ILIPOISHIA:
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati
nataka kufumbua macho nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani,
akikunja usukani ghafla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka
kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto
kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,”
alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
SASA ENDELEA...
“Nikikamatwa je?”
“Nenda, hakuna mtu yeyote atakayekukamata
wala kukuona, usiongee chochote na mtu yeyote, hata wakikusemesha usijibu,”
alisema baba. Basi huku nikitetemeka, nilitoka na kile kipande cha mgomba,
nikatembea harakaharaka mpaka pale barabarani.
Lile gari dogo lilikuwa limepata ajali
mbaya na kupinduka, matairi yakiwa juu, likiwa limegeukia kule lilikotokea. Kwa
mtu yeyote lazima angejiuliza sana kilichosababisha ajali hiyo kwa sababu
kwanza lilikuwa ni eneo la tambarare na hakukuwa na kona wala tuta lolote.
Damu zilikuwa zimetapakaa kuanzia
barabarani mpaka kando ya barabara, pale gari hilo lilipokuwa limepinduka.
Ilibidi nifanye kile nilichoambiwa kabla watu hawajaanza kujaa. Niliinama
kwenye upande aliokuwa amekaa yule mtoto, nikakitingisha kioo ambacho
kilishapasuka kwa sehemu kubwa, kikamwagika chote kwenye lami.