ILIPOISHIA:
“Naam baba,” niliitikia huku nikijaribu
kumtoa Rahma maana alikuwa amenishika kimahaba, baba akaja mbiombio na
kunishika mkono, akamwambia Rahma kuna kazi hatujamaliza kwa hiyo anisubiri,
alinishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea nje lakini tulipofika kwenye kingo
za mlango tu, jambo la ajabu lilitokea.
SASA ENDELEA...
Kishindo kikubwa kilisikika, nikamuona
baba akianza kuyumbayumba kama amelewa, na mimi nikaanza kusikia kizunguzungu
kikali huku damu zikianza kututoka wote, mdomoni na puani. Muda huo tulikuwa
tumeshavuka kizingiti cha mlango.
Sijui nilipata wapi ujasiri kwani ni
muda huo ndipo nilipogundua kwamba kuna kosa nilikuwa nimelifanya, Isri
aliniambia kwamba nisitoke nje mpaka giza litakapoingia, jambo ambalo
nililikiuka kwa hiyo ili kurekebisha makosa, nilimvuta baba kwa nguvu, wote
tukaangukia upande wa ndani wa mlango.
Kilisikika kishindo kingine kisha baba
akawa ni kama amezinduka kutoka kwenye usingizi mzito.
“Nini kimetokea?” baba aliniuliza huku
na yeye akiwa ni kama amepigwa na butwaa, akainua shingo na kutazama huku na
kule, nikamuona akishtuka zaidi baada ya kuona damu zinamtoka mdomoni na puani
pale chini.
“Hata mimi sijui,” nilimjibu huku
nikisimama, na yeye akasimama kisha akawa anajifuta damu huku akitazama vizuri
pale mlangoni. Aliangalia kwa sekunde kadhaa kisha akanigeukia na kunitolea
macho ya ukali.
“Umeweka nini hapa?” aliniuliza kwa
ukali.
“Una uhakika?” aliniuliza huku
akinisogelea mwilini. Miongoni mwa sifa za baba, huwa hapendi kabisa mtu
muongo, ni bora akikuuliza unyamaze kuliko kutoa majibu ya uongo. Ili kuepusha
shari, nilinyamaza na kujiinamia.
“Si naongea na wewe?”
“Wakati naingia nilipakaza damu hapo
kwenye mlango,” nilisema, akaonesha kushtuka mno, hakusema kitu zaidi ya
kunishika mkono, akawa ananivutia ndani huku akiendelea kujifuta damu.
Tulienda mpaka kwenye kile chumba
changu, tukaingia huku baba akiwa makini kuhakikisha hakuna mtu yeyote
anayetutazama. Wakati naingia, nilitupia macho kwenye mlango wa chumba cha
Rahma, nikamuona akiwa anatuchungulia. Nilimuonesha ishara kwamba anisubiri,
akatingisha kichwa kuniitikia.
“Mimi ni nani kwako?”
“Ni baba yangu.”
“Haya nataka unieleze kila kitu,
umetokaje mahabusu na nini kimetokea mpaka ukapaka damu kwenye mlango,” alisema
baba kwa sauti ya chini, lakini akionesha kutokuwa na hasira na mimi.
Kabla sijamjibu, niliingiza mkono
mfukoni na kutoa ile dawa ya ajabu ambayo kwa kiasi kikubwa ilinisaidia sana.
“Hiyo ni mimi nilikuwekea muda ule
wakati polisi wanakuchukua, naamini imekusaidia sana,” alisema baba huku
akiichukua ile dawa mikononi mwangu na kuiweka kwenye mfuko wa shati. Ni hapo
ndipo nilipoanza kupata picha juu ya nini kilichotokea.
“Sasa baba, unataka nikueleze nini
wakati kumbe unajua kila kitu na wewe ndiye uliyenielekeza jinsi ya kutoka
mahabusu?”
“Unachokisema ni sawa lakini najua kuna
mambo mengi yametokea ukiachilia mbali wewe kutoka mahabusu na ndiyo maana
nimekutoboa mkono wako na kukinga damu yako, mimi ni baba yako na hakuna mtu
mwenye uchungu na wewe kuliko sisi wazazi wako, ni lazima ujifunze kuniamini na
kuwa muwazi kwangu,” alisema.
Kiukweli sikuwahi kumsikia baba
akizungumza kwa busara na mimi kiasi hicho, yaani ni kama alikuwa akizungumza
na mkubwa mwenzake na hata ule ukali wake wa siku zote, hakuuonesha kabisa.
Nilishusha pumzi na kukaa vizuri,
sikuona sababu ya kuendelea kumficha, nilianza kumueleza kila kitu
kilichotokea, kuanzia nilipofikishwa kituoni, wale wachawi waliokuja usiku kule
mahabusu na jinsi yule mwingine alivyobadilika sura na kufanana na mimi.
Nilipofikia kipengele hicho, baba
alinikatisha, akaniambia kwamba dawa aliyokuwa amenipa, ina nguvu kubwa ya
kufanya chochote ninachokitaka. Akaniambia kwamba yule mchawi aliyebadilika
sura, alishindwa kutoka mpaka asubuhi na askari walipoingia kwa ajili ya
kufanya ukaguzi.
“Nasikia wameshtuka sana kumuona,
wakadhani ni wewe lakini tofauti ikawa ni kwamba sura mmefanana lakini yeye ni
mzee na amekutwa hana nguo hata moja, mtaani kote ndiyo gumzo na hata vyombo
vya habari vimeanza kuripoti tukio hilo la ajabu,” alisema baba.
Kauli yake ilinifanya niwe na shauku
kubwa ya kutaka kujua nini kimeendelea, akaniambia nisiwe na wasiwasi
atanieleza lakini pia akaniambia kwamba anataka kumtumia yule mchawi kama funzo
kwa watu wengine wenye tabia ya kufanya uchawi wa kijinga.
Aliposema uchawi wa kijinga, sikumuelewa
anamaanisha nini, nikataka kumuuliza tena lakini aliniambia niendelee kumueleza
kilichotokea. Nilimueleza kila kitu na jinsi nilivyokutana na yule msichana
usiku ule.
“Lakini si nilishakukataza kuwa karibu
na Isri?” alisema huku akinitazama usoni, nilishtuka kumsikia baba akimtaja
jina. Kwa ilivyoonesha, kumbe baba alikuwa akimfahamu vizuri msichana huyo na
hata aliponikataza kuwa naye karibu, alikuwa na maana yake.
“Huyo si ndiye aliyekusababishia
matatizo mpaka ukakamatwa kwa tuhuma za mauaji? Ina maana wewe hukushtuka mtu
amekufia mchana gesti halafu usiku unakutana naye tena? Akili zako zinafanya
kazi sawasawa kweli?” baba alinibadilikia, nikawa nataka kujitetea lakini
alinikatisha na kuniambia anaelewa kila kitu kilichotokea kati yetu.
“Hebu hiyo mikono yako,” alisema,
nikasita kidogo lakini baadaye nilimpa, akaishika na kuanza kuitazama upande wa
mbele kisha akanitazama usoni.
“Na wewe umeshakuwa kama yeye,” alisema
huku akiniachia, akaniambia nifumbue mdomo wangu. Nilifanya hivyo, akawa
anayatazama meno yangu kwa makini. Bado nilikuwa na maswali mengi kuliko majibu
na ilionesha kwamba baba anamfahamu vizuri sana Isri.
Kitendo cha kutazama mikono yangu kisha
wakati huohuo akaanza kukagua meno yangu, kilitosha kunifanya nielewe kwamba
kumbe anajua jinsi msichana huyo alivyonigeuza na kuwa kiumbe wa ajabu.
“Umewapa ushindi maadui zangu kwa sababu
ya mambo yako ya kipumbavu,” alisema baba huku akiinuka, bado damu zilikuwa
zikimtoka puani ingawa safari hii haikuwa kwa wingi kama ilivyokuwa mwanzo.
Alipotaka kutoka, nilimuita, akageuka na
kunitazama, nikamwambia Isri ameniambia nisitoke nje mpaka giza litakapoingia,
akanijibu kwa kifupi kwamba anajua kisha akaondoka zake.
Harakaharaka niliinuka na kukimbilia
bafuni kwani nilikuwa najisikia aibu kukutana na Rahma nikiwa na harufu mbaya
kiasi kile, nikajifungia na kufungulia maji kwa wingi, nilivua nguo zangu kisha
nikaanza kujimwagia maji huku nikijikagua kama hakukuwa na kitu chochote
kisicho cha kawaida mwilini mwangu.
Mara nilisikia mlango wa bafu ukigongwa,
nikahisi ni Rahma amenifuata, harakaharaka nikaufungua, nikakutana uso kwa uso
na baba.
“Ogea hii,” alisema huku akinipa ile
dawa ambayo aliwahi kunipa niogee, ambayo ukiogea mwili unatoa uchafu mweusi
kama mkaa. Nilimshukuru na kufunga mlango, nikaendelea kuoga. Maji machafu,
meusi tii yalianza kunitoka, safari hii nikawa sina wasiwasi maana nilikuwa
naelewa kinachotokea.
Nilioga mpaka uchafu wote ukaniisha
mwilini, nikachukua nguo zangu na kuzikung’uta sana kisha nikavaa na kutoka.
Rahma alikuwa amesimama kwenye mlango wa chumba chake, akionesha kunisubiri kwa
shauku kubwa.
Hakuwa amevaa chochote zaidi ya
kujifunga upande wa khanga nyepesi, akawa ananitazama usoni kwa macho yake
mazuri, ambayo yalikuwa ni kama yana usingizi kwa jinsi yalivyolegea.
Nilitazama huku na kule, nilipoona
hakuna mtu anayetutazama, nilimsogelea, akanikumbatia kwa mahaba kisha
akanivutia ndani. Hatukukumbuka hata kufunga mlango, kwa makusudi aliuachia ule
upande wa khanga, ukadondoka chini, nikawa kama fisi aliyeona mfupa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment