ILIPOISHIA:
“Tunaenda Chunya, hutakiwi kwenda
kinyume na maelekezo tunayokupa, ukifanya uzembe tu, kitakachokutokea ni juu
yako,” alisema baba kwa sauti ya msisitizo, nikawa natingisha kichwa
kukubaliana naye. Tulikaa chini na kuweka kama duara hivi, tukashikana mikono
kisha nikaambiwa nifumbe macho.
SASA ENDELEA...
Kweli nilifumba macho, baba na baba yake
Rahma wakawa wanazungumza maneno fulani ambayo sikuwa nayaelewa kwa
kuyarudiarudia, kisha nikaanza kusikia kama upepo mkali ukianza kuvuma kwa
nguvu, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka niliposikia baba akinitingisha kwa
nguvu.
“Tumeshafika! Fumbua macho,” alisema
baba, nikafumbua macho na kujikuta nikiwa kwenye mazingira tofauti kabisa.
Sikuelewa tumetumia muda gani maana ninachofahamu mimi kuna umbali mrefu sana
kutoka Mbeya mpaka Dar es Salaam, ni safari ya kutoka alfajiri na mapema na
kufika usiku.
“Unashangaa nini tumeshafika!” baba
alisema huku akinivuta mkono maana kiukweli nilikuwa nimepigwa na butwaa,
nikishangaa huku na kule, nikijaribu kukumbuka kama eneo lile nalifahamu.
“Mungu wangu!” nilijisemea moyoni baada
ya kugundua kwamba tulikuwa kwenye shule ya msingi niliyosoma pale Chunya,
chini ya mti mkubwa uliokuwa nyuma ya shule ambao kwa kipindi kirefu nilikuwa
nikisikia watu wakisema kwamba una majini.
“Tumefikaje huku?” niliuliza nikiwa bado
nashangaashangaa nikiwa siamini. Yaani nifumbe macho nikiwa kwenye makaburi ya
Wagiriki, Kunduchi jijini Dar halafu ninapofumbua macho muda mfupi baadaye,
usiku huohuo nijikute nipo Chunya, ilikuwa ni zaidi ya maajabu.
“Huu si muda wa maswali,” baba
aliniambia huku akinitaka niongeze mwendo, tukawa tunatembea kuelekea upande wa
Magharibi mwa shule, kulipokuwa na njia ya kuingilia na kutokea shuleni hapo.
Baba alikuwa mbele, mimi katikati na
nyuma alikuwepo baba yake Rahma, tukawa tunatembea na baadaye tukafika kwenye
eneo la uwanja wa shule. Japokuwa ilikuwa ni usiku, uwanja ulionesha kuwa na
pilikapilika nyingi sana, watu wengi walikuwa wamekusanyika na kuweka makundi
matatu, kundi la kwanza lilikuwa upande wa goli la kwanza, wengine walikuwa
katikati ya uwanja na wengine kwenye goli jingine.
Ilionesha kama kuna shughuli fulani
zinaendelea ingawa zilionesha kwamba si za kawaida kwa sababu watu wengine
walikuwa watupu, wengine walikuwa wakicheza ngoma za kienyeji na wengine
walikuwa wamekaa chini.
“Hutakiwi kugeuka nyuma, ni mwiko,” baba
aliniambia wakati tukiendelea kuchanja mbuga, tukawa tunapita kwenye njia
ambayo wakati nasoma, ndiyo niliyokuwa nikiitumia kwenda na kurudi shule.
Tulipita kwenye vichaka kadhaa na
baadaye tukatokezea kwenye nyumba za nyasi zilizokuwa pembezoni mwa kijiji,
tukasimama ambapo baba aliniambia kwa sababu mimi ndiye ninayefahamu nyumbani
kwa huyo rafiki yangu, Sadoki ambaye ndiye niliyemchagua kumtoa kafara,
nitangulie mbele.
Akarudia kunisisitiza kwamba sitakiwi
kugeuka nyuma wala kuzungumza hovyo, kazi yangu ni moja tu, kuongoza njia.
Nilitii nilichoambiwa huku nikitetemeka sana. Mara kwa mara taswira ya Sadoki
ilikuwa ikinijia ndani ya kichwa changu, nikawa najisikia uchungu mno ndani ya
roho yangu hasa kutokana na ukweli kwamba yeye ndiye aliyekuwa tegemeo la
familia yao.
Niliongoza njia na kwa sababu vichochoro
vyote vya Chunya nilikuwa navijua kwa sababu hapo ndipo nilipozaliwa na
kukulia, sikupata tabu. Baada ya kutembea kwa dakika kadhaa, hatimaye
tuliwasili kwenye nyumba chakavu ya akina Sadoki. Nikaonesha kwa ishara kwamba
tayari tumeshafika, baba akanivuka na kutangulia mbele.
Kwa muda wote huo, baba yake Rahma
alikuwa kimya kabisa, baba akaanza kutoa maelekezo kwamba tunatakiwa kuizunguka
nyumba hiyo mara saba, kutokea upande wa kulia kwenda kushoto. Nilichojifunza,
mambo mengi yanayofanywa na watu wa jamii hizi, huwa yanakwenda kinyume na
utaratibu wa kawaida, tukaanza kufanya vile baba alivyosema.
Tulikuwa tukipiga hatua fupifupi huku
baba na baba Rahma wakiimba nyimbo fulani za kutisha ambazo hata sikuwa
nazielewa, tukazunguka mpaka ilipofika raundi ya saba, tukamalizia pale kwenye
kona ya nyuma tulipoanzia kuzunguka.
Baba alipiga mguu wa kushoto chini, mara
ukuta ukawa kama umefunguka, akatangulia yeye kuingia kinyumenyume, akapotelea
ndani.
Tukabaki mimi na baba Rahma, akaniambia
na mimi nipige mguu wa kushoto chini kwa nguvu, nikafanya hivyo, ule uwazi
ukatokea tena, akanielekeza kuingia kinyumenyume, nikafanya hivyo na kujikuta
nipo ndani, pembeni ya baba ambaye alikuwa amesimama akitusubiri.
Mara baba yake Rahma naye akaingia kwa
mtindo uleule. Wasichokijua wengi ni kwamba watu wabaya wanapoamua kuingia
ndani ya nyumba yako, huwa hawatumii mlango kwa hiyo hata ufunge milango kwa
makufuli makubwa, ujenge fensi hata yenye umeme na uweke walinzi wenye silaha
nzito, huwezi kuwazuia watu wenye nguvu za giza kuingia ndani kwako.
Maisha waliyokuwa wakiishi akina Sadoki
yalikuwa ya chini sana maana hata sebuleni kwao hakukuwa na kitu chochote cha
maana zaidi ya viti vya mbao na meza ndogo, na vyombo vya jikoni. Japokuwa
nyumba yote ilikuwa giza, cha ajabu ni kwamba nilikuwa na uwezo wa kuona kila
kitu, mpaka kijiko.
Tulianza kutafuta chumba anacholala
Sadoki na kwa sababu nilishawahi kuwa naingia mpaka chumbani kwake,
niliwaongoza, tukaenda mpaka kwenye chumba chake na kumkuta Sadoki akiwa
amelala na mdogo wake wa kiume juu ya kitanda cha kamba.
Kwa wale waliowahi kuishi vijijini
watakuwa wananielewa vizuri ninapozungumzia kitanda cha kamba. Maskini! Sadoki
alikuwa akikoroma pamoja na mdogo wake, wakiwa hawaelewi chochote
kinachoendelea.
Baba alinielekeza kukizunguka kitanda
hicho na kusimama upande ambao kichwa cha Sadoki kilikuwepo, nikafanya hivyo,
baba akasimama upande wa miguuni na baba yake Rahma akasimama pale katikati.
Moyo ulikuwa ukiniuma sana na sikuelewa
natakiwa kufanya nini, nikawa nasubiri maelekezo tu, huku moyo wangu ukijihisi
kuwa na hatia kubwa mno. Sadoki hakuwa amefanya kosa lolote baya kustahili
adhabu kali kiasi kile maana kama ni kupishana maneno, kilikuwa ni kitu cha
kawaida kabisa kwa marafiki walioshibana.
Baba alinielekeza kuinamisha kichwa
kumuelekea Sadoki pale kitandani, nao wakafanya hivyohivyo kisha baba
akaanzisha wimbo ambao mimi sikuwa naujua, baba yake Rahma akawa anaitikia.
Niliogopa sana kwa sababu walikuwa wakiimba kwa sauti ya juu ambayo ingeweza
kuwaamsha watu waliokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Baada ya kuimba mara kadhaa, baba alitoa
kichupa kidogo kilichokuwa na ungaunga mweusi ndani, akakitingisha kwa nguvu
kisha akampa baba Rahma ili anipe mimi, kikanifikia ambapo alinipa maelekezo
kwa ishara kwamba nikitingishe kwa nguvu kisha nichukue ungaunga kidogo na
kumpaka Sadoki kwenye paji la uso wake.
Nilifanya kama nilivyoelekezwa,
nikampaka kwenye paji la uso kwa kuchora ishara kama ya msalaba hivi, kisha
baba akanipa maelekezo kwamba natakiwa kugeuka na kumpa mgongo Sadoki,
nikageuka, na wao wakageuka kisha baba akapiga makofi akiashiria tugeuke tena.
Tulipogeuka, nilishtuka sana kumuona
Sadoki akiwa amekaa kweye kitanda chake lakini akiwa amefumba macho. Baba
akanielekeza kwamba nimshike mkono, kweli nikafanya hivyo, nikamshika,
akasimama kisha baba akanionesha ishara kwamba nimuangalie kwa makini
anachokifanya.
Alisogea kwenye pembe moja ya chumba na
kupiga mguu chini kwa nguvu, ukuta ukafunguka ambapo alitoka nje kinyumenyume,
huku nikitetemeka na mimi nikasogea kwenye ile kona huku nikiwa nimemshika
Sadoki mikono yake yote miwili. Japokuwa alikuwa amesimama, bado alikuwa
amefumba macho.
Nikapiga mguu chini kwa nguvu na
kugeuka, nikawa nataka kutoka lakini nilishangaa mwili wangu ukiwa mzito kama
ninayevutwa na kitu kurudi ndani. Sijui nini kilitokea kwani nilishtukia baba
Rahma ameyeyuka, nikabaki mimi na Sadoki, nikapiga tena mguu kwa nguvu na
kutaka kutoka lakini safari hii, ukuta haukufunguka kabisa, kijasho chembamba
kikaanza kunitoka.
Nikiwa bado nashangaa nikiwa sijui nini
cha kufanya, Sadoki alifumbua macho, tukawa tunatazama ana kwa ana. Ni kama
fahamu zake zilikuwa zimemrejea kwani alishtuka sana kuniona ndani ya chumba
chake, akageuka huku na kule huku akijaribu kujitoa kwenye mikono yangu kwa
hofu kubwa.
“Togoo! Umeingiaje humu?” aliniuliza kwa
sauti ya juu, nikasikia mlango wa chumba cha pili ukifunguliwa kuashiria kwamba
kuna mtu alikuwa amesikia na sasa anatoka.
“Nimekwisha!” nilijisema huku nikigeuka
huku na kule, sikumuona baba wala baba yale Rahma, Sadoki akanibadilikia na
kunishika kwa nguvu ii nisipate nafasi ya kukimbia.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment