Sunday, September 2, 2018

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 4


ILIPOISHIA:
“Kumbe wakati napanda kwenye ule mti, mmoja kati ya walinzi wa eneo hilo, alikuwa ameshaniona na akawa anasubiri aone mwisho wangu. Nikiwa pale chini, nilishtukia bomba la baridi likinigusa shingoni, likifuatiwa na sauti ya ‘tulia hivyohivyo kwa usalama wako)’, nikajua nimepatikana.
SASA ENDELEA...
Miongoni mwa vitu ambavyo Mungu amenijaalia, ni kutokuwa na hofu au woga ndani ya moyo wangu na pengine hiyo ndiyo sifa iliyokuwa inawafanya watu wote wanaonijua wawe wananiogopa au kuniheshimu, yaani kama huniheshimu basi uniogope kwani sikuwa na hata chembe ya woga.
Licha ya yule mtu kunigusisha bomba ambalo bila hata kuuliza nilijua lazima litakuwa ni mtutu wa bunduki, kwa jinsi ninavyowajua walinzi wengi wa Kibongo, huwa hawafanyi kazi kwa weledi.
Unaweza ukashangaa kwa nini nasema hivyo, lakini nikiri tu kwamba nimepitia mambo mengi sana hapa duniani, mengine makubwa na ya kutisha mno ambayo hata nikikusimulia, unaweza usiamini kwa haraka utakachokisikia.
Na miongoni mwa matukio mengi niliyoyafanya, yalikuwa yakiwahusu zaidi walinzi kwa hiyo nilikuwa najua jinsi walivyo wazembe.

Miongoni mwa sheria ambazo serikali inatakiwa kuzibadilisha mapema sana, ni hili suala la kampuni za ulinzi kukabidhiwa dhamana ya kulinda kwenye maeneo yenye mali za gharama, na kibaya zaidi kampuni hizi nyingi huwaajili wazee ambao hawawezi kupambana na majambazi wenye njaa, mwisho wanaishia kuuawa kama kuku.
Kwa hiyo nilichokifanya, nilijifanya kama nasalimu amri na kuinua mikono juu kisha kwa kasi ya kimbunga nikageuka na kumrukia yule mlinzi mwilini huku mikono yangu ikiwahi kuushika mtutu wa bunduki na kuugeuzia juu.
Kwa jinsi nilivyojirusha kwa nguvu, yule mlinzi hakutegemea kabisa kwa hiyo tukadondoka wote mpaka chini kama mizigo, tukawa tunagombea ile bunduki. Katika zile purukushani, nilifanikiwa kumzidi nguvu, nikampiga na kitako cha bunduki yake mwenyewe, akapoteza fahamu.
Harakaharaka nilimburuta mpaka pembeni, nikamfunga mikono na miguu na kumjaza matambara mdomoni kisha nikaanza kuutafuta mlango wa kuingilia ndani. Kwa nje kulikuwa na utulivu wa hali ya juu mno, usingeweza kuamini kwamba ndani kulikuwa na ulimwengu mwingine wa tofauti kabisa.
Basi nilifanikiwa kufika kwenye mlango wa nyuma na kwa kuwa ulikuwa umefungwa kwa ndani, nilitumia mbinu ya kufyatua kitasa kwa kutumia sindano niliyokuwa natembea nayo.
Kwa watu waliowahi kushiriki kwenye haya mambo ya uhalifu, nadhani watakuwa wananielewa vizuri ninapozungumzia masuala ya sindano na vitasa. Hakuna kitasa kinachoweza kufua dafu kwa mtumiaji mzuri wa sindano na mafuta ya breki.
Basi niliingia ndani kimyakimya na nikaiweka vizuri bunduki yangu, tayari kwa chochote. Basi nilienda moja kwa moja mpaka kwenye vyoo vya uani, nikaingia kwenye moja kati ya vyoo hivyo na kujibanza humo, wakati nikitafakari nini cha kufanya.
Mara nilisikia vishindo vya mtu akija kule chooni, nikaikamata vizuri bunduki yangu, tayari kwa chochote. Kwa bahati nzuri, aliingia kwenye choo cha pili, akajisaidia na muda mfupi baadaye, akawa anatoka.
Niliamua kumtumia kama chambo kwa sababu wasichokijua watu wengi, ni kwamba milango miwili mikubwa ya kutokea kwenye jengo lile, kuanzia mlango wa nyuma hadi mlango wa mbele, ilikuwa ikifunguliwa kwa kadi maalum za ‘ku-swap’.
Kwa jinsi jengo hilo lilivyokuwa limejengwa, kadi moja ilikuwa inatakiwa kutumika na mtu mmoja tu na bila kadi hiyo, uwezekano wa kuingia ndani ulikuwa mgumu na hiyo ndiyo sababu iliyonifanya nijibanze kule chooni kusubiri mzembe mmoja nipambane naye.
“Samahani,” nilisema huku nikimgusa begani yule mtu baada ya kuwa nimenyata na kumsogelea, nikamuwahi wakati anataka kuswap kadi ili mlango ufunguke. Alipogeuka tu, nilimtwisha kitako cha bunduki, damu zikaruka hewani kisha akadondoka mpaka chini kama mzigo huku kadi ikigeukia pembeni.
Unajua wakati mwingine ninapokumbuka mambo niliyoyafanya, najisikia vibaya sana kwa sababu watu wengi wasio na hatia walikuwa wakiteseka na wengine kuuawa kwenye mikono yangu. Wasichokijua watu wengi, kitako cha bunduki ni silaha mbaya sana, kiwe kimekatwa au kipo kizima. Mtu yeyote ukimpiga na kitako cha bunduki kichwani, hata kama awe nunda vipi, lazima apoteze fahamu, hasa kama unajua namna ya kutumia .
Basi harakaharaka nilimburuza na kumlaza kwenye maua, damu zikawa zinaendelea kumtoka lakini sikujali. Ilikuwa ni lazima nimfikie Seba ambaye naye kama alivyokuwa Suma, alikuwa pande la mtu la miraba minne, ambalo kazi yake ni kufanya michezo ya hatarihatari.
Niliswap ile kadi na kuingia ndani huku nikijitahidi sana kujichanganya ili asiwepo yeyote anayeweza kunihisi kwamba nimevamia nikiwa na nia ovu ndani ya klabu hiyo ambayo wateja wake ni watu maalum pekee.
Nilikaa kwenye moja kati ya kona zilicojificha, nikawa naangaza macho huku na kule kumtafuta Seba na baada ya dakika kadhaa, macho yangu yalimnasa akiwa anacheza kamari na wenzake. Miongoni mwa matatizo aliyokuwa nayo Seba, ambayo nahisi ndiyo yaliyomfanya akaingia kwenye kazi za kutumia silaha za moto, ni kupenda sana kamari.
Hata akipata fedha nyingi kiasi gani, Seba alikuwa na tabia ya kukesha hata siku mbili mfululizo akicheza kamari, yaani mpaka fedha zimuishie ndiyo akili zinamrudia laikini vinginevyo, hawezi kutulia.
Niliamua kumfuata palepale alipokuwa akiendelea kucheza mchezo maarufu wa kamari uitwao ‘poker’, kwa wale wazungukaji wa kwenye kumbi za starehe watakuwa wanaujua mchezo huu maarufu.
Nilifika kimyakimya na kusimama nyuma yake, sikutaka mtu yeyote ajue kinachoendelea kwa hiyo nikawa najipanga namna ya kumteka kimyakimya bila mtu kujua.
“Tulia hivyohivyo, hii ni bunduki, tena AK47, ukileta ujuaji nakumwaga kinyesi sasa hivi,” nilimnong’oneza Seba, kwa sababu na yeye ni mhuni aliyekubuhu, aliamua kunisaidia kazi yangu, akajifanya eti anataka kwenda toilet ili wale wenzake wasishtukie chochote.
Akanitazama usoni kama anayeuliza nini cha kufanya, nikampa ishara ya kusimama, kweli akasimama, nikampa ishara ya kuelekea kule nyuma, kweli akakubali kirahisi. Nimewahi pia kufanya kazi na Seba na miongoni mwa sifa zake kubwa, alikuwa siyo mwepesi wa kukubali kushindwa.
Ukichanganya na ukubwa wa mwili wake uliojengeka vyema kimazoezi, nilijua lazima anaweza kuleta ubishi lakini nikawa nimejiandaa kukabiliana naye. Alitembea harakaharaka mpaka alipoufikia mlango, akawa anataka kusap ili kufungua na kutoka nje lakini nikamzuia.
Nilijua akitoka nje atamuona yule mtu aliyekuwa amepoteza fahamu baada ya kupigwa na kitako cha bunduki lakini pia anaweza kumuona yule mlinzi ambaye naye nilikuwa nimemtwanga na kumfunga kamba.
“Nataka usimame hapohapo,” nilimwambia, akageuka taratibu na kunitazama huku akionesha kutokuwa na hata chemba ya masihara.
“Yaani wewe ndiyo wa kunishikia bomba mimi?”
“Unajifanya mjanja si ndiyo? Sitaki kujua kwa nini mmechoma nyumba yetu, nataka kujua mahalia liko Saima.”
“Kinachokupa ujeuri ni hiyo bunduki uliyoshika mkononi si ndiyo?”
“Ukijibu vizuri hakuna kitakachoharibika. Huu siyo muda wa mchezo, nitakufumua ubongo sasa hivi,” nilisema huku nikiwa sina hata chembe ya masihara na ili kumuonesha kwamba kweli licha ya mwili mkubwa aliokuwa nao ambao nilikuwa simfikii hata nusu yake, kweli nilikua nimevurugwa na nilikuwa tayari kufanya chochote, nilikoki bunduki na kuikamata vizuri huku nikimtazama machoni.
“Mdogo wangu, nakuomba tuliza mashetani yako. Nakujua wewe ukishavuta mibange yako hakuna anayeweza kukuzuia, nakuomba shusha ‘chuma’ chini,” alisema, nikaona kama ananichanganya kichwa.
“Saima yuko wapi?”
“Sasa mdogo wangu, wewe si unajua kabisa kwamba sisi ni vibaraka tu tunatumwa?”
“Narudia kwa mara ya tatu, Saima yuko wapi?” nilisema, safari hii nikiwa natetemeka kwa jazba. Kwa watu wote waliowahi kufanya na mimi dili chafu huwa wananielewa nikifikia hatua ya kutetemeka huwa nini kinafuatia. Tayari nilishaanza kusikia harufu ya damu kwenye pua zangu na kilichokuwa kinafuatia, hakikuwa kizuri hata kidogo.
“Kibaha! Tumempeleka Kibaha kwenye shamba la bosi, lakini yupo salama.”
“Shamba lipi?”
“La machinjioni,” alisema na kwa sababu alinisumbua, sikutaka kumuacha Seba hivihivi, nilitaka kutuma salamu kupitia yeye kwa hiyo nilichokifanya, nilivuta ‘trigger’ kwa ufundi, risasi moja ikapiga kwenye mguu wake wa kushoto upande wa chini, katikati ya vidole na kisigino.
Kelele za mlio wa risasi kutoka kwenye bunduki iliyokatwa mtutu na kelele alizozipiga Seba, ziliwashtua watu wengine waliokuwa wakiendelea kula raha, wakiwa hawajui chochote kinachoendelea, wakaanza kukimbia huku an kule huku Seba akiwa ameshaanguka chini, damu nyingi zikiwa zinamtoka pale nilipompiga risasi.
Nilifungua mlango na kutoka na ili kuzuia wasije wakatokana kunifuata, nilipiga risasi kwenye eneo la kuscan kadi za kufungulia mlango, nikawa na uhakika kwamba hakuna mtu anayeweza kuingia wala kutoka kwa kutumia mlango huo.
Harakaharaka niliruka ukuta na kudondokea upande wa nje, nikaanza kukimbia kutokomea gizani. Kumbe kulikuwa na askari waliokuwa doria jirani na eneo hilo kwa hiyop ule mlio wa risasi, uliwafanya wafike eneo la tukio haraka sana.
Kwa bahati mbaya, wakati nikikimbia kuvuka barabara, taa za gari la polisi lililokuwa linakimbia kwa kasi kuelekea eneo la tukio, zilinimulika na kunifanya nichanganyikiwe kidogo, unajua ukimulikwa gizani na mwanga mkali lazima uchanganyikiwe.
Nilisikia gari hilo likifunga breki kali, hapo ndiyo na mimi nikapata akili za kukimbia kwa sababu kwanza mwili wangu ulikuwa na damu lakini kibaya zaidi, nilikuwa na bunduki hatari ambayo kama ningekamatwa na polisi, huenda maisha yangu yote yaliyosalia ningeyamalizia gerezani.
Nilikimbia na kujaribu kuruka ukuta lakini kabla sijaruka, nikasikia wale askari wakifungua milango na kuruka kwenye gari lao kwa kasi kubwa, mmoja kati yao akatoa amri ya kunitaka nisimame na kuinua mikono juu, jambo ambalo niliona kama haliwezekani.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Championi Jumatatu. 

2 comments:

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...