Tuesday, September 26, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 45


ILIPOISHIA:
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati nataka kufumbua macho nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani, akikunja usukani ghafla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,” alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
SASA ENDELEA...
“Nikikamatwa je?”
“Nenda, hakuna mtu yeyote atakayekukamata wala kukuona, usiongee chochote na mtu yeyote, hata wakikusemesha usijibu,” alisema baba. Basi huku nikitetemeka, nilitoka na kile kipande cha mgomba, nikatembea harakaharaka mpaka pale barabarani.
Lile gari dogo lilikuwa limepata ajali mbaya na kupinduka, matairi yakiwa juu, likiwa limegeukia kule lilikotokea. Kwa mtu yeyote lazima angejiuliza sana kilichosababisha ajali hiyo kwa sababu kwanza lilikuwa ni eneo la tambarare na hakukuwa na kona wala tuta lolote.
Damu zilikuwa zimetapakaa kuanzia barabarani mpaka kando ya barabara, pale gari hilo lilipokuwa limepinduka. Ilibidi nifanye kile nilichoambiwa kabla watu hawajaanza kujaa. Niliinama kwenye upande aliokuwa amekaa yule mtoto, nikakitingisha kioo ambacho kilishapasuka kwa sehemu kubwa, kikamwagika chote kwenye lami.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 41


ILIPOISHIA:
“Habari za saizi nesi,” Raya alimsalimia Shamila kwa unyenyekevu, jambo ambalo hakuwahi kulifanya kabla. Shamila naye akajibu kwa uchangamfu, nikabaki njia panda. Sikujua walizungumza nini muda ule mpaka wakamaliza tofauti zao. Raya akaja mpaka pale kitandani na kunibusu mdomoni, Shamila akageuka na kulishuhudia tukio hilo.
SASA ENDELEA...
Alipogundua kwamba namtazama, harakaharaka Shamila alijifanya kama hakuwa ameona chochote.
“Leo nimekupikia chakula kizuuri, naamini utakipenda,” alisema Raya huku akianza kuniandalia chakula. Nikawa nimetulia pale kitandani huku akilini mwangu mawazo mengi yakipita. Nilikuwa nimeingia kwenye mtego hatari sana ambao sasa ilikuwa ni lazime nifanye kila kinachowezekana kujikomboa.
Njia pekee ambayo ingenisaidia, ilikuwa ni kuhakikisha baba yake Shenaiza na kundi lake lote wanafikishwa mbele ya sheria na mamia ya watu ambao maisha yao yalikuwa hatarini, wanaokolewa kutoka kwenye shimo la mauti.

Monday, September 25, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 40


ILIPOISHIA:
“Nimekikuta kwenye kitanda cha Shenaiza, na anaonekana kama hana fahamu, rangi ya ngozi yake imebadilika na kuwa ya kijivu,” nilimwambia, akashusha pumzi ndefu na kunitazama usoni.
SASA ENDELEA...
“Benzodiazepam,” Shamila alisema kwa sauti ya juu, akitamka maneno yaliyokuwa yameandikwa kwenye kile kichupa nilichokikuta pembeni ya kitanda cha Shenaiza.
“Kwani ni dawa gani?”
“Mungu wangu! Wameamua kummalizia kabisa mdada wa watu. Hii ni dawa ya usingizi ambayo hairuhusiwi kutumika bila uangalizi wa kutosha wa daktari. Mtu anapotumia dozi kubwa, husababisha muda wote awe analala tu na kama hali hii ikiendelea kwa muda, husababisha mgonjwa kupoteza kumbukumbu na kuwa kama mtu aliyechanganyikiwa.”
“Haa! Na siyo kwamba dawa hii hutumika kuwatibu wagonjwa wa akili?”
“Hapana Jamal, hii hutumika tu kuwatuliza watu wenye msongo mkali wa mawazo au stress kiasi kwamba wanakosa usingizi. Wakitumia dawa hii chini ya uangalizi wa daktari, huwasaidia kupata usingizi na kuwapunguzia msongo mkali au ‘stress’, lakini narudia tena, ni lazima itumiwe chini ya uangalizi mkali wa daktari.”
“Sasa kwa nini wanampa Shenaiza?”
“Jibu ni moja tu, wanataka watu wote waamini kwamba kweli amechanganyikiwa. Kama kwa siku chache tu alizokaa hapa hospitalini kichupa kimeshaisha, maana yake ni kwamba anapewa dozi kubwa sana ambayo ndani ya muda mfupi tu, itamfanya apoteze kumbukumbu na kuwa mwendawazimu.”

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 45


ILIPOISHIA:
Kitu cha mwisho nilichokumbuka, wakati nataka kufumbua macho nilimuona yule mwanamke aliyekuwa kwenye usukani, akikunja usukani ghafla kama aliyeona kitu cha hatari mbele na sasa anataka kukikwepa, ndipo kikafuatia kile kishindo.
“Nenda haraka, hakikisha unamtoa mtoto kwenye gari na kuja naye hapa, pale kwenye gari ulipomtoa utaweka hiki,” alisema baba huku akinipa kipande cha mgomba.
SASA ENDELEA...
“Nikikamatwa je?”
“Nenda, hakuna mtu yeyote atakayekukamata wala kukuona, usiongee chochote na mtu yeyote, hata wakikusemesha usijibu,” alisema baba. Basi huku nikitetemeka, nilitoka na kile kipande cha mgomba, nikatembea harakaharaka mpaka pale barabarani.
Lile gari dogo lilikuwa limepata ajali mbaya na kupinduka, matairi yakiwa juu, likiwa limegeukia kule lilikotokea. Kwa mtu yeyote lazima angejiuliza sana kilichosababisha ajali hiyo kwa sababu kwanza lilikuwa ni eneo la tambarare na hakukuwa na kona wala tuta lolote.
Damu zilikuwa zimetapakaa kuanzia barabarani mpaka kando ya barabara, pale gari hilo lilipokuwa limepinduka. Ilibidi nifanye kile nilichoambiwa kabla watu hawajaanza kujaa. Niliinama kwenye upande aliokuwa amekaa yule mtoto, nikakitingisha kioo ambacho kilishapasuka kwa sehemu kubwa, kikamwagika chote kwenye lami.
Nikaingiza mikono na kumvuta mtoto huyo aliyekuwa amebanwa pale kwenye siti, kwa kuwa nilikuwa na nguvu za kutosha, nilifanikiwa kumtoa, nikamlaza barabarani kisha nikachukua kile kipande cha mgomba na kukirudishia palepale nilipomtoa yule mtoto, kama baba alivyonielekeza.

Friday, September 22, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 44



ILIPOISHIA:
“Niangalie vizuri namna ya kuchimba maana tukitoka hapa inabidi na wewe ukafanye majaribio kama wenzako,” alisema baba. Muda huo ulikuwa ni kama saa sita hivi za usiku, giza nene likiwa limetanda kila sehemu.
SASA ENDELEA...
Huku nikitetemeka, nilianza kumtazama vizuri baba alivyokuwa akichimba, alikuwa akifukua shina la ule mti huku akiuzunguka, akitamka maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa. Baada ya kuuzunguka karibu mara saba, tayari alishakuwa ameifikia mizizi, akatoa kisu na kuanza kuichambua na kuikata mmoja baada ya mwingine.
“Hutakiwi kukata mizizi zaidi ya saba kwenye mti mmoja, na hutakiwi kuchimba mti ambao unaonekana tayari umeshachimbwa katika siku za hivi karibuni,” alisema baba, nikawa natingisha kichwa kumkubalia. Baada ya kumaliza, alinikabidhi tochi, akaniambia niutazame vizuri ule mti, nikaumulika vizuri.
“Sasa na wewe unatakiwa kutafuta mti kama huuhuu, ipo mingi lakini lazima uwe makini kutafuta wa kuchimba dawa,” aliniambia baba, basi nikaanza kumulika huku na kule, baba akiwa upande wa kushoto na baba yake Rahma upande wa kulia.
Muda mfupi baadaye, kweli nilifanikiwa kuupata lakini ulikuwa umezongwa na miiba mingi, baba akaniambia ni lazima niitoe kwanza miiba yote ndiyo nianze kuchimba, nilifanya hivyo na baada ya muda, nilikuwa nimepasafisha pale kwenye shina la mti huo.
Nikaanza kuchimba huku baba akinielekeza hatua kwa hatua, akaniambia kwa kuwa ndiyo kwanza naanza hakuna umuhimu wa kunuiza maneno kama alivyokuwa akifanya yeye bali natakiwa kuweka nia moyoni kwamba nahitaji damu kwa ajili ya kafara.
Nilifanya hivyo, nikawa naufukua ule mti na nilipozunguka mara ya saba, tayari mizizi ilikuwa ikionekana, baba akanipa kisu na kuniambia kwamba natakiwa kuchagua mizizi ya katikati, yaani isiwe mikubwa sana wala midogo sana na isizidi saba.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 39


ILIPOISHIA:
Akaendelea kuniambia kwamba Shenaiza alikuwa akifahamu kinachofanywa na baba yake na kwa sababu ilifika hatua akawa amechoshwa na ukatili huo, alimtishia baba yake kuwa atatoa siri, jambo lililosababisha ateswe sana, ikawa mtu yeyote akionekana kuwa karibu naye, baba yake anahisi anaweza kupewa siri hiyo hivyo anauawa haraka kabla hajafumbua mdomo wake.
“Kumbe ndiyo maana na mimi wananiwinda kutaka kuniua?” nilijikuta nikisema kwa sauti kubwa.
SASA ENDELEA...
“Na bado wataendelea kukuwinda mpaka watakapoyakatisha maisha yako, unapaswa kuwa makini sana mpenzi wangu,” alisema Shamila lakini alichokisema ni kama hakikuingia akilini mwangu.
Akili yangu ilianza kunienda mbio kuliko kawaida, nikawa naunganisha matukio, kuanzia siku Shenaiza aliponipigia simu na kuniambia kwamba ana tatizo kubwa na anahitaji nimsaidie, baada ya awali kuwa amekosea namba.
“Lazima nikazungumze na Shenaiza, atakuwa anajua mambo mengi zaidi,” nilisema huku nikijaribu kuinuka, Shamila akanizuia na kuniuliza kama ninakumbuka kilichotokea muda mfupi uliopita kwenye maegesho ya magari.
Japokuwa nilikuwa na shauku ya kwenda kuonana na Shenaiza, maneno hayo ya Shamila yalinivunja nguvu kabisa. Nilikumbuka jinsi wale wanaume wenye asili kama ya Shenaiza walivyokuwa wakiniwinda kwa udi na uvumba.

Thursday, September 21, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 38


ILIPOISHIA:
“Mara ya mwisho mlizungumza naye lini?”
“Kiukweli tangu aondoke hatujawahi kuzungumza naye, wanasema hospitalini hawaruhusu kutumia simu,” alijibu mwanaume huyo, nikashusha pumzi ndefu.
SASA ENDELEA...
Majibu ya watu hao wawili tu yalitosha kunifanya nielewe kilichokuwa kinaendelea lakini ili kupata ushahidi mkubwa zaidi, niliendelea kuwapigia simu wengine. Wachache hawakuwa wakipatikana hewani lakini karibu watu 16 wote walikuwa wakipatikana na majibu yao hayakuwa yakitofautiana.
Wapo waliosema kwamba ndugu zao walichukuliwa kwenda kusoma nje ya nchi kwa msaada wa shirika hilo, wengine wakasema walipelekwa kwa matibabu lakini asilimia kubwa walisema kwamba ndugu zao walichukuliwa kwa ahadi ya kwenda kutafutiwa kazi nchi za Uarabuni, India, Marekani na nchi za Ulaya.
“Kwani binti yako ana elimu kiasi gani mpaka uamini kwamba anaenda kutafutiwa kazi nzuri huko anakokwenda?”
“Kiukweli wala hajasoma, aliishia darasa la saba tu lakini tukaambiwa kule kuna watu wanatafutwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi za ndani, na mshahara wake ni mkubwa kuliko hata mameneja wengi wa Tanzania, ndiyo maana tukamruhusu kwa shingo upande.
“Isitoshe kabla ya kuondoka, viongozi wa shirika hilo walitupa shilingi milioni moja kama shukrani tu na hapo ni nje ya mshahara wa binti yetu,” mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Akilimali, aliniambia wakati akizungumza nami kwenye simu.

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 43



ILIPOISHIA:
“Hapana! Hapanaaa,” nilisema kwa sauti ya juu, ikabidi baba anizibe mdomo maana alihisi naweza kuropoka mambo mengine na kuwafanya wasiohusika wajue.
“Huna haja ya kuogopa, zipo njia za kutimiza hicho ulichoambiwa bila kuonekana kama wewe ndiyo umefanya moja kwa moja, mbona sisi huwa tunafanya sana tu,” alisema baba, macho yakanitoka.
SASA ENDELEA...
Aliondoa mkono wake mdomoni mwangu, akaniambia wameniamini ndiyo maana wameniunganisha kwenye jamii yao, akaniambia faida nitakazozipata ni nyingi na kubwa sana kwa hiyo sina sababu ya kuogopa kutimiza sharti lile dogo nililopewa.
“Sijawahi kuua mtu hata siku moja, nitaanzaje,” nilisema, baba akatabasamu na kumgeukia baba yake Rahma, wakacheka na kugongesheana mikono. Sikuelewa kwa nini wao wacheke wakati mimi nilikuwa kwenye hali mbaya kiasi hicho, hofu kubwa ikiwa imetanda kwenye moyo wangu.
“Unatakiwa ujue namna ya kudhibiti hofu yako, ukiwa mwoga hivi huwezi kufanya chochote,” alisema baba, baba yake Rahma akamuunga mkono, wakawa wananieleza kwamba mtihani niliopewa ni mdogo sana na endapo nitashindwa nitakuwa nimewaangusha sana na kila mtu atanicheka.
“Utathibitisha kwamba kauli yangu niliyoitoa juu yako ni sahihi.”
“Kauli gani?”

Tuesday, September 12, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 37


ILIPOISHIA:
Niliendelea ‘kuperuzi’ yake mafaili, moja baada ya jingine. Kama nilivyokuwa nimeona awali, yalikuwa yamejaa taarifa za watu mbalimbali, wakubwa kwa wadogo, yakiwa na taarifa kuhusu hali zao za kiafya na viungo mbalimbali kwenye mwili, bado nikawa sielewi. Niliendelea kuchimba kwa undani, taratibu nikaanza kugundua mambo ambayo ama kwa hakika yalinishangaza sana.
SASA ENDELEA...
Kwa jinsi ilivyoonesha, kulikuwa na mtandao mpana sana wa watu kutoka hapa nyumbani Tanzania, India, Marekani, Uingereza na nchi za Kiarabu ambao ulikuwa ukihusisha hospitali kubwakubwa duniani ambao walikuwa wakifanya biashara ambayo nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka kuijua.
Nilipoendelea kufuatilia kwenye mafaili yake, niligundua kuwa kulikuwa na namba za mawasiliano za kila mtu ambaye taarifa zake zilikuwa zimeandikwa na kama hiyo haitoshi, pia kulikuwa na taarifa za mtu wa karibu (next of keen), nikawa nimepata pa kuanzia.
“Naomba ukaninunulie kalamu na daftari dogo kule nje ya hospitali,” nilimwambia Raya lakini akanikatalia na kuja juu.
“Ina maana unaona afya yako siyo muhimu kuliko hicho unachokifanya? Siendi popote mpaka ule kwanza,” alisema huku akinisogezea chakula, nikashusha pumzi ndefu na kuiweka laptop pembeni, nikanyoosha mikono nikiashiria aninawishe, nikaanza kula.
“Unaonekana kuwa na pilikapilika nyingi, kwa nini hujionei huruma mpenzi wangu? Inabidi upone kwanza, afya yako ni muhimu kuliko kitu kingine chochote,” Raya alisema kwa upole huku akinibembeleza nile, nikawa nakula huku mara kwa mara macho yangu yakigongana na ya nesi Shamila.

Monday, September 11, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 42


ILIPOISHIA:
Kwa akili yangu nilijua kwamba tayari kazi imekwisha, kumbe kulikuwa na kazi nyingine, nikaanza kutetemeka tena huku nikigeuka huku na kule kuwatazama wale watu ambao wote walikuwa na nyuso za furaha. Nilipogeuka upande wa kushoto, nilimuona mtu aliyenifanya nishtuke mno, nilifikicha macho nikiwa ni kama siamini.
SASA ENDELEA...
Alikuwa na Isrina, naye akiwa amevaa kama wale watu wengine wote waliokuwepo eneo lile. Alikuwa ametulia akinitazama kwa makini, ilionesha kwamba kumbe naye muda wote wakati yale mambo yakiendelea alikuwepo na alikuwa akinifuatilia hatua kwa hatua.
Nilishtuka kupita kiasi, nikageuka na kumtazama baba, naye akanitazama huku akitingisha kichwa kama ishara ya kuniambia ninachokiona ni kweli. Ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini mara kwa mara baba alikuwa akinikanya kuwa karibu na msichana huyo huku akiniuliza mara kwa mara kama najua ana malengo gani na mimi.
Nilijikuta kama kichwa kikiwa kizito, kwa tafsiri nyepesi, Isrina au Isri kama mwenyewe alivyokuwa akipenda kuitwa, alikuwa akifahamiana vizuri na baba kwa sababu wote walikuwa jamii moja. Bado sikutaka kuamini kama Isrina naye anahusika na hayo mambo, nilijaribu kuvuta kumbukumbu ya siku niliyokutana naye kwa mara ya kwanza.
Bado sikuwa na majibu ilikuwaje mpaka tukapanda basi moja, ilivyoonesha ni kama kukutana kwetu hakukuwa bahati mbaya bali ni jambo ambalo lilipangwa. Sasa kama anafahamiana na baba, kwa nini hataki kabisa niwe karibu naye? Kwa nini anamchukia? Nilijiuliza maswali mengi yasiyo na majibu.

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 41


ILIPOISHIA:
Nikiwa bado nashangaa, mwili ukiwa unatetemeka kwa hofu, nilishtukia wale watu wakikimbilia pale kwenye moto na kujipanga foleni, yule babu akasogea kwenye zile nyama, akawa anagawa, kila mmoja anapita na kupewa kipande chake kisha anatafuta sehemu ya kwenda kukaa na kuanza kula. Nilihisi kama nipo ndotoni lakini haikuwa hivyo.
“Hongera, umekuwa sasa,” alisema baba huku akinikumbatia, akanishika mkono na kunipeleka kwenye foleni, akaniingiza kwenye foleni.
SASA ENDELEA...
“Hapana baba, siwezi! Siwezi...” nilisema huku nikitaka kutoka kwenye foleni lakini baba alinishika mkono kwa nguvu. Nilikuwa natafuta upenyo ili nijitie vidole mdomoni kujitapisha ile nyama lakini ni kama baba alinishtukia.
Hakunipa upenyo hata kidogo, nikawa naendelea kutetemeka kwa hofu kubwa, nikiwa sielewi hatima ya yote yale itakuwa nini. Tofauti na mimi, watu wengine wote waliokuwepo eneo lile, akiwemo baba, baba yake Rahma na wale watu wengine wote, walikuwa na furaha kubwa ndani ya mioyo yao.
Kingine kilichonishangaza na kuniacha na maswali mengi, kila mtu aliyekuwa akifika pale mbele kwa yule babu aliyekuwa akigawa nyama, akikabidhiwa yake alikuwa akifurahi sana na kwenda kukaa pembeni na kuanza kuila bila wasiwasi wowote.
Nimewahi kusikia sana kuhusu stori za watu wanaokula nyama za watu lakini siku zote nilikuwa naona kama ni mambo ya kutunga, iweje mtu amle mwenzake? Ni hapo ndipo nilipoelewa kwamba kumbe siyo stori za kusadikika tu bali ni mambo ambayo yapo na yanafanyika kwa wingi.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 36


ILIPOISHIA:
Ghafla akiwa anakuja mbio, lile gari lilitokeza tena na kuja kwa kasi pale lilipokuwa limepaki awali, nikashtuka kugundua kuwa kumbe wale watu hawakuwa wameondoka, nikajua lazima watashtukia mahali nilipo kutokana na jinsi Raya alivyokuwa anakuja kwa kasi.
SASA ENDELEA...
“Naomba unisaidie kitu, huyu dada akifika hapa kuniulizia mwambie nimeshashuka kwenye gari nimeelekea upande wa wodi za wanaume, nikishuka funga huu mlango haraka,” nilimwambia dereva teksi ambaye alibaki ameduwaa, akiwa haelewi kinachoendelea.
Harakaharaka nikafungua mlango wa upande wa pili, nikashuka kwa kasi na kubingirika mpaka chini ya ile teksi, nikatulia huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio kuliko kawaida. Nilimuona Raya akikimbia mpaka pale kwenye ile teksi, nikajikausha kimya.
“Kaka samahani, nimeelekezwa kuwa mgonjwa wangu yupo ndani ya hili gari, yuko wapi?” nilimsikia Raya akimuuliza yule dereva teksi huku akihema.
“Alikuwepo lakini ameshuka ameelekea kule kwenye wodi za wanaume,” yule dereva teksi alijibu kama nilivyomuelekeza. Nikasikia Raya akiguna akiwa ni kama haamini, mara nikaliona lile gari limekuja na kupaki palepale lilipokuwa limepaki mara ya kwanza, nikaiona miguu ya watu wakishuka na kusogea pale Raya alipokuwa amesimama akizungumza na dereva teksi.

Sunday, September 10, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 35


ILIPOISHIA:
Harakaharaka tukatoka na kuingia ndani ya teksi, safari ya kurudi hospitalini ikaanza huku muda wote Shamila akiwa na furaha ya ajabu, akawa ananimwagia mvua ya mabusu. Dakika kadhaa baadaye, tuliwasili hospitalini lakini mazingira ya pale yalinishtua mno, hofu kubwa ikaukumba moyo wangu tulipofika kwenye maegesho ya magari.
SASA ENDELEA...
Gari jeusi lililokuwa na vioo vya rangi nyeusi (tinted), Isuzu Bighorn lilikuwa limepaki kwenye maegesho hayo huku milango ya upande mmoja ikiwa wazi. Kumbukumbu zangu zilionesha kwamba hiyo haikuwa mara ya kwanza kuliona gari hilo machoni mwangu, nikawa najaribu kukumbuka ni wapi?
Shamila alimlipa dereva teksi na kutaka kushuka lakini nikamzuia, akabaki anashangaa. Niliendelea kulitazama lile gari na kwa makini, ghafla kengele ya hatari ikalia ndani ya kichwa changu baada ya kumuona mmoja kati ya watu waliokuwa ndani ya gari hilo.

Saturday, September 9, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 34


ILIPOISHIA:
Safari hii maneno hayakuwa mengi, tuliendelea kupasha miili yetu, tayari kwa ngwe ya pili ya pambano letu la kirafiki. Safari hii yeye ndiye aliyekuwa akiniongoza nini cha kufanya, nami nikawanafuatisha kwa utii mkubwa, haikuchukua muda, kipyenga kikalia kuashiria kuanza kwa ngwe ya pili, huku safari hii akionesha kupania kuwa nyota wa mchezo.
SASA ENDELEA…
Mikikimikiki iliendelea, kwa mud nilisahau kama nilikuwa mgonjwa ambaye haukuwa umepita muda mrefu tangu nizinduke kutoka kwenye usingizi wa kifo, wala usingeweza kuamini kwamba ndiye mimi ambaye nilifikishwa hospitalini kila mmoja akiamini kwamba siwezi kurejewa na fahamu zangu.
“Jamal! Jamaa..aa..al!” Shamila alipiga ukelele na kunikumbatia kwa nguvu kifuani kwangu kuonesha kwamba tayari alishasalimu amri, mapigo ya moyo wake yakawa yanamuenda mbio kuliko kawaida, huku kila kiungo cha mwili wake kikiwa kimelegea kama mlenda.
Akaangukia pembeni, na mimi nikaangukia upande mwingine, huku kijasho chembamba kikinitoka. Ni hapo ndipo nilipogundua kwamba kuna majimaji yalikuwa yakinitoka pale kwenye jeraha langu, nikahisi huenda ni jasho.

Friday, September 8, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 40


ILIPOISHIA:
Nilipokisogeza kibuyu hicho karibu na pua, nilikumbana na harufu kali kwelikweli, ikabidi nizibe pua, nikanywa huku nikiwa nimefumba macho. Kabla sijameza, nilisikia vitu vikinitembea mdomoni, nilipotazama vizuri kile kibuyu, pale kwenye mdomo wa kunywea, sikuyaamini macho yangu, nikataka kutema lakini tayari nilishachelewa, vitu vyote vilikimbilia tumboni vyenyewe.
SASA ENDELEA...
Pale kwenye sehemu ya kunywea, ndipo paliponipa picha kwamba nilichokunywa kilikuwa ni kitu gani. Minyoo mingi ya rangi mbalimbali, ilikuwa imechanganywa na maji machungu yenye harufu mbaya mno. Jambo lile, la kugundua kwamba nilikuwa nimekunywa minyoo, lilinifanya nisisimke sana, nilijaribu kujitapisha lakini ilikuwa sawa mna kazi bure.
Kwa jinsi minyoo yenyewe ilivyokuwa imechangamka, muda mfupi tu baadaye, nilisikia tumbo likianza kutibuka, hofu kubwa ikanitanda ndani ya moyo wangu. Sikujua nini itakuwa hatma yangu.
Yule babu alikichukuaa kibuyo na kukifunga, akakirudisha pale chini, nikamuona akichaguachagua na muda mfupi baadaye, alichukua kibuyu kingine lakini hiki kilikuwa kidogo kuliko kile cha awali. Akawatazama wale watu wengine waliokuwa wamekaa pembeni na kutulia kisha akawapa ishara fulani, nikaona wanaume wawili wakiinuka.
Wakatembea harakaharaka kusogea mpaka pale nilipokuwa nimekalishwa. Sikutaka kuyaamini macho yangu, ilibidi nijifikiche macho nikidhani labda nipo ndotoni.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 33


ILIPOISHIA:
“Nakuapia kama ningekutana na wewe kabla ya Raya, huenda wewe ndiyo ungekuwa mpenzi wangu na si ajabu ningeshakuwa nimekuoa, naogopa kukueleza ukweli wa moyo wangu kwa sababu mtu mwenyewe unakuwa mkali kwangu,” nilizidi kumseti kwa maneno matamu, akashindwa kujizuia na kuniinamia pale kitandani, akanibusu kwa hisia za hali ya juu na kunikumbatia bila kujali kwamba anaweza kunitonesha tena jeraha langu la kifuani.
SASA ENDELEA...
“Hata mimi nakupenda sana Jamal lakini nilikuwa nashindwa namna ya kukufikishia ujumbe, ahsante kwa kuzielewa hisia zangu,” alisema Shamila huku akiwa amenikumbatia, akaendelea kunibusu sehemu mbalimbali za mwili wangu.
Niliona jinsi kitendo changu cha kuingiza masuala ya mapenzi kilivyomfurahisha, tukaendelea kupiga stori mbalimbali huku mara kwa mara akinikumbatia na kunibusu, na mimi nikawa nazidi kumsifia kwani miongoni mwa ‘maradhi’ ya wanawake, ni kupenda kusifiwa! Dalili za kutimia kwa nilichokuwa nakitaka zikaanza kuonekana waziwazi.
Hatukuwa nesi na mgonjwa kama ilivyokuwa awali, sasa tukawa zaidi ya hapo, nikamuona Shamila akizidi kuninyenyekea, kunipa huduma bora zaidi na muda mwingi akiwa pembeni ya kitanda changu.

Thursday, September 7, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 32


ILIPOISHIA:
Nilipomtazama usoni, macho yake yalikuwa mekundu na yamevimba kuonesha kwamba alikuwa amelia kwa muda mrefu, hata ule uchangamfu wake haukuwepo tena. Macho yake yakatua kwenye fulana niliyokuwa nimevaa, akanikazia macho.
SASA ENDELEA...
“Umebadilisha nguo saa ngapi? Na hiyo fulana umeipata wapi mbona inanukia pafyumu ya kike?” alinihoji Raya uso akiwa ameukunja, nikashusha pumzi ndefu na kumtazama usoni, huku nikiuvaa ujasiri wa kiume.
“Yaani hiyo ndiyo salamu? Ama kweli mapenzi yamepungua, kwa hiyo hata nikifa huwezi kujali tena?” ilibidi nimgeuzie kibao Raya. Moyoni nilikuwa najua kwamba nakosea lakini ilikuwa ni lazima nifanye hivyo ili kutuliza hali ya mambo.
“Wewe ndiyo wa kunitamkia mimi maneno hayo? Nikupende vipi Jamal, kwa nini unautesa moyo wangu?” alisema Raya na kuanza kuangua kilio. Kauli yangu ni kama ilikuwa imeenda kutonesha donda ndani ya nafsi yake.
Nilijisikia vibaya lakini ikabidi niendelee ‘kumkazia’, nikamwambia wakati anaondoka kwa kususa, nilikuwa nikimfuata lakini kwa bahati mbaya nikaanguka na kusababisha jeraha langu lifumuke na kuanza kumwaga damu.
“Huoni kwamba nimefungwa plasta na bandeji upya? Kama huamini muulize yule nesi, amenisaidia sana, huenda sasa hivi ungekuja na kukuta stori nyingine,” nilimwambia Raya, kauli ambayo ilionesha kumshtua mno.

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 31


ILIPOISHIA:
Alionesha kama kuna jambo muhimu anataka kuniambia kuhusu Shenaiza na baba yake ingawa sikujua ni jambo gani.
“Ha..pa...na! Hapana!” nilijibu kwa kubabaika huku nikiwa makini kutaka kusikia ataniambia nini.
SASA ENDELEA...
“Kuwa makini, baba yake siyo mtu mzuri,” alisema nesi huyo ambaye baadaye nilikuja kugundua kwamba anaitwa Shamila.
“Unamaanisha nini?” nilimuuliza kwa sauti ya chini, akanisogelea zaidi na kukaa pembeni ya kitanda changu.
“Kuwa tu makini, nakupenda na sitaki jambo lolote baya likutokee,” alisema huku akinitazama kwa macho yake mazuri, macho yetu yakagongana. Tulitazamana kwa sekunde kadhaa, akakwepesha macho yake huku aibu za kikekike zikiwa zimetawala uso wake.
“Ahsante kwa kunisaidia kunifunga upya jeraha langu,” nilimwambia tena, nikamuona akitabasamu kisha akanishika mkono wangu.
“Usijali, hiyo ni kazi yangu ila inabidi uijali afya yako. Hata kama angekuwa ni mgonjwa mwingine, ningemsaidia kama nilivyokusaidia wewe.”
“Ahsante pia kwa fulana uliyonipa, ni nzuri na inanukia vizuri,” nilimwambia kwa sauti ya chini, akatabasamu tena na kuniambia:

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 39


ILIPOISHIA:
Nilifungua zipu kisha nikaanza kufanya kama vile nilivyoelekezwa. Nikiwa naendelea na kitendo kile cha aibu na cha aina yake, nilisikia watu wote waliokuwa sebuleni wakishtuka, nadhani waliniona nilichokuwa nakifanya, sikuwajali, nikaendelea kuumwaga, mara kilisikika kishindo kikubwa ambacho kilinifanya nishindwe kuendelea kufumba macho, nikayafumbua.
“Mungu wangu!” nilisema kwa sauti ya juu.
SASA ENDELEA...
Kile kilichokuwa kikinitoka, hakikuwa haja ndogo kama mwenyewe nilivyokuwa nadhani, ilikuwa ni damu, tena nzito kabisa yenye wekundu uliokolea kisawasawa, na kile kishindo kilichosikika, kilikuwa ni cha dude kubwa lililoanguka kutoka angani.
Sijui niliiteje dude hilo kwa sababu kwanza lilikuwa na miiba kama nungunungu, lakini pia lilikuwa na mabawa yenye kucha kama popo, ukubwa wake ulikuwa kama ng’ombe mdogo.
Usoni lilikuwa na pembe zilizojikunja na sehemu ya macho, kulikuwa kumezibwa kabisa, kwa kifupi halikuwa na macho. Ile damu iliendelea kunitoka, hata pale nilipotaka kuikata haja ndogo, iliendelea kunitoka kwa wingi utafikiri inavutwa na bomba.
Lile dude la ajabu, lilijiburuta chini na kusogea mpaka pale nilipokuwa natolea haja ndogo, kwenye vizingiti vya milango, likafumbua mdomo kidogo na kutoa ulimi mrefu uliokuwa umegawanyika katikati kama wa nyoka, likaanza kulamba kile nilichokuwa nakitoa.

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 38


ILIPOISHIA:
“Wewe sasa hivi una mambo ya kikubwa, hutakiwi kuwa unachanganyikana na wenzako, inabidi uanze kukaa na sisi baba zako, vuta kiti kaa hapa,” alisema baba, akawa ametibua shoo nzima, nilitaka kutoa visingizio lakini hakutaka kusikia chochote kutoka kwangu, ikabidi nikae na kujiinamia, wote wakawa wananitazama.
SASA ENDELEA...
“Una matatizo gani?” baba aliniuliza baada ya kuniona nikiwa nimekaa huku uso wangu nikiwa nimeukunja.
“Unajua hata sisi wote unaotuona hapa, kuna kipindi tulikuwa kama wewe, sote tulikuwa vijana hapa na tulipitia yote unayoyapitia, kwa hiyo usitake kujifanya mjanja, umenisikia?” baba alisema kwa msisitizo.
“Na nyie mlipitia mauzauza kama yangu? Kwa nini kila siku huniambii ukweli mimi ni nani?” kwa mara ya kwanza nilimpandishia baba sauti mbele ya baba yake Rahma, nikaona wameacha kucheza karata, wakawa wanatazamana kisha wote wakanigeukia.
“Sisi ni baba zako, hutakiwi kuzungumza kwa namna hiyo, umesikia mwanangu,” alisema baba yake Rahma huku akinipigapiga begani. Tofauti kati ya baba na baba yake Rahma, yeye alikuwa na busara na mpole lakini baba yeye alizoea kufokafoka tu.
“Hapana mimi nimechoka, kila siku nikimuuliza baba aniambie ukweli hataki, mauzauza yanazidi kunitokea kila siku, mambo ya ajabu yananikumba mimi tu, mbona ndugu zangu hakuna anayepata shida kama mimi,” nilisema kwa uchungu huku machozi yakianza kunilengalenga.

Tuesday, September 5, 2017

Simulizi ya Nilimuua Nimpendaye Audio- Part 3

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 30


ILIPOISHIA:
“Ukikamilisha kazi nitakupa zawadi ya ushindi,” alisema Shenaiza huku akinifinyia kijicho kimoja, nilishaelewa alimaanisha nini. Nikasimama na kumshukuru, nikambusu kwenye paji la uso wake na kugeuka nyuma ili nirudi kule wodini kwangu.
SASA ENDELEA...
Sijui Raya alikuwa amefika muda gani eneo hilo kwani nilipogeuka tu, macho yangu na yake yaligongana, japokuwa alikuwa umbali wa mita kadhaa, niliweza kuona hali aliyokuwa nayo. Ilionesha hata kitendo cha mimi kumbusu Shenaiza alikiona kwa macho yake, nikamuona akianza kububujikwa na machozi.
Nilijikuta mwili wangu ukipigwa na ganzi, nikabaki nimesimama nikihisi hata miguu ilikuwa mizito kuinyanyua. Raya alipoona nimemuona, aligeuka na kuanza kutembea harakaharaka huku akiendelea kulia. Niljihisi kuwa na hatia kubwa sana ndani ya moyo wangu.
Japokuwa mimi na Shenaiza hatukuwa tumebusiana kwa nia mbaya, nilijaribu kujiweka kwenye nafasi ya Raya na kuhisi maumivu ambayo alikuwa anayahisi kwa wakati huo. Kwa wale ambao wamewahi kupitia maumivu ya mapenzi watakuwa wanaelewa vizuri ninachomaanisha!
Ukimpenda mtu halafu ukasikia au ukahisi mtu mwingine pia anampenda, ukiwaona pamoja lazima moyo uume sana, na hapo ni ukiwaona kawaida tu, iwe wameongozana barabarani au wamekaa sehemu! Raya alishajua kwamba kuna kitu kipo kati yangu na Shenaiza na kama hakipo basi kinakuja lakini kibaya zaidi, alikuwa amenifuma laivu nikimbusu msichana huyo!
Uso wangu ulinishuka kwa haya, sikujua nitatumia maneno gani kumlainisha Raya, nikawa nazidi kuongeza mwendo kumfuata lakini ghafla nikahisi kitu kikinipasua pale kwenye jeraha langu kifuani ambalo japokuwa nilikuwa na nafuu kubwa, bado halikuwa limepona kabisa.

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 37


ILIPOISHIA:
Nilitazama huku na kule, nilipoona hakuna mtu anayetutazama, nilimsogelea, akanikumbatia kwa mahaba kisha akanivutia ndani. Hatukukumbuka hata kufunga mlango, kwa makusudi aliuachia ule upande wa khanga, ukadondoka chini, nikawa kama fisi aliyeona mfupa.
SASA ENDELEA...
Harakaharaka nilichojoa magwanda yangu huku nikiwa na pupa isiyo na mfano, muda mfupi baadaye tulikuwa saresare maua, nikamnyanyua Rahma juujuu na kumbwaga kwenye uwanja wa fundi seremala. Mwenyewe alionesha kufurahia sana, akanibana kwenye kifua chake kilichojaa vizuri, tukagusanisha ndimi zetu.
Hata hivyo, tofauti na mara zote ninapokuwa kwenye mazingira kama hayo, ambapo ‘Togo’ wangu huwa mkali kama nyoka koboko, nilishangaa akiwa kimya kabisa, kama hajui ni nini kilichokuwa kinataka kutokea.
Kama nilivyoeleza tangu mwanzo, sikuwa najua chochote kwenye ulimwengu wa kikubwa na Rahma ndiye aliyekuwa wa kwanza kuniingiza kwenye ulimwengu huo, akifuatiwa na Isri, tena ndani ya siku chache tu. Kwa hiyo, sikuwa mzoefu na hicho kilichotokea, kilikuwa kitu kigeni kabisa kwangu.
Nimewahi kusikia kwamba, kwa mwanaume, hakuna aibu kubwa kama kuwa na mwanamke faragha halafu ukashindwa kazi, nikajikuta nikiwa na wasiwasi mkubwa kweli ndani ya moyo wangu. Sikujua Rahma atanichukuliaje, sikujua atanidharau kwa kiasi gani, nikajikuta kijasho chembamba kikinitoka huku akili ikiwa imehama kabisa.
“Togo, vipi?” aliniuliza Rahma baada ya kubaini mabadiliko niliyokuwa nayo. Swali lake lilinifanya nizidi kujisikia aibu, nilikosa cha kujibu na kiukweli sikuwa na majibu. Alipeleka mkono bondeni yaliko makazi ya ‘Togo’ na kujaribu kumpa hamasa kwa kutumia mikono yake laini lakini ilikuwa sawa na kazi bure.
“Mshukuru sana Mungu wako, ulikuwa unaenda kumuua mtoto wa watu, mshenzi sana wewe,” nilisikia sauti ya baba ikiniongelea sikioni kwa ukali, ikafuatiwa na msonyo mrefu, nikakurupuka kwa hofu kubwa, nikawa namtazama Rahma nikiwa nimekodoa macho, kijasho chembamba kikinitoka.

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 36


ILIPOISHIA:
“Naam baba,” niliitikia huku nikijaribu kumtoa Rahma maana alikuwa amenishika kimahaba, baba akaja mbiombio na kunishika mkono, akamwambia Rahma kuna kazi hatujamaliza kwa hiyo anisubiri, alinishika mkono na kuanza kunivuta kuelekea nje lakini tulipofika kwenye kingo za mlango tu, jambo la ajabu lilitokea.
SASA ENDELEA...
Kishindo kikubwa kilisikika, nikamuona baba akianza kuyumbayumba kama amelewa, na mimi nikaanza kusikia kizunguzungu kikali huku damu zikianza kututoka wote, mdomoni na puani. Muda huo tulikuwa tumeshavuka kizingiti cha mlango.
Sijui nilipata wapi ujasiri kwani ni muda huo ndipo nilipogundua kwamba kuna kosa nilikuwa nimelifanya, Isri aliniambia kwamba nisitoke nje mpaka giza litakapoingia, jambo ambalo nililikiuka kwa hiyo ili kurekebisha makosa, nilimvuta baba kwa nguvu, wote tukaangukia upande wa ndani wa mlango.
Kilisikika kishindo kingine kisha baba akawa ni kama amezinduka kutoka kwenye usingizi mzito.
“Nini kimetokea?” baba aliniuliza huku na yeye akiwa ni kama amepigwa na butwaa, akainua shingo na kutazama huku na kule, nikamuona akishtuka zaidi baada ya kuona damu zinamtoka mdomoni na puani pale chini.
“Hata mimi sijui,” nilimjibu huku nikisimama, na yeye akasimama kisha akawa anajifuta damu huku akitazama vizuri pale mlangoni. Aliangalia kwa sekunde kadhaa kisha akanigeukia na kunitolea macho ya ukali.
“Umeweka nini hapa?” aliniuliza kwa ukali.
“Hakuna kitu.”

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 35



ILIPOISHIA:
NIKIWA bado hata sijui nini cha kufanya, nilishtukia nikifungwa mikono na miguu, nikajaribu kukurupuka lakini sikuweza kufanya chochote, ikabidi nitulie na kuanza kumtazama ni nani aliyenifanyia kitendo hicho na alikuwa na lengo gani kwangu maana niliona kifo changu kikiwa kimewadia. Na hata kama ningeuawa, kila mtu angeamini aliyekufa ni mbwa mkubwa.

SASA ENDELEA...
“MIMI sipendi mtu mkaidi, siku nyingine nitakuacha uwe mbwa koko, unafikiri unaweza kunikimbia mimi?” alikuwa ni Isri, akiwa anahema huku jasho likimvuja kwa wingi. Nilitaka nimuombe msamaha lakini sauti haikutoka, nikawa naendelea kutokwa na machozi kwa wingi.
Aliniinamia pale chini, akanionyesha ishara nifumbue mdomo, nikafanya hivyo, akaingiza mkono mfukoni na kutoa kichupa kilichokuwa na maji, akayamimina yote mdomoni mwangu. Yalikuwa machungu sana lakini nilivumilia, akanionyesha ishara kwamba niyameze.
Nilifanya hivyo, nikahisi kama mwili wangu wote unawaka moto kwa maumivu lakini kufumba na kufumbua, nilijikuta nikibadilika na kurudi kwenye hali yangu ya kawaida. Alinifungua ile kamba ya shingoni kisha mikononi na miguuni, akaniambia nisimame lakini nilishindwa kufanya hivyo kwani sikuwa na nguo hata moja mwilini, akafungua kimfuko alichobeba mgongoni na kunirushia nguo zangu.

Sunday, September 3, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 29


ILIPOISHIA:
“Kuna kazi nimepewa ya kuhakikisha namzuia baba yake Shenaiza hicho anachokifanya, na ni lazima nitimize.”
“Kazi? Nani aliyekupa hiyo kazi? Halafu umzuie kwani anafanya nini na wewe umejuaje?” Raya alinibana kwa maswali, nikawa nashindwa hata namna ya kumjibu.
SASA ENDELEA...
“Si naongea na wewe Jamal!”
“Aah! Unajua ni stori ndefu kidogo na... na... ni...” nilijikuta nikishikwa na kigugumizi, Raya alikuwa akinitazama huku amenikazia macho. Nadhani kuna mambo alianza kuhisi kama hayaendi sawa.
Nilichokifanya ilikuwa ni kumzugazuga na kubadilisha mada, nikamhakikishia kwamba nitakapokaa na kutulia nitamueleza kwa kirefu kila kitu kilichokuwa kinaendelea. Bado Raya alionesha kutoridhishwa na maelezo yangu na kikubwa kilichokuwa kikimsumbua ilikuwa ni wivu.
Kwa sababu kihistoria alishajenga mawazo akilini mwake kwamba mimi simpendi isipokuwa yeye ndiyo analazimisha mapenzi, alikuwa akiteseka sana ndani ya moyo wake akiamini kwamba akitokea mwanamke ambaye nitampenda, kama alivyokuwa akihisi kwa Shenaiza, nitamuacha jumla, jambo ambalo hakuwa tayari kuona linatokea.
“Halafu kuna mambo yananichanganya sana kichwa changu, sijui ni ndoto, maruweruwe au uchawi hata sielewi. Mbona nakumbuka kama mimi na wewe kuna sehemu tulikutana halafu tukaongea mambo mengi tu? Na kubwa zaidi mbona nakumbuka kama na mimi nilikufa?” kauli aliyoitoa Shenaiza muda mfupi uliopita ilijirudia ndani ya kichwa changu, nikawa natazama juu darini nikitafuta majibu ya maswali yangu.
Alichokisema Shenaiza ndicho kilichokuwa ndani ya akili yangu, ni kweli mimi na yeye kuna sehemu tulikutana na tukaongea mambo mengi tu, akanieleza kwamba ameamua kujiua kwa kujiovadozi madawa ya kulevya, akanihakikishia na mimi kwamba nilikuwa nimekufa lakini nikawa nambishia.

Saturday, September 2, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 28


ILIPOISHIA:
Niliendelea kumkumbatia msichana huyo huku marafiki na jamaa zangu wengine wakiwa pembeni wakitutazama, tukiwa kwenye hali hiyo, nilisikia mlango wa wodi ukifunguliwa na mtu akaingia mbiombio mpaka pale kitandani kwangu, nikashtuka na kumuachia Raya, Raya naye akainua uso wake, watu wote tukawa tunamtazama kwa mshangao mtu yule aliyeingia, tukiwa ni kama hatuamini.
SASA ENDELEA...
Hakuwa mwingine, bali Shenaiza ambaye alikuwa amevaamavazi ya hospitalini hapo kuonesha kwamba alikuwa amelazwa, mkononi akiwa na sindano iliyofungwa na plasta, nafikiri kwa ajili ya kumuingizia dawa au kumtundikia dripu, nikawa namtazama usoni, naye akawa ananitazama.
“Jama! Kumbe ni kweli hujafa?” alisema Shenaiza kwa sauti ya kukwamakwama, wote tukatazamana tena kisha nikageuka na kumtazama Shenaiza, alionesha kabisa kwamba hakuwa sawa, nikawa najiuliza maswali mengi kichwani ambayo sikuwa na majibu yake.
Nilikumbuka kwamba kuna muda mimi na Shenaiza tulikuwa tumnekaa siti moja kwenye treni la ajabu, tukielekea kusikojulikana, giza likiwa limetanda kila sehemu. Kama mimi nilikuwa kitandani, wodini, na Shenaiza naye alikuwa hospitalini hapo akiwa amelazwa, ina maana kwamba mimi na yeye tulikutana wapi?
Nilikumbuka pia kwamba yeye mwenyewe aliniambia kwamba ameamua kuyakatisha maisha yake kwa kujiovadozi dawa ya usingizi, na kwamba aliamua kufanya hivyo kama njia ya kupumzika na mateso aliyokuwa anayapata, sasa Shenaiza aliyejiua ni nani na huyo aliyekuwa amesimama mbele yangu ni nani?
Nilihisi kama kichwa kinapata moto kwa sababu ya utata wa kilichokuwa kinaendelea, hata hivyo nilipoemndelea kutuliza kichwa changu, nilianza kupata baadhi ya majibu.
“Kumbe kweli hukufa?” Shenaiza aliniuliza tena swali lile ambalo lilinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.

Friday, September 1, 2017

Seven Days in Hell (Siku Saba Kuzimu)- 27



ILIPOISHIA:
Nilipokuja kushtuka, nilijikuta nikiwa nimelala kitandani, mapigo yangu ya moyo yakinienda mbio kuliko kawaida, nikiwa nimeunganishwa mashine ya kunisaidia kupumua huku mwili wangu ukiwa umeunganishwa na vifaa vingi vya kitabibu, milio ya mashine mbalimbali ikisikika ndani ya chumba kile ambacho hata bila kuuliza, niligundua kwamba ni wodini.
“Amefumbua macho! Dokta... amefumbua macho! Njooni haraka!”
SASA ENDELEA...
Harakaharaka madaktari wengi waliingia ndani ya kile chumba na kuzunguka kitanda changu, kwa mbali nikawa nawatazama mmoja baada ya mwingine, wote wakionekana kukiinamia kitanda changu. Macho yangu yalikuwa na ukungu, hali iliyonifanya nisiwe na uangavu wa kutosha machoni kuwaona ingawa bado nilikuwa na uwezo wa kutambua sura zao.
“Unaendeleaje Jamal?” nilisikia daktari mmoja akiniuliza. Kwa jinsi sauti yake ilivyokuwa ikisikika, ilikuwa mithili ya inayotoka kwenye redio mbovu. Nilijaribu kufumbua mdomo lakini nilishindwa kwani nilikuwa nimeunganishwa na mabomba mengi, mdomoni na puani, nikawa natingisha tu kichwa kuashiria kwamba najisikia vizuri.
Jopo la madaktari waliendelea kunizunguka pale, nikamuona mwingine akinipima kwa kutumia kifaa maalum kusikiliza mapigo ya moyo wangu, mwingine akaniweka ‘thermometer’ kwapani kwa lengo la kunipima joto huku mwingine akiwa bize kufuatilia maandishi yaliyokuwa yanaonekana kwenye mashine inayofanana na kompyuta, iliyokuwa ikipiga kelele kwa kutoa milio ya ‘kubipu’ kila mara.
“He is recovering! His heartbeats are stabilizing, blood sugar is coming to normal and the wound is healing!” alisema daktari mmoja wakati akiwaambia wenzake, kwa kuwa Kiingereza hakikuwa kikinipiga chenga, niliweza kuelewa vizuri kwamba alikuwa akiwaambia wenzake kwamba nimeanza kupata nafuu, mapigo yangu ya moyo yanaimarika, kiwango cha sukari kinarudi kwenye hali ya kawaida na jeraha langu linapona.

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...