ILIPOISHIA:
Kwa
mbali niliwaona watu kadhaa wakiwa wamevaa nguo zilizokuwa zikifanana na zile
nilizovaa, lakini kila mmoja akiwa ameinamisha kichwa kuonesha kwamba yupo
usingizini. Kasi ya treni ilizidi kuongezeka na kadiri tulivyokuwa tunasonga
mbele, milio ya ajabu ilianza kusikika kwa mbali, ukichanganya na muungurumo wa
treni lile la ajabu, na giza totoro lililokuwepo, hali ilikuwa ya kutisha mno.
SASA
ENDELEA...
“Poooh! Pooh!” honi kali ya treni
ilisikika ikifuatiwa na msuguano mkali wa vyuma, nikaona watu wote waliokuwa
mle ndani ya treni la ajabu wakirushwa upande wa mbele. Nilijishikilia kwa
nguvu, treni likajisugua juu ya reli na kusababisha cheche nyingi ziruke, eneo
lote likawa kama karakana ya kutengenezea vifaa vya chuma.
Treni liliposimama, nilishtukia
nimeshashuka, hata sikumbuki nilipitia mlango gani, macho yangu yakatua kwenye
kitu kilichosababisha treni hiyo ifunge breki za ghafla kiasi kile. Msichana
mmoja, aliyekuwa na macho yanayong’ara kama paka awapo gizani, nywele ndefu
zilizokosa matunzo na kucha kama mnyama wa porini alikuwa amekaa katikati ya
reli huku akinguruma kama mnyama wa kutisha.
Sijui nilipata wapi ujasiri wa
kumsogelea, kadiri nilivyokuwa nasogea mbele ndivyo msichana yule alivyozidi
kutoa mlio wa kunguruma na kusababisha nipatwe na hofu kubwa mwilini. Lakini
cha ajabu, eti muda huohuo nilikuwa nasikia sauti ya Junaitha ikiniambia
napaswa kuishinda hofu yangu, nikazidi kumsogelea.
Kwa msaada wa taa moja kubwa iliyokuwa
mbele ya lile treni, kufumba na kufumbua, nilishangaa yule niliyekuwa namuona
kama msichana akibadilika na kuwa jibwa lenye meno na kucha ndefu, likaanza
kubweka kwa nguvu huku likitokwa na mate mengi mdomoni.
Kiukweli nafsi yangu ilielemewa na hofu
lakini eti cha ajabu sauti ya Junaitha ikawa inaendelea kusikika ndani ya moyo
wangu ikiniambia sipaswi kuogopa chochote, nikapiga hatua moja mbele na sasa
tukawa tumekaribiana sana na jibwa hilo ambalo lilikuwa likiendelea kubweka kwa
hasira lakini lilipoona sishtuki, liligeuka na kuanza kutimua mbio huku
likiendelea kubweka.
Nikasikia sauti ikiniambia nianze
kulifukuza jibwa lile, bila hata kuuliza nikaanza kukimbia kuelekea kule
lilikokimbilia, huku nyuma nikasikia lile treni likianza kunguruma tena kwa
kasi, moshi mwingi ukatanda eneo lote kisha likaanza kuondoka.
Nilifunga breki za ghafla na kugeuka
nyuma, nilishindwa kuelewa kama lile treni linaondoka mimi nitaondokaje kwenye
mazingira yale ambayo kwanza sikuwa najua ni wapi halafu yalikuwa yakitisha
sana?
“Mkimbize Jamal, utakosa vyote,”
ilisikika sauti ya Junaitha, nikaachana na treni hilo na kuanza kutimua mbio,
lile jibwa lilikuwa likikimbia na kufika mbali kidogo, linasimama na kugeuka
kunitazama, likawa linaendelea kubweka kwa nguvu na likiniona nakuja, linaanza
tena kukimbia.
Japokuwa kulikuwa na giza nene, niliweza
kuyatambua mazingira hayo kuwa ilikuwa ni katikati ya msitu mkubwa wenye miti
iliyofungana kwani hata nilipojaribu kutazama juu, sikuona mwezi wala nyota,
kila sehemu kulikuwa na giza. Kilichosaidia niweze kuelewa jibwa lile
lilikokimbilia, ilikuwa ni mwanga wa macho ya lile jibwa, ambayo sasa yalikuwa
yaking’aa sana.
Niliendelea kukimbia, mara nikajikuta
nimetokezea sehemu iliyokuwa na majimaji, nikawa kila nikipiga hatua nakanyaga
kwenye matope, sikupunguza mwendo, niliendelea kutimua mbio, nikawa najikwaa
kwenye visiki, wakati mwingine nakanyaga miiba lakini sikuchoka, mara
tukatokezea kwenye sehemu ambayo hakukuwa na giza kama kule tulikotoka.
Giza lake lilikuwa ni kama katikati ya usiku
wa manane na mapambazuko, kwamba kunakuwa na giza lakini siyo totoro na kwa
mbali kuna mwanga unaonekana. Hali hiyo ilifanya niweze kuona vizuri mazingira
yote, nikawa pia na uwezo wa kuliona vizuri jibwa lile ambalo liliendelea
kutimua mbio huku likibweka kwa hasira.
“Huyo siyo mbwa, ni binadamu, mganga wa
baba yake Shenaiza, anajua siri nyingi sana kumhusu na ndiye atakayetusaidia
kuiona nafsi ya Shenaiza ilikofungiwa, jitahidi uishike ile kamba yake ya
shingoni, usijali hata kama litakurarua,” sauti ya Junaitha ilisikika tena
ingawa sikuwa na uwezo wa kumuona. Kauli hiyo ilinitisha sana, nikaanza kuamini
kwamba kumbe zile stori nilizokuwa nazisikia tangu kitambo, kwamba kuna
binadamu wanaoweza kubadilika na kuwa mbwa, zilikuwa za kweli.
Nilipiga moyo konde, nikaongeza mwendo
na hatimaye nikawa nimelikaribia kabisa lile jibwa ambalo sasa lilipoona
naelekea kulizidi mbio, liligeuka kwa hasira na kutaka kunirukia, likiwa
limetoa makucha yake. Nilifanya kama nilivyoagizwa na ile sauti, mkono mmoja
nikautumia kuibana miguu yake ya mbele iliyokuwa na nguvu kubwa, likadondoka
chini kama mzigo.
Kwa bahati mbaya sikuweza kuidhibiti
miguu ya nyuma, likaitumia kunirarua mapajani mwangu ambapo kama isingekuwa
uzito wa ile nguo niliyokuwa nimevaa, huenda lingenijeruhi zaidi ya vile.
Japokuwa nilisikia maumivu makali, sikujali,
nikalishika shingoni ambapo lilikuwa limefungwa kwa kamba iliyokuwa na
mafundofundo kadhaa.
“Unaniuaaaa, nisamehe unaniuaaa,”
nilishangaa mno kuona jibwa lile likibadilika na kuwa mtu ambaye alianza kupiga
kelele akiniomba msamaha. Bado nilijihisi kama nipo ndotoni, nikawa nimekodoa
macho nikiwa ni kama siamini.
Nikiwa bado nimepigwa na butwaa,
nilishangaa Junaitha naye akidondoka kutoka kusikojulikana kama mzigo,
harakaharaka akainuka na kujikung’uta, akasogea pale nilipokuwa nimelikaba lile
jibwa ambalo sasa lilibadilika na kuwa mwanamke, tena mzee tofauti na msichana
ambaye nilimuona pale treni liliposimama ghafla.
“Nilikwambia nitakupata tu ukabisha,
sasa yako wapi?” nilimsikia Junaitha akisema wakati akinisaidia kumfunga
mwanamke yule ambaye bado alikuwa akiendelea kupiga kelele huku akifurukuta.
Nilishangaa kugundua kwamba kumbe Junaitha alikuwa akifahamiana na yule mtu wa
maajabu.
Nikawa najiuliza maswali mengi
yaliyokosa majibu, Junaitha alipomaliza kumfunga mikono kwa kutumia kamba za
miti, alihamia miguuni. Akamfunga na kumgeuza, akamburuza na kumkalisha akiwa
ameegamia kisiki cha mti.
“Unaona ulivyomuumiza? Haya nataka
umtibu sasa hivi, vinginevyo nitakufunza adabu,” alisema Junaitha kwa hasira
huku akimshika nywele na kumtingisha, kwa msaada wa mwanga hafifu nikawa
namshangaa yule mwanamke jinsi alivyoumbwa usoni.
Alikuwa na masikio makubwa, pua nene ya
duara na meno yaliyochongoka pembeni. Ama kwa hakika alikuwa akitisha. Baada ya
Junaitha kumwambia vile, huku akitetemeka alitoa ishara kwamba nifunue lile
eneo alilokuwa amenijeruhi, akatoa ulimi wake na kunipa ishara kwamba nisogeze
majeraha yangu anilambe, jambo ambalo nilisita.
“Sogea tu hawezi kukufanya chochote, si
unaona nimeshamvua kamba yake ya shingoni,” alisema Junaitha huku akinionesha
kamba iliyokuwa na mafundo kadhaa aliyokuwa ameishika mkononi. Nikasogeza
mapaja yangu ambapo alitoa ulimi wake mrefu na kuanza kunilamba damu zilizokuwa
zinachuruzika.
Ulimi wake ulikuwa mgumu na unaokwangua
kama wa mnyama mkali, nikashangaa maumivu niliyokuwa nikiyasikia yakiyeyuka
ghafla, Junaitha akanihakikishia kwamba nitapona baada ya muda mfupi, nikawa
bado nimepigwa na butwaa.
“Ukitaka kuendelea kuishi, kazi ni moja
tu, tunataka utuoneshe Shenaiza alipo na pia utuambie mbinu zote za kishirikina
ulizomfanyia baba yake alipokuja kwako kuomba kinga ya kufanikisha mambo yake
ya kishetani,” alisema Junaitha, mwanamke huyo akaanza upya kulia huku
akitingisha kichwa chake, hali iliyozidi kunifanya nikose majibu.
Aliendelea kulia na mara akaanza tena kutoa
muungurumo kama mnyama mkali wa porini, akawa anafurukuta kwa nguvu.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment