ILIPOISHIA:
Lakini ni hapo pia nilipokumbuka ile
ajali nyingine ya bodaboda niliyoisababisha na pia nikakumbuka kisanga cha
dereva wa Bajaj aliyekuwa akipaki jirani na hapo kwa akina Rahma na jinsi
nilivyomkomesha asubuhi hiyo. Sikujua kama amesharudi au la na sikujua siku
atakaponiona tena atasema nini.
Nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo,
nilisikia mlango ukifunguliwa, Rahma akaingiza kichwa na kuchungulia ndani,
macho yangu na yake yakagongana.
SASA ENDELEA...
“Togo!” aliita Rahma kwa sauti ya udadisi
huku akiingia ndani na kuurudishia mlango taratibu, nikakaa vizuri kumsikiliza
maana nilikuwa najua kabisa kwamba alikuwa na maswali mengi ya kuniuliza
kutokana na mabadiliko makubwa niliyokuwa nayo kwa siku kadhaa zilizopita.
“Najua kwamba nalazimisha mapenzi kwako,
najua kwamba unajisikia aibu kuwa na mpenzi ambaye amekuzidi umri na najua pia
kwamba kama isingekuwa mimi kukuanza usingekuwa na mawazo yoyote ya kutoka
kimapenzi na mimi kwa sababu hunipendi,” alisema Rahma kwa sauti ya kulalama
mno, akionesha kuwa na maumivu makali ndani ya moyo wake.
“Leo nataka uniambie jambo moja tu,
nimechoka kuteseka kimapenzi, kwa kipindi chote tangu nikiwa msichana mdogo
nimekuwa nikijitunza na kujiheshimu sana, sasa isiwe kwa sababu nimetokea
kukupenda basi ukaanza kunitesa kwa makusudi na kunidhalilisha, nataka uniambie
kwamba hunitaki ili nijue moja,” alisema Rahma, safari hii machozi yakiwa
yanamchuruzika na kulowanisha uso wake mzuri.
Nilijisikia kuwa na hatia kubwa ndani ya
moyo wangu kwa jinsi Rahma alivyokuwa akilalamika na kulia kwa sababu yangu.
Rahma hakustahili kulia kwa sababu yangu kwa sababu maskini ya Mungu hakuwahi
kunifanyia jambo lolote baya na ndani ya kipindi kifupi tu nilichokaa naye,
alinionesha mapenzi ya dhati kabisa kutoka moyoni mwake.
Mimi pia sikuwa mtu wa kujihusisha na
mambo ya mapenzi na Rahma ndiye aliyekuwa mwanamke wangu wa kwanza tangu nipate
akili za kikubwa, na kipindi hichohicho pia nikakutana na Isrina, kwa hiyo siyo
kweli kwamba nilikuwa nikimtesa kwa makusudi.
“Naongea na wewe, nataka uniambie jambo
moja tu,” alisema Rahma na safari hii, alinishika mkono wangu na kuuvuta.
Katika hali ambayo hakuna aliyetegemea, alinishika pale nilipokuwa nimeifunga
ile hirizi, nikamuona akishtuka na kunitazama usoni.
“Hiki ni nini?” aliniuliza na kabla
sijajibu chochote, tayari alishanifunua mkono wangu na kwa kuwa nilikuwa
nimevaa shati la mikono mifupi, aliweza kuiona vizuri ile hirizi.
”Hiki ni nini Togo? Si naongea na wewe?”
alizidi kunibana lakini sikuwa na majibu, akazidi kunitumbulia macho.
“Samahani, nitakufafanulia baadaye, kuna
jambo nilikuwa naomba unisaidie kwanza,” niliongea kwa sauti ya upole.
“Jambo gani?”
“Naomba kachukue pini uje unisaidie
kunitoa miiba miguuni,” nilisema huku nikiinua nyayo zangu na kumuonesha Rahma,
akazidi kushtuka maana nilikuwa na miiba mingi niliyoikanyaga kule Mlandizi
wakati nikikimbia lile sakata, tena nikiwa mtupu.
Licha ya mshtuko alioupata, Rahma
alitoka na muda mfupi baadaye, alirudi akiwa na beseni dogo, wembe, pini,
spirit, mafuta na sabuni. Nilichokuwa nampendea Rahma, alikuwa akinijali sana,
yaani hakuwa tayari kuona nasumbuliwa na kitu chochote, alikuwa na mapenzi ya
dhati kwangu ingawa ndiyo hivyo tena, tayari kikwazo kikubwa kilikuwa kimeingia
katikati yetu.
“Hii miiba umeikanyaga wapi yote hii
jamani Togo!” aliniuliza wakati akinisafisha miguu, tayari kwa kazi ile.
Alinimwagia ‘spirit’ kwa wingi, jambo lililonifanya nisikie maumivi makali
kuliko kawaida. Alianza kunitoa mwiba mmoja baada ya mwingine na baada ya
karibu nusu saa ya maumivu makali, tayari alikuwa amemaliza. Akanisafisha upya
na kunipaka mafuta.
Kwa jinsi nilivyokuwa nikisikia maumivu,
hata kusimama sikuweza, nikajilaza vizuri huku nikimshukuru sana kwa wema wake.
Alitoa vile vifaa, aliporudi alikuja na kifungua kinywa, akakaa pembeni ya
kitanda na kuanza kunisihi ninywe chai.
“Halafu mbona una chale nyingi hivi
mwilini? Na zote zinaonesha ni mbichi kabisa,” alihoji Rahma na kuzidi
kunikosesha raha, hata chai yenyewe ikawa hainyweki tena. Hiyo ndiyo sababu
kubwa iliyonifanya tangu nianze yale mambo nikwepe kukaa naye karibu maana
nilihofia mambo kama hayo.
Ilibidi nivungevunge tu, nikawa nataka
kubadilisha mada lakini bado aliendelea kuniganda kwa maswali ambayo yalizidi
kunikosesha amani ndani ya moyo wangu.
“Ni kweli kwamba wewe ni mchawi?”
“Mimi? Masihara hayo Rahma, mimi na
uchawi wapi na wapi?”
“Mbona yule Dick dereva Bajaj anasema
usiku umemuwangia kichawi na asubuhi ameamka na kujikuta yupo Kimara na alikuwa
anakuota wewe? Na hiyo hirizi ni ya nini?” Rahma aliniambia kitu kilichonishtua
sana, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
“Amesemaje?”
“Anasema eti wewe ulimtishia na usiku
alipoenda kulala, ndiyo umemtokea na kumbeba kichawi na Bajaj yake mpaka
Kimara, ameshtuka na kujikuta amelala kwenye usukani,” Rahma alizidi
kusisitiza, ikabidi nicheke ili kumhadaa.
“Huyo atakuwa mwendawazimu, sijui
chochote anachokisema.”
“Kwani jana usiku ulikuwa wapi?”
“Si nilikuwa nimelala jamani?”
“Mbona nilikuja kukuangalia huku
chumbani sikukuona na hata chakula cha usiku hukula?”
“Nilitoka kidogo na baba yangu na baba
yako, tulikuwa hukohuko tulikoenda, tulirudi mapema tu mbona?”
“Mh! Na asubuhi pia ulikuwa wapi maana
nilikuja pia kukuchungulia nikamuona mdogo wako amelala peke yake.”
“Hukuangalia vizuri, nilikuwepo,” nilizidi
kutetea uongo wangu. Niliona Rahma akinyamaza kimya, nikajua lazima atakuwa
amejiongeza mwenyewe na kupata majibu kichwani mwake maana hakuwa mtoto mdogo.
Alichoniambia kuhusu yule dereva Bajaj
kilinikasirisha sana, hasa kusikia kwamba alikuwa akinitangazia mbovu mtaani
kwamba eti nimeenda kumuwangia, nikajikuta hasira juu yake ziki kuongezeka.
Hata hivyo, kuna mambo bado yalikuwa yananitatiza kichwa.
Nilikutana na huyo dereva Bajaj nje,
akiwa ameshaamka mwenyewe na akielekea kwenye kituo chao, iweje aseme kwamba
nilimfuata usiku? Ina maana muda ule nakutana naye mwenyewe alikuwa anajua yupo
ndotoni? Ni kweli kwamba fahamu zake zilimrudia akiwa Kimara, pale nilipomuacha
baada ya Bajaj yake kuishiwa mafuta?
“Kwa nini hutaki tena kukutana kimwili
na mimi? Ndiyo masharti yenu mliyopewa?” rahma aliniuliza swali ambalo sasa
lilinipa picha kwamba alikuwa anaelewa kila kitu kinachoendelea, ikabidi niwe
mkali maana kama ningeendelea kumchekea, angeendelea kuniingia.
“Kwa hiyo na wewe unaamini kwamba mimi
ni mchawi si ndiyo? Umefikia hatua ya kunikosea heshima kiasi hicho?”
“Ooh! Samahani Togo, naomba unisamehe tu
bure, basi yaishe baba’angu,” alisema Rahma huku akinisogelea na kunibusu,
machozi yakiwa yameshaanza kumlengalenga. Japokuwa nilikuwa najua kwamba siruhusiwi
kabisa kukutana tena kimwili na Rahma, sikuwa na namna yoyote ya kumtuliza na
kumuondolea huzuni ambayo sasa ilikuwa ikijionesha waziwazi kwenye uso wake.
“Na mimi si tayari nimeshakuwa na nguvu
za ziada? Chochote kitakachotokea nitapambana kuhakikisha namuokoa, kwanza
akina baba hawawezi kukubali kuona akipatwa na jambo baya wakati uwezo wa
kumsaidia wanao,” nilijisimea moyoni na ghafla nikajikuta nikipata ujasiri
mkubwa ndani ya moyo wangu.
Nilimvutia Rahma kwenye kifua changu,
kumbe na yeye ni kama alikuwa akisubiri tu nifanye hivyo kwani naye
alinikumbatia kwa nguvu huku akiendelea kulia kwa kugugumia ndani kwa ndani.
“Kwa nini unanifanyia hivi Togo? Ina
maana nimekosea kukupenda?” alisema huku machozi yakizidi kumtoka, nikaanza
kumbembeleza huku nikimfuta machozi, nikimchombeza kwa maneno matamu, zoezi
hilo lilienda sambamba na kupashana misuli, tayari kwa mpambano wa kukata na
mundu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment