ILIPOISHIA:
Sijisifii lakini ukweli ni kwamba katika
suala la mbio, nilikuwa na uwezo mkubwa sana, dakika chache baadaye nikawa
nimeshatokomea kwenye mashamba ya mikorosho na minazi, kelele za wale watu
waliokuwa wakinifukuza zikiwa bado zinaendelea kusikika, sauti ya baba
ikasikika tena masikioni mwangu lakini safari hii, ilikuwa na maelezo ambayo
yalinimaliza kabisa nguvu, nikajua mwisho wangu umewadia. Niliujutia sana
uamuzi wangu wa kujipeleka mwenyewe kwenye mdomo wa mamba.
SASA ENDELEA...
“Inabidi uvue nguo zote na kukimbia
kuelekea upande wa Magharibi mpaka uvuke barabara ya lami kisha kimbia mpaka
utakapoukuta mti mkubwa wa mbuyu, uzunguke mara saba kisha fumba macho,
usifumbue mpaka nitakapokwambia,” sauti ya baba ilisikika masikioni mwangu.
Yaani nivue nguo zote na kuanza kukimbia
nikiwa mtupu? Kibaya zaidi, upande huo wa Magharibi aliokuwa anausema ilikuwa
ni kulekule nilikokuwa nakimbia. Kwa lugha nyepesi nilitakiwa kuanza upya
kukimbia kurudi kule nilikotoka, safari hii nikiwa mtupu! Ilikuwa ni zaidi ya
mtihani.
Kitu pekee nilichokuwa nakihitaji,
ilikuwa ni kuokoa na balaa hilo kwani kwa jinsi wale wazee waliokuwa
wakinikimbiza walivyokuwa na hasira, kama wangenitia mikononi mwao sijui nini
kingetokea. Ilibidi nipige moyo konde, harakaharaka nikavua nguo zote na viatu,
nikavikunja na kuvitia kwapani.
Mpaka namaliza, lile kundi lilikuwa
limenikaribia sana, kitu pekee ambacho nilikuwa nacho makini, ilikuwa ni
kuifunga vizuri ile hirizi yangu mkononi, nikaanza kukimbia kulifuata lile
kundi huku nikiwa na hofu kubwa mno moyoni.
Cha ajabu, japokuwa nilikuwa nikikimbia
kuelekea kule walikokuwa wanatokea, tena nikiwa mtupu kabisa, ilionesha dhahiri
kwamba hakuna aliyekuwa akiniona kwani waliendelea kuangaza macho huku na kule
huku wakiendelea kukimbia. Nikawafikia na kupishana nao katika namna ambayo
nilikuwa makini kuhakikisha simgusi yeyote wala wao hawanigusi kama baba
alivyonieleza.
“Hebu simameni kwanza, mbona nywele
zinanisisimka hivi?” mmoja kati ya wale wazee. Nadhani yeye alihisi uwepo wangu
mahali hapo, wote wakafunga breki na kusimama, wakawa wanatazama huku na kule
lakini walishachelewa kwani nilizidi kutimua mbio kama kiberenge.
Nikakwepa kidogo pale kwenye msiba na
kupita pembenipembeni kwa kasi kubwa, kizaazaa kikawa kuvuka barabara ya lami.
Ikumbukwe kwamba kote huko nilikokuwa napita, japokuwa ilikuwani asubuhi na
kulikuwa na watu, ilionesha dhahiri kwamba hakuna aliyekuwa akiniona ingawa
mimi nilikuwa nawaona vizuri.
Nilipofika barabarani, kuna pikipiki
ilikuwa ikitokea upande wa Morogoro, sikuiona mapema, ile nimeshaingia
barabarani ndiyo nikaishtukia ikiwa inakuja kwa kasi kubwa, nikajua kama
nisipokuwa makini, inaweza kunigonga na kwa kasi iliyokuw anayo, sijui nini
kingetokea.
Nilichokifanya, nilijirusha juu,
nikashangaa mwili umekuwa mwepesi sana, nikamruka yule dereva na bodaboda yake
lakini kwa bahati mbaya, mguu mmoja nilimgonga kichwani, nikaenda kuangukia
ng’ambo ya pili ya barabara na kuinuka haraka, nikataka niendelee kutimua mbio
lakini ghafla nilishtushwa na kishindo kizito barabarani.
Ilibidi nijiibe na kugeuza kidogo shingo
kwa sababu miongoni mwa masharti niliyoelekezwa na baba, ni mwiko kugeuka
nyumaunapokuwa kwenye shughuli zinazotumia nguvu za giza. Nilimshuhudia yule
dereva wa bodaboda akiwa ameanguka katikati ya barabara na kujibamiza kwa
nguvu.
Nilishtuka sana, nikajua kwa vyovyote
mimi ndiyo nimesababisha kwa sababu hata kama yeye hakuwa ameniona, mimi
nilimuona na ndiyo maana nilimkwepa lakini kwa bahati mbaya, nikamgonga
kichwani. Kilichonitisha zaidi, ni kasi aliyokuwa nayo na uzito wa kishindo
chenyewe, nikajua tayari mambo yameshaharibika.
“Mungu wangui, hawezi kupona yule,”
nilisikia sauti za mmoja kati ya waombolezaji waliokuwa pale kwenye msiba kwa
sababu tukio hilo lilikuwa limetokea mita chache tu pembeni, hasa ukizingatia
nilishaeleza kwamba nyumba yenye msiba ilikuwa karibu na barabarani.
Waombolezaji wengi walikimbilia eneo la
tukio kujaribu kutoa msaada lakini wengi walisikika wakisema kwa jinsi
alivyokula mzinga hawezi kupona. Nilitamani kwenda kushuhudia kilichotokea
lakini kwa sababu na mimi nilikuwa na majanga yangu, niliendelea kukimbia.
Nilikimbia sana, miba mikali ikinichoma miguuni lakini sikujali.
Mbele kabisa nikauona mbuyu mkubwa kama
baba alivyonielekeza, nikaendelea kukimbia mpaka nilipoufikia, nikaanza
kukimbia kuuzunguka kutokea upande wa kushoto kuelekea kulia. Nilipofikisha
raundi ya saba, nilisikia kizunguzungu kikali, nikadondoka chini kisha nikaona
kama giza nene likitanda kwenye upeo wa macho yangu, sikuelewa tena
kilichoendelea.
“Wewe Togo, hebu amka,” sauti ya chini
ya baba iliyoambatana na teke zito ubavuni ndiyo iliyonizindua kwenye usingizi
wa kifo, nikafumbua macho na kushtuka nikiwa nyuma ya nyuma ya akina Rahma,
tena nikiwa uchi wa mnyama.
“Vaa nguo haraka, unajifanya mjuaji sana
wewe, siku nyingine sikusaidii, pumbavu,” alisema baba huku akiniongezea teke
lingine la ubavuni lililosababisha nijisikie maumivu makali.
Niliijizoazoa huku nikijiziba sehemu za
mbele kwa mikono yangu, nikaokota nguo zangu zilizokuwa pembeni na kuanza kuvaa
huku nikijiuliza nimefikaje nyumbani bila kupata majibu.
“Sijui kwa nini nimeenda kukuandikisha
mtu mjinga kama wewe,” alisema baba kwa hasira huku akinishika masikio yangu
mawili na kuyavuta kwa nguvu, akiwa ni kama anataka kuninyanyua juu,
akanisindikizia na kofi zito lililosababisha nishindwe kujizua, machozi yakawa
yananitoka.
Zilikuwa zimepita siku nyingi sana bila
baba kunipiga lakini naona siku hiyo nilikuwa nimemuudhi sana, nikawa nahisi
kama masikio yangu yananyofoka kwa jinsi alivyoyavuta kwa nguvu, na ule upande
alionizabua kofi nao nikawa nahisi kama unawaka moto.
“Chumbani moja kwa moja na ole wako
utoke,” alisema baba kwa hasira, nikatembea harakaharaka huku machozi
yakinitoka, uso wangu nikiwa nimeuinamisha. Ile naingia tu mlangoni niligongana
na Rahma lakini kwa kuwa nilikuwa nalia na akili ilikuwa na mawenge,
sikukumbuka hata kumsalimu, nikatembea harakaharaka huku nikichechemea kwani
miguu ilikuwa na miba ya kutosha na sikuwa nimepata hata muda wa kuitoa.
Niliingia chumbani na kujilaza kitandani
nikiwa bado najiuliza nimefikaje eneo hilo, nikalia kwanza kupunguza hasira
zangu kisha nikaanza kutafakari kwa kina mlolongo wa kila kitu kilichotokea.
Yaani ndani ya saa chache tu kulikuwa kumetokea matukio mengi mno ya kutisha,
ya kuhuzunisha, ya kushangaza na kuchanganya kichwa.
Bado moyo wangu ulikuwa na huzuni kubwa
kutokana na hali niliyoiona kule msibani, na japokuwa malengo yangu ya kwenda
Hospitali ya Tumbi kuona hiyo maiti ya yule mtoto hayakuwa yamekamilika, bado
nilikuwana shauku kubwa ya kutaka kujua kilichotokea. Lakini ni hapo pia
nilipokumbuka ile ajali nyingine ya bodaboda niliyoisababisha na pia
nikakumbuka kisanga cha dereva wa Bajaj aliyekuwa akipaki jirani na hapo kwa
akina Rahma na jinsi nilivyomkomesha asubuhi hiyo. Sikujua kama amesharudi au
la na sikujua siku atakaponiona tena atasema nini.
Nikiwa nimezama kwenye dimbwi la mawazo,
nilisikia mlango ukifunguliwa, Rahma akaingiza kichwa na kuchungulia ndani,
macho yangu na yake yakagongana.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment