ILIPOISHIA:
Tangu nizaliwe, sikuwahi kuchinja hata
kuku tu, achilia mbali ndege tuliokuwa tukiwawinda kule kijijini kwetu lakini
sasa eti nilikuwa natakiwa nimchinje binadamu, mtoto asiye na hatia yoyote ili
nifaulu mtihani na kuwa mwanachama kamili, nilijikuta nikitetemeka kuliko
kawaida.
Nilikichomoa kisu pale kiunoni
nilipokiweka, mikono ikawa inatetemeka kuliko kawaida, nikawa namtazama mtoto
yule usoni, nilijikuta nikiingiwa na huruma isiyo ya kawaida.
SASA ENDELEA...
Kisu kikadondoka na kwenda kujikita
kwenye udongo. Nikamuona Mkuu akinikata jicho la ukali, akatembea kwa hatua zenye
vishindo vizito mpaka pale nilipokuwa nimesimama, akainama kwa tabu na
kukichomoa kile kisu, akanishikisha mkononi.
Baada ya hapo aliingiza mkono kwenye
kimkoba chake kidogo cha ngozi, akatoa kichupa kilichokuwa na ungaunga mweusi,
akamimina kwenye viganja vya mikono yake kisha akanipulizia usoni bila kusema
chochote, nikapiga chafya mbili mfululizo kisha nikaanza kuona kama akili zangu
zinabadilika jinsi ya ufanyaji kazi wake.
Hata sijui nini kiliendelea lakini
baadaye akili zangu zilipokuja kukaa sawa, nilikuwa nimeshika kisu kwa nguvu
huku mwili wangu ukiwa umetapakaa damu, watu wote wakawa wanashangilia kwa
nguvu.
Yule mtoto hakuwepo tena pale kwenye
kile kitanda cha miti, nadhani alishaondolewa maana niliwaona watu wengine
kadhaa wakiwa wamezunguka pale ambapo jana yake palikuwa na furushi la nyama,
wakawa ni kama kuna kazi wanaifanya, hakuna hata aliyegeuka nyuma.
Mkuu alinisogelea huku uso wake ukiwa na
tabasamu pana, sikuwahi kumuona akiwa na furaha kama aliyokuwa nayo, akaja na
kunishika kichwani kama mtoto anavyomsalimia mkubwa wake, akanishika pia
kifuani kisha akainama na kunishika vidole gumba vya miguu.
Alipoinuka, alifungua kimkoba chake,
akatoa hirizi nyeusi na kunifunga kwenye mkono wa kushoto, akaniambia kwamba
hicho ndiyo kitambulisho na silaha yangu na kwamba maelekezo mengine nitapewa
na watu walionizidi, watu wote wakapiga makofi kwa nguvu na kuanza kuimba
nyimbo za ajabuajabu huku wakicheza kwa mtindo ambao hata sikuuelewa.
Nilimuona baba akija mpaka pale
katikati, akatoa salamu kwa Mkuu kisha akanikumbatia kwa nguvu. Hakujali zile
damu nilizokuwa nazo, akakichukua kile kisu na kukifuta damu kisha
akakichomesha kwenye mshipi wake kiunoni, akanishika mkono huku akiendelea
kucheza sawa na wale watu wengine, akanipeleka mpaka sehemu aliyokuwa amekaa
yeye na baba yake Rahma.
Sauti ya pembe la ng’ombe ilisikika
kisha watu mbalimbali wakaanza kuja pale nilipokuwa pamoja na baba na baba yake
Rahma, wakawa wananisogelea kisha wanainamisha vichwa vyao kama ishara ya
heshima.
Baba aliniambia kwamba hiyo ni ishara ya
kukaribishwa kwenye ulimwengu wao na kila mwanachama mpya anayetimiza masharti,
huwa anafanyiwa hivyo. Waliendelea kuja kwa wingi lakini wengi sura zao
zilikuwa ngeni kabisa kwangu.
Kulikuwa na wazee, watu wa makamo,
vijana kama mimi na watoto wadogo, wanaume kwa wanawake. Wengine walikuwa ni
wasichana wazuri tu ambao wala usingeweza kudhania kwamba nao wanahusika na
yale mambo. Wengine walikuwa ni watu wazima wenye heshima zao.
Unajua watu wengi huwa wakisikia neno
‘mchawi’, tafsiri ambayo wanaijenga vichwani mwao, ni mtu fulani wa ajabuajabu,
anayetisha, aliyezeeka au aliyedhoofika mwili. Ukweli ni kwamba mchawi hana
alama, mwingine unaweza kuwa unamuona kama bosi fulani, au mwingine unamuona
kama msichana mrembo, mzee wa heshima au mtoto mdogo lakini kumbe akawa
anahusika na mambo hayo.
Wakati wakiendelea kuja, mara nilimuona
Isri akitokezea, akanitazama na mimi nikamtazama, tukatazamana kwa sekunde
kadhaa, tukio ambalo baba aliliona ‘mubashara’, akanigeukia na kunitazama
usoni, nikaacha kumtazama Isri na kumtazama baba kisha harakaharaka
nikakwepesha macho yangu.
Isri alisogea mbele kisha akainamisha
kichwa kama wale wengine wote kisha tararibu akaondoka na kutoa nafasi kwa watu
wengine kuendelea na zoezi hilo. Zoezi likaendelea na baadaye, nilishtuka
kuziona sura za watu ambao niliwakumbuka vizuri.
Wa kwanza alikuwa ni yule bibi kizee
aliyenizabua kibao siku nilipokuwa mahabusu, usiku walioingia na kuanza kuwanga
ndani ya chumba cha mahabusu. Nakumbuka siku aliponipiga na kunisababisha maumivu
makali, nilijiapiza kwamba siku nitakayokutana naye lazima nilipize kisasi.
Wakati akinisogelea, nilitazama kushoto
na kulia, baba akawa ameshajua ninachotaka kukifanya, akanionesha ishara kwamba
sitakiwi kufanya chochote. Yule bibi naye ni kama alinikumbuka, aliponitazama
vizuri usoni akawa ni kama ameshtuka, akasogea kwa kujihami na kutoa ishara
kwangu huku akinitazama kwa macho ya kuibia, moyoni nikajiapiza kwamba ipo siku
yake lazima nilipe kisasi.
Nyuma yake alikuwa ameongozana na wale
watu wote alioingia nao siku ile mahabusu, wote wakawa wananitazama kwa macho
yenye ujumbe fulani, mwisho akatokeza yule ambaye nilisababisha akanasa ndani
ya mahabusu kisha mimi nikatoka kimiujiza.
Tofauti na wenzake wote, huyu alionesha
kuwa na hasira na mimi maana jicho alilonikata, mpaka nilijishtukia, baba na
baba yake Rahma wakawa wanacheka. Ni kama walikuwa wanajua kila kitu
kinachoendelea. Basi pilikapilika ziliendelea kama kawaida, ukafika muda wa
chakula ambapo sikuogopa sana kama siku ya kwanza.
Baada ya hapo, ulifika muda wa kucheza
ngoma za kienyeji na baadaye tulitawanyika, sikujua nimefikaje nyumbani lakini
nilichokuwa nakikumbuka ni kwamba baba na baba yake rahma walinishika mikono,
wakawa wanaagana na wenzao na muda mfupi baadaye, nilijikuta nikiwa kwenye kona
ya chumba nilichokuwa nalala.
Ni hapo ndipo nilipopata muda wa kutosha
kuanza kutafakari kilichotokea, nilijihisi kuwa na hatia kubwa ndani ya moyo
wangu na nikajiapiza kwamba lazima asubuhi niende Kibaha kufuatilia taarifa za
ile ajali na kuona nini hasa ambacho watu wengine watakiona.
Sikupata hata lepe la usingizi, nikawa
najiuliza maswali mengi yasiyo na majibu, mara kwa mara nikawa naitazama ile
hirizi niliyopewa na Mkuu na kuvalishwa kwenye mkono wangu. Ilikuwa nyeusi tii,
ikiwa imefungwa kwa kamba nyekundu.
Kwa kuwa muda ulikuwa umeenda sana, muda
mfupi baadaye kulianza kupambazuka, kwa kuwa sikuwa nimelala kabisa, nilienda
bafuni kutaka kujimwagia maji kupunguza uchovu lakini ghafla nilikumbuka kwamba
baba aliniambia sitakiwi kugusa maji kwa muda wa siku saba.
Ikabidi nijifutefute tu usoni na miguuni
na kwenye yale madoa ya damu kisha nikarudi chumbani kwangu, nikaanza kujiandaa
kuelekea Kibaha. Sikuwa na nauli na sikutaka kumuaga mtu yeyote, nilitaka
kwenda kujionea nini hasa kilichotokea.
Wakati natoka kwa kunyata, nilipitia
sebuleni, nikafungua droo ambayo wenyeji wetu huwa wanaweza chenji zinazobaki
kwenye manunuzi yao, niliijua kwa sababu mara kadhaa nilimuona Rahma akichukua
fedha, nikachukua noti mbili za shilingi elfu mojamoja, nikanyata na kutoka
mpaka nje.
Tofauti ambayo niliiona dhahiri, safari
hii nilikuwa najiamini sana, sikuwa Togo yule wa saa chache zilizopita, mara
kwa mara nikawa najishika pale mkononi kuhakikisha kinga yangu ipo sehemu yake.
Nilipofika mita kadhaa kutoka kwenye
geti kubwa, nilimuona yule kijana aliyekuwa akinicheka mara kwa mara kwamba eti
mimi ni muuaji. Nilikumbuka maneno aliyoyatoa jioni iliyopita wakati nikiwa na
baba na baba Rahma tukielekea kule eneo la tukio, nikaona huo ndiyo muda
muafaka wa kumaliza hasira zangu.
“Broo vipi unaenda?” alisema huku
akisimamisha Bajaj yake jirani kabisa na pale nilipokuwa nimesimama, nadhani
kwa sababu ya kigiza kile cha alfajiri hakuwa ameniona vizuri, aliniponisemesha
na mimi kumtazama usoni, niliona jinsi alivyoshtuka, akataka kuondoa Bajaj yake
haraka lakini alishachelewa.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment