ILIPOISHIA:
Nilipofika, na mimi nilijifanya ni
mwombolezaji wa kawaida tu, nikawasalimia baadhi ya watu kisha nikajichanganya
na waombolezaji wengine. Ghafla nilishtuka baada ya kuona kitu ambacho
sikukitarajia, nikahisi kijasho chembamba kikianza kunitoka, mara hirizi yangu
ikaanza kunibana kwa nguvu, kufumba na kufumbua kamba yake ikakatika,
ikadondoka chini!
SASA ENDELEA...
“Mungu wangu!” nilijikuta nimetamka kwa
sauti, hali iliyofanya watu wote washtuke, hata wale ambao hawakuwa wameniona
nikiwasili eneo hilo, waligeuka na kunitazama, nikajihisi mwili ukiishiwa nguvu
na kunyong’onyea kama nimepigwa na shoti ya umeme.
Sikujua nifanye nini kwa wakati huo,
watu wakawa bado wamenikazia macho, kila mtu akiwa na shauku kubwa ya kutaka
kujua mimi ni nani na nini kimetokea mpaka nikashtuka kiasi hicho.
“Wasalimu watu wote kwa heshima kisha
wape pole,” nilisikia sauti ya baba masikioni mwangu, ghafla nikajikuta
nimepata nguvu na kuwa na imani kubwa kwamba hata iweje, baba ameshajua
kinachoendelea kwa hiyo atanisaidia.
“Shikamooni jamani na poleni sana kwa
msiba!” nilizungumza kwa kujitutumua huku sauti yangu ikiwa bado na dalili za
kutetemeka. Wengine walijibu salamu yangu na wengine walikaa kimya lakini kwa
kiasi kikubwa, kitendo cha mimi kuwasalimu, kiliwafanya wengi wanione kama
muombolezaji wa kawaida.
Wengine waliendela na mazungumzo yao na
wachache walibaki wakinitazama, nikawa natafuta ‘taiming’ ya kuiokota ile
hirizi. Kwa harakaharaka niligundua kwamba kulikuwa na zaidi ya watu saba
waliokuwa bado wamenikazia macho, nikawa najaribu kuzuga, sikutaka kutazamana
na mtu yeyote usoni kwa sababu nilihisi ile hatia niliyokuwa nayo isingeweza
kufichika.
Kwa bahati nzuri, nikiwa bado nazugazuga
pale nikitafuta namna ya kuiokota ile hirizi pale chini, kulisikika sauti za
wanawake wakilia kwa nguvu mara tu baada ya kushuka kwenye gari kwani msiba
haukuwa mbali na barabara kuu ya lami ya kuelekea Morogoro.
Watu karibu wote waligeukia kule vile
vilio vilikokuwa vinatokea, nikaona huo ndiyo muda pekee wa kufanya kile
nilichokusudia. Kwa kasi kubwa niliinama na kuikwapua ile hirizi pale chini
kisha nikaisokomeza kwenye mfuko wa suruali. Wakati nikiamini kwamba hakuna mtu
aliyeniona, nilishtuka kugundua kwamba wale watu niliokuwa nahisi kwamba
wananitazama, wala hawakujishughulisha kuwatazama wale watu waliokuwa wakilia,
kumbe bado walikuwa wamenikazia macho na kitendo cha kuikota ile hirizi pale
chini, walikishuhudia live bila chenga, kwa mara nyingine nikajikuta nikiishiwa
nguvu.
Japokuwa ilikuwa ni asubuhi, nilihisi nikilowa
kwapani kwa kijasho chembamba.
“Usipokuwa makini utakiona cha mtema
kuni leo, nani aliyekutuma kwenda msibani? Ni mwiko kabisa kwa sheria zetu,
bora hata ungeenda makaburini,” sauti ya baba ilisikika tena masikioni mwangu
na kuzidi kunipa hofu kubwa ndani ya moyo wangu.
Niligeuka huku na kule, nikagundua
kwamba kumbe kulikuwa na watu wengine nyuma yangu waliokuwa bado wakinitazama,
nikazidi kuingiwa na hofu. Sikuwa najua natakiwa kufanya nini, nikaamua
kuchukua maamuzi magumu.
Kwenye moja kati ya maturubai yaliyokuwa
yakiendelea kufungwa, kulikuwa na mshumaa wa rangi ya zambarau ambao tayari
ulishawashwa na pembeni yake, kulikuwa na picha kubwa iliyowekwa kwenye fremu
ya kioo, sambamba na daftari na kibakuli kilichokuwa na fedha.
Bado watu wengi walikuwa wanawatazama
wale waombolezaji waliokuwa wakiendelea kulia kwa uchungu huku wakisaidiwa na
wenyeji wao kupelekwa pale msibani, nikatembea kwa hatua za kusuasua mpaka pale
kwenye ile picha ya marehemu, nikaitazama.
Kiukweli hakuna siku ambayo nimewahi
kujihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo wangu kama siku hiyo. Maskini ya
Mungu, bado alikuwa binti mdogo kabisa na kwenye picha hiyo alikuwa ameachia
tabasamu pana, akionesha kuwa na matumaini mwengi kwenye maisha yake ya
baadaye.
Nilijisikia vibaya sana kushiriki
kuyakatisha maisha ya msichana yule mdogo asiye na hatia, nikashindwa kujizuia,
machozi yakanitoka kwa wingi na kulowanisha uso wangu.
Sikukumbuka tena kama kuna watu walikuwa
wakinifuatilia hatua kwa hatua, kwa uchungu niliokuwa nao, niligeuka haraka na
kutafuta sehemu ya kujificha kwa sababu huwa sipendi kabisa mtu yeyote ayaone
machozi yangu. Kwa kutumia viganja vya mikono yangu nilijiziba usoni, nikasogea
mbali kabisa na wale waombolezaji wengine, nikasimama chini ya mwembe uliokuwa
jirani, donge kubwa likiwa limeniganda kooni.
“Kijana, wewe ni nani na hapa umefuata
nini?” sauti nzito ya mwanaume nisiyemjua ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye
hali ile, harakaharaka nikajifuta machozi na kugeuka kumtazama.
Alikuwa ni mwanaume wa makamo, mweusi
tii, akiwa na macho mekundu sana, huku mishipa mingi ikiwa imesimama kwenye
kichwa chake. Kabla ya kumjibu, haraka sana nilimtazama kwenye mikono yake. Cha
ajabu, nilimuona akiwa ameweka ile ishara kama ambayo baba alinifundisha,
alikuwa ameziba kucha ya kidole chake kidogo kwa dole gumba.
Alipoona nimekazia macho kwenye mkono
wake, aliuficha kwa nyuma kisha akarudia tena kuniuliza swali lake.
“Usimjibu chochote, mkazie macho usoni,”
nilisikia sauti ya baba, nikafanya kama alivyoniambia. Japokuwa alikuwa na sura
ngumu, nilijikakamua kisabuni nakumkazia macho usoni, akashtuka kuona namtazama
machoni.
Cha kushangaza, na yeye aliponikazia
macho kwa sekunde kadhaa na kurudia tena kuniuliza swali lile, alipoona bado
nimekomaa kumtazama machoni, aliachia vile vidole vyake alivyokuwa amevibana,
akawa ni kama anababaika machoni maana hakuweza tena kunitazama machoni.
“Usifikiri watu wote hapa ni wajinga,
kwa usalama wako ondoka haraka,” alisema kwa sauti ya kukwamakwama lakini
sikumjibu chochote zaidi ya kuendelea kumkazia macho, nikamuona akiufyata mkia
na kugeuka, akatembea harakaharaka na kwenda kujichanganya na wenzake.
Nikiwa bado namtazama, alipokaa tu
niliona wazee wengine kadhaa ambao walikuwa miongoni mwa watu waliokuwa
wakinitazama kwa macho ya ukali wakimfuata pale alipokuwa amekaa, wakawa
wanazungumza kisha nikaona wote wamegeuka na kunitazama.
“Iweke hiyo hirizi chini ya ulimi na
kimbia haraka uwezavyo kuondoka eneo hilo kabla hawajakufikia,” sauti ya baba
ilisikika tena masikioni mwangu. Harakahara nikaingiza mkono mfukoni na kuitoa
ile hirizi, japokuwa ilikuwa kubwa niliingiza mdomoni na kuibana chini ya
ulimi.
Kabla hata sijamaliza kufanya kitendo
hicho, nilishtukia lile kundi la wale wazee likija kwa kasi pale chini ya
mwembe, nikageuka haraka na kuanza kutimua mbio, sikuwa naijua mitaa ya
Mlandizi lakini kwa jinsi baba alivyoongea kwa msisitizo na hali halisi
ilivyokuwa, nilijua nikilemaa, kweli nitaadhirika.
Kila mtu alibaki amepigwa na butwaa pale
msibani maana ilikuwa ni zaidi ya kituko, nilitimua mbio ambazo sikumbuki kama
nimewahi kukimbia maishani mwangu, nikawa nakatiza mitaani huku watu wengine
wakishtuka wakidhani labda nilikuwa mwizi, kwa nyuma nikawa nasikia kelele kwa
wingi kuonesha kwamba wale watu walikuwa wameniungia tela.
Sikujua nini kitanipata endapo watanitia
mikononi na kugundua kwamba mimi ndiye niliyesababisha kifo cha yule mtoto huku
mama yake akiwa mahututi, na kusababisha watui wote wawe na huzuni kiasi kile.
Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika
suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa
nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu
waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba
ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo
yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana
uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.
Je,
nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Championi Jumatatu.
This comment has been removed by the author.
ReplyDelete