Monday, September 3, 2018

KIVURUGE WA TANDALE- 7



ILIPOISHIA:
“Mungu wangu, nitasema nini nyumbani,” alisema huku akikurupuka na kuanza kutafuta nguo zake, nikaona analeta masihara, ataondokaje muda huo wakati hata kipindi cha pili kilikuwa bado?
SASA ENDELEA... 

Harakaharaka aliwasha simu yale ya bei mbaya ambayo kwa muda wote huo alikuwa ameizima. Nikamuona anavyohangaika, nadhani alikuwa akitafutwa sana kwenye simu.
“Sijui nitamwambia nini baba, sijawahi kukaa nje mpaka usiku mnene kiasi hiki.”
“Kwani wewe bado unaishi na wazazi wako?” 

“Ndiyo! Naishi na wazazi, sasa wewe ulikuwa unafikiri naishi na nani?”
“Sasa si unaweza tu kumwambia upo kwenye bethidei ya rafiki yako?”
“Hilo siyo tatizo, ilitakiwa nitoe taarifa mapema, sasa unafikiri saa saba hii naanzaje kuwaeleza kitu kama hicho? Umeniponza Ashrafu, umenisababishia matatizo,” alisema huku akianza kulia. Ilibidi niamke pale kitandani na kumfuata pale alipokuwa amesimama, nikawa najaribu kumtuliza.


“Wewe umeshakuwa mkubwa sasa, hutakiwi kuwahofia wazazi wako kwa kiasi hicho, kwani wao hawajui kwamba wewe umeshakuwa mkubwa?”
“Stop it!” alisema kwa ukali akimaanisha hataki niendelee kuzungumzia suala hilo. Kwa jinsi alivyonibadilikia, sikuwa na namna zaidi ya kumruhusu tu aondoke lakini nilifanya hivyo kwa shingo upande. 

Licha ya kazi kubwa iliyofanyika, huwezi kuamini kwamba bado mtandao ulikuwa ukisoma 4G, nikawa najitahidi kujizuia mwenyewe kwa mbinu zangu. Alivaa harakaharaka na muda mfupi baadaye, alikuwa ameshamaliza kila kitu, akanigeukia na kushtushwa na hali niliyokuwa nayo. 

“Una matatizo gani?”
“Sina tatizo lolote.”
“Mbona hivyo sasa?”
“Aah! Kawaida tu, kwani kuna tatizo?” nilisema huku na mimi nikijisikia aibu. 


“Ashrafu, naomba unisamehe baba, muda umekuwa mbaya sana, sipendi kukuacha na hali kama hii lakini nakuomba uniruhusu, nitatafuta muda mzuri wala usijali,” alisema kwa upole huku akiwa amenikumbatia, akanibusu kimahaba na kwa kiasi fulani, moyo wangu ulikunjuka.


Ilibidi na mimi nivae harakaharaka, nikawa najiuliza sijui itakuwaje maana ilikuwa hatari sana kutembea mtaani kwetu muda kama huo. Nilipiga moyo konde kwamba liwalo na liwe, tukatoka huku nikiwa nimemshikia simu na mkoba wake, safari ya kuelekea barabarani ikaanza.


Kwa bahati nzuri, mpaka tunafika barabarani, hatukuwa tumekutana na vibaka, nikamsimamishia bodaboda. Harakaharaka alipanda, nikamkabidhi vitu vyake na kumpa noti ya shilingi elfu kumi kwa ajili ya nauli, alitaka kukataa lakini nikamshikisha. 

Alimuelekeza dereva huyo wa bodaboda sehemu ya kumpeleka na wakaondoka kwa kasi. Kwa usalama wa dereva wa bodaboda na abiria wake, inapofika mida ya usiku mitaa ya kwetu ni lazima mpite kwa kasi kubwa, vinginevyo mnaweza kung’ang’aniwa na vibaka wakaiba mpaka bodaboda.
Hivyo ndivyo alivyofanya yule dereva, ndani ya muda mfupi tu tayari walikuwa wameshatoweka eneo hilo, harakaharaka nikaanza kukatiza vichochoro kurudi nyumbani kupumzika maana muda ulikuwa umeenda sana. 

Niliporudi ndani, kutokana na uchovu niliokuwa nao, nilijitupa kitandani na haukupita muda, nilipitiwa na usingizi mzito. Nilipokuja kuzinduka, tayari kulikuwa kumepambazuka, harakaharaka nikaamka na kuelekea bafuni kuoga kwa sababu nilikuwa natakiwa kuwahi kazini. 

Saa kumi na mbili na nusu, tayari nilikuwa nimeshamaliza kujiandaa, nikajitazama kwenye kioo kilichokuwa humo ndani kwangu, nikajiridhisha kwamba nilikuwa nimependeza. Hakuna kitu ambacho nilikuwa nakizingatia kama mwonekano wangu hususani mavazi.


Basi nilitoka mpaka kituoni, nikapanda daladala na safari ya kuelekea kazini ikaanza. Ni hapo ndipo nilipopata wazo la kuitazama simu yangu, ilikuwa na ‘missed calls’ nyingi za Nancy, za Madam Bella na za Salma na nyingi zilionekana kuwa ni za usiku uliopita.


Kulikuwa pia na meseji nyingi, ikabidi nianze kusoma moja baada ya nyingine. Madam Bella alikuwa amenitumia meseji eti akinishukuru kwa kilichotokea, akaniambia kama alikuwa amenikosea basi anaomba nimsamehe sana lakini nisimwambie mtu yeyote kuhusu kilichotokea. 

Nilijikuta nikitabasamu baada ya kusoma meseji hiyo, nikawa najiuliza sijui nitamtazama vipi usoni nitakapofika kazini. Nikajipa moyo kwamba hakukuwa na chochote kibaya nilichokifanya kwa sababu kama isingekuwa visa vyake alivyonifanyia, pengine nisingefikia uamuzi wa ‘kumuadhibu’ palepale ofisini. 

Kulikuwa pia na meseji za Salma na kama kawaida yake yeye alikuwa akilalamika. Aliniambia amenipigia simu mara nyingi lakini sipokei simu zake kwa makusudi, akaenda mbele zaidi kwa ‘kunichana’ kwamba eti nisidhani kama yeye ni mwanamke ‘cheap’ kiasi hicho ila hata mwenyewe haelewi nini kilichotokea mpaka akaniachia nimfaidi. 

Yeye ndiye aliyekuwa ametuma meseji nyingi zaidi na kati ya zote alizotuma, zilizojaa lawama kwa nini sipokei simu yake, kwa nini nimeondoka kazini bila kumuaga, kwa nini sijamjulia hali baada ya kufika nyumbani na nyingine nyingi, ni moja tu iliyonifurahisha. 

Aliniambia kwamba hakutegemea kama eti kama naweza kumfanya akajihisi kuwa mwanamke aliyekamilika na kujisikia kama vile alivyozoea kusikia kwa wenzake wakisimulia kuhusu raha ya kuangua madafu.


Nilijikuta nimecheka bila mwenyewe kujijua mpaka abiria aliyekuwa amekaa upande wa dirishani, kwenye siti niliyokaa akanigeukia. Kwa aibu, nilijikausha haraka na mimi nikamgeukia, tukatazamana. Nilishtuka sana, sijui ni kwa nini!


Tangu nimepanda daladala, sikuwa nimetulia kiasi kwamba sikupata hata muda wa kujua kwamba kulikuwa na mtu, sikumsalimia yule abiria niliyemkuta kwenye ile siti, wala sikupata hata muda wa kumtazama usoni. Alikuwa ni mwanamke ambaye kwa kumtazama alionesha kwamba lazima atakuwa ni mke wa mtu maana mkononi alikuwa na pete ya ndoa. 

Miongoni mwa vitu ambavyo huwa naviogopa, ni wanawake wenye pete za ndoa kwenye vidole vyao, pamoja na utundu wangu wote kuhusu hawa viumbe, nilikuwa mwoga sana wa mali za watu.
“Hujambo!” aliniuliza baada ya kuona nimebaki namkodolea macho. 

“Sijambo, shikamoo!” nilimsalimu salamu ambayo haikuwa ikifanana naye huku nikijaribu kuvaa tabasamu la uongo lililochanganyikana na aibu, nikawa nasubiri nione kama ataitikia kwa sababu japokuwa ni kweli alikuwa na pete kidoleni, hakuwa mkubwa sana kwangu kustahili shikamoo. 

Badala ya kujibu salamu yangu, aliachia tabasamu lililoshiba kisha akaweka vizuri ‘headphone’ kwenye masikio yake, akageukia dirishani, akawa anatazama nje, nikabaki na maswali mengi sana.
“Kwa nini anacheka?” nilijiuliza moyoni, nikaamua kuachana naye, nikaigeukia simu yangu na kuendelea kufanya kile nilichokuwa nakifanya. Niliendelea kuangalia meseji nilizotumiwa, nikakutana na ya Nancy na ilionesha ilitumwa kama saa nane hivi za usiku.


“Nimefika salama lakini baba kanigombeza sana, kasema kukikucha ana mazungumzo na mimi,” ilisomeka meseji ya Nancy, nikashusha pumzi ndefu na kuendelea kuangalia meseji nyingine. 

Kumbe hiyo alinitumia alipofika tu, nikakutana na nyingine ambazo alikuwa akinisifia sana na kunishukuru kwa nilichomfanyia kwa muda mfupi niliokaa naye, akaniambia japokuwa nimemsababishia ‘msala’ kwa wazazi wake, ataumaliza mwenyewe hilo suala, akaniambia tangu awe na akili zake, hajawahi kukutana na mtu aliyemfanya ajisikie kama alivyojisikia muda aliokuwa na mimi. 

Nilijikuta nikitabasamu mwenyewe, sijui nini kilinituma nitazame dirishani, macho yangu yakamfuma yule abiria mwenzangu akiwa ‘bize’ kusoma meseji zangu. Alipoona nimemshtukia, alitabasamu tena na kunitazama usoni. Sasa niligundua ni nini kilichomfanya ashindwe kuitikia salamu yangu na badala yake aishie kutabasamu! Kumbe alikuwa akisoma meseji zangu.


Badala ya kukasirika, nilijikuta nikizidi kujisikia aibu, maana kama alikuwa akinifuatilia kuanzia mwanzo, maana yake ameona yote yaliyoandikwa na Madam Bella, Nancy na Salma, tena yote yakihusu kitu kimoja.


Aliendelea kunitazama usoni huku akiwa ametabasamu, na mimi nikawa nimemkazia macho huku nikijaribu kuzificha hisia za aibu zilizokuwa zimenijaa.
“Unaitwa nani?”
“Mimi?”
“Ndiyo, kwani hapa nazungumza na nani?” aliniuliza huku akizidi kunitazama machoni.”
“Ashrafu!” nilimjibu huku na mimi nikizidi kumtazama usoni.
  
Tukiwa tunaendelea kutazamana, mara redio iliyokuwa ndani ya gari ilianza kupiga wimbo wa Kivuruge wa Nandy. Kiukweli huu wimbo mimi huwa siupendi, si kwa sababu ni mbaya hapana bali ni kwa sababu mara nyingi wadada walikuwa wakitumia maneno yake kunisimanga. 

Nakumbuka wakati naachana na Asnath wa Tabata Segerea baada ya kunifuma nikiwa na shoga yake waliyesoma pamoja, Kuruthum, alinitumia meseji kali sana na mwisho eti akaniandikia ‘dedication’ ya wimbo huo wa Kivuruge (nitaeleza baadaye kwa kina kuhusu mimi na Asnath, jinsi tulivyopendana kabla ya baadaye kuja kuishia kuwa maadui wakubwa).


“Umekuwa kivuruge unavuruga sanaaa...” yule dada aliacha kuzungumza na mimi, eti akawa anaimba kwa mapozi kufuatisha muziki huo kwenye redio, huku akinitazama, tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake.


Akiwa anaimba, niligundua kitu kuhusu huyu dada! Kwanza alikuwa na meno meupe sana, yaliyopangika vizuri nakumfanya awe na mvuto wa kipekee. ‘Lipstic’ aliyokuwa amepaka ilizidi kumfanya awe na mvuto sana, nikawa namtazama macho yake, nikagundua kwamba pia yalikuwa mazuri! 

Sijui ni pepo au ni kitu gani, nilijikuta nikivutiwa naye sana, hata sauti yake ilikuwa ni ile kavu flani hivi, ambayo huwa napenda sana kuisikia masikioni mwangu, basi nikawa namtazama tu anavyoendelea kuimba huku nikijua kabisa alifanya vile kwa makusudi kama anayenipiga kijembe baada ya kusoma meseji zangu. 

“Kumbe unajua kuimba vizuri hivyo, itabidi nikupeleke studio,” nilimchombeza, akacheka sana, tayari tulishafika maana konda alipaza sauti akisema hapo ndiyo mwisho wa gari, abiria wengine wakawa wanateremka lakini mimi nikajikuta nikipata uzito na kubaki nimekaa, naye hakuonesha kuwa na haraka sana, akawa amekaa akiwa ni kama anayenisubiri niinuke ili na yeye ainuke. 

Ndani ya muda mfupi tu tayari tulishakuwa tumezoeana f’lani hivi, akili fulani ndani ya kichwa changu ikawa inaniambia ‘jaribu kutupia mistari’.



Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.

No comments:

Post a Comment

THE DARKEST HOURS (SAA ZA GIZA TOTORO)- 1

Mtunzi: Hashim Aziz (Hashpower) 0719401968 “Ngo! Ngo! Ngo! Fungua!” “Nanii?” “Fungua!” “Jitambulishe kwanza, wewe nani?” “Nimese...