ILIPOISHIA:
Nilichopanga kichwani, ni kuchukua
maelekezo vizuri kwa yule mtu aliyesema marehemu ni jirani yake kisha kwenda
kwanza mpaka eneo la ajali na baada ya hapo, nitakwenda Tumbi kujionea hali ya
mgonjwa na hiyo maiti kama nitapata nafasi. Nilikuwa na shauku kubwa ya kujua
kila kitu maana moyo wangu ulikuwa na hatia kubwa, hasa kutokana na jinsi
taarifa za ajali ile zilivyowaumiza mioyo abiria wengi.
SASA ENDELEA...
Safari iliendelea na hatimaye tukawasili
Kibaha, gari liliposimama tu, nilimuwahi yule abiria aliyekuwa akisimulia
kuhusu ile ajali, nikamsalimu na kumuomba anielekeze ulipo msiba kwa sababu
aliyefariki ni ndugu yangu.
“Ni Mlandizi, ukishuka tu pale kituoni,
uliza mtu yeyote eti kwenye msiba wa mtoto aliyekufa kwenye ajali ni wapi?
Huwezi kupoteza, mtoto alikuwa anafahamika sana yule kutokana na jinsi
alivyokuwa na heshima,” alisema yule abiria, nikamshukuru.
Nilipoachana naye, nilimfuata dereva ili
anielekeze sehemu gari lilipopata ajali kwani kuna muda nilimsikia akisema
kwamba eneo hilo ni baya sana, ajali huwa zinatokea mara kwa mara. Eneo lenyewe
nilikuwa nalifahamu lakini sikujua naweza kufikaje.
“Siyo mbali sana kutoka hapa, hata kwa
miguu unaweza kufika, panaitwa machinjioni,” alisema yule dereva, nikamshukuru
na kuanza kutembea kuelekea eneo la tukio. Tayari kulishaanza kupambazuka na
lile giza la afajiri lilianza kupungua na kumezwa na nuru ya alfajiri.
Kila nilipokuwa napita, wafanyabiashara
na wasafiri walikuwa wakizungumzia ajali iliyotokea usiku wa siku hiyo. Kila
mtu alikuwa akizungumza lake lakini kama baba alivyoniambia usiku, eneo hilo
huwa linatumiwa sana na wachawi, hasa waliopo mafunzoni kama mimi kusababisha
ajali.
Kila mtu alikuwa anashauri eneo hilo
watafutwe waganga waliobobea au wachungaji wakaliombee kwani kulikuwa na nguvu
za giza au ‘nyoka chunusi’ anayesababisha ajali. Njiani sikuwa peke yangu,
baadhi ya watu nao waliposikia kuhusu ajali hiyo, walitaka kwenda kujionea
wenyewe.
Niliongozana na vijana kadhaa, tukawa
tunatembea pembeni ya barabara na dakika kadhaa baadaye, tulifika eneo ajali
hiyo ilipotokea. Nilipofika eneo hilo, nilishangaa nywele zikianza kusisimka
kuliko kawaida huku harufu ya damu ikitawala kwenye pua zangu. Gari lililopata
ajali bado lilikuwa eneo la tukio, pembeni ya barabara, yaani kwa jinsi lilivyokuwa
limeharibika, kila mmoja alibaki kushika kichwa.
Mjadala uliotawala kwa wote waliokuwa
wamefika kushuhudia ajali hiyo, ulikuwa ni nini kilichosababisha ajali hiyo.
Kwa sababu kulishapambazuka, niliweza kuliona vizuri eneo hilo, lilikuwa ni
tambarare kabisa, hakukuwa na kona wala mteremko, achilia mbali mlima wa kuweza
kusababisha ajali mbaya kiasi kile.
Nilitazama kule tulikokuwa tumekaa na
baba na baba yake Rahma, ambako baada ya kuuchukua ule mwili wa yule mtoto
niliupeleka, nikashangaa kuona kwamba eneo lote lilikuwa jeupe kabisa kiasi
kwamba ungeweza kuona umbali wa karibu mita mia tano.
Hakukuwa na miti wala vichaka, eneo lote
lilikuwa jeupe kabisa. Nikawa najiuliza pale kwenye migomba tulipokuwa tumekaa
ni wapi? Ule mgomba uliokatwa kisha nikapewa ulitoka wapi? Nikahisi labda
nimechanganya upande, nikageukia upande wa pili wa barabara, nako kulikuwa
kweupe kabisa, nikawa ni kama nimechanganyikiwa.
“Vipi kijana, mbona unaonesha kutotulia?
Unatafuta nini?” niligeuka baada ya kusikia sauti hiyo, nikamtazama aliyekuwa
akinisemesha. Alikuwa ni mzee mmoja mwenye ndevu nyingi zilizofunika mdomo
wote. Mkononi alikuwa na mkongojo na kwa jinsi alivyokuwa amevaa, ilionesha
haishi mbali na eneo hilo.
“Aah! Hamna kitu, nashangaa tu jinsi hii
ajali ilivyotokea.”
“Mh! Hebu nitazame usoni,” alisema,
nikamtazama na yeye akanitazama. Kitendo cha kutazama naye tu, nilihisi ile
hirizi niliyoivaa mkononi ikinibana. Maelezo aliyonipa baba, ni kwamba nikiona
inanibana ghafla, lazima kutakuwa na mtu eneo hilohilo mwenye nguvu za giza
anajaribu kunipima.
Akaniambia nikishaona hali hiyo, haraka
sana nizibe kucha ya mkono wa kushoto kwa kutumia kidole gumba cha mkono
huohuo, jambo ambalo nililifanya bila yule mzee kunishtukia. Nikashangaa
ameanza kupiga chafya mfululizo, tena kwa nguvu. Alipiga chafya kama kumi hivi,
kamasi na machozi vikawa vinamtoka kwa wingi, mpaka watu wengine waliokuwa eneo
hili wakawa wanamshangaa.
“Mtoto mbaya sana wewe, mtazame bichwa
lake,” alisema mzee huyo kwa hasira, akawa anaondoka huku akiendelea kunitukana
na kupiga chafya.
“Hivi vizee ndiyo vichawi vyenyewe,
unakiona kile kibabu kilivyokuwa kinapiga chafya, inaonesha kimenogewa na
harufu ya damu,” alisema mmoja kati ya watu waliokuwa eneo lile, wengine
wakacheka huku wengine wakiendelea kusikitika.
“Mbona yule mzee anakutukana, kwani
umemfanya nini?”
“Mzee gani?”
“Yule aliyekuwa anapiga chafya?”
mwanamke mmoja wa makamo aliniuliza, kumbe alikuwa ameshuhudia kila kitu,
nikaamua kuvunga maana kuendelea kuzungumza kungefanya watu waanze kunitazama
kwa makini, jambo ambalo sikuwa tayari kuona likitokea.
“Mh! Labda umeangalia vibaya, mbona mimi
simfahamu na wala sijaongea naye chochote?” nilijibu huku nikigeuka na kumpa
mgongo yule mwanamke, nikaona bado ananifuata kwa manenomaneno.
“Itakuwa kuna jambo baya umemfanyia,
haiwezekani mzee kama yule aanze tu kukutukana, nataka uniambie, unajua yule ni
nani kwangu,” alisema mwanamke huyo huku akizidi kunisogelea mwilini. Kitendo
cha kunisogelea tu, nilishtukia ile hirizi ikianza tena kunibana, safari hii
kwa nguvu kuliko mwanzo.
Ikabidi nikae chonjo kwa sababu ubanaji
wake ulikuwa wa nguvu na baba alishaniambia kwamba ukiona inabana kwa nguvu,
ujue upo jirani na mtu mwenye nguvu kubwa ambaye usipokuwa makini anaweza
kukudhalilisha mbele za watu.
Haraka niliibana kucha ya kidole kidogo
kwa kidole gumba changu na safari hii, nilitumia mikono yote miwili. Kwa mtu
asiyejua, angeweza kudhani labda nachezea tu vidole vya mikono yangu kumbe
nilikuwa na shughuli nyingine kabisa.
Kitendo hicho kilisababisha mwanamke
yule awe ni kama amepandwa na mashetani, akaanza kukimbia huku na kule huku
akiongea maneno yasiyoeleweka, akawa anasema kwamba eti pale eneo la tukio
pamejaa wachawi na yeye ni miongoni mwa hao wachawi.
Kila mtu alibaki kumshangaa, ikabidi
niachie vidole haraka maana kwa jinsi alivyokuwa akiongeaongea huku mara kwa
mara akinigeukia na kunitazama kwa macho ya woga, angeweza kunisababishia
kizaazaa.
Nilipoachia tu vidole vyangu, alidondoka
chini na kuzimia, wanawake wengine wawili ambao inaonesha ni kama alikuja nao,
wakawa wanampepea huku wakinitazama kwa macho mabaya. Kwa hali ilivyokuwa,
ilibidi tu nianze kuangalia utaratibu wa kuondoka eneo hilo maana hali
ilishaanza kuwa tete na sikutaka akizinduka anikute bado nipo eneo hilo.
Nilizugazuga kisha nikajichanganya na
watu waliokuwa wakielekea kule upande wa stendi, tayari kulishapambazuka na
kijua cha asubuhi kilishachomoza. Kilichonishangaza, ni kugundua kwamba licha
ya ajali yenyewe kutokea katika mazingira ya kishirikina, bado kulikuwa na
wachawi miongoni mwa watu waliokuwa wakishuhudia kilichotokea.
Nilipanga niende kwanza msibani kisha
nikiwa narudi ndiyo nipitie kule Hospitali ya Tumbi kwenda kumwangalia majeruhi
wa ajali ile na kama ikiwezekana nikaione na maiti ya huyo mtoto maana ukweli
ni kwamba mimi ndiye niliyemchukua kutoka eneo la tukio na sehemu yake nikaweka
kipande cha mgomba.
Nilikuwa na shauku kubwa sana ya kutaka
kujua mambo mengi ambayo kwangu yalikuwa mageni kabisa. Nilipofika stendi,
sikuwa na muda wa kupoteza, nilipanda kwenye gari linaloenda Mlandizi ambalo
nalo ilikuwa ni lazima lipite pale eneo la ajali.
Safari ilianza, tulipokaribia eneo hilo,
nilitoa kichwa nje ili nichungulie tena, nikamuona yule mwanamke aliyekuwa
akinichokoza akiwa amekaa kitako chini kuonesha kwamba fahamu zimemrudia, ndugu
zake wakawa wanajaribu kumuinua. Nilijikuta nikitabasamu huku moyoni
nikijisikia fahari kubwa kuwashikisha adabu waliokuwa wakitaka kunichokoza.
Baada ya muda, gari liliwasili Mlandizi,
hiyo ndiyo ilikuwa mara yangu ya kwanza kukanyaga ardhi ya eneo hilo.
Niliposhuka, niliwauliza wenyeji mahali kulikokuwa na msiba ambapo bila hiyana
walinionesha. Tayari watu wengi walikuwa wamekusanyika nje ya nyumba moja nzuri
na ya kisasa, huku wengine wakihangaika kuweka maturubai.
Nilipofika, na mimi nilijifanya ni
mwombolezaji wa kawaida tu, nikawasalimia baadhi ya watu kisha nikajichanganya
na waombolezaji wengine. Ghafla nilishtuka baada ya kuona kitu ambacho
sikukitarajia, nikahisi kijasho chembamba kikianza kunitoka, mara hirizi yangu
ikaanza kunibana kwa nguvu, kufumba na kufumbua kamba yake ikakatika,
ikadondoka chini!
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment