ILIPOISHIA:
Tukaanza kuulizana maana ya kile
kilichofanyika mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila ambapo Junaitha alianza
kutufundisha mambo ambayo hakuna aliyekuwa akiyajua kati yetu, ambayo kama
hujui ungeweza kusema ni uchawi wa hali ya juu.
“Hata ukitaka kuingia benki na kuchukua
kiwango chochote cha fedha unachotaka, inawezekana, mbona rahisi tu,
nitawafundisha,” alisema.
SASA ENDELEA...
“Mh!” niliguna kama ishara ya kutoamini
kile alichokisema, akanigeukia na kuniambia hakuna kitu kisichowezekana chini
ya jua. Alianza kutufafanulia jinsi nguvu zisizoonekana kwa macho zilivyo na uwezo
wa kufanya chochote na kikatimia.
“Hujawahi kuona mtu anakunja kijiko kwa
kukitazama tu au mtu anahamisha glasi ya maji kwa kuitazama tu?” alisema.
Nilishawahi kusikia habari hizo lakini sikutaka kabisa kuziamini mpaka
nishuhudie mwenyewe.
“Kabla ya yote nataka kujua nini
kilichotokea mpaka tukafanikiwa kumuokoa Shamila?” niliuliza, nikamgeukia
Shamila ambaye muda wote alikuwa kimya kabisa, akionesha bado kuwa na hofu
kubwa ndani ya moyo wake.
“Eti kwani wewe ulihisi nini wakati
tumekuja kukuokoa?”
“Yaani hata sielewi kilichotokea,
nakumbuka nilikuwa nimewekwa chini ya ulinzi, tena mambo yakiwa yamenikalia
kooni kwelikweli kwa sababu jambo la kwanza nilitakiwa kulipa bili za matibabu
za wewe na Shenaiza ambazo kimsingi ni kubwa sana kisha baada ya hapo ndiyo
taratibu za kisheria zingefuatia.
“Nilishaanza kuwasikia wakisema kwamba
kwa jinsi tukio lenyewe lilivyokuwa limenikalia vibaya, ningeenda kufungwa,
tena si kifungo cha chini ya miaka saba,” alisema Shamila, akaendelea:
“Nikiwa nimekaa pale ndani ghafla
nikaanza kuhisi kama upepo hivi unavuma, mara wale askari waliokuwa wakinilinda
wakapitiwa na usingizi mzito na kufumba na kufumbua, nilishangaa nikisombwa na
kimbunga kikali na sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipozinduka na
kujikuta humu ndani. Kwani ilikuwaje?” Shamila naye alinigeuzia mimi swali.
“Labda tumuulize mama mdogo,” na mimi
nililikwepa swali, wote tukamgeukia Junaitha ambaye alishusha pumzi ndefu kisha
akatuambia hawezi kueleza kilichotokea kwa maneno machache tukamuelewa,
tunahitaji kukaa darasani na kupata muda wa kutosha kujifunza.
“Ila kwa kifupi kilichotokea ni
uthibitisho wa jinsi kila mmoja wetu hapa alivyo na nguvu kubwa ndani yake
ambayo iwe anajua au hajui, ina uwezo wa kufanya mambo makubwa sana. Na
tukiunganisha nguvu hiyo ndiyo tunaweza kufanya mambo makubwa yakautingisha
ulimwengu wote.
“Ukishajua kucheza na nguvu hizi unao
uwezo hata wa kwenda kuzimu na kurudi, yaani roho ikatengana na mwili kabisa na
kila mmoja akaamini kwamba umekufa kisha baada ya muda ukazinduka tena na kuwa
hai,” alisema Junaitha huku akinitazama, nikajua alikuwa akinilenga mimi jambo
fulani ingawa sikuwa na uhakika.
“Hayo tutaendelea nayo baadaye lakini
niwape onyo, kama kuna yeyote anayeshiriki mapenzi nje ya ndoa aache kwa sababu
hiyo ni sumu kubwa sana katika udhibiti wa nguvu za ndani na najua hakuna
aliyeoa au kuolewa kati yenu. Tuna kazi ya kumzindua Shenaiza kwa hiyo lazima
kila mmoja ajitahidi mwili wake kuwa msafi vinginevyo hakuna kitakachofanyika,”
alisema Junaitha.
Akilini mwangu nilielewa kwa nini
ameyasema maneno hayo, ndani ya kichwa chake alishahisi kwamba miongoni mwa
wale wasichana lazima kuna ambaye natoka naye kimapenzi na kwa sababu tayari
nilishamuonjesha asali, alikuwa tayari kuchonga mzinga ila hakutaka mtu
mwingine yeyote aendelee kuchangia naye.
Aliposema hivyo niliwaona wote watatu,
Shamila, Raya na Firyaal wakinitazama kwa macho ya chinichini kama wanaosema
‘potelea mbali’. Alituchukua wote na kutupeleka kwenye chumba alichokuwa
amelala Shenaiza akiwa hana fahamu.
“Roho yake imekwenda mbali kabisa na
mwili, tunatakiwa kuivuta mpaka irudi mahali pake na hilo likifanyika tu,
atazinduka. Tutakuwa na kazi kubwa kwa sababu licha ya kuwa roho yake imekwenda
mbali, pia nguvu za ubongo wake zimevurugwa na madawa makali aliyokuwa
anachomwa kule hospitalini, haitakuwa kazi nyepesi,” alisema Junaitha kwa
msisitizo.
Wote tukawa kimya kabisa tukisubiri
maelekezo yake, akatuambia kwamba itabidi wenye nguvu kati yetu ndiyo watoke
kuifuata roho yake mahali ilipo na wale wengine wajazie nguvu zao kwetu.
“Narudia tena, haitakuwa kazi nyepesi na
pengine tutachoka kuliko hata ilivyokuwa mwanzo,” alisema, sote tukashusha
pumzi ndefu na kuendelea kumsikiliza. Akatuambia kabla ya yote, kila mmoja
anatakiwa kwenda kuoga kwa maji mengi na kuhakikisha amevaa nguo safi,
akatuambia kama hatukuwa na nguo safi tusijali atatupa mavazi maalum ambayo
huwa anayatumia kwenye shughuli kama hizo.
“Shughuli kama hizi? Zipi?”
“Za kusaidia watu wenye matatizo kama
wewe,” alijibu Junaitha huku akinitazama kwa macho ambayo yalimaanisha yupo
kikazi zaidi. Kwa kututazama, usingeweza kuamini kwamba ndiyo sisi ambao muda
mfupi uliopita tulikuwa tukisakata kabumbu kwenye uwanja wa fundi seremala.
Tofauti na wanawake wengine, Junaitha alionesha kuwa na uwezo mkubwa wa
kuzimudu vyema hisia zake.
Hakukuwa na muda wa kupoteza,
harakaharaka tulienda kuoga, kwa kuwa karibu kila chumba kilikuwa na bafu la
ndani, muda mfupi tu baadaye tayari wote tulikuwa tumeshaoga, ingawa ilibidi
mimi nijitenge peke yangu ili kuzuia mtafaruku unaoweza kutokea.
Muda mfupi baadaye wote tulikuwa
tumevalia mavazi maalum kama yale yanayotumika kwenye hoteli kubwakubwa kwa
ajili ya kulalia, yote yakiwa na rangi nyeupe.
“Hamuoni mmependeza?” alisema Junaitha,
wote tukacheka, tukarudi kwenye chumba alichokuwa amelala Shenaiza. Ilibidi
tusaidiane kumshusha kutoka pale kitandani mpaka chini kwenye jamvi, kisha na
sisi tukakaa mkao maalum wa kukunja miguu na kutengeneza duara kumzunguka
Shenaiza ambaye hakuwa akielewa chochote.
“Tunafanya kama tulivyofanya wakati wa
kumuokoa Shamila,” alisema Junaitha, kwa sababu wote tulikuwa tunakumbuka
tulichokifanya, tulishikana mikono na kufumba macho, kila mmoja akaanza kuvuta
hewa kwa utaratibu maalum na kuiachia, haikuchukua muda eneo lote likatawaliwa
na utulivu wa hali ya juu.
Ile hali ilianza tena kunirudia kama
mwanzo, nikaanza kuhisi kama napaa huku nikishuhudia jinsi mwili wangu
usioonekana ulivyokuwa ukiachana na huu unaoonekana. Tofauti na mwanzo ambapo
nilikuwa nahisi hofu kubwa ndani ya moyo wangu, safari hii nilikuwa najisikia
ku-relax sana.
Kuna muda nilitamani hata maisha yangu
ya kila siku niwe kwenye ulimwengu huo mwingine. Hata hivyo, hali niliyokuwa
naisikia ilikuwa ya muda, ghafla nikaanza kuhisi mtikisiko mkubwa, ukasikika
mlio mkali wa radi na mandhari yakabadilika hapohapo.
Kelele za vyuma vingi vilivyokuwa
vikigongana, pamoja na muungurumo wa kutisha sambamba na moshi mwingi mweusi
unaopalia kooni vikanizingira kila upande.
“Mbona kama nimewahi kufika kwenye haya
mazingira?” niliwaza lakini cha ajabu nikasikia sauti ya kile nilichokuwa
nakiwaza ikijirudia kama mwangwi mkali, nikajua kazi imeanza.
Nilipogeuka huku na kule, nilijikuta
nimekaa kwenye kiti cha chuma kilichokuwa na kutu nyingi, nikageuka tena na
kutazama huku na kule, nikagundua kwamba nipo kwenye lile treni ambalo siku ile
nilipojeruhiwa na kupoteza fahamu kisha kuhamia kwenye ulimwengu mwingine,
nililipanda.
Kwa mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa
wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa
ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo usingizini. Kasi ya treni ilizidi
kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga mbele, milio ya ajabu ilianza
kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa treni lile la ajabu, na giza
totyoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
am waiting for the next one !
ReplyDeleteOk sir
ReplyDelete