ILIPOISHIA:
Ndani ya dakika mbili tangu tukae mkao huo,
kuna mambo ya ajabu yalianza kunitokea, mapigo ya moyo yakawa yanazidi kwenda
mbio kuliko kawaida kutokana na kile nilichokuwa nakishuhudia.
SASA ENDELEA...
Nilianza kuona ile hali kama ambayo ilinitokea
siku ile nilipovamiwa barabarani na kujeruhiwa vibaya na baadaye kuingia kwenye
ulimwengu wa tofauti, nikawa najihisi kwamba japokuwa nilikuwa nimekaa pale
chini na wenzangu, taswira nyingine ya mwili wangu ilikuwa ikianza kupaa juu na
kuelea angani, nikawa sielewi nini kinachotaka kutokea.
Cha ajabu ni kwamba, yule aliyekuwa akianza
kupaa ndiyo alikuwa mimi kwa sababu nilikuwa najitambua kabisa, nikainamisha
kichwa na kutazama chini, nikajiona nikiwa nimekaa pale juu ya zulia, nikiwa
nimeshikana mikono na yule mwenyeji wetu, Raya na Firyaal, jambo ambalo
lilisababisha hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
“Noo! Sitaki kufa tena, sitakiii,” nilisema
kwa sauti ya juu, nikashtukia nikiporomoka kutoka pale juu nilipokuwa nikielea,
nikaanguka chini kama furushi na kujibamiza sakafuni kwa kishindo.
Nilipofumbua macho, kila mtu alikuwa amepigwa
na butwaa akiwa ni kama haamini kilichotokea, nikawa nahema kwa nguvu huku
nikiwa nimelala sakafuni, sikukumbuka hata niliwaachia wenzangu mikono saa
ngapi, wote wakabaki kunishangaa.
“Hutaki kufa tena? Unamaanisha nini?”
aliniuliza yule mwenyeji wetu, nikainuka pale nilipokuwa nimeanguka na kukaa,
nikawa nawatazama mmoja baada ya mwingine huku nikijihisi aibu kubwa usoni.
“Naongea na wewe kijana, vipi mbona
sikuelewi?” yule mwenyeji wetu alizidi kunibana kwa maswali lakini sikuwa na
cha kujibu, Raya na Firyaal wote wakawa wanaendelea kunitazama kwa macho ya
mshangao, kila mmoja akionesha kuwa na shauku kubwa ya kutaka kusikia nitajibu
nini.
“Hata sielewi kilichotokea,” nilisema, wote
wakashusha pumzi ndefu na kutazamana.
“Hebu naombeni mtupishe mara moja mimi na
Jamal, alisema yule mwanamke ambaye kiumri alikuwa mtu mzima, Raya na Firyaal
wakasimama na kutoka mle chumbani, wakaenda kukaa sebuleni, nikawa nawasikia
wanazungumza lakini sikuelewa walikuwa wakizungumzia nini ingawa nilijua kwamba
walikuwa wakiniongelea.
“Hebu niambie ukweli, umeona nini au kipi
kilichokutokea?” aliniuliza mwanamke huyo wa makamo, mweupe na mnene kiasi,
niligeuka huku na kule na nilipohakikisha tupo wawili tu, nilimuuliza swali juu
ya swali.
“Umesema OBE ni nini?”
“Mbona nakuuliza swali unaacha kunijibu na
wewe unaniuliza? Tupo nyuma ya muda na tunatakiwa kufanya haraka kumsaidia
Shamila, niambie nini kimetokea?”
“Ninachotaka kukwambia kinahusiana na hiyo OBE
na nahisi hii si mara ya kwanza kutokewa na hiki kilichonitokea,” nilimwambia,
kwa mara nyingine akashusha pumzi ndefu na kunitazama. Nadhani alihisi kwamba
sikuwa huru kuzungumza kwa sababu mara kwa mara nilikuwa nikigeuka na kutazama
mlangoni.
Ikabidi ainuke na kwenda mpaka mlangoni,
akaufunga na kurudi pale nilipokuwa nimekaa, safari hii akanisogelea karibu
huku akinitazama kwa macho ya udadisi.
“Shamila si ni rafiki yako?”
“Ndiyo.”
“Unamuamini?”
“Ndiyo. Vipi kwani?”
“Kama unamuamini Shamila basi nakuomba
uniamini na mimi, your secrets are safe with me (siri zako zitakuwa salama
ukiwa na mimi) aliongea kwa kuchanganya na Kiingereza kuonesha kwamba alikuwa
ameenda shule. Kabla sijamjibu, akaendelea:
“Nikikutazama kuna kitu nakiona lakini siwezi
kukielezea mpaka mwenyewe uniambie. Halafu inaonekana kuna jambo halipo sawa
kwenye mwili wako, una wapenzi wangapi?” aliniuliza swali ambalo lilinishtua
sana, nikashindwa kumuelewa alikuwa ameona nini kwangu na swali lile lilikuwa
na uhusiano gani na nilichomuuliza.
Nikashindwa cha kumjibu zaidi ya kubaki
nikimkodolea macho usoni, akanishika mkono na kunifanya nizinduke. Sijui kwa
nini hali ya mawazo kutengana na mwili wangu ilikuwa ikinitokeatokea sana
safari hii. Yaani ilikuwa unaweza kuniona nakutazama ukahisi akili zangu zipo
pale lakini kumbe nikawa nawaza kitu kingine tofauti kabisa.
“Shamila ni mwanangu, mimi ni mama yake mdogo
kwa hiyo nakuomba tena usiwe na wasiwasi unapokuwa na mimi, hebu nijibu maswali
yote niliyokuuliza, sawa baba,” aliongea kwa lugha ya upole na kubembeleza,
nikashusha pumzi ndefu na kidogo nikaanza kuhisi amani ndani ya moyo wangu.
“Nina mpenzi mmoja tu, kwa nini umeniuliza?”
“Unajua kwa mtu mwenye utaalamu wa elimu ya
nguvu zisizoonekana kama mimi, nikikutazama tu naweza nikajua wewe ni mtu wa
namna gani. Nikikuangalia naona kama kwa siku za hivi karibuni umekutana
kimwili na zaidi ya mwanamke mmoja na inaonesha pia upo kwenye mipango ya
kufanya hivyo kwa wanawake wengine zaidi, kama nimekosea naomba unisamehe,”
alisema yule mwanamke, kauli iliyozidi kunishangaza mno.
Alichokisema kilikuwa kweli, nilikuwa
nimekutana kimwili na Raya na Shamila kwa kuwachanganya ingawa wenyewe hawakuwa
wakijua chochote na kama hiyo haitoshi, nilikuwa kwenye mipango ya kufanya
hivyo kwa Firyaal pia ambaye yeye ndiye aliyeonesha kunipenda mimi zaidi na
kujikuta nikishindwa kuendelea kuvunga.
“Anyway, najua hayo ni mambo ya ujana tuachane
nayo lakini kubwa nahisi kama umewahi kutokewa na jambo kubwa sana
linalokufanya uwe tofauti na binadamu wengine na ndiyo maana hapa umekwamisha
tulichokuwa tunataka kukifanya. Inaonesha una nguvu kubwa sana ambazo pengine
hata wewe mwenyewe hujui na ndizo zinazokutesa,” alisema na kuzidi
kunichanganya kichwa.
“Unamaanisha nini unaposema nguvu
zisizoonekana?”
“Kwani wewe uliposema hutaki kufa tena na
ukavuruga kazi tuliyokuwa tunaifanya ulimaanisha nini?” mfumo wa swali juu ya
swali uliendelea kutawala katika mazungmzo yetu.
“Umewahi kufika kuzimu?” aliniuliza swali
lingine, nikatingisha kichwa harakaharaka kukataa lakini alinigundua kwamba
kuna jambo namficha.
“Hapo kifuani umefanya nini?” aliniuliza, eti
na mimi nikawa najitazama kama najishangaa, akajua kwamba nilikuwa na mambo
mengi ninayoyaficha, akazungumza kwa sauti yenye mamlaka sasa”
“Sikia, kama bado huniamini huwezi kuwa na
msaada wowote katika hili tunalotaka kulifanya, itabidi wewe ukakae sebuleni
utusubiri mimi na hao wenzako tufanye kinachowezekana kumuokoa Shamila, haupo
tayari kushirikiana na sisi, yaani ni kama nakulazimisha hivi.”
“Hapana, siyo hivyo.”
“Siyo hivyo nini? Muda unazidi kuyoyoma, Shamila
yupo kwenye matatizo, kila nachokuuliza unanichenga sasa unataka nifikirie
nini?” alisema huku akisimama, akionesha kuchukia.
Siyo kwamba sikuwa tayari kumjibu maswali yake
lakini alichonichanganya alikuwa akitaka kujua vitu vingi kwa wakati mmoja,
wakati mambo yenyewe hayakuwa mepesi kuyafafanua mpaka mtu akaelewa.
“Nataka kumsaidia Shamila,” nilisema.
“Nijibu maswali yote niliyokuuliza.”
“Nitakujibu lakini itakuwa ni baada ya
kumaliza kazi ya kumsaidia Shamila.”
“Hapana, wewe una nguvu kubwa sana ambazo
mwenyewe hujui namna ya kuzitumia, unaweza kufanya tena kama hiki ulichokifanya
hapa ukasababisha tudhalilike huko nje tunakokwenda.”
“Hapana, nitajitahidi naomba uniamini.”
“Unaniahidi?”
“Ndiyo,” nilisema kwa kujiamini, akanitazama
usoni kisha akaenda mlangoni na kufungua, akawaita Raya na Firyaal, wakaingia
ndani na tukakaa tena kama tulivyokuwa tumekaa mwanzo, kazi ikaanza upya huku
akinisisitiza kuwa makini na kuishinda hofu ndani ya moyo wangu, nikatingisha
kichwa kama ishara ya kukubaliana naye.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment