Monday, September 11, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 42


ILIPOISHIA:
Kwa akili yangu nilijua kwamba tayari kazi imekwisha, kumbe kulikuwa na kazi nyingine, nikaanza kutetemeka tena huku nikigeuka huku na kule kuwatazama wale watu ambao wote walikuwa na nyuso za furaha. Nilipogeuka upande wa kushoto, nilimuona mtu aliyenifanya nishtuke mno, nilifikicha macho nikiwa ni kama siamini.
SASA ENDELEA...
Alikuwa na Isrina, naye akiwa amevaa kama wale watu wengine wote waliokuwepo eneo lile. Alikuwa ametulia akinitazama kwa makini, ilionesha kwamba kumbe naye muda wote wakati yale mambo yakiendelea alikuwepo na alikuwa akinifuatilia hatua kwa hatua.
Nilishtuka kupita kiasi, nikageuka na kumtazama baba, naye akanitazama huku akitingisha kichwa kama ishara ya kuniambia ninachokiona ni kweli. Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini mara kwa mara baba alikuwa akinikanya kuwa karibu na msichana huyo huku akiniuliza mara kwa mara kama najua ana malengo gani na mimi.
Nilijikuta kama kichwa kikiwa kizito, kwa tafsiri nyepesi, Isrina au Isri kama mwenyewe alivyokuwa akipenda kuitwa, alikuwa akifahamiana vizuri na baba kwa sababu wote walikuwa jamii moja. Bado sikutaka kuamini kama Isrina naye anahusika na hayo mambo, nilijaribu kuvuta kumbukumbu ya siku niliyokutana naye kwa mara ya kwanza.
Bado sikuwa na majibu ilikuwaje mpaka tukapanda basi moja, ilivyoonesha ni kama kukutana kwetu hakukuwa bahati mbaya bali ni jambo ambalo lilipangwa. Sasa kama anafahamiana na baba, kwa nini hataki kabisa niwe karibu naye? Kwa nini anamchukia? Nilijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.

Nikiwa bado naendelea kujiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, yule babu ambaye baba aliniambia anaitwa Mkuu, alinishika mkono baada ya kuona nimepigwa na butwaa. Licha ya uzee wake na mwili wake kuchoka, Mkuu alikuwa na nguvu kwelikweli, akanivutia kwake na kuanza kutembea na mimi kuelekea pale katikati nilipokuwa nimelazwa kwa mara ya kwanza.
Mara nilishtuka kuona wanaume wanne, wakitoka kule pembeni na kusogea mpaka pale tulipokuwa, wakiwa wamebeba jeneza. Sikuelewa lile jeneza ni la nini lakini kwa jinsi walivyolibeba, ilionesha kama lipo tupu.
Walilisogeza mpaka pale jirani na kuliweka chini, wakasimama wakiwa ni kama wanasubiri maagizo kutoka kwa Mkuu huku wote wakinitazama. Niligeuka na kumtazama baba, akawa ni kama ananipa ishara kwamba nisiogope, nikageuka na kumtazama Isri, bado alikuwa amenikazia macho muda wote, nikashusha pumzi ndefu na kumgeukia Mkuu.
Alitoa kichupa kutoka kwenye mkoba wake wa ngozi aliokuwa ameuvaa kiunoni, akakitingisha kisha akakifungua na kunipa ishara kwamba ninuse kilichokuwemo ndani. Nilipofanya hivyo tu, nilianza kupiga chafya mfululizo kutokana na ukali wa ile dawa iliyokuwa mle ndani ya kichupa.
Nikapiga chafya zisizo na idadi, mara nikaanza kuhisi kizunguzungu kikali, nikawa napepesuka, wale wanaume wakanishika ili nisianguke, Mkuu akanisogelea pale nilipokuwa nimeshikwa, akaninusisha tena na safari hii, hakukitoa haraka kile kichupa puani, nikaendelea kupiga chafya nyingi, mwisho giza nene likatanda kwenye uso wangu na mwili wote ukawa ni kama umekufa ganzi.
Licha ya hali hiyo, bado nilikuwa naweza kuelewa kinachoendelea ingawa sikuwa na uwezo wa kufanya chochote, nikasikia wakinilaza chini kisha lile jeneza likagongwagongwa na kitu kizito, nadhani walikuwa wakilifungua.
Nikiwa bado sielewi hatma yangu, nilishtukia wakininyanyua na kunilaza ndani ya jeneza. Sikuwa hata na uwezo wa kufumbua macho ingawa bado nilikuwa na fahamu zangu. Baada ya hapo, nilisikia tena jeneza likigongwagongwa juu yangu, nikajua mimi ndiyo nimewekwa kwenye jeneza.
Mara nilisikia tena lile pembe la ng’ombe likipulizwa kisha Mkuu akapaza sauti na kutamka haraka maneno ambayo sikuyaelewa, wale watu wengine wakaanza kuimba nyimbo kama za maombolezo, nikahisi lile jeneza nililowekwa ndani yake likinyanyuliwa na waliolibeba wakaanza kutembea.
Ilikuwa ni kama nipo kwenye ndoto lakini tofauti yake ni kwamba nilikuwa najielewa. Wale watu waliendelea kuimba huku nao wakionesha kuwafuata wale walionibeba kwenye jeneza. Wakatembea umbali fulani kisha nikahisi jeneza likishushwa chini huku wale watu wakiendelea kuimba.
Nikiwa sielewi nini hatima yangu, nilihisi kama jeneza linahamishwa tena na safari hii, lilikuwa kama linaingizwa kwenye shimo, mara nikashtukia vitu vizito vikianza kuangushiwa juu ya jeneza.
Kwa jinsi vilivyokuwa vikidondoka kwa vishindo, nilielewa moja kwa moja kwamba ulikuwa ni udongo, nikajiuliza ina maana wamenipeleka makaburini? Ina maana wananizika nikiwa hai? Sikupata majibu.
Vile vishindo viliendelea na muda mfupi baadaye, zile sauti za watu waliokuwa wakiimba nazo zilianza kufifia na baadaye zikatoweka kabisa, ukimya mkubwa ukiwa umetanda kila sehemu. Sikuelewa tena kilichoendelea kwani hata zile fahamu zangu, sasa zilinitoka kabisa.
Nilipokuja kushtuka, ilikuwa tayari kumepambazuka na licha ya yote yaliyotokea, nilijikuta nikiwa kwenye chumba changu, nikiwa nimelala kitandani, mwili wangu ukiwa hauna nguvu kabisa.
“Vipi unajisikiaje?” sauti ya baba ilinishtua, nikageuza shingo na kumtazama, alikuwa amekaa pembeni yangu, mkononi akiwa na bakuli la uji. Hata nguvu za kumjibu sikuwa nazo, pembeni pia alikuwepo baba yake Rahma ambaye uso wake ulikuwa na furaha.
Walisaidiana kuniinua kidogo upande wa shingoni, wakaniwekea mto na baba akaanza kuninywesha ule uji.
“Jitahidi kunywa ili upate nguvu,” alisema baba, nikajilazimisha hivyohivyo, kweli nikamaliza lile bakuli maana ni kweli tumbo nalo lilikuwa tupu kabisa.
“Inabidi uendelee kupumzika, leo hutakiwi kufanya shughuli yoyote mpaka utakapopewa maagizo na Mkuu,” aliniambia baba, nikatingisha kichwa kuashiria kukubaliana na alichokisema ingawa sikuelewa huyo Mkuu atanipaje hayo maagizo. Yaani nilivyokuwa nikijisikia, ni kama mtu aliyeumwa kwa kipindi kirefu sana na kusababisha mwili uishiwe nguvu kabisa kiasi cha kushindwa hata kujigeuza pale kitandani.
Waliinuka na kutoka, mimi nikapitiwa tena na usingizi mzito. Nikiwa usingizini, nilianza kuota ndoto ya kutisha, nilijiona nipo kulekule porini lakini tofauti na mara ya kwanza, safari hii tulikuwa tumebaki wawili tu, mimi na Mkuu. Akawa ananiambia ili nguvu zangu nilizopewa zianze kufanya kazi, ni lazima nitoe kafara na kafara hilo ndiyo utakuwa mtihani wangu wa kwanza.
Aliniambia kwamba wachawi wote, sifa ya kwanza ni lazima wawe na uwezo kuua na kwamba kadiri mtu anavyoua watu wengi zaidi ndivyo anavyopanda ngazi. Alisema maneno hayo kwa msisitizo kisha baada ya kumaliza, alicheka kicheko cha nguvu kilichokuwa kinasikika kama mwangwi kisha akayeyuka.
Kwa jinsi ndoto ile ilivyokuwa inatisha nilijikuta nikishtuka, kutazama nje bado ilikuwa mchana, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida. Kumbe pale wakati nashtuka, nilipiga kelele zilizomfanya baba na baba yake Rahma waje haraka kule chumbani kwangu.
Cha ajabu, nilipowahadithia nilichoota, hakuna aliyeonesha kushtuka, sanasana baba akapigilia msumari kwa kusema kwamba ile haikuwa ndoto bali ni Mkuu alikuwa akiwasiliana na mimi.
“Baba!” nilisema kwa mshtuko nikiwa bado palepale kitandani.
“Nini sasa.”
“Mimi niue mtu?” nilipotamka maneno hayo, baba alinionesha ishara kwamba nisipige kelele, wote wakanisogelea pale kitandani na kuniambia kwa sauti ya chini kwamba Mkuu akishatoa maagizo kwa mtu, kinachofuatia huwa ni utekelezaji tu na endapo mtu akishindwa kutekeleza alichoambiwa, anakufa yeye. Nilishtuka mno, nikamtazama baba, nikamtazama baba yake Rahma, wote walionesha kumaanisha kile walichokisema.
“Hapana! Hapanaaa,” nilisema kwa sauti ya juu, ikabidi baba anizibe mdomo maana alihisi naweza kuropoka mambo mengine na kuwafanya wasiohusika wajue.
“Huna haja ya kuogopa, zipo njia za kutimiza hicho ulichoambiwa bila kuonekana kama wewe ndiyo umefanya moja kwa moja, mbona sisi huwa tunafanya sana tu” alisema baba, macho yakanitoka.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa kwenye Gazeti la Ijumaa.


No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...