Tuesday, December 12, 2017

The Graves of The Innocents (Makaburi ya Wasio na Hatia)- 53


ILIPOISHIA:
“Kwa nini unanifanyia hivi Togo? Ina maana nimekosea kukupenda?” alisema huku machozi yakizidi kumtoka, nikaanza kumbembeleza huku nikimfuta machozi, nikimchombeza kwa maneno matamu, zoezi hilo lilienda sambamba na kupashana misuli, tayari kwa mpambano wa kukata na mundu.
SASA ENDELEA...
Sijui baba alijuaje kinachotaka kufanyika kule chumbani kwani wakati tukiwa kwenye maandalizi ya mwishomwisho kuelekea kwenye mpambano huo wa kirafiki, kila timu ikiwa imekamia mchezo, tulishtuka baada ya kusikia mlango ukigongwa kwa nguvu, Rahma akakurupuka na kuvaa nguo zake harakaharaka, mlango ukawa unaendelea kugongwa kwa nguvu.
Ilibidi na mimi nivae zangu na kwenda kufungua, baba akaingia mzimamzima akiwa ameongozana na baba yake Rahma.
“Kuna nini kinachoendelea hapa,” baba aliuliza huku akitazama huku na kule. Hali aliyoikuta mle ndani, ilitosha kutoa majibu juu ya kilichokuwa kikitaka kufanyika, nikavaa sura ya ‘ukauzu’ na kumjibu:
“Rahma alikuwa ananitoa miiba miguuni.”
“Miba gani?” baba aliniuliza kwa ukali, ikabidi niinue nyayo zangu na kumuonesha, wote wawili wakanisogelea na kuanza kunitazama kwa makini. Niliona wametazamana kisha wakapeana kama ishara fulani.
“Rahma nenda kwa wenzako jikoni, kesi yako itaamuliwa na mama zako,” baba yake Rahma alisema kwa sauti ya chini, harakaharaka Rahma akasimama na kutoka, huku akionesha dhahiri jinsi alivyokuwa na hofu ndani ya moyo wake.

 “Najua unampenda binti yangu Togo, lakini nakuomba sana mwanangu, ukifanya naye mapenzi tutampoteza, yeye si miongoni mwa jamii yetu na mwili wake hauna kinga yoyote, hebu zingatia sana ninachokwambia, nakuomba usimguse,” baba yake Rahma alizungumza kwa sauti ya chini lakini yenye msisitizo mkubwa.
Tofauti na baba ambaye kila akiongea alikuwa akifokafoka, baba Rahma alikuwa akizungumza kwa utaratibu sana na nikajikuta nikimuelewa sana.
Jambo ambalo nilishindwa kulikataa ndani ya moyo wangu ni kwamba nilikuwa nikimpenda sana Rahma kwa hiyo akili za harakaharaka zilianza kunituma kufikiria namna ninavyoweza kukivuka kikwazo kilichokuwepo kati yetu kwani kiukweli sikuwa tayari kumpoteza.
“Kwa hiyo na yeye akiwa miongoni mwetu tutaruhusiwa kuoana?” niliuliza swali ambalo liliwafanya baba na baba Rahma watazamane kwa sekunde kadhaa.
“Lakini si unajua kwamba mwenzako anasoma na siku chache zilizopita mama yake alikuwa akifuatilia mambo ya chuo?”
“Hata akimaliza hakuna shida,” nilijibu huku nikiwa na wasiwasi na atakachokisema baba.
“Wewe mtoto mpumbavu sana, yaani umeshupalia kabisa, ina maana hujui kama nyie mmeshakuwa ndugu? Halafu hiyo michezo ya mapenzi umeianza lini wakati wewe bado mdogo?”
“Lakini baba mimi nampenda Rahma.”
“Unampenda? Unajua maana ya kupenda wewe? Toka lini wewe ukampenda mtu? Hebu toa wendawazimu wako hapa, yaani badala uelekeze nguvu kwenye ulimwengu mpya tuliokufunulia unaanza mambo yako ya mapenzi hapa, una akili wewe?” baba alinifokea.
“Hapana, huna haja ya kuwa mkali mzee mwenzangu,” baba yake Rahma alimkatisha baba kisha akanisogelea pale nilipokuwa nimekaa.
“Unampenda kwa kiasi gani?”
“Nampenda sana baba.”
“Lakini nyie mmeshakuwa ndugu?”
“Mbona undugu wetu siyo wa damu?”
“Kama kweli unampenda, nakuomba uzingatie nilichokwambia, hayo mengine tuachieni sisi wazazi wenu,” baba yake Rahma alisema kwa upole. Ilihitaji ujasiri mkubwa kuzungumza mambo yale mbele ya baba lakini kwa kuwa baba Rahma alikuwa mwelewa, na mimi nilijikuta nikipata nguvu.
Majibu aliyonipa, yaliufanya moyo wangu ufurahi sana, nikajiapiza kwamba sitakutana naye tena kimwili kwa kuhofia kumpoteza lakini nikawa nafikiria mbinu nyingine mbadala na harakaharaka akili zangu zilinituma kutafuta muda wa kutosha wa kukaa na Rahma na kumweleza ukweli kuhusu mimi, baba na baba yake na mwisho nimshawishi na yeye ajiunge kwenye jamii yetu.
Tayari nilishaanza kuona dalili za ushindi, tabasamu pana likachanua kwenye uso wangu, hisia tamu zikawa zinapita kwenye mishipa yangu huku nikivuta picha ya miaka kadhaa baadaye, nikiishi na Rahma kama mume na mke halali.
“Kilichotuleta hapa siyo hiki tulichokuwa tunakizungumza,” baba yake Rahma alivunja ukimya, baba akawa anatingisha kichwa kukubaliana naye huku akiwa amenitolea macho ya ukali.
“Leo umefanya kitu cha ajabu sana na kama isingekuwa nguvu za ziada kutumika, ungeweza hata kuuawa kule Mlandizi, kama hiyo haitoshi umesababisha majanga mengine ambayo hayakuwepo kwenye ratiba, umesababisha yule dereva wa bodaboda amepoteza maisha,” alisema baba yake Rahma, kauli ambayo ilinishtua kuliko kawaida.
Kilichonishtua zaidi ni kusikia kwamba yule dereva wa bodaboda amekufa, moyo ulishtuka kuliko kawaida.
“Kibaya zaidi umesababisha watu hapa mtaani waanze kututilia mashaka, kwa nini umeenda kumroga huyo kijana dereva wa Bajaj hapo nje? Hujui kama ni hatari sana watu kujua kama unajishughulisha na haya mambo ya giza? Mtoto mpumbavu sana wewe,” baba aliongezea kwa ukali, nikajiinamia kwani kiukweli nilikuwa nimefanya makosa makubwa.
“Lakini nilikuwa nataka kujifunza,” nilijibu kwa sauti ya chini, baba yake Rahma akaniambia kwamba mambo hayo huwa hujifunzi kama unavyojifunza mambo mengine, bali kuna utaratibu wake.
Akaniambia kwamba nilichokifanya kilikuwa makosa makubwa kwa watu wa jamii yetu na kama zilivyo sheria, yeyote anayeenda kinyume lazima akumbane na rungu la Mkuu. Kauli hiyo ilizidi kunitisha moyoni mwangu, nikajaribu kuvuta taswira ya Mkuu, yule kiongozi wa watu wa jamii yetu, hofu ikazidi kunijaa.
“Ili kumfurahisha, inabidi usiku wa leo ufanye juu chini nyama zipatikane, tukifika tutaenda kukuombea msamaha na kwa kuwa utakuwa na mzigo, bila shaka atakupa adhabu ndogo, kinyume na hapo anaweza hata kuamuru uliwe nyama ukiwa hai,” alisema baba yake Rahma, nikajikuta nikitokwa na kijasho chembamba.
Baba Rahma aliniona hali niliyokuwa nayo, akaniambia nisijali watanisaidia lakini kitu cha kwanza, ilikuwa ni lazima nikatoe sadaka ya kitu ninachokipenda zaidi, nje ya familia yangu.
Sikumuelewa kauli yake hiyo, akanifafanulia kwamba wanaposema kitu, kwenye imani yao wanamaanisha mtu kwa hiyo ilikuwa ni lazima nimfikirie rafiki yangu ninayempenda zaidi ambaye ndiye angetolewa kafara usiku ili mimi nisamehewe na Mkuu kwa kitendo changu cha kwenda kwenye msiba wa mtu ambaye tumemla nyama na mimi ndiye niliyesababisha kifo chake.
“Mimi sina rafiki hapa mjini, kwanza sijazoeana na mtu yeyote,” nilijitetea, baba akaniambia kwamba anawajua marafiki zangu wengi tu Chunya.
“Sasa nitaendaje Chunya?”
“Hutakiwi kuhoji kwa sababu hakuna kisichowezekana, unachotakiwa ni kututajia mtu, vinginevyo wewe ndiyo utaaliwa leo,” baba alisema, mapigo ya moyo wangu yakawa yananienda mbio kuliko kawaida.
Nimewahi kusikia kwamba wachawi huwa na kawaida ya kuwatoa kafara watu wao wa karibu na ndiyo maana watu wakishajua kwamba wewe ni mchawi wanajitenga na kukuogopa sana lakini nilikuwa naona kama ni hadithi za kufikirika tu, lakini sasa yalikuwa yamenifika.
Ni kweli nilikuwa na marafiki wengi wanaonipenda kule nyumbani Chunya lakini sikuwa tayari hata kidogo kuona mtu yeyote asiye na hatia anapatwa na matatizo kwa sababu yangu. Nilijikuta nikijilaumu sana kwa upumbavu wangu wa kutaka kwenda kujionea mwenyewe kilichotokea kule Mlandizi.
“Tunasubiri jibu lako,” baba alinizindua kutoka kwenye lindi la mawazo.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...