ILIPOISHIA:
Madam Bella hakusema lolote zaidi ya kusimama,
akawa anatutazama huku akionesha kushtuka sana kutokana na hali aliyotukuta
maana Salma alikuwa amepeleka mkono wake shingoni kwangu kwa lengo la kunikagua
ile aliyosema mwenyewe lipstiki, kwa hiyo mazingira yalionesha ni kama tulikuwa
tumekumbatiana.
SASA ENDELEA...
“Yaani
badala ya kufanya kazi iliyowaleta mna kazi ya kukumbatiana kwenye korido! Hivi
mna akili kweli nyie?”
“Hapana
Madam, nilikuwa namsaidia kumfuta madoa ya lipstiki kwenye shati lake, hebu
angalia mwenyewe,” alisema Salma kwa namna ya kujihami sana.
“Lipstiki?
Sasa lipstiki kwenye shati lake wewe inakuhusu nini?”
“Nisamehe
Madam!”
“Ile cheki
niliyokupa umeshaipeleka uhasibu?”
“Hapana
bosi, ndiyo nilikuwa na...”
“Salma!
Kuwa makini, kama kilichokuleta ni kazi, fanya kazi. Na wewe Ashrafu, unatakiwa
kuheshimu kazi ninayokupa, yaani mimi nakutuma kitu halafu badala ya kwenda
kufanya nilichokwambia unaanza kufanya mambo yako mengine.”
“Nisamehe
bosi,” nilisema huku nikijitahidi kuvaa uso ambao hautamfanya Salma ashtukie
chochote. Kweli hilo lilifanikiwa, Madam Bella alitoa amri ya kila mmoja
kuendelea na kazi zake, harakaharaka Salma akapita mbiombio na kuelekea uhasibu
na mimi nikaondoka haraka kuelekea ofisini kwangu.
Sikukaa
sana, niliweka kila kitu changu vizuri, nikatoka mpaka pale mapokezi,
nikamdanganya Salma kwamba kuna kazi bosi amenituma nje ya ofisi kwa hiyo
natoka, akanijibu kwa kutingisha tu kichwa akionesha kutokuwa na furaha.
Nadhani
kitendo cha kufokewa na bosi mbele yangu kilimkasirisha sana, akawa hataki hata
kunitazama. Aliitikia kwa kutingisha kichwa, nikateremka kwenye ngazi
harakaharaka kwa lengo la kumfanya mtu yeyote asijue kwamba natoka na bosi.
Nilipofika
chini nilimuuliza kama nimsubiri pale chini au la, akanijibu kwa meseji kwamba
nipande Bajaj tutakutana Mnazi Mmoja.
Kwa kuwa
mfukoni nilikuwa na vihela kidogo, sikutaka kupoteza muda, nilikalia Bajaj na
muda mfupi baadaye tayari nilikuwa Mnazi Mmoja, nikakaa kituoni kumsubiri bosi
huku muda wote nikigeuka huku na kule kuangalia kama hakuna mtu yeyote
aliyekuwa ananijua.
“Pipii!
Pipiii,” honi iliyopigwa taratibu pembeni yangu ndiyo iliyonishtua kutoka
kwenye mawazo ya hofu niliyokuwa nayo. Sijui kwa nini sikuwa nataka watu wajue
kwamba natoka na Madam Bella, nilipogeuka nilikutana uso kwa uso na bosi akiwa
kwenye gari lake la kifahari, Toyota Lexus, akashusha kioo na kunipa ishara
kwamba na mimi niingie.
Niliingia
na kukaa siti ya nyuma lakini akaniambia natakiwa kukaa naye mbele. Sikuwana
namna, nilishuka na kufungua mlango wa mbele, nikaingia na kuufunga
harakaharaka. Kwa bahati nzuri gari lake lilikuwa na vioo vya giza (tinted),
nikawa na uhakika kwamba hakuna tena mtu ambaye angetuona.
Aliondoa
gari taratibu, akawa anageuka na kunitazama akionesha kuwa na dukuduku ndani ya
moyo wake, na mimi nikajikausha maana nilishajua kwamba kitendo cha kunikuta na
Salma pale koridoni hakukifurahia kabisa.
“Unatoka
na Salma si ndiyo?”
“Aah!
Hapana bosi, umewahi kuniona au kuhisi chochote zaidi ya leo?”
“Kwa nini
mlikuwa mmekumbatiana?”
“Hatukuwa
tumekumbatiana, alikuwa ananishangaa kwa nini nina lipstiki kwenye nguo ndiyo
na wewe ukatokea, si unaona alama za lipstiki yako hizi,” nilisema huku
nikijitahidi kumgeuzia kibao, ionekane yeye ndiye aliyekosea kunibusu wakati
anajua amepaka lipstiki inayoacha alama.
“Hebu
tuone,” alisema huku akinigeukia, safari hii ule ‘usiriasi’ ukiwa umepungua,
kweli kulikuwa na alama ya lipstiki kwenye shati langu, basi akacheka sana na
kuendelea kuendesha gari, muziki laini ukawa unapiga ndani ya gari sambamba na
kipupwe cha nguvu, nikawa najihisi kama nipo kwenye dunia nyingine.
“Kwani
nyumbani kwako unaishi na nani?”
“Naishi
peke yangu bosi.”
“Unajua
nataka kupumzika maana jana nilichoka sana lakini sitaki kwenda hotelini,
unajua watu tunaoheshimika kama sisi, ukionekana tu hotelini, hasa na mtu wa
jinsia nyingine tofauti ni rahisi watu kukuhisi vibaya,” alisema bosi lakini
moyoni nikawa sijauafiki kabisa uamuzi wake.
Hadhi ya
bosi ilikuwa si ya kwenda naye Tandale hata kidogo, kama nilivyosema kuanzia
mwanzo, japokuwa alikuwa mwanamke wa makamo, alikuwa na uzuri fulani hivi wa
aina yake ambao huwezi kuuona kwa urahisi kwa wanawake wanaotokea familia za
kawaida.
Nilijaribu
kutoa visingizio vingi lakini bado alishikilia msimamo wake, akawa ananiambia
kwamba nisimchukulie ‘kiivyo’ kwa sababu kabla ya kupata mafanikio aliyokuwa
nayo, amewahi kuishi kwa msoto wa nguvu.
“Cha
msingi tupate sehemu salama ya kupaki gari, mengine hayo wala usijali! Au
hujafua mashuka nini?” alinitania, tukacheka kwa nguvu. Aliniambia kwamba
anataka kabla hatujafika kwangu, tupitie kwanza sokoni kununua mahitaji yote
muhimu kwa sababu anataka eti akanipikie chakula ambacho sijawahi kula sehemu
yoyote.
Sikuwa na
namna, nilikubali kila alichokuwa akikisema, tukapitia Manzese ambapo tulinunua
mazagazaga kibao, tukaenda moja kwa moja mpaka Mtogole, nikamuelekeza sehemu
nzuri ya kupaki gari ambapo hakuna kibaka anayeweza kuiba ‘saiti mira’ wala
‘pawa windo’.
Mimi ndiyo
nilikuwa wa kwanza kuteremka kwenye gari, nikashuka na vifurushi vya mazagazaga
kibao, basi bosi naye alipoteremka, watu karibu wote eneo hilo waliacha kila
walichokuwa wakikifanya na kumtolea macho.
Kwa jinsi
mwonekano wake ulivyokuwa, alikuwa kiumbe adimu kwenye mazingira kama hayo, basi
tukakatiza vichochoro huku kila mtu akiendelea kutushangaa kwa sababu bado
ilikuwa ni asubuhi na hatimaye tukawasili nyumbani.
Kwa bahati
mbaya, wakati tunafika, mke wa mwenye nyumba ambaye tumezoea kumuita mama
Ababuu, alikuwa akifua nguo zake uani, tena kiti chake akiwa amekiweka karibu
kabisa na mlango wangu.
Siku zote
nilikuwa namheshimu sana mama Ababuu na sikuwahi kumuonesha tabia zozote mbaya,
nikaona kitendo cha mimi kuingia na Madam Bella ‘magetoni’, kingemfanya anione
kama mtu wa ajabu sana kwa sababu kulikuwa na tofauti kubwa ya kimwonekano na
kimwili kati yangu na Madam Bella.
Nilijikaza
kiume, nikamsalimu na kufungua mlango huku Madam Bella akishangaa mazingira ya
pale, nikamkaribisha ndani ambapo kama ilivyokuwa kwa Nancy, alipoingia tu,
alinisifu kwamba chumba changu ni kizuri sana, basi nikamshukuru na
kumkaribisha sana.
“Unanikaribishaje
hivyo?” alisema huku akitanua mikono yake kama anayesema ‘njoo unikumbatie’.
Basi na mimi nilifanya kama alivyotaka, nikaenda na kumkumbatia kwa nguvu, muda
mfupi baadaye midomo yetu ilikuwa imegusana, hata sijui nini kilitokea,
nilishtukia tu tayari tukiwa kwenye uwanja wa fundi seremala, mara mlango
ukagongwa kwa nguvu.
“Ngo! Ngo!
Ngooo!”
Je, nini
kitafuatia? Usikose Jumatano kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko.
No comments:
Post a Comment