ILIPOISHIA:
Ni kweli nilikuwa na marafiki wengi
wanaonipenda kule nyumbani Chunya lakini sikuwa tayari hata kidogo kuona mtu
yeyote asiye na hatia anapatwa na matatizo kwa sababu yangu. Nilijikuta
nikijilaumu sana kwa upumbavu wangu wa kutaka kwenda kujionea mwenyewe
kilichotokea kule Mlandizi.
“Tunasubiri jibu lako,” baba alinizindua
kutoka kwenye lindi la mawazo.
SASA ENDELEA...
“Lakini baba...”
“Lakini nini? Hakuna mjadala,
kinachotakiwa hapa ni utekelezaji tu,” alisema baba na kunitishia kwamba endapo
sitatoa majibu, kwa kuwa yeye anawafahamu marafiki zangu, atapendekeza jina
lolote.
Kwa mara nyingine nilikuwa nimeingia kwenye
mtego hatari wa kutaka kupoteza maisha ya mtu asiye na hatia kwa sababu ya
uzembe wangu. Nilijisikia vibaya sana, nikashindwa kuzuia machozi
yasiulowanishe uso wangu.
“Hata sisi mwanzo tulikuwa kama wewe,
utazoea tu,” alisema baba yake Rahma. Sikujua ni nini hasa kilichotokea kwenye
akili za baba na baba yake Rahma mpaka wachukulie kitendo cha kukatisha maisha
ya mtu asiye na hatia kuwa cha kawaida kiasi kile.
Baada ya kulumbana kwa muda mrefu,
baadaye niliamua kusalimu amri, nikamtaja rafiki yangu kipenzi, Sadoki.
Kilichosababisha nikamchagua Sadoki, ni kwa sababu dakika za mwisho, urafiki
wetu ulikuwa umeingia dosari baada ya siku moja kumkuta akishirikiana na watu
wengine kumteta baba yangu kwamba alikuwa mchawi.
Kwa kipindi hicho, nilikuwa bado sijajua
ukweli kwamba baba ni mchawi au mganga kwa sababu mara zote nilizokuwa
namuuliza alikuwa akisema kwamba yeye ni mganga na wala si kweli kwamba
anajihusisha na mambo ya kishirikina kwa hiyo yeyote niliyemsikia akizungumza
mabaya ya baba, alikuwa akigeuka na kuwa adui yangu.
Siku nyingi zilikuwa zimepita tangu siku
tulipotaka ‘kuzichapa’ maana baada ya kumkuta akimsema vibaya baba, nilimjia
juu sana, kama isingekuwa watu wazima waliokuwa jirani nasi, huenda tungepigana
na kuumizana sana.
Hata hivyo, tukio hilo moja halikuharibu
ukweli kwamba tulikuwa marafiki wakubwa kwa sababu nakumbuka mara kwa mara
alikuwa akija kwetu, na mimi nilikuwa nikienda kwao. Kwa kifupi ni kwamba
ukiachilia mbali hiyo dosari ndogo iliyotokea, tulikuwa tumeshibana kisawasawa.
Baada ya kumtaja jina, sikuweza
kuendelea kukaa mle chumbani, nilitoka na kwenda bafuni huku nikichechemea,
nikajifungia na kuanza kulia kwa uchungu, baba na baba yake Rahma wakabaki
chumbani kwangu wakiendelea kujadiliana mambo yao. Nililia mpaka macho yakawa
mekundu kabisa, nilimuonea huruma Sadoki, nilimuonea huruma mama yake na wadogo
zake.
Walikuwa wakimtegemea kwa sababu baba yao
alifariki wakiwa bado wadogo kwa hiyo baada tu ya kumaliza shule ya msingi,
Sadoki alikuwa akienda kufanya vibarua kwenye machimbo ya dhahabu na fedha
kidogo alizokuwa akizipata ndizo zilizokuwa zikiihudumia familia yao.
Nikiwa bado naendelea kulia kule bafuni,
baba alikuja kunigongea, ikabidi ninawe uso harakaharaka, nikatoka huku uso
wangu nikiwa nimeuinamisha. Tulirudi chumbani kisha akaanza kunipa maelekezo
kwamba usiku wa siku hiyo tunatakiwa kusafiri kuelekea Chunya.
“Tukifika, inabidi twende mpaka nyumbani
kwa huyo rafiki yako, kuna dawa utaitega mlangoni, asubuhi akiwa anatoka
anatakiwa airuke, akishairuka tu kazi itakuwa imekwisha.
“Sasa tutaendaje Chunya na kufanya hivyo
unavyosema kabla hakujapambazuka?” niliuliza kwa sababu kama ni mabasi, muda
huo tusingeweza kupata la kwenda Mbeya na hata kama lingepatikana, tusingewahi
kama baba alivyokuwa anasema.
“Hutakiwi kuhoji sana, sikiliza kwa
makini ninachokueleza,” baba alinikatisha, akaendelea kunipa maelezo ya namna
ya kukamilisha zoezi hilo ambayo kwangu yalikuwa yakiingilia sikio la kushoto
na kutokea la kulia.
Sikuona sababu yoyote ya kumuadhibu
Sadoki kwa makosa ambayo nilikuwa nimeyafanya mwenyewe, nikajikuta nikijihisi
hatia kubwa mno ndani ya moyo wangu. Basi tuliendelea kuzungumza pale, kisha
baba akaniambia nijiandae kwa safari.
Walitoka na kuniacha nimejilaza
kitandani, machozi yakaanza kunitoka tena na kwa sababu nilikuwa nimejilaza kwa
kutazama juu, yalikuwa yakichuruzika kupitia kona za macho yangu mpaka kichwani
na kupotelea kwenye shuka lililokuwa limetandikwa pale kitandani.
“Hivi ndiyo nimeshakuwa mchawi?”
nilijiuliza swali kama mwendawazimu. Ni mimi ndiye niliyekuwa na shauku kubwa
ya kuwa na nguvu zile za ajabu lakini sijui ni kutoelewa au ni kitu gani, ndani
ya muda mfupi tu nilishaanza kuhisi kwamba pengine nimebeba mzigo mzito ambao
sina uwezo nao. Zile kauli za baba akinikebehi kwamba bado nina akili za kitoto
zikawa zinajirudia ndani ya kichwa changu.
Niliendelea kutafakari kwa kina na
baadaye usingizi mzito ulinipitia, nikiwa usingizini nilianza kuota ndoto za
ajabuajabu na kusababisha niwe nashtuka mara kwa mara. Baadaye ndoto hizo
zisizoeleweka zilikoma, nikalala mpaka majira ya saa mbili za usiku nilipokuja
kuzinduliwa na sauti ya baba aliyekuwa akiniita, nikakurupuka na kuamka.
“Umeshajiandaa?”
“Ndiyo,” nilimjibu huku nikijifikicha
macho na kujinyoosha. Ukweli ni kwamba sikuwa nimejiandaa chochote.
“Haya nifuate.”
“Lakini bado sijala.”
“Utaenda kula mbele ya safari,” alisema
baba huku akinihimiza nisimame. Nilishuka kitandani, miguu ikawa inauma sana
hasa kwenye nyayo kutokana na majeraha ya ile miiba niliyotolewa na Rahma.
Ilibidi nijikaze kisabuni kwa sababu ni mambo ambayo nilijitakia.
Tulitoka mpaka nje bila kuonekana na mtu
yeyote, tukamkuta baba yake Rahma amesimama mlangoni, akionesha kwamba alikuwa
akitusubiri. Alinipa kofia kubwa na kuniambia niivae, sikumuelewa kwa sababu
gani amefanya vile. Tulitoka, mimi nikiwa katikati na kwenda hadi pale kwenye
maegesho ya Bajaj, tukaingia kwenye mojawapo na baba yake Rahma akampa
maelekezo dereva kwamba atupeleke Mwenge.
Sikuwa napajua Mwenge zaidi ya kupasikia
tu, ni hapo ndipo nilipoelewa kwa nini baba yake Rahma alinipa ile kofia kwa
sababu japokuwa nilikuwa nimeivaa, na kuziba sehemu kubwa ya uso wake, wale
madereva Bajaj walikuwa wakinitazama kama wanaotaka kuhakikisha kama ni mimi
kweli au laah!
Sikuwajali zaidi ya kuwadharau kwa
sababu sasa nilikuwa na uwezo wa kumfanya mtu yeyote ninavyotaka mimi. Bajaj
ilianza kukata mitaa na baada ya muda, tuliingia kwenye barabara ya lami
iliyokuwa na magari mengi.
Safari ikaendelea mpaka tulipofika
mahali kwenye mataa yenye mwanga mkali ambayo licha ya kwamba ilikuwa ni usiku,
yalikuwa yakiangaza sehemu yote, watu wakiendelea na shughuli zao utafikiri ni
mchana.
Tulishuka kwenye Bajaj huku nikishangaa
huku na kule, moyoni nikawa najisemea ‘mjini kuzuri sana’. Tukaanza kuvuka
barabara mbili pana ambazo katikati zimetenganishwa na bustani ya maua.
Kiukweli kama ningekuwa peke yangu,
nisingeweza kuvuka kwa sababu kulikuwa na magari mengi mno, nikawa
naung’ang’ania mkono wa baba Rahma maana baba naye alionesha kuwa na mchecheto.
Tulivuka salama mpaka upande wa pili
ambako tulipanda magari mengine yanayoelekea Kunduchi. Kila kitu kilikuwa
kigeni kwangu, safari ikaanza mpaka tulipofika Kunduchi, tukashuka kwenye gari
na kuanza kutembea kwa miguu. Sikuwa najua tunaelekea wapi, baada ya muda
tukatokezea kwenye makaburi yaliyokuwa karibu na bahari.
“Haya ni makaburi ya Wagiriki, ni ya
zamani sana na hapa ndiyo hutumika kama njia ya kuingia na kutoka kwenda sehemu
yoyote,” baba yake Rahma alinielekeza kwa sauti ya upole, tukaingia mpaka
katikati kabisa ya makaburi hayo, mahali palipokuwa na mti mkubwa wa mbuyu.
“Tunaenda Chunya, hutakiwi kwenda
kinyume na maelekezo tunayokupa, ukifanya uzembe tu, kitakachokutokea ni juu
yako,” alisema baba kwa sauti ya msisitizo, nikawa natingisha kichwa
kukubaliana naye. Tulikaa chini na kuweka kama duara hivi, tukashikana mikono
kisha nikaambiwa nifumbe macho.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.