ILIPOISHIA:
“Ndiyo,” nilisema kwa kujiamini, akanitazama
usoni kisha akaenda mlangoni na kufungua, akawaita Raya na Firyaal, wakaingia
ndani na tukakaa tena kama tulivyokuwa tumekaa mwanzo, kazi ikaanza upya huku akinisisitiza
kuwa makini na kuishinda hofu ndani ya moyo wangu, nikatingisha kichwa kama
ishara ya kukubaliana naye.
SASA ENDELEA...
Kazi ilianza upya, akatusisitiza kila mmoja
awe anavuta pumzi ndefu kwa kutumia tumbo na siyo kifua kama wengi tunavyopumua,
pia akatutaka kuhakikisha kila mmoja akili yake aielekeza eneo la tukio.
Muda mfupi baadaye, ile hali ilianza kunitokea
tena, nikawa najihisi kama naelea angani huku mwili mwingine ukiwa palepale
tulipokuwa tumekaa. Hofu ilianza kunijia tena lakini nilipokumbuka maneno ya
yule mwanamke, nilijitahidi kuishinda hofu.
Nikaendelea kutuliza kichwa na kufumba na
kufumbua, nilijikuta nikiwa pale hospitalini nilipokuwa nimelazwa. Niliweza
kuona kila kitu kilichokuwa kikiendelea, wagonjwa waliokuwa wakiingia na kutoka,
manesi na madaktari waliokuwa wakikimbizana huku na kule kuelekea kwenye ukumbi
wa mikutano.
Upande wa Kaskazini kulikuwa na magari matatu
ya polisi yaliyokuwa yamepaki huku askari wengi wenye silaha wakirandaranda
huku na kule.
“Kumetokea nini kwani leo hapa?”
“Nasikia kuna wagonjwa wametoroshwa usiku sasa
ndiyo polisi wamekuja kutafuta wahusika.”
“Mh! Yaani wagonjwa kutoroshwa tu ndiyo zije
difenda kibao na askari utafikiri kuna vita?”
“Nasikia huyo mgonjwa mmoja ni mtoto wa kigogo
mmoja mkubwa ndiyo maana unaona hali ipo hivi,” niliwasikia watu wawili
wakihojiana, wakiwa wamesimama chini ya kivuli cha mti.
Ghafla nikasikia vishindo vya mtu akitembea
kwa kasi nyuma yangu, nikageuka, katika mazingira ambayo sikutegemea, nilimuona
askari mmoja mwenye bunduki, akiwa ananifuata pale nilipokuwa nimesimama,
nikajua ameshaniona na kunitambua, nikawa natetemeka.
Cha ajabu, ni kwamba alinipita akiwa ni kama
hajaniona na kuwafuata wale watu waliokuwa wakiendelea na majadiliano pale
chini ya mti, nikamsikia akiwapa amri kwamba hatakiwi mtu yeyote asiyekuwa na
shughuli maalum kuonekana ndani ya hospitali hiyo, akawataka watoke nje ya geti
na kwenda nje kabisa.
Kidogo nilishusha pumzi kwani nilikumbuka mara
nyingi ninapokuwa kwenye hali kama ile, huwa siwezi kuonekana kwa macho ya
kawaida. Harakaharaka nikawa nawafuata wale manesi na madaktari kule walikokuwa
wanaelekea kwa lengo la kwenda kuona kinachojadiliwa.
Cha ajabu zaidi, nilipofika kwenye mlango wa
kuingilia kwenye ule ukumbi, nilimkuta yule mwanamke, mama yake mdogo Shamila
naye akiwa ameshafika, nikamtazama nikiamini yeye hawezi kuniona. Cha ajabu na
yeye aligeuka haraka na kunikazia macho, tukawa tunatazamana.
Nilijifunza kitu kingine kwamba kumbe ukiwa
katika hali ambayo huwezi kuonekana kwa macho ya kawaida, akija mtu mwingine
ambaye naye anakuwa kwenye hali kama yako, mnaweza kuonana vizuri, yaani yeye
akakuona na wewe ukamuona ingawa watu wengine wa pembeni wanakua hawana uwezo
wa kumuona yeyote kati yenu.
Alinisogelea na kunigusa, kingine cha ajabu ni
kwamba nilihisi kabisa kwamba nimeguswa na mtu, akanivutia pembeni na kuanza
kuzungumza na mimi kwa sauti ya chini, akaniambia Shamila yuko ndani na
amewekwa chini ya ulinzi, amejaribu kumtorosha lakini ameshindwa peke yake,
akaniomba tukaunganishe nguvu ili tumtoe haraka iwezekanavyo.
“Sasa tutafanyaje” nilimuuliza huku hofu
ikianza kuniingia kwani kwa mbali niliwaona askari wengine wawili wenye silaha
wakija, akaniambia tukiingia niwe namfuatisha kila anachokifanya, nikatingisha
kichwa kuonesha kukubaliana naye. Akaniminya mkono na kunitazama usoni,
akaniambia natakiwa niishinde hofu ndani ya moyo wangu. Nadhani aliniona jinsi
nilivyoanza kuingiwa na wasiwasi, nikatingisha tena kichwa.
Pale kwenye geti la kuingilia, alinionesha
ishara kwamba tunatakiwa kuingia kinyumenyume, tukafanya hivyo na muda mfupi
baadaye tayari tulikuwa ndani. Madaktari na manesi walikuwa tayari wameshakaa
kwenye nafasi zao huku wengine wakiendelea kuingia.
Mbele kabisa kulikuwa na meza kuu ambako
walikuwa wamekaa watu walioonesha kuwa viongozi wa juu wa hospitali hiyo pamoja
na askari aliyekuwa na nyota nyingi mabegani, nadhani alikuwa ni kiongozi wa
polisi.
Upande wa kushoto, alikuwa amekaa Shamila huku
amezungukwa na askari wawili wa kike, mmoja kila upande. Pembeni kidogo,
walikuwa wamekaa wale walinzi tuliowapita getini usiku wakati tukitoroka, ambao
nao ilionesha wamewekwa chini ya ulinzi. Tulipita mpaka mbele kabisa huku mtu
yeyote akiwa hatuoni.
Akanipa ishara kwamba tunatakiwa kuwazunguka
wale askari waliokuwa wamemuweka chini ya ulinzi Shamila mara saba kwa uelekeo
tofauti, yaani mimi nianzie kulia kwenda kushoto na yeye kushoto kwenda kulia.
Tulianza kufanya kazi hiyo huku kukiwa hakuna
mtu yeyote aliyekuwa akielewa kinachoendelea. Tulizunguka mzunguko wa kwanza,
wa pili na hatimaye mizunguko saba ilitimia, akanionesha ishara kwamba
inatakiwa tuwaguse vichwani wale askari, kweli tulifanya hivyo.
Katika hali ambayo sikuitegemea, nilishangaa
kuwaona wale askari wawili wa kike, wote wakishikwa na usingizi wa ghafla,
Shamila naye akawageukia mmoja baada ya mwingine, akashangaa akiwa haelewi
chochote kinachoendelea.
Wakati hayo yakiendelea, pale meza kuu daktari
mmoja alikuwa akizungumza kwa kutumia kipaza sauti, akielezea jinsi tukio la
kutoroshwa wagonjwa wawili lilivyofanyika usiku.
Hatukuwa na muda wa kupoteza, alionesha ishara
kwamba tukamshike Shamila, mmoja kwenye bega la kushoto na mwingine bega la
kulia, tukafanya hivyo kisha akanionesha ishara kwamba akihesabu mpaka tatu,
tupige mguu wa kushoto chini kwa nguvu na kufumba macho na nisifumbue mpaka
atakaponiambia.
Akaanza kuhesabu, moja! Mbili! Taaatu,
nikakanyaga mguu wangu wa kushoto chini kwa nguvu, sawasawa na yeye, mara umeme
ukakatika jengo zima, nikafumba macho kama alivyoniambia huku nikiwa
nimemshikilia Shamila kwa nguvu, nikahisi kama tumezolewa na kimbunga chenye
nguvu kubwa.
“Fumbua macho,” alisema, nilipofumbua macho,
sikuamini nilichokiona. Tulikuwa tumerejea ndani ya kile chumba tulichokuwemo
mwanzo lakini tofauti na awali, safari hii kila mmoja alikuwa amelala sakafuni,
kuanzia mimi, yule mwanamke, Raya na Firyaal huku akiwa ameongezeka mtu
mwingine kati yetu, Shamila.
Bado wale wenzetu wote walikuwa kama
wamepitiwa na usingizi mzito isipokuwa mimi na yule mwanamke pekee,
nikajivutavuta na kuinuka pale nilipokuwa nimelala, nikashangaa mwili wangu
ukiwa umechoka kupita kiasi huku viungo vyote vikiniuma.
Yule mwanamke naye aliinuka na kukaa kwa
kujiegemeza ukutani, naye akionesha kuchoka kuliko kawaida.
“Kweli wewe ni mwanaume wa shoka, njoo
nikupongeze,” alisema kwa sauti ya kichovu, nikajikokota na kusimama, nikasogea
mpaka pale alipokuwa amekaa, akanionesha ishara kwamba nikae chini pembeni
yake, nikafanya hivyo huku sote macho yetu yakiwa kwa Shamila.
“Sikuwahi kudhani kwamba unaweza kuwa na nguvu
kubwa kiasi hicho, hongera sana, utanifaa sana wewe,” alisema huku akipitisha
mkono wake mmoja begani kwangu kichovu kisha akanigeukia, tukawa tunatazamana.
Katika hali ambayo sikuitegemea hata kidogo, nilishangaa yule mwanamke
akinibusu, tena mdomoni, nikashtuka mno.
“Hongera sana, ila inabidi upunguze mambo ya
wanawake, utakuwa na nguvu zaidi ya hizi ulizonazo,” aliniambia huku
akinitazama usoni.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
Nitaifuatilia mpaka mwisho hii, ni nzuri mno.
ReplyDeleteKaribu sana
Delete52 wapiiiii???
DeleteSimulizi nzr hadi raha
But unachukua muda mrefu sana kutu postia, maana nimesubiri weee nacheki kila siku hola. shukrani nyingi sana
ReplyDeleteNitajitahidi kuwa naposti mara kwa mara, karibu sana
Delete