Friday, September 22, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 44



ILIPOISHIA:
“Niangalie vizuri namna ya kuchimba maana tukitoka hapa inabidi na wewe ukafanye majaribio kama wenzako,” alisema baba. Muda huo ulikuwa ni kama saa sita hivi za usiku, giza nene likiwa limetanda kila sehemu.
SASA ENDELEA...
Huku nikitetemeka, nilianza kumtazama vizuri baba alivyokuwa akichimba, alikuwa akifukua shina la ule mti huku akiuzunguka, akitamka maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa. Baada ya kuuzunguka karibu mara saba, tayari alishakuwa ameifikia mizizi, akatoa kisu na kuanza kuichambua na kuikata mmoja baada ya mwingine.
“Hutakiwi kukata mizizi zaidi ya saba kwenye mti mmoja, na hutakiwi kuchimba mti ambao unaonekana tayari umeshachimbwa katika siku za hivi karibuni,” alisema baba, nikawa natingisha kichwa kumkubalia. Baada ya kumaliza, alinikabidhi tochi, akaniambia niutazame vizuri ule mti, nikaumulika vizuri.
“Sasa na wewe unatakiwa kutafuta mti kama huuhuu, ipo mingi lakini lazima uwe makini kutafuta wa kuchimba dawa,” aliniambia baba, basi nikaanza kumulika huku na kule, baba akiwa upande wa kushoto na baba yake Rahma upande wa kulia.
Muda mfupi baadaye, kweli nilifanikiwa kuupata lakini ulikuwa umezongwa na miiba mingi, baba akaniambia ni lazima niitoe kwanza miiba yote ndiyo nianze kuchimba, nilifanya hivyo na baada ya muda, nilikuwa nimepasafisha pale kwenye shina la mti huo.
Nikaanza kuchimba huku baba akinielekeza hatua kwa hatua, akaniambia kwa kuwa ndiyo kwanza naanza hakuna umuhimu wa kunuiza maneno kama alivyokuwa akifanya yeye bali natakiwa kuweka nia moyoni kwamba nahitaji damu kwa ajili ya kafara.
Nilifanya hivyo, nikawa naufukua ule mti na nilipozunguka mara ya saba, tayari mizizi ilikuwa ikionekana, baba akanipa kisu na kuniambia kwamba natakiwa kuchagua mizizi ya katikati, yaani isiwe mikubwa sana wala midogo sana na isizidi saba.

Nikakata wa kwanza, pale nilipokata pakawa panatoka yale majimaji kama damu, nikakata wa pili, wa tatu mpaka saba ilipotimia, shina lote likawa limelowa na yale majimaji ya ule mti kama damu.
“Haya fukia lakini hakikisha hiyo mizizi hauiweki chini, ishike vizuri,” aliniambia na kunielekeza kwamba wakati wa kufukia, natakiwa kwenda kinyume na vile nilivyokuwa nafukua, yaani kama wakati wa kufukua nilikuwa nauzunguka mti kwa kuelekea upande wa kulia, ninapofukia natakiwa kuanzia upande wa kushoto na hivyo ndivyo nilivyofanya.
Baada ya kumaliza, baba alisema tunapaswa kwenda kuziosha dawa zetu mtoni na kuzitengeneza vizuri. Sikuwa mwenyeji wa Kibaha na hata sikuwa najua kama kuna mto, nikawa kama bendera fuata upepo.
Tulitembea tukikatiza vichaka na mapori, hatimaye tukatokezea mahali palipokuwa na kama chemchemi hivi, pembeni kukiwa na bustani za mbogamboga nyingi, baba akatangulia mpaka pale kwenye chemchemi, kabla ya yote, alitoa kisu chake na kukata jani kubwa la mgomba, akalikata vipande vitatu, kimoja akanipa, kingine akampa baba Rahma na kingine akabaki nacho yeye.
Alitoa ile mizizi aliyoichimba, akaniambia nimtazame kwa makini anachokifanya, ilikuwa imebadilika rangi na kuwa nyekundu kama damu, akaanza kuiosha ikiwa juu ya jani la mgomba, akafanya hivyo kwa dakika kadhaa mpaka ilipobadilika rangi na kurejea kwenye rangi yake halisi ambayo ni kama kahawia fulani hivi.
Ilifika zamu yangu, na mimi nikafanya vilevile, nikaitoa mfukoni na kuiosha vizuri, kisha ikafika zamu ya baba yake Rahma ambapo baba alimtolea na kumpa mizizi yake, akaiosha kwa uzoefu wa hali ya juu kisha tukaondoka eneo hilo.
Hapakuwa mbali sana na barabara kwani hata kelele za magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi kubwa tuliweza kuzisikia. Kadiri tulivyokuwa tukisonga mbele ndivyo hofu ilivyozidi kutanda kwenye moyo wangu.
Tulikatiza vichaka, mapori na mashamba ya watu na hatimaye tukawa tumetokezea barabara ya lami. Sikujua eneo lile linaitwaje lakini kwa mzunguko tulioupiga, kuanzia pale tuliposhuka kwenye gari, tulivyoelekea njia ya Tumbi na baadaye kuingia porini kisha kurudi barabarani, nilijua kwamba si mbali sana na pale tuliposhukia.
“Mtu yeyote akikusemesha hutakiwi kujibu chochote, eneo hili lina watu kutoka jamii mbalimbali ambao huwa wanapenda kupimana nguvu, umenielewa?” baba aliniambia, nikatingisha kichwa kuonesha kumkubalia.
“Leo ni zamu yako, kwa hiyo inatakiwa unisikilize kwa makini,” baba aliniambia, akasema kati ya ile mizizi saba, mmoja natakiwa kwenda kuufunga kwenye mti au jani lolote upande wa pili wa barabara, mwingine natakiwa kuuweka katikati ya barabara, mwingine natakiwa kuufunga upande ule tuliokuwepo, mmoja natakiwa kuutafuna na kuumeza na miwili natakiwa kubaki nayo mwilini, mmoja niweke kwenye mfuko wa kushoto wa suruali na mwingine niubane kwenye kwapa langu la kushoto kama kipima joto.
Yalikuwa ni maelezo marefu lakini nilijitahidi kuwa mwelewa maana nilikuwa na shauku kubwa ya kuona nini kitatokea. Kweli baada ya hali kutulia, kwa maana kukiwa hakuna gari kutoka upande wowote, nilivuka barabara kinyumenyume mpaka upande wa pili.
Kwa kutumia uzi mweusi alionipa baba, niliufunga ule mzizi kwenye tawi moja la mti mdogo uliokuwa pale pembeni ya barabara, nikarudi tena kinyumenyume mpaka katikati ya barabara na kukaa chini kabisa, nikaweka ule mzizi kisha nikajiburuza kwa makalio kinyumenyume mpaka pale baba na baba yake Rahma walipokuwa wamesimama.
Nikasimama na kusogea kwenye kimti kingine kidogo kilichokuwa kando ya barabara, usawa wa kile nilichokifunga, nikaenda kufunga ule mzizi kwa kutumia ule uzi kisha kinawasogelea akina baba ambao walikuwa wakinitazama kwa makini kuhakikisha sikosei hatua hata moja.
“Safi sana,” alisema baba kisha akaanza kuniuliza kama mpaka hapo nimeshaelewa ni gari linalotokea upande gani ndiyo litapata ajali. Sikuwa naelewa chochote. Akaniambia kwa sababu nimesota kwa makalio kutokea katikati ya barabara kuelekea upande wa kushoto wa Barabara ya Morogoro, gari litakalopata ajali litakuwa ni linalotoka Dar es Salaam kuelekea upande wa Morogoro.
Sikuelewa anamaanisha nini, ikabidi nitulie kuona nini kinachoenda kutokea. Tulisogea pembeni kabisa, umbali wa kama mita mia moja hivi, vichakani kabisa, tukakaa kwa kukunja miguu na kutengeneza duara. Kulikuwa na mbu wengi lakini wote walikuwa wakiishia kutuzunguka tu, hata sijui kwa nini hawakuwa wakituuma.
“Nataka ufumbe macho halafu utulie huku ukitafuna huo mzizi mmoja, nitakachokuuliza unijibu,” baba aliniambia, nikafanya kama alivyoniambia. Cha ajabu, nilipofumba macho tu, japokuwa tulikuwa mbali kidogo na barabara, niliweza kusikia sauti za magari na pikipiki vikipita kwa kasi, cha kushangaza zaidi, niliweza kusikia hata sauti za madereva na abiria, nikashtuka sana.
Nikiwa nimeendelea kutulia, japokuwa nilikuwa nimefumba macho, kadiri nilivyokuwa nikizidi kutafuna ule mzizi ndivyo nilivyoanza kuona taswira ya kila kilichokuwa kikiendelea barabarani utafikiri nilikuwa nimesimama pembeni ya barabara, tena nikiwa nimefumbua macho.
“Unaona magari mangapi?”
“Mengi tu.”
“Yanayoelekea upande wa Morogoro ni mangapi?”
“Ni matatu.”
“Ambalo lipo nyuma kabisa lina abiria wangapi?”
“Abiria mmoja ambaye ni mtoto na dereva mwanamke.”
“Safi, hiyo ndiyo kazi yako ya leo, likazie macho hilo gari kwa nguvu na likikaribia hapo ulipo fumbua macho ghafla halafu tena hicho kilichopo mdomoni mwako,” alisema baba, kweli nikawa nalitazama gari hilo.
Lilikuwa ni gari dogo na ndani yake kulikuwa na watu wawili tu, dereva mwanamke na mtoto, ilionesha ni kama ni wanafamilia wanarudi makwao. Sikuelewa nini kitawapata lakini kwa sababu ya shauku niliyokuwa nayo, nilijikuta nikifanya kile baba alichoniambia, nikafumbua macho ghafla na kutema mabaki ya ule mzizi, nikashtukia nimemtemea baba usoni.
Mara kikasikika kishindo kikubwa kule barabarani, kilichonishtua mno. Sikuelewa nini kimetokea pale kwa sababu nilipokuwa nimefumbamacho, nilikuwa najiona kabisa kwamba nipo barabarani lakini nilipofumbua tu, nilijikuta nikiwa nimekaa palepale tulipokuwa tumekaa na baba na baba yake Rahma.
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati nataka kufumbua machom nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani, akikunya usukani gahfla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,” alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...