ILIPOISHIA:
Alionesha
kama kuna jambo muhimu anataka kuniambia kuhusu Shenaiza na baba yake ingawa
sikujua ni jambo gani.
“Ha..pa...na!
Hapana!” nilijibu kwa kubabaika huku nikiwa makini kutaka kusikia ataniambia
nini.
SASA
ENDELEA...
“Kuwa
makini, baba yake siyo mtu mzuri,” alisema nesi huyo ambaye baadaye nilikuja
kugundua kwamba anaitwa Shamila.
“Unamaanisha
nini?” nilimuuliza kwa sauti ya chini, akanisogelea zaidi na kukaa pembeni ya
kitanda changu.
“Kuwa
tu makini, nakupenda na sitaki jambo lolote baya likutokee,” alisema huku
akinitazama kwa macho yake mazuri, macho yetu yakagongana. Tulitazamana kwa
sekunde kadhaa, akakwepesha macho yake huku aibu za kikekike zikiwa zimetawala
uso wake.
“Ahsante
kwa kunisaidia kunifunga upya jeraha langu,” nilimwambia tena, nikamuona
akitabasamu kisha akanishika mkono wangu.
“Usijali,
hiyo ni kazi yangu ila inabidi uijali afya yako. Hata kama angekuwa ni mgonjwa
mwingine, ningemsaidia kama nilivyokusaidia wewe.”
“Ahsante
pia kwa fulana uliyonipa, ni nzuri na inanukia vizuri,” nilimwambia kwa sauti
ya chini, akatabasamu tena na kuniambia:
“Nilijinunulia
hiyo fulana kama zawadi siku ya Valentine Day.”
“Kwa
nini ujinunulie mwenyewe zawadi katika siku muhimu kama hiyo? Kwani shemeji
hakukupa zawadi?”
“Shemeji?
Shemeji gani? Niliamua kujionesha upendo mwenyewe.
“Unataka
kusema msichana mrembo kama wewe unaweza kuwa huna mtu?”
“Huwezi
kuamini, sina mtu yeyote karibia mwaka unaelekea kuisha sasa. Niliyekuwa naye
aliniumiza sana moyo wangu na kunifanya niyachukie mapenzi,” alisema Shamila
kwa sauti ya upole, nikawa namtazama usoni alivyokuwa anaongea.
“Mbona
unaniangalia sana usoni? Mi nasikia aibu bwana,” alisema huku akiniachia mkono
wake na kusimama, aibu zikiendelea kutawala uso wake.
“You
are so beautiful Shamila!” (Wewe ni mrembo sana Shamila) nilimwambia, akacheka
sana na kurudi tena kukaa pale pembeni ya kitanda changu, akaniambia zimepita
siku nyingi hajasikia kauli kama hiyo kutoka kwenye kinywa cha mwanaume mzuri
kama mimi, wote tukacheka na kugongesheana mikono.
Kuna
jambo kubwa lilikuwa limebadilika maishani mwangu, kwa kipindi kirefu sikuwa na
mazoea ya kukaa karibu na wasichana wala kupiga nao stori.
Mtu
pekee niliyekuwa nimezoeana naye alikuwa ni Raya ambaye hata hivyo mara kwa
mara nilikuwa nikimkwepa lakini cha ajabu, katika siku za karibuni, nilijikuta
nikivutiwa na wasichana wawili, Shenaiza na sasa Shamila, achilia mbali Raya
ambaye tayari tulishaanza naye uhusiano wa kimapenzi.
Hata
ujasiri wa kuzungumza pia ulikuwa umeongezeka. Nikaendelea kupiga stori za hapa
na pale na Shamila, nikawa namchangamsha kwa sababu nilijua kuna jambo nilikuwa
nimemkera lakini pia nilitaka kumuingia ili nipate habari kumhusu Shenaiza na
baba yake kwani ilionesha kwamba nesi huyo anawajua vizuri.
“Hujaniambia
ubaya wa baba yake Shenaiza, kwani amefanya nini?”
“Tuachane
na hayo, usije ukaenda kumwambia binti yake bure, inaonesha unampenda sana.
Hivi nikuulize, kwani wewe una wapenzi wangapi?”
“Nijibu
kwanza swali langu na mimi nitakujibu la kwako. Ubaya wa baba yake Shenaiza ni
upi?” nilimkomalia Shamila, akashusha pumzi ndefu na kugeuka huku na kule kama
anayehakikisha kwamba hakuna mtu aliyekuwa akitusikiliza.
“Anafanya
biashara za hatari sana, siyo mtu mzuri hata kidogo.”
“Biashara
za hatari ndiyo biashara gani? Anauza madawa ya kulevya?”
“Si
bora hata angekuwa anauza madawa ya kulevya! We elewa kwamba anafanya biashara
za hatari sana, kama huamini endelea kumchunguza taratibu.”
“Nitamchunguza
vipi wakati hata simfahamu?”
“Humfahamu?”
aliniuliza Shamila kwa mshangao, nikamhakikishia kwamba simfahamu kabisa.
Aliniambia inawezekanaje nikawa na ukaribu na Shenaiza lakini nisimfahamu baba
yake? Sikuwa na cha kumjibu lakini ukweli ni kwamba sikuwa nimewahi kumuona
zaidi ya kusikia tu habari zake.
Akaniambia
kuwa muda mwingi huwa hakai nchini na hata akija, huwa haonekani kwa urahisi.
Nikamuuliza yeye amemfahamia wapi? Akanijibu kwamba huwa anakuja mara kwa mara
hospitalini hapo kwa sababu ana marafiki wengi ambao ni madaktari.
“Kwani
na yeye ni daktari?”
“Hapana.”
“Sasa
iweje awe na marafiki madaktari?” nilimuuliza, akashusha pumzi ndefu na
kuniambia kwamba ana urafiki nao kwa sababu huwa anashirikiana na baadhi yao
wasio waaminifu kwenye hizo biashara zake.
Nilijaribu
kumbana aniambie ni biashara ya namna gani anayofanya na madaktari lakini
hakuwa tayari kuniambia chochote kwa maelezo kwamba anahofia maisha yake.
Nilimbana sana lakini alikataa katakata kuniambia zaidi ya kunitaka niendelee
kufuatilia mwenyewe nitaujua ukweli.
Kiukweli
alinichanganya kichwa lakini alinipa mwanga. Ukichanganya na yale maelezo ya
Shenaiza, tayari nilikuwa na sehemu ya kuanzia, nikajiapiza ndani ya moyo wangu
kwamba ni lazima nitaujua ukweli na nitafanya kazi niliyotumwa, ya kumzuia
kuendelea kufanya alichokuwa anakifanya japokuwa sikujua ni kitu gani.
Ni
kazi ambayo nilipewa nikiwa kule kwenye ulimwengu mwingine kama masharti ya
kurejea kwenye ulimwengu wa kawaida. Sikujua nitafanya nini lakini
nilichojiapiza ni kwamba ilikuwa ni lazima nifanikiwe kumzuia alichokuwa
anakifanya.
“Mbona
kama umezama kwenye dimbwi la mawazo?” Shamila aliniuliza na kunizindua kutoka
kwenye mawazo mazito, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni.
“Haya
na wewe nijibu maswali yangu!” alisema Shamila huku tabasamu likianza kuchanua
kwenye uso wake. Jambo ambalo sikuwa na uhakika nalo, ni juu ya uchangamfu wa
Shamila. Sikujua huwa anachangamka hivyohivyo akiwa na watu wengine au ni
kwangu tu.
“Nimekuuliza
una wapenzi wangapi?”
“Mmoja
tu, anaitwa Raya, yule niliyekuwa namkimbilia muda ule.”
“Muongo
wewe, na Shenaiza?”
“Shenaiza
siyo mpenzi wangu, ni rafiki yangu tu.”
“Rafiki
yako ndiyo mna-kiss? Yaani hamjifichi kabisa, inaonesha ni mpenzi wako.
“Siyo
mpenzi wangu, kweli tena,” nilimwambia Shamila lakini akaendelea kukataa,
akaniambia hata Shenaiza mwenyewe alikuwa akiwaambia manesi kwamba mimi ndiyo
mpenzi wake na tuna mipango ya kuja kufunga ndoa, kauli iliyonishangaza sana.
Shamila
aliendelea kunishutumu kwamba sijatulia, naonesha nina wanawake wengine wengi
na ndiyo maana nashindwa kuwathamini watu wanaonipenda kwa dhati. Sikuelewa
msingi wa lawama zake ni nini kwa sababu mimi na yeye ndiyo kwanza tulikuwa
tumejuana, akaendelea kuniambia kwamba kwa sababu sijatulia nitakosa vitu
vizuri.
Akaonesha
kususa na kutoka wodini kwa hasira, akaniacha nikiwa na maswali mengi
yaliyokosa majibu, wakati anatoka mlangoni, alipishana na Raya aliyekuwa
akiingia akiwa na kikapu ambacho hata bila kuuliza nilijua kwamba kina chakula.
Nilipomtazama usono, macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba kuonesha kwamba
alikuwa amelia kwa muda mrefu, hata ule uchangamfu wake haukuwepo tena. Macho
yake yakatua kwenye fulana niliyokuwa nimevaa, akanikazia macho.
Je,
nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment