ILIPOISHIA:
“Mara
ya mwisho mlizungumza naye lini?”
“Kiukweli
tangu aondoke hatujawahi kuzungumza naye, wanasema hospitalini hawaruhusu
kutumia simu,” alijibu mwanaume huyo, nikashusha pumzi ndefu.
SASA
ENDELEA...
Majibu ya watu hao wawili tu yalitosha kunifanya
nielewe kilichokuwa kinaendelea lakini ili kupata ushahidi mkubwa zaidi,
niliendelea kuwapigia simu wengine. Wachache hawakuwa wakipatikana hewani
lakini karibu watu 16 wote walikuwa wakipatikana na majibu yao hayakuwa
yakitofautiana.
Wapo waliosema kwamba ndugu zao
walichukuliwa kwenda kusoma nje ya nchi kwa msaada wa shirika hilo, wengine
wakasema walipelekwa kwa matibabu lakini asilimia kubwa walisema kwamba ndugu
zao walichukuliwa kwa ahadi ya kwenda kutafutiwa kazi nchi za Uarabuni, India,
Marekani na nchi za Ulaya.
“Kwani binti yako ana elimu kiasi gani
mpaka uamini kwamba anaenda kutafutiwa kazi nzuri huko anakokwenda?”
“Kiukweli wala hajasoma, aliishia darasa
la saba tu lakini tukaambiwa kule kuna watu wanatafutwa kwa ajili ya kwenda
kufanya kazi za ndani, na mshahara wake ni mkubwa kuliko hata mameneja wengi wa
Tanzania, ndiyo maana tukamruhusu kwa shingo upande.
“Isitoshe kabla ya kuondoka, viongozi wa
shirika hilo walitupa shilingi milioni moja kama shukrani tu na hapo ni nje ya
mshahara wa binti yetu,” mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Akilimali,
aliniambia wakati akizungumza nami kwenye simu.
“Uko bize sana na simu mpenzi wangu,
kitaalamu simu huwa inatoa mionzi ambayo siyo mizuri kwa mtu kama wewe kwani
inaweza kukuongezea matatizo mpenzi, au wewe hulioni hilo?” alisema Shamila
baada ya kuingia wodini, ikiwa imepita takribani nusu saa tangu nilipomtaka
yeye na Raya watoke na kunipisha.
Nilishindwa hata nimjibu nini,
akanisogelea na kunibusu kwenye paji la uso wangu, akakiweka kitanda vizuri
kisha akakaa pembeni yangu.
“Eti, unalijua shirika linaloitwa Black
Heart?” nilimuuliza Shamila, akanitazama kwa macho ya mshangao kama
anayejiuliza ‘umelijuaje?’.
“Jamal!” aliniita huku sauti yake
ikionesha kuwa na hofu kubwa.
“Kumbe hicho ndicho ulichokuwa
ukikihangaikia muda wote?”
“Ndiyo, kwani kuna tatizo?”
“Ni hatari mpenzi wangu, nakupenda sana
na sitaki kuona ukipatwa na jambo lolote baya.”
“Kivipi? Mbona sikuelewi Shamila?”
nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
“Kuna siku uliniuliza kuhusu yule
mgonjwa anayeitwa Shenaiza, nikakueleza kwa kifupi kwamba baba yake siyo mtu
mzuri hata kidogo.”
“Ndiyo nakumbuka, sasa kwani kuna
uhusiano gani na hiki nilichokuuliza?” nilimtega Shamila kwani ilionesha kuna
mambo mengi anayajua lakini anaogopa kuniambia.
“Usinifanye mimi mjinga Jamal, najua
kila kitu kuhusu unachokifanya tangu mwanzo, najua kwamba unachimba kutaka
kujua baba yake Shenaiza anashughulika na nini lakini nakuomba sana, achana na
hicho unachokifanya.
“Watu wengi wameshapotea kwa sababu ya
kumfuatilia huyo mzee! Jamal, mwenzio nakupenda na sitaki kuona ukipotea ndiyo
maana nakwambia achana na hayo mambo.”
“Hapana, ni lazima niikamilishe hii kazi
Shamila, nimerudi duniani kwa ajili ya kazi hii, sitaogopa chochote wala sitarudi
nyuma,” nilimwambia kwa msisitizo, akanitazama tena machoni na kushusha pumzi
ndefu kwa mara nyingine, akatazama huku na kule kuhakikisha hakuna mtu
anayetusikiliza.
“Mhusika mkuu wa hiyo Black Heart ni
baba yake Shenaiza.”
“Ni shirika la nini?”
“Kwa nje linajitambulisha kama shirika
la kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali, kuwasafirisha wagonjwa kwenda
kutibiwa nje ya nchi, kuwalipia gharama za masomo watoto na vijana kutoka
kwenye familia maskini pamoja na kuwatafutia kazi nzuri wananchi nje ya nchi.”
“Umesema kwa nje, vipi kwa ndani?”
“Jamal, unajua mpaka nafikia hatua ya
kuufungua mdomo wangu kukwambia masuala haya ninayahatarisha maisha yangu kwa
kiasi kikubwa kwa sababu ikija kufahamika kwamba mimi ndiyo niliyekwambia
nitauawa mwenzako,” alisema Shamila kwa hofu kubwa. Sikuelewa hasa hofu yake
ilikuwa ikisababishwa na nini. Nikamtoa wasiwasi kwamba nitamlinda, akaniambia
kuwa sina uwezo wa kumlinda kwa sababu hata mimi mwenyewe nilikuwa nahitaji
kulindwa ndiyo maana nilishindwa kujitetea siku nilipovamiwa na kutaka kuuawa.
Ni kweli alizungumza pointi lakini
nilijivisha roho ya kiume, nikaendelea kumtoa wasiwasi na kujitutumua kwamba
siku hiyo walinibahatisha tu, akakubali kunieleza kwa upana.
Aliniambia kwamba licha ya shirika hilo
kujinadi kwa sura hiyo ya nje, likijifanya linasaidia jamii ya watu maskini,
ukweli ni kwamba lilikuwa likifanya biashara haramu ya viungo vya binadamu.
Akaendelea kuniambia kwamba shirika lilikuwa na mtandao mpana, likiwagusa
viongozi kadhaa wa ngazi za juu serikalini pamoja na watu wengine wenye taaluma
mbalimbali, wakiwemo madaktari.
Aliniambia kwamba watu wote waliokuwa
wakisafirishwa kwenda nje ya nchi na shirika hilo, walikuwa wakienda kutolewa viungo
vyao muhimu, kama moyo, mapafu, figo na vingine vingi, vikitolewa na
kupandikizwa kwa watu waliokuwa wakivihitaji.
Akaniambia kwamba kwenye nchi
zilizoendelea, kuna watu wengi wanaojiweza kifedha lakini wanakuwa na matatizo
mbalimbali ya kiafya kiasi kwamba fedha zao haziwasaidii kupona kwa kutumia
madawa mbalimbali ya hospitalini. Ni hao ndiyo waliokuwa wateja wakubwa wa
viungo hivyo vya binadamu.
Akanifafanulia kwamba; kwa mfano kama
kuna tajiri ana matatizo ya figo au ini na ameshatumia madawa yote bila kupata
nafuu, njia nyepesi ya kumrudishia afya bora ilikuwa ni kupandikizwa viungo vingine
kutoka kwa mtu asiye na matatizo.
Akasema kwa kuwa uhitaji ni mkubwa siku
hizi kutokana na mtindo wa maisha, hasa kwa nchi zilizoendelea, njia nyepesi
iliyokuwa inatumiwa na baba yake Shenaiza na wenzake, ilikuwa ni kuwasafirisha
watu kutoka nchi za kimaskini na kwenda kuwauza kwa bei ghali kwa ajili ya
kutolewa viungo vyote muhimu ambavyo huwekewa watu wanaojiweza kiuchumi.
Maelezo yake yalinishangaza na kunishtua
sana, akanihakikishia kwamba tangu shirika hilo lianze kufanya kazi miaka
kadhaa iliyopita, hakukuwa na hata mtu mmoja ambaye aliondoka na kurejea
nyumbani salama, wengi walikuwa wakirejeshwa wakiwa maiti na wengine hawakuwa
wakirejeshwa kabisa.
Ndugu zao wanapowaulizia, hutulizwa kwa
kupewa fedha na kuambiwa wapo salama na ipo siku watarejea nchini.
“Ina maana serikali kupitia kwa vyombo
vya usalama hawajui kuhusu hiki kinachoendelea?”
“Watu wanajua sana, lakini
nimeshakwambia huu ni mradi wa vigogo wakubwa serikalini, hakuna anayeweza
kufumbua mdomo wake na ukijaribu tu, basi ujue kifo kinakuita.”
Japokuwa mle wodini mlikuwa na kipupwe,
nilijikuta nikitokwa na kijasho chembamba, mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio
kuliko kawaida. Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini Shamila alikuwa akinikataza
kujihusisha na mambo yale.
Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza
alikuwa akifahamu kinachofanywa na baba yake na kwa sababu ilifika hatua akawa
amechoshwa na ukatili huo, alimtishia baba yake kuwa atatoa siri, jambo
lililosababisha ateswe sana, ikawa mtu yeyote akionekana kuwa karibu naye, baba
yake anahisi anaweza kupewa siri hiyo hivyo anauawa haraka kabla hajafumbua
mdomo wake.
“Kumbe ndiyo maana na mimi wananiwinda
kutaka kuniua?” nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment