ILIPOISHIA:
Kauli yake hiyo ilitufurahisha sana mimi
na Shamila, tukawa na uhakika kwamba sasa kazi itakuwa nyepesi kwa sababu
tayari tutakuwa na mtu kutoka ndani kabisa, ambaye angetusaidia kutimiza lengo
letu la kupambana na mtu huyo hatari.
SASA ENDELEA...
“Kwa hiyo tunaanzia wapi?” nilimuuliza
Shamila, akawa ni kama anayetafakari kitu kisha akaniambia ameshapata majibu.
“Ngoja niende kwanza na huyu binti
nikampe hiyo hard disk yake,” alisema Shamila.
“Utaweza kuichomoa kwenye kompyuta?”
“Mimi naweza, nasomea Information
Technology niko mwaka wa pili,” alisema Firyaal ambaye alikuwa amefanana sana
na Shenaiza, yaani hata bila kuuliza ungemjua tu kwamba ni ndugu yake.
“Sijamaliza kukopi data ninazozihitaji
lakini.”
“Nitakusaidia pia, ninayo ‘back up’
kubwa tu nyumbani, naweza kuhamisha data zote na kukuletea,” alisema msichana
huyo, nikawa namtazama usoni kwani aliyokuwa akiyasema hayakuwa yakifanana na umri
wake.
Kwa kumtazama alionekana kama msichana
mdogo ambaye kwa makadirio ungeweza kudhani yupo kidato cha pili au cha tatu
lakini kumbe tayari alishafika kidato cha sita na sasa alikuwa chuoni.
“Nitashukuru sana ukinisaidia
dada’angu,” nilisema kwa sauti ya kiungwana, Firyaal akanitazama usoni, na mimi
nikamtazama, macho yetu yakagongana, harakaharaka akakwepesha macho yake huku
aibu za kikekike zikiwa zimemtawala.
“Basi usitoke kwenda sehemu yoyote, mimi
ngoja niende naye nyumbani,” alisema Shamila, akanisogelea pale kitandani na
kunibusu kisha harakaharaka akamshika mkono Firyaal na kuanza kutoka naye nje.
Walipofika mlangoni, nilimuona Firyaal
akigeuka na kunitazama, na mimi nikamtazama, macho yetu yakagongana kwa mara
nyingine. Tofauti na mwanzo, safari hii hakukwepesha macho yake, tukaendelea
kutazamana mpaka walipotoka nje. Sikuelewa sababu iliyofanya awe ananitazama
vile kwa sababu kimsingi hiyo haikuwa mara ya kwanza mimi na yeye kuonana.
Ilikuwa ni mara ya pili. Hata hivyo
sikutilia sana maanani, nikampotezea.
Nikashusha pumzi ndefu na kutulia
kitandani, mawazo mengi yakiendelea kupita ndani ya kichwa changu. Ni kweli
nilikuwa bado sijapona vizuri lakini ilikuwa ni lazima niondoke hospitalini
hapo kabla mambo hayajaharibika. Kutokana na sifa nilizokuwa nazisikia,
nilijikuta nikimuogopa mno baba yake Shenaiza kama malaika mtoa roho.
Niliendelea kutulia pale kitandani,
japokuwa Shamila aliniambia nisitoke, nilipata wazo la kwenda kwenye wodi
aliyokuwa amelazwa Shenaiza kwenda kuangalia anaendeleaje. Hata hivyo,
nilipomkumbuka yule mtu aliyekuwa akinitazama sana kwa makini mle ndani ya wodi
ya vichaa, nilijikuta nikipatwa na hofu moyoni, nikaghairi.
Kwa hesabu zangu za harakaharaka
ukichanganya na maelezo niliyoyapata kutoka kwa Shamila, nilikuwa nimekaa
hospitalini hapo kwa wiki mbili mfululizo, huku kati ya hizo, siku saba nikiwa
nimepoteza kabisa fahamu.
Nilijaribu kuvuta kumbukumbu ya mambo
yote yaliyotokea ndani ya kipindi hicho nilichokuwa hospitalini hapo, ungeweza
kudhani kama nimekaa hospitalini kwa kipindi cha mwaka mzima. Kila kitu
kilikuwa kikitokea kwa kasi kubwa mno kiasi cha kufanya hata akili yangu
isipate muda wa kupumzika.
Kitu ambacho kilinipa faraja kubwa ndani
ya moyo wangu, ni kuona jinsi wafanyakazi wenzangu pamoja na bosi wetu
walivyokuwa wakinijali. Japokuwa nilikuwa chini ya uangalizi maalum ambapo watu
hawakuwa wakiruhusiwa kuja mara kwa mara kunitazama, Raya alinihakikishia
kwamba katika zile siku nilizokuwa nimepoteza fahamu karibu kila siku watu
kutoka kazini walikuwa wakija kunitazama.
Baada ya kama dakika arobaini tangu
Shamila na yule mdogo wake Shenaiza waondoke, Raya alikuja tena. Kiukweli
japokuwa nilikuwa nikimuendea kinyume, Raya alikuwa akijitahidi sana kuwa
karibu na mimi.
Muda wote yeye alikuwa akinifikiria mimi
tu kiasi cha kumfanya kazini asiwe anaenda wala nyumbani kwao asiwe anatulia,
muda wote ilikuwa ni kiguu na njia, kuja hospitali na kurudi kwao.
“Vipi unaendeleaje mume wangu,” alisema
Raya kwa sauti ya chini, akionesha kuwa na mawazo lukuki ndani ya kichwa chake.
“Naendelea vizuri mke wangu, vipi mbona
nakuona kama mudi yako iko chini sana, nini kinakusumbua,” nilimwambia Raya kwa
upole, akajisogeza na kupitisha mkono wake mmoja shingoni kwangu, akanibusu
kwenye paji langu la uso na kuanza kuniambia kwamba tangu nilipomweleza ukweli
wa kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia, alikosa raha kabisa.
“Nahisi kama nitakupoteza mpenzi wangu
na mimi siwezi kuishi bila wewe, hata sijui itakuwaje,” alisema kwa huzuni,
nikashusha pumzi ndefu na kuanza kumtuliza. Nikamwambia asiwe na wasiwasi,
hakuna jambo lolote baya litakalotokea nakuhakikishia,” nilimwambia.
Kidogo kujiamini kwangu kulimfanya naye
aanze kuona kwamba kumbe halikuwa tatizo kubwa mbele yetu, nikamueleza pia juu
ya mipango ya kutoroka tuliyokuwa tumeipanga kwa ajili ya kumkimbia baba yake
Shenaiza. Nilimuona naye akiniunga mkono, nadhani hata yeye hakuwa na imani
kabisa juu ya usalama wangu hospitalini hapo.
Tulizungumza mambo mengi, Raya akawa
ananisisitiza kwamba yeye amejitoa kwa asilimia mia moja kunisaidia, isije
ikatokea kwamba nikamgeuka na kumuona hana maana tena. Kauli yake iliugusa sana
moyo wangu kwa sababu ni kweli Raya alikuwa amejitoa kwa kila kitu lakini kwa
bahati mbaya sana shetani alionekana kunizidi nguvu.
Nikawa namhakikishia kwamba asiwe na
wasiwasi lakini ukweli, sikuwa namaanisha kile nilichokuwa nakisema. Akaniambia
kwamba atashirikiana na Shamila kuhakikisha wananitorosha hospitalini hapo
usiku bila mtu yeyote kujua, swali likawa nikishatoroshwa nitaenda kukaa wapi?
Raya alisema anataka nikakae nyumbani
kwao kwa sababu pale kuna usalama zaidi, nikamwambia ni rahisi wabaya zangu
kujua kwamba niko pale kwa sababu kuna baadhi ya watu walikuwa wakijua kuhusu
uhusiano wetu wa kimapenzi. Nikatumia nafasi hiyo kumpigia chapuo Shamila,
nikamwambia Raya kwamba amesema yupo tayari kunificha nyumbani kwake.
Nilimuona Raya akishtushwa kidogo na
nilichokisema lakini nikamtoa wasiwasi na kumwambia kwamba mimi na yeye
tutakuwa pamoja kwa hiyo asiwe na wasiwasi wowote. Akakubali kwa shingo upande,
nadhani bado alikuwa na wivu juu ya ukaribu wangu na Shamila.
Muda ulizidi kuyoyoma, baadaye Shamila
alirudi akiwa peke yake, akaniambia kwamba kila kitu kimeenda kama
tulivyokubaliana, akaniambia kwamba Firyaal alikuwa mtundu sana kwenye mambo ya
kompyuta na kwamba tayari alishanikopia data zote na kuziacha pale nyumbani
kwake kama tulivyokubaliana, tukaanza kupanga mipango ya namna ya kutoroka
usiku huku Raya naye akiwepo.
Jambo ambalo kuanzia mwanzo Raya hakuwa
akilijua, ni kwamba katika mpango wetu huo ilikuwa ni lazima pia tumtoroshe na
Shenaiza, akashtuka kusikia hivyo.
Bado nikaendelea kumsisitiza kwamba
ilikuwa ni lazima tuondoke na Shenaiza kwa sababu bila yeye mimi nisingeingia
kwenye mtego huo na kuanzia mwanzo alikuwa akinisisitiza kwamba mimi ndiye mtu
pekee ninayeweza kumsaidia.
“Usiwe na wasiwasi, hawa wote wataenda
kukaa nyumbani kwangu, mimi nina nyumba kubwa, hata na wewe ukitaka tukae
pamoja tusaidiane kuwahudumia wagonjwa haina shida,” alisema Shamila, nikamuona
Raya akishusha pumzi ndefu na kunitazama, akatingisha kichwa kama ishara ya
kukubaliana na mimi.
Ilibidi Raya abaki palepale hospitalini
mpaka usiku ili iwe rahisi kufanya kazi yetu, muda ukazidi kuyoyoma na hatimaye
giza likaingia, ule muda tuliokuwa tukiusubiri kwa hamu ukawa umewadia.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
nzuri sana
ReplyDeletekaribu sana
Delete