ILIPOISHIA:
“Sikuwahi kudhani kwamba unaweza kuwa na nguvu
kubwa kiasi hicho, hongera sana, utanifaa sana wewe,” alisema huku akipitisha
mkono wake mmoja begani kwangu kichovu kisha akanigeukia, tukawa tunatazamana.
Katika hali ambayo sikuitegemea hata kidogo, nilishangaa yule mwanamke
akinibusu, tena mdomoni, nikashtuka mno.
“Hongera sana, ila inabidi upunguze mambo ya
wanawake, utakuwa na nguvu zaidi ya hizi ulizonazo,” aliniambia huku
akinitazama usoni.
SASA ENDELEA...
“Sijakuelewa,” nilimwambia, akashusha pumzi
ndefu na kukaa vizuri pale juu ya zulia. Bado si Raya, Shamila wala Firyaal
waliokuwa wamezinduka.
“Utanielewa tu,” inabidi kwanza tukaoge
kuondoa uchovu halafu tuwasaidie na hawa nao warudi kwenye hali yao ya kawaida,
tuna kazi nyingine ya kumsaidia Shenaiza, ni lazima arudiwe na fahamu zake,
tena ikiwezekana haraka iwezekanavyo,” alisema mwanamke huyo kisha akapiga
miayo mfululizo na kujinyoosha.
“Kwa kawaida, kila binadamu huwa anazalisha
nguvu, nadhani hilo nilishakueleza kutoka mwanzo ingawa ni wachache sana
wanaolitambua hili.
“Yaani ni kama kupepesa kope, unajua ni mpaka
mtu akukumbushe kwamba muda wote macho yako yanapepesa kope ndiyo unakumbuka?”
alisema, nikawa sioni chochote kipya kwenye mazungumzo yake kwa sababu ni jambo
ambalo nilikuwa nimeshalisikia sana maishani mwangu kwamba kila binadamu
anazalisha nguvu zisizoonekana.
“Nguvu tunazozalisha huwa zinatengeneza kitu
kinachoitwa aura ambacho wengine huwa wanakiita ni mwili usioonekana juu ya
mwili unaoonekana. Sasa kwa mtu mwenye utambuzi wa nguvu hizi, anao uwezo wa
kuuona mwili huu.
“Kwa mtu ambaye anaishi maisha ya kitakatifu,
yaani hanywi pombe, havuti sigara, hafanyi zinaa, hawasemi vibaya watu wengine,
hana wivu wala kinyongo, ana upendo wa dhati kwa watu wote na ambaye moyo wake
uko safi, hii aura huwa na kawaida ya kung’aa sana. Mtu akikutazama tu anaiona
nguvu inayokuzunguka.
“Lakini vilevile kama mtu anaishi maisha ya
hovyo, pengine ni mlevi sana, anafanya ngono hovyohovyo, ana wivu, hasira,
vinyongo na tabia mbayambaya, kwa kawaida huwa aura yake inafifia sana na kama
una utambuzi wa nguvu hizi, ukimtazama tu unamjua ndiyo maana nilikwambia
vile,” alisema yule mwanamke na kuzidi kunishangaza.
Kitu alichokisema sikuwa nimewahi kukisikia
sehemu yoyote, nikabaki nimepigwa na butwaa, akaendelea:
“Japokuwa watu wengi huwa hawaelewi kuhusu
aura kwa hiyo hawajui umuhimu wa kuishi kitakatifu hata kama huna dini, siyo
kitu cha mchezomchezo. Aura ya mtu huanza kuishi kabla mtu hajazaliwa na
huendelea pia mpaka mtu anapokufa. Ndiyo maana mtoto anapokaribia kuzaliwa,
tafiti zinaonesha kwamba huwa ana uwezo wa kuelewa kinachoendelea kwenye
ulimwengu wa nje.
“Hii ni kwa sababu tayari mwili wake ambao
hauonekani unakuwa umeshaingia kwenye ulimwengu wa kawaida. Akishazaliwa, huwa
inatakiwa mwili wake halisi uungane na hii aura na hiyo hufanyika katika
kipindi cha siku arobaini tangu mtoto azaliwe ndiyo maana kuna tamaduni nyingi
kwamba mtoto anatakiwa kuanza kutolewa nje baada ya siku arobaini kwani pale
inakuwa tayari aura yake na mwili halisi vinakuwa vimeungana hivyo anakuwa na
kinga dhidi ya mambo mabaya yasiyoonekana kwenye ulimwengu wa kaiwada.
“Hiyo pia hutokea pale mtu anapokufa ambapo
nafsi inapotengana na mwili, aura huwa inaendelea kuishi mpaka baada ya siku
arobaini ndiyo nayo hutoweka, ndiyo maana pia huwa kuna tamaduni za kufanya
arobaini ya marehemu kwani pale ndiyo uhai huwa unakuwa umefikia mwisho.”
Maelezo hayo yalinifanya nikune kichwa kwani
siyo siri yalikuwa yamenichanganya sana akili. Ni mambo ambayo sikuwahi
kuyasikia kabla lakini kwa jinsi alivyokuwa akiyafafanua, ilionesha dhahiri
kwamba ni kweli. Hata mimi sikuwahi kupata jibu la kwa nini mtoto anatakiwa
atolewe nje baada ya siku arobaini tangu azaliwe na kwa nini mtu akifa, msiba
huwa unahitimishwa baada ya siku arobaini.
“Lakini mamdogo...”
“Usiniite mamdogo, ningependa zaidi uniite kwa
jina langu halisi ambalo ni watu wachache huwa wanalijua. Nina majina mengi
lakini jina langu halisi ni Junaitha,” alisema huku akiinuka pale alipokuwa
amekaa.
“Hakuna cha lakini... punguza wanawake ili
aura yako ing’ae na kukuongezea nguvu, mimi sijui nina mwaka wa ngapi simjui
mwanaume,” alisema huku tayari akiwa amesimama, akanipa mkono kama ishara ya
kutaka anisaidie kuinuka.
Nilibaki kumtazama tu usoni, mambo mengi
yalikuwa yakipita ndani ya kichwa changu.
“Mbona unanitumbulia macho? Amka twende
ukaoge, bado kuna kazi kubwa leo,” alisema yule mwanamke, nikampa mkono,
akanishika na kunivuta kidogo, nikasimama.
“Halafu inatakiwa pia uwe makini na vyakula
unavyokula, inaonesha mwili wako hauna uzito unaotakiwa, hata hao wanawake
unaotembea nao hovyo huwa unawaridhisha kweli? Wanaume wa siku hizi wana tatizo
kubwa la upungufu wa nguvu za kiume, na wewe usije kuwa miongoni mwao,” alisema
huku akitabasamu.
Japokuwa mwenyewe alichukulia kama masihara
lakini kwa hulka za kiume, niliona kama amenidharau sana. Maneno yake ni kama
yalikuwa yakihitaji nifanye kitu fulani kumthibitishia kwamba sikuwa mtu wa
mchezomchezo bali mwanaume niliyekamilika.
Nilipounganisha na tukio la yeye kunibusu
kwenye midomo yangu wakati akinipongeza, akili nyingine zilianza kupita ndani
ya kichwa changu.
“Kwa hiyo unaishije bila mume?”
“Kwani wewe unapata faida gani
kubadilishabadilisha wanawake?” aliniuliza swali juu ya swali ambalo
lilinifanya nijiulize sana kwa nini alikuwa akinikomalia kuhusu suala la mimi
kuwa na wanawake wengi. Elimu aliyonipa ilikuwa imetosha kunifanya nijitambue
lakini kwa nini alikuwa akiendelea kuulizauliza kuhusu mimi kuwa na wanawake?
Sikupata majibu.
“Mbona unakuwa mkali sana kwangu Junaitha? Au
kuna kitu nimekuudhi?”
“Ndiyo umeniudhi, kwa nini kijana mtanashati
kama wewe usitafute mwanamke mmoja tu anayejitambua ukatulia naye?” nilijikuta
nikishindwa kujizuia, nikaangua kicheko kwani tayari nilishaanza kupata picha
ya kilichokuwa kikiendelea ndani ya kichwa chake.
“Kwa hiyo unanidharau si ndiyo? Yaani mi
naongea mambo ya maana wewe unacheka,” alisema, akatoka na kuniacha nimesimama
palepale, nikiwaangalia wale waliokuwa wamelala juu ya zulia, kila mmoja akiwa
hajitambui kwa uchovu.
“Hebu njoo huku,” nilisikia sauti ya Junaitha
ikitokea chumbani kwake, harakaharaka nikatoka pale na kuelekea kule sauti
ilikokuwa inatokea.
“Ingia tu mlango upo wazi,” alisema, nikageuka
huku na kule kwanza kwa sababu sikuona kama ni heshima kwa mtoto wa kiume
kuingia chumbani kwake, hasa ukizingatia ukweli kwamba alikuwa amenizidi sana
umri. Nikapiga moyo konde na kuingia ndani ya chumba hicho cha kisasa
kilichokuwa na vitu vingi vya thamani.
“Chukua taulo pale kabatini ingia bafuni
ukaoge,” alisema akiwa amekaa juu ya kitanda kikubwa cha kisasa akihangaika
kufungua zipu ya gauni alilokuwa amevaa, nikaelekea pale kwenye kabati
aliponielekeza, nikachukua taulo na kuanza kuelekea kwenye lile bafu la ndani
kwa ndani kule chumbani kwake.
Nililazimika kuingia na nguo zote bafuni kwani
nilikuwa naona aibu kuvua hata shati mbele ya macho yake.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment