ILIPOISHIA:
“Nataka nikalale na dada Shenaiza,”
alisema kwa sauti ya kudeka huku akinisogelea na kujilaza kifuani kwangu,
nikapitisha mkono wangu na kumshika kiunoni, nikamuona akiruka kama aliyepigwa
na shoti ya umeme.
SASA ENDELEA...
“No! Usifanye hivyo,” alisema Firyaal
huku akinitoa mkono kwa staili ya ‘sitaki nataka’, nikamvutia kwangu na
kusababisha tuwe tunatazamana katika umbali usiozidi nchi tano, kiasi cha kila
mmoja kuwa anazisikia pumzi za mwenzake.
“This is not the right time,” (Huu siyo muda
muafaka) alisema huku akiipitisha mikono yake na kunishika shingoni, kwa mara
nyingine nikamshika kiunoni, akashtuka tena, safari hii kwa nguvu zaidi na
kufumba macho yake mazuri, tukagusanisha ndimi zetu na kuanza kuwaiga njiwa
wanavyoyalisha makinda yao.
Jambo la ajabu lilitokea kwenye hisia
zangu, nikawa nahisi kama nipo kwenye ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa,
tuliendelea kugandana kama ruba kwa sekunde chache, kelele za kitasa cha chumba
alichokuwa amelala Raya ndizo zilizotushtua.
Harakaharaka nikamuachia Firyaal na
kumuonesha kwa ishara kwamba aende chumbani alikokuwa amelala dada yake, kweli
alifanya hivyo, akakimbia kwa kunyata wakati mimi nikienda kumfungulia Raya.
“Vipi?” nilimuuliza baada ya kumfungulia
mlango ambao ni mimi ndiye niliyemfungia kwa nje ili nipate nafasi nzuri ya
kuwa na Firyaal.
“Wewe ndiyo ulinifungia mlango kwa nje?”
“Mh! Saa ngapi tena mpenzi wangu?
Itakuwa labda mlango ulijiloki,” nilimwambia.
“Kwani ulikuwa hujalala mpaka saa hizi?”
“Nilikuwa namsubiri Firyaal arudi ndiyo
nifunge geti, amesharudi na nafikiri muda huu ameshalala na dada yake na mimi
nilikuwa najiandaa kulala,” nilijenga mazingira ya kujitetea. Nikampachika
swali jingine:
“Mbona umeamka wakati ndiyo kwanza
ulikuwa unaanza kulala?”
“Nimeota ndoto mbaya sana mpaka
nimeshtuka,” alisema Raya huku akijinyoosha.
“Ndoto gani tena?”
“Inatisha sana, please Jamal mi siwezi
kulala peke yangu, nakuomba tukalale wote,” alisema Raya huku akinikumbatia,
nikashusha pumzi ndefu kwani niliona ananiharibia sana ‘taiming’ zangu. Hata
hivyo sikuwa na namna zaidi ya kukubaliana naye, nikamshika mkono na kuelekea
naye kwenye kile chumba ambacho Shamila alinipa mimi nilale.
Hata hivyo, moyoni nilishajiapiza kwamba
sitafanya chochote na Raya hasa ukizingatia kwamba tayari nilishampa udhuru
mapema kwamba hali yangu haikuwa nzuri. Baada ya kuingia chumbani, kwa sababu
muda ulikuwa tayari umeenda sana, hatukuwa na cha ziada zaidi ya kupanda
kitandani na kulala.
Japokuwa Raya alikuwa pembeni yangu,
akili zangu zote zilikuwa kwa Firyaal, ni kama nilikuwa nimepandwa na pepo
ndani ya kichwa changu. Nilikumbuka kila kitu kilichofanyika muda mfupi
uliopita, nikawa nazilaumu ndoto za Raya kwani kama asingeota na kushtuka kama
mwenyewe alivyosema, huenda tayari ningeshakuwa naelea kwenye ulimwengu
mwingine tofauti kabisa.
Wasiwasi wangu mkubwa ulikuwa ni je,
Firyaal akija kunigongea usiku huo itakuwaje? Sikupata majibu. Kwa kuwa Raya
alikuwa amechoka sana, nilipomkumbatia tu, hakuchukua muda, akaanza kukoroma
tena, akiwa amelala fofofo. Niliendelea kutafakari mambo mengi na hatimaye
usingizi ukanipitia.
Mlio wa simu ya mezani ndiyo ulionishtua
kutoka kwenye usingizi mzito, nikamsogeza Raya pembeni na kuamka, nikatoka
mpaka sebuleni na kwenda kuipokea simu hiyo.
“Haloo!”
“Haloo Jamal, umeamkaje mpenzi wangu?”
“Ooh! Shamila, ni wewe? Nimeamka salama,
vipi wewe huko?”
“Huku kuna matatizo mpenzi wangu,
nimekupigia kukwambia kwamba inawezekana nikawa sipatikani hewani, ishu
imeshtukiwa huku na imebainika kwamba nimehusika kuwatorosha wagonjwa wawili, wewe
na Shenaiza, hIvi ninavyoongea na wewe tunaingia kwenye mkutano wa dharura na
viongozi wetu pamoja na polisi.”
“Mungu wangu, kwa hiyo itakuwaje?”
“Nimekupigia simu kukutaarifu kwamba
hapo nyumbani kwangu hapafai tena, kuna uwezekano mkubwa polisi wakaja kufanya
upekuzi kwa hiyo nakuomba muondoke haraka iwezekanavyo. Chukua kalamu na
karatasi, andika namba hii nitakayokutajia,” alisema Shamila na kunifanya
mapigo ya moyo wangu yawe yananienda mbio kuliko kawaida.
Nikachukua kalamu na karatasi.
‘Tayari nimeshachukua,” nilimwambia
Shamila baada ya kuuinua tena mkonga wa simu, akanitajia namba hiyo ya simu na kuniambia
kwamba ni ya mama yake mdogo anayeishi Kimara Temboni.
“Nimeshampigia na kumwambia kila kitu,
yupo tayari kuwasaidia, mpigie sasa hivi,” alisema Shamila kisha akakata simu.
Nilipoweka mkonga wa simu chini, nilitazama saa ya ukutani iliyokuwa inaonesha
kwamba ilikuwa ni tayari saa kumi na mbili asubuhi, harakaharaka nikaelekea
kwenye chumba alichokuwa amelala Firyaal na Shenaiza ambaye bado hakuwa amerejewa
na fahamu zake.
“Firyaal, Firyaal,” nilisema huku
nikigonga mlango wa chumba hicho, nilipoona kimya nikanyonga kitasa, kumbe hata
hakuwa amefunga mlango, nadhani alijua kwa vyovyote usiku ule nitamfuata tena.
Nikaingia na kutupa macho kitandani,
Firyaal alikuwa amelala kihasarahasara, akiwa amejifunga khanga moja tu huku
dada yake, Shenaiza akiwa amelala kwenye kitanda kingine maana ndani ya chumba
hicho kulikuwa na vitanda viwili.
Nilishusha pumzi ndefu kwani nikiri
kwamba Firyaal alikuwa akiyafanya mapigo ya moyo wangu yaniende mbio sana, hasa
kutokana na hali niliyomkuta nayo, mwenyewe akiwa hana habari ameuchapa
usingizi.
Taratibu nilimsogelea, nikainama pale
kitandani na kumbusu kwenye paji la uso wake, akafumbua macho na kunitazama, akaachia
tabasamu hafifu na kunishika mkono wangu, joto la kikekike likazidi kunifanya
nisisimke mno.
“Mbona umechelewa kuja Jamal wangu, hata
mlango sikufunga kwa ajili yako,” alisema huku akinivutia pale kitandani ili na
mimi nilale.
“Kuna tatizo Firyaal,” nilimwambia,
kauli yangu ikamfanya ayakodoe macho yake mazuri ambayo yalikuwa yamelegea sana
kwa sababu ya usingizi.
“Tatizo gani tena mpenzi?” aliniuliza
kwa sauti iliyojaa shauku.
“Shamila amepiga simu anasema huko
kazini kwao kimenuka, wamemshtukia kwamba yeye ndiye aliyetutorosha na hivi
tunavyoongea wameingia kwenye kikao cha dharura, anasema inabidi tuondoke hapa
haraka iwezekanavyo,” nilimwambia.
“Mungu wangu,” alisema huku akikurupuka
pale kitandani, akasimama huku akinitazama kwa wasiwasi, mkono mmoja akautumia
kuirudisha ile khanga yake ambayo alipoinuka ilifunuka upande na kusababisha
niyaone tena maungo yake ambayo ama kwa hakika yalikuwa yakimuamsha shetani
wangu wa mahaba.
“Kwa hiyo itakuwaje?”
“Inabidi tujiandae tuondoke, oga fastafasta
kisha muandae mgonjwa, ngoja na mimi nikamuamshe Raya,” nilisema, akatingisha
kichwa huku akiendelea kunitazama kwa macho yake mazuri, nikageuka na kutaka
kutoka, akanishika mkono huku akiliita jina langu.
“Nambie,” nilijibu kwa upole,
akanisogelea hadi mwilini na kunikumbatia kwa nguvu.
“Nakupenda Jamal,” alisema kisha
akanibusu kwenye shavu langu la upande wa kushoto, mwili wote ukasisimka tena,
nikakosa hata cha kujibu zaidi ya mimi kumkumbatia pia na kumbusu, uvuguvugu wa
joto la mwili wake ukanifanya nitamani niendelee kumkumbatia lakini
nilipokumbuka mtihani mzito uliokuwa mbele yangu, nilimuachia, nikatoka haraka
na kwenda kumuamsha Raya, harakaharaka tukaanza kujiandaa.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu
kwenye Championi Jumatatu.
Big story
ReplyDeleteYou are welcome sir
Delete