuwa pale pembeni ya
barabara, nikarudi tena kinyumenyume mpaka katikati ya barabara na kukaa chini
kabisa, nikaweka ule mzizi kisha nikajiburuza kwa makalio kinyumenyume mpaka
pale baba na baba yake Rahma walipokuwa wamesimama.
Nikasimama na kusogea kwenye kimti
kingine kidogo kilichokuwa kando ya barabara, usawa wa kile nilichokifunga,
nikaenda kufunga ule mzizi kwa kutumia ule uzi kisha kinawasogelea akina baba
ambao walikuwa wakinitazama kwa makini kuhakikisha sikosei hatua hata moja.
“Safi sana,” alisema baba kisha akaanza
kuniuliza kama mpaka hapo nimeshaelewa ni gari linalotokea upande gani ndiyo
litapata ajali. Sikuwa naelewa chochote. Akaniambia kwa sababu nimesota kwa
makalio kutokea katikati ya barabara kuelekea upande wa kushoto wa Barabara ya
Morogoro, gari litakalopata ajali litakuwa ni linalotoka Dar es Salaam kuelekea
upande wa Morogoro.
Sikuelewa anamaanisha nini, ikabidi
nitulie kuona nini kinachoenda kutokea. Tulisogea pembeni kabisa, umbali wa
kama mita mia moja hivi, vichakani kabisa, tukakaa kwa kukunja miguu na
kutengeneza duara. Kulikuwa na mbu wengi lakini wote walikuwa wakiishia
kutuzunguka tu, hata sijui kwa nini hawakuwa wakituuma.
“Nataka ufumbe macho halafu utulie huku
ukitafuna huo mzizi mmoja, nitakachokuuliza unijibu,” baba aliniambia,
nikafanya kama alivyoniambia. Cha ajabu, nilipofumba macho tu, japokuwa
tulikuwa mbali kidogo na barabara, niliweza kusikia sauti za magari na pikipiki
vikipita kwa kasi, cha kushangaza zaidi, niliweza kusikia hata sauti za
madereva na abiria, nikashtuka sana.
Nikiwa nimeendelea kutulia, japokuwa
nilikuwa nimefumba macho, kadiri nilivyokuwa nikizidi kutafuna ule mzizi ndivyo
nilivyoanza kuona taswira ya kila kilichokuwa kikiendelea barabarani utafikiri
nilikuwa nimesimama pembeni ya barabara, tena nikiwa nimefumbua macho.
“Unaona magari mangapi?”
“Mengi tu.”
“Yanayoelekea upande wa Morogoro ni
mangapi?”
“Ni matatu.”
“Ambalo lipo nyuma kabisa lina abiria
wangapi?”
“Abiria mmoja ambaye ni mtoto na dereva
mwanamke.”
“Safi, hiyo ndiyo kazi yako ya leo,
likazie macho hilo gari kwa nguvu na likikaribia hapo ulipo fumbua macho ghafla
halafu tena hicho kilichopo mdomoni mwako,” alisema baba, kweli nikawa
nalitazama gari hilo.
Lilikuwa ni gari dogo na ndani yake
kulikuwa na watu wawili tu, dereva mwanamke na mtoto, ilionesha ni kama ni
wanafamilia wanarudi makwao. Sikuelewa nini kitawapata lakini kwa sababu ya
shauku niliyokuwa nayo, nilijikuta nikifanya kile baba alichoniambia,
nikafumbua macho ghafla na kutema mabaki ya ule mzizi, nikashtukia nimemtemea
baba usoni.
Mara kikasikika kishindo kikubwa kule
barabarani, kilichonishtua mno. Sikuelewa nini kimetokea pale kwa sababu
nilipokuwa nimefumbamacho, nilikuwa najiona kabisa kwamba nipo barabarani
lakini nilipofumbua tu, nilijikuta nikiwa nimekaa palepale tulipokuwa tumekaa
na baba na baba yake Rahma.
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati
nataka kufumbua machom nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani,
akikunya usukani gahfla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka
kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto
kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,”
alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment