ILIPOISHIA:
Ilibidi
Raya abaki palepale hospitalini mpaka usiku ili iwe rahisi kufanya kazi yetu,
muda ukazidi kuyoyoma na hatimaye giza likaingia, ule muda tuliokuwa
tukiusubiri kwa hamu ukawa umewadia.
SASA
ENDELEA...
“Tunakusikiliza wewe Shamila!”
“Yaah! Inabidi mnisikilize kwa makini
vinginevyo hakuna kitakachofanikiwa.”
“Tunaanzia wapi?” nilimuuliza Shamila
huku mapigo ya moyo wangu yakinienda mbio.
“Tulia Jamal, mbona una haraka namna
hiyo,” alisema Shamila, nikashusha pumzi ndefu na kutulia, hakuna muda ambao
nilikuwa nahitaji msaada wake kama huo na kubwa zaidi, sikuwa mimi tu ambaye
nilikuwa nahitaji msaada wake, bali Shenaiza pia.
Shamila aliingia kwenye chumba cha
kubadilishia nguo, muda mfupi baadaye alitoka akiwa na gauni jingine, akampa Raya
na kumuelekeza kuingia kule ndani kwenda kubadilisha nguo. Kweli akatii
alichoambiwa, muda mfupi baadaye akatoka akiwa ndani ya mavazi ya kinesi,
usingeweza kumtambua kwamba hakuwa nesi.
“Sasa wewe kazi yako itakuwa ni kutoka
na mgonjwa mpaka nje, unaona hili faili lake, inatakiwa ulishike na kufuata
maelekezo ya nitakachokuwa nakwambia. Ukikosea tu basi hakuna
kitakachowezekana,” alisema Shamila wakati akimpa maelekezo Raya, akatingisha
kichwa kwa utiifu kuonesha kwamba alikuwa ameelewa alichokuwa ameambiwa.
“Inabidi pia njia ambayo itatumika
kukutoa wewe itumike pia kwa Shenaiza, tena kwa wakati mmoja kwa hiyo
tutaongozana wote, sijui kama mnanielewa,” alisema Shamila huku akiwa amevaa
uso wa ‘usiriaz’, wote tukaitikia kuonesha kwamba tulikuwa tumemuelewa.
“Mimi nitaenda kumchukua Shenaiza wakati
huo nyie mtakuwa mkinisubiri hapo chini, tutatoka pamoja mpaka pale getini,
mimi nitaongea na walinzi, wakituruhusu kutoka tu, Firyaal yupo nje anatusubiri
na gari la familia yao kwa hiyo hakutakuwa na muda wa kupoteza, tumeelewana?”
alisema Shamila ambaye aligeuka na kuwa mwalimu wa kutuelekeza, sisi kazi yetu
ikawa ni kuitikia tu.
“Nifuate,” alimwambia Raya huku
akinitaka na mimi nivae vizuri nguo maalum za wagonjwa.
“Kamanda, huyu mgonjwa inatakiwa
akafanyiwe kipimo cha MRI kesho sasa kwa sababu mashine ya hapa hospitalini ni
mbovu na kesho kutakuwa na foleni kubwa, tumeomba akafanyiwe kipimo hicho usiku
huu pale kwenye maabara za Lancert zilizopo nje ya hospitali,” Shamila
alimwambia mlinzi aliyekuwa nje ya wodi ile kwa sauti ya juu, japokuwa mimi
nilikuwa ndani niliweza kusikia kila kitu, nikatabasamu na kutikisa kichwa
kwani ama kwa hakika mbinu ya Shamila ilikuwa kali mno.
Muda mfupi baadaye, nilisikia mlango
ukifunguliwa, Shamila akatangulia kuingia, nyuma yake akafuatia Raya aliyekuwa
akisukuma kiti cha magurudumu (wheel chair) huku akionesha dhahiri jinsi
alivyokuwa na hofu kubwa moyoni mwake.
“Inatakiwa uchangamke, ukiwa unatetemeka
hivyo watatushtukia, muone kwanza,” Shamila alimshushua Raya kwa sauti ya chini,
nikanyamaza kimya kama sijasikia chochote. Wakasogeza ile wheel chair mpaka
pale pembeni ya kitanda changu, Shamila akaniambia anajua ninao uwezo wa
kutembea mwenyewe lakini ni lazima nikubali kusukumwa kwenye kiti cha
magurudumu ili isiwe rahisi kwa mtu yeyote kutushtukia.
Basi nikashuka kitandani na kukaa kwenye
kitanda cha magurudumu, Shamila akamuelekeza Raya namna ya kukisukuma na
akarudia kumsisitiza kwamba anatakiwa kuchangamka. Ilibidi vitu vyangu vingine
vyote niviache mlemle wodini, tukatoka mpaka kwenye korido, nikamuona yule
mlinzi akisimama na kutusaidia kubonyeza kitufe kwenye lifti.
Hakuwa na mawazo kabisa kwamba ndiyo
tunamtoka kiaina. Nikiri wazi kwamba hilo halikuwa zoezi langu la kwanza
kutoroka hospitalini kwa sababu tayari nilishamtorosha Shenaiza lakini hali
haikuwa tete kama ilivyokuwa muda huo, na kikubwa kilichokuwa kikinipa hofu
kubwa ndani ya moyo wangu ni kujua aina ya watu niliokuwa nadili nao; baba yake
Shenaiza na watu wake.
“Inawezekana kabisa kuna watu
wamepandikizwa hapa hospitalini na baba yake Shenaiza kufuatilia nyendo zako na
binti yake, kwa hiyo unatakiwa kujiinamia muda wote ili mtu yeyote asikuone
usoni, mtanisubiri nikamchukue Shenaiza,” alisema Shamila wakati tukiwa ndani
ya lifti tukishuka chini, tukamuitikia.
Tulishuka mpaka chini, akatuelekeza
kufuata korido mpaka mbele ambapo alisema tumsubiri, Raya akawa ananisukuma
taratibu, yeye akaelekea kwenye wodi ya wagonjwa wa akili alikokuwa amelazwa
Shenaiza.
“Im scared Jamal, I cant take it!”
(Naogopa Jamal, siwezi!)
“You need to do this my love, do it for
me!” (Unatakiwa kufanya mpenzi wangu, fanya kwa ajili yangu) Raya alinisemesha
kwa Kimombo si unajua tena yeye alikuwa akitoka familia bora? Nikawa naendelea
kumpa maneno ya kumtia nguvu, tukawa tunaendelea kutembea taratibu kwenye
korido huku Raya pia akiwa na faili langu.
“Hivi akitokea mlinzi hapa na kutuuliza
tunaenda wapi usiku huu tutajibu nini?”
“Tunaenda kufanyiwa kipimo cha MRI pale
nje kwenye maabara za Lancert kwa sababu mashine za humu ndani zimeharibika,”
nilijibu kwa kujiamini, nikaona hofu ikipungua ndani ya moyo wake.
“Maelezo haya inabidi wewe nesi ndiyo
uyatoe, sio mimi mgonjwa,” nilisema kwa msisitizo, Raya akawa ananiitikia
lakini jambo ambalo bado hakuweza kulidhibiti, ni hofu iliyokuwa ndani ya moyo
wake.
Tulifika mpaka pale Shenaiza
alipotuambia kwamba tumsubiri, tukasimama na kuanza kuangalia uelekeo wa wodi
ya wagonjwa wa akili alikokuwa ameelekea. Hata hivyo, hakutokea haraka kama
tulivyodhani, muda ukaanza kuyoyoma mara dakika tano zikakatika, kimya! Tano
nyingine zikakatika bila Shamila kurudi, tukaanza kuingiwa na hofu.
Pale tulipokuwa tumesimama, wauguzi na
ndugu za wagonjwa mbalimbali walikuwa wakitupita lakini hakuna aliyekuwa na
habari na sisi kwani walijua tupo kwenye taratibu za kawaida za tiba.
“Tunavyozidi kusimama hapa ndivyo
tunavyozidi kujiweka kwenye hatari zaidi, wanaweza kutushtukia.”
“Sasa tufanyeje?” nilimuuliza Raya
lakini kama bahati, kwa mbali tuliona mlango wa wodi ya wagonjwa wa akili
ukifunguliwa, Shamila akatoka akiwa anasukuma kitanda cha magurudumu kama kile
nilichokuwa nimekalia, wote tukashusha pumzi ndefu na kumshukuru Mungu kwani
tulishaanza kuchanganyikiwa.
Kwa mbali akatuonesha ishara kwamba
tuendelee kusonga mbele, naye akawa anakuja huku akikisukuma kile kitanda
ambacho hata bila kuuliza, niligundua kwamba aliyekuwa amekaa pale alikuwa ni
Shenaiza.
Akazidi kutukaribia na muda mfupi
baadaye, tayari alikuwa ametufikia, tukawa tunatembea bila yeyote kati yetu
kumsemesha mwenzake. Kwa watu ambao hawakuwa wakielewa kinachoendelea,
wangedhani kwamba ni manesi walikuwa wakiwapeleka wagonjwa wao kupata matibabu
ya kawaida.
Kwa mbinu ile ilikuwa vigumu sana kwa
mtu yeyote kutushtukia, tukazidi kusonga mbele huku nikijitahidi kuibia macho
pembeni na kumtazama Shenaiza ambaye alikuwa amekaa kwenye kiti cha magurudumu
akiwa haelewi chochote kilichokuwa kinaendelea.
Nguo maalum aliyofunikwa upande wa
kichwani, ilifanya iwe vigumu kwa mtu yeyote kumtambua, tukaendelea kusonga
mbele mpaka tulipofika kwenye geti la kutokea nje ya hospitali, hapo
tukakumbana na kipingamizi ambacho hakuna aliyekitegemea, mapigo ya moyo wangu
yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment