ILIPOISHIA:
Ghafla akiwa anakuja mbio, lile gari
lilitokeza tena na kuja kwa kasi pale lilipokuwa limepaki awali, nikashtuka
kugundua kuwa kumbe wale watu hawakuwa wameondoka, nikajua lazima watashtukia
mahali nilipo kutokana na jinsi Raya alivyokuwa anakuja kwa kasi.
SASA ENDELEA...
“Naomba unisaidie kitu, huyu dada
akifika hapa kuniulizia mwambie nimeshashuka kwenye gari nimeelekea upande wa
wodi za wanaume, nikishuka funga huu mlango haraka,” nilimwambia dereva teksi
ambaye alibaki ameduwaa, akiwa haelewi kinachoendelea.
Harakaharaka nikafungua mlango wa upande
wa pili, nikashuka kwa kasi na kubingirika mpaka chini ya ile teksi, nikatulia
huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio kuliko kawaida. Nilimuona Raya
akikimbia mpaka pale kwenye ile teksi, nikajikausha kimya.
“Kaka samahani, nimeelekezwa kuwa
mgonjwa wangu yupo ndani ya hili gari, yuko wapi?” nilimsikia Raya akimuuliza
yule dereva teksi huku akihema.
“Alikuwepo lakini ameshuka ameelekea
kule kwenye wodi za wanaume,” yule dereva teksi alijibu kama nilivyomuelekeza.
Nikasikia Raya akiguna akiwa ni kama haamini, mara nikaliona lile gari limekuja
na kupaki palepale lilipokuwa limepaki mara ya kwanza, nikaiona miguu ya watu
wakishuka na kusogea pale Raya alipokuwa amesimama akizungumza na dereva teksi.
Yaani kama mtu angepata wazo la
kuchungulia chini ya ile teksi, basi huenda siku hiyo ndiyo ingekuwa mwisho
wangu.
“Habari yako kaka,” nilimsikia mmoja
kati ya wale wanaume walioshuka kwenye lile gari, Isuzu Bighorn.
“Safi!”
“Kuna mtu tunamtafuta, tunahisi yupo
ndani ya hili gari lako,” alisema mwingine kwa sauti nzito, bila kusubiri
kujibiwa, nikawasikia wakifungua milango ya teksi hiyo, yule dereva na Raya
wakawa wanashangaa.
“Kwani nyie ni akina nani?” nilimsikia
Raya akiwauliza lakini hakuna aliyemjibu, nikasikia wakibamiza milango ya teksi
hiyo kwa nguvu, nadhani ni baada ya kufungua na kunikosa.
Nikawaona wakiondoka kwenye teksi hiyo
bila kusema kitu, wakaelekea kwenye gari lao, wakapanda kisha nikaona gari
likirudi nyuma na kuondoka tena.
“Kwani wale ni akina nani? Mbona
wamekuja kisharishari namna hiyo?” nilimsikia Raya akimuuliza yule dereva teksi
lakini hakuwa na majibu. Baada ya kuhakikisha wameshaondoka na gari lao,
nilibingirika na kutoka uvunguni mwa gari.
Kwa bahati nzuri, pale kwenye maegesho
ya magari palikuwa na lami kwa hiyo sikuchafuka sana, Raya akapigwa na butwaa
kuniona nikitoka uvunguni mwa gari.
“Jamal! Ooh maskini pole mpenzi wangu,
wale ni akina nani wanaokusaka kama jambazi?” alisema Raya huku akinisogelea na
kunikumbatia huku akinimwagia mvua ya mabusu.
“Na muda wote huo ulikuwa umeenda wapi?
Mbona nimekuja muda mrefu tu kukuletea chakula lakini haukuwepo?” Raya alizidi
kunihoji, nikamwambia atulie kwanza nitamueleza kila kitu vizuri.
Yule dereva teksi akawa ananitazama kwa
macho yaliyoonesha kuwa na maswali mengi yasiyo na majibu.
“Yule daktari alikuwa anasemaje kule
wodini?” nilimuuliza Raya kimitego, akanijibu kwamba alikuwa akiniulizia kwa
madai kwamba kuna kipimo inatakiwa nikafanyiwe nje ya hospitali, akawa
anashangaa kwa nini sikuwepo wodini.
“Kwani wewe ulikuwa wapi mpaka madaktari
wanakutafuta?” Raya aliniuliza tena, nikaendelea kumjibu vilevile kwamba
atulie, nitamueleza kila kitu baadaye.
“Basi twende ukale nimekuletea chakula
unachokipendaga,” alisema Raya, nikamjibu kwamba hospitalini hapo hapakuwa
sehemu salama tena kwangu. Sikutaka kumuudhi Raya lakini pia sikutaka afahamu
kwamba nilikuwa nimetoka nyumbani kwa Shamila na tayari mimi na yeye
tulishaanzisha uhusiano wa kimapenzi.
“Naomba hicho chakula kaniletee kwenye
gari, nichukulie na vitu vyangu mle wodini,” nilimwambia, akaondoka
harakaharaka huku akigeuka huku na kule.
“Kaka kwani nini kinaendelea? Mbona
sielewielewi?” alisema yule dereva teksi, naye nikamjibu tu kwa kifupi kwamba
mambo yalikuwa magumu.
“Hawa jamaa mbona wamekuja kibabe sana
halafu yule mmoja anaonekana kama ana mashine kwenye koti?” alisema yule
dereva, nikashtuka sana kusikia kwamba kumbe mmoja kati yao alikuwa na bunduki,
nikahisi maisha yangu yako hatarini zaidi.
“Au wanakudai?” yule dereva teksi
alizidi kunihoji lakini bado sikumpa ushirikiano aliokuwa anautaka.
Akili yangu ilikuwa ikiwaza mambo
tofauti kabisa, kwanza ilikuwa ni lazima nijue kuhusu biashara aliyokuwa
akiifanya baba yake Shenaiza lakini pia ilitakiwa niwe makini kulinda maisha
yangu kwani kwa ilivyoonesha, tayari walikuwa wameshtukia kwamba nawafuatilia.
Muda mfupi baadaye, Raya alirudi akiwa
ameongozana na Shamila, wote wakaingia kwenye ile teksi, Raya akakaa pembeni
yangu na Shamila akakaa siti ya pembeni ya dereva.
“Nimepata wazo, unajua hapa kuna wodi za
‘private’ ambazo zinalindwa, unaonaje tukikuhamishia huko maana hali
imeshachafuka,” alisema Shamila, wazo ambalo kwa kiasi fulani niliona kama ni
la msingi.
“Kwani huyu ni nani?” Raya aliuliza
baada ya kumsikia Shamila.
“Huyu ndiyo nesi anayesimamia matibabu
yangu lakini ameguswa na matatizo yangu na ndiyo maana ameamua kunisaidia kwa
karibu. Shamila, kutana na Raya, mchumba wangu,” nilisema kwa kujiamini,
nikamuona Shamila akitoa tabasamu la uongo.
Dereva teksi kwa kuwa alikuwa anajua
mchezo unavyoenda, alijifanya yuko bize kurekebisharekebisha vitu pale kwenye
‘dashboard’ ya gari lake.
“Nimefurahi kukufahamu,” Raya alijibu
kwa kifupi, Shamila akanyoosha mkono na kumpa, wakashikana kwa sekunde chache
na kuachiana. Ilikuwa ni lazima nifanye vile na kusimama kama mwanaume kwani
nilishaanza kumuona Raya akikosa raha.
“Unalionaje wazo alilolitoa nesi?”
nilimuuliza Raya, naye akaliunga mkono.
“Basi tufanye hivyo haraka, wanaweza
kurudi tena,” nilisema, wote tukashuka kwenye teksi harakaharaka na kuanza
kumfuata Shamila ambaye ndiye aliyekuwa akituongoza.
“Usitembee haraka hivyo, utajiumiza tena
kidonda,” alisema Raya huku akitaka kunipokea laptop niliyokuwa
nimeing’ang’ania lakini nikamkatalia. Muda mfupi baadaye tayari tulikuwa kwenye
lifti, tukapanda mpaka ghorofani kulikokuwa na wodi za private.
Mazxingira ya wodi hizo yalikuwa mazuri
kwa sababu kwanza kulikuwa na walinzi wenye silaha koridoni, halafu milango ya
wodi ilikuwa imara, kidogo nikawa na amani moyoni mwangu. Tulipoingia tu
wodini, harakaharaka niliiwasha ile laptop na kuanza kuyaangalia yale mafaili
machache niliyokopi kutoka kwenye ile ‘hard disk’.
“Hivyo ni vitu gani unavyoviangangalia
kwenye hiyo laptop?” Raya aliniuliza wakati akiandaa chakula huku Shamila naye
akiwa bize kuwekaweka vitu vyote vizuri ndani ya wodi hiyo, nikamdanganya Raya
kwamba kuna kazi nilikuwa nimetumiwa kutoka kazini.
“Mh! Kutoka kazini? Nani anayeweza
kukupa kazi wakati watu wote wanajua kwamba unaumwa? Isitoshe asubuhi nilipitia
kule kazini na kila mtu akawa anakupa pole,” Raya alizidi kunibana, nikamwambia
nitamfafanulia baadaye.
Niliendelea ‘kuperuzi’ yake mafaili,
moja baada ya jingine. Kama nilivyokuwa nimeona awali, yalikuwa yamejaa taarifa
za watu mbalimbali, wakubwa kwa wadogo, yakiwa na taarifa kuhusu hali zao za
kiafya na viungo mbalimbali kwenye mwili, bado nikawa sielewi.
Niliendelea kuchimba kwa undani,
taratibu nikaanza kugundua mambo ambayo ama kwa hakika yalinishangaza sana. Kwa
jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na mtandao mpana sana wa watu kutoka hapa nyumbani
Tanzania, India, Marekani, Uingereza na nchi za kiarabu ambao ulikuwa
ukihusisha hospitali kubwakubwa duniani.
Nilipoendelea kufuatilia kwenye mafaili
yake, nikaanza kugundua kwamba kumbe kulikuwa na biashara ya viungo vya
binadamu ilikuwa ikifanyika katika nchi mbalimbali, kwamba baba yake Shenaiza
alikuwa akiwakusanya watu kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na kuwasafirisha kwenda
kwenye hospitali kubwakubwa duniani kwa ajili ya kuchangia viungo mbalimbali
vya miili yao.
Kilichonishangaza sana ni kugundua kuwa
wengi walikuwa wakisafirishwa kutoka Tanzania, wakiwa hawajui chochote
kinachoenda kuwatokea. Mbaya zaidi, kulikuwa na watu ambao wameandikwa kwamba
wanaenda kuchangia moyo, ninavyofahamu mimi binadamu anakuwa na moyo mmoja tu,
kwa hiyo akichangia inakuwaje?
Nikajiuliza pia kwamba kuna baadhi ya
watu ilionesha kwamba wanaenda kuchangia ubongo, sasa ukichangia ubongo na wewe
nini kinakutokea? Unawezaje kubaki ukiwa hai? Kengele ya hatari ikalia ndani ya
kichwa changu, nikawa nahisi pengine nipo ndotoni.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment