ILIPOISHIA:
“Inuka na ufanye ninachokueleza,
ukizingua unajua nini kitatokea,” nilisema kwa sauti ya chini lakini yenye
mamlaka, yule mwanamke akakurupuka akiwa ni kama haamini kilichotokea, Suma
naye akawa anatetemeka akiwa haelewi nimeingiaje pale.
SASA ENDELEA...
“Snox! Nakuomba mdogo wangu, please
show me some mercy!” (Nionee huruma tafadhali) alisema Suma huku akiwa
anatetemeka kuliko kawaida lakini sikumjali.
“Look at my face!” (Nitazame usoni),
nilimwambia kwa Kiingereza kilichonyooka, akanitazama usoni halafu akawa ni
kama ameshtuka kidogo.
“Mlikuja mkanipiga na kunijeruhi kiasi
hiki, mkamteka Saima wangu na kama hiyo haitoshi, mmekuja kuchoma moto nyumba
yetu. Bado unategemea kwamba nitakuonea huruma?” nilisema huku na mimi
nikitetemeka kwa hasira.
”No! Nisikilize kwanza Snox,” alisema
huku akiniita kwa jina langu la kazi. Watu wengi mitaani huwa wanaamini Snox ni
jina langu halisi kwa sababu kila ninakoenda ndilo linalotumika lakini ukweli
ni kwamba halikuwa jina langu halisi wala halikuwa na uhusiano wowote na jina
langu halisi.
Kiuhalisia jina langu naitwa Keneth au
Kenny lakini kama nilivyosema, waliokuwa wakinijua kwa jina hilo, walikuwa
wachache mno, tena wale wanaonijua tangu nikiwa mdogo lakini wengine wote
walikuwa wakiniita Snox.
“Najua mlitumwa, nataka kujua mhusika
ni nani,” nilisema huku nikimkokota taratibu kuelekea kule uani. Yaani
ungeshuhudia kilichokuwa kinaendelea, pengine ungepata picha halisi ya kile
wanachosema ‘sungura kamkaba tembo’.
Suma alikuwa na mwili mkubwa
uliojengeka kimazoezi lakini licha ya ukweli kwamba mimi nilikuwa na kamwili
kadogo ka wastani, nilikuwa namkokota kama ng’ombe anayepelekwa machinjioni.
Kwa jinsi nilivyoingia eneo lile mpaka
kumpata, bado alikuwa amepigwa na butwaa na hiyo pekee ilitosha kumchanganya kichwa
na kibaya alikuwa anafahamu akili zangu nikishika ‘mashine’ zinakuwaje kwani
tumewahi kufanya ‘kazi’ pamoja.
“Nataka jibu, sitaki blaah! Blaah!”
nilisema huku nikizidi kulikandamiza bomba la AK47 kwenye ubavu wake, nikaikoki
na kumfanya ashtuke.
“Nitakwambia Snox, mimi na wewe
tumeshakuwa kama ndugu, huna haja ya kutumia nguvu kwangu,” alisema Suma kwa
upole, nikatega masikio kwa makini kumsikiliza.
“Mzee anasema umemsaliti, anataka
kuhakikisha unapata taabu mpaka mwenyewe ukome.”
“Mzee gani?”
“Aah Snox, kwani nikisema mzee wewe
unaelewaje? Kuna mwingine tena zaidi ya bosi?”
“Nimemsaliti kivipi?”
“Kitendo cha kukataa kazi bila sababu
za msingi, kimemkasirisha sana na anasema atahakikisha anakomaa na wewe mpaka
aone mwisho wako,” alisema Suma lakini maneno yake hayakuniingia akilini.
Nilijua kabisa kwamba ananidanganya kwa sababu alichokisema hakikuwa na uzito
wowote wa kumfanya mtu aniwinde kwa kiasi kile.
“Saima yuko wapi?”
“Sijui chochote kuhusu Saima,
sikuhusika kwenye hiyo kazi.”
“Unanificha si ndiyo?”
“Snox, sina sababu ya kukuficha
chochote ndugu yangu, ila labda Seba anaweza kuwa anajua chochote maana siku
hizi ndiyo mtu wa karibu zaidi na mzee.”
“Nitampata wapi?”
“Lazima muda huu atakuwa anakula bata
Trace Element, kule Masaki,” alisema Suma akitegemea kwamba baada ya maelezo
hayo nitamuachia.
Kwa walichonifanyia, japokuwa sikuwa
na nia ya kukatisha maisha ya mtu yeyote, lakini ilikuwa ni lazima niwashikishe
adabu wote waliohusika halafu mwisho nitamalizia na huyo aliyewatuma, ambaye
nilikuwa na hasira kali sana juu yake kwa alichonifanyia maishani mwangu.
Nilimsukuma Suma kwa nguvu, akakimbia
na kusimama mbele hatua kadhaa mbele, akanigeukia haraka huku akiwa ameinua
mikono juu maana alikuwa anajua ni nini ninachotaka kukifanya. Mara nyingi kama
mtu amekuteka na mkononi ana silaha ya moto, anapokwambia ukimbie, au
anapokusukumia mbali na yeye, usidhani anafanya hivyo kwa sababu kweli
amekusamehe, mara nyingi ni kwa sabahu anataka apate nafasi ya kukulenga vizuri
ili akupige risasi. Suma alilijua hilo na ndiyo maana alifikia hata hatua ya
kunipigia magoti akiomba nisimfanyie chochote.
Sikutaka kusikiliza la muadhini wala
mchota maji, nilifanya kile nilichoona kinafaa, mlio mkali wa bunduki
ulisikika, na hasa ukizingatia kwamba ilikuwa imekatwa mtutu, mlio wake ulikuwa
mkubwa na wa kutisha sana.
Sikupoteza muda, nilimruka pale chini
alipokuwa ameangukia akitokwa na damu nyingi, nikachumpa kwenye ukuta na muda
mfupi baadaye, nilikuwa nikiteremka upande wa pili wa ukuta. Nilijua kwa
vyovyote lazima mlio huo urtasikika kwa polisi waliokuwa doria ambao lazima
watakuja eneo hilo kwa hiyo nilipita njia tofauti na niliyojia.
Wateja waliokuwa wakiendelea
kuburudika mle ndani kwa vinywaji na muziki, walishtuka mno kusikia mlio wa
bunduki, tena kutokea ndani kabisa ya ‘chimbo’ lao, kila mmoja akaanza kutimua
mbio kuokoa maisha yake, wengine wakikanyagana hovyo na kusababisha madhara
yawe makubwa.
Zile purukushani zilinisaidia hata
mimi kuondoka eneo hilo kwa urahisi zaidi kwani nilijichanganya na kujifanya na
mimi naogopa mlio wa risasi, nikawa nakimbia ‘mdogo-mdogo’. Ungeniona wala
usingeweza kuhisi kwamba mimi ndiyo nilikuwa chanzo cha mshike-mshike uliokuwa
unaendelea.
Nilitokezea Sinza ya Mugabe baada ya
kuwa nimekatiza sana vichochoro ili nisionekane na mtu yeyote. Nilisimama kando
ya barabara na muda mfupi baadaye, bodaboda moja ilikuja, nikaipungia mkono na
hatimaye ikasimama.
‘Duh, baba umepiga pigo za kijambazi
kabisa! Niuzie hilo koti,” alisema dereva wa bodaboda huku akichekacheka,
nikanyamaza tu kwani ninapokuwa nimeivaa sura ya kazi huwa sipendi kucheka kwa
sababu nimewahi kufundishwa kwamba unapocheka, unaondoa uzingativu wa akili.
“Nipeleke Trace Element.”
“Trace Element au Element?”
“Nimekwambia Trace Element,” nilisema
kwa msisitizo, yule dereva wa bodaboda akanywea na nikamuona kama ananitazama
kwa macho ya kuibia hivi. Basi aliwasha pikipiki na tukaondoka huku kila mtu
akiwa kimya kabisa. Njia nzima nilikuwa namsisitiza kuongeza kasi nadhani mpaka
mwenyewe baadaye alikoma.
Basi baada ya kama dakika thelathini,
tayari tulikuwa tumewasili Masaki, nikateremka kwenye bodaboda na kumlipa fedha
zake kisha harakaharaka nikajichanganya na kuelekea kwenye chimbo lingine
liitwalo Trace Element.
Unajua watu wengi wanapajua Club
Element lakini hawajui kwamba kuna chimbo lingine la kijanja liitwalo Trace
Element, ambalo ndani yake kuna watu wabaya wa kila aina.
Mara nyingi, wau wabaya huwa
hawachangamani na watu wazuri mara kwa mara, hata wanapokunywa pombe, huwa
wanatenga kujificha kwenye machimbo yao ambayo wanakutana wenyewe kwa wenyewe,
hapo ndipo wanapokuwa na amani ndani ya mioyo yao kwani wakijichanganya na watu
wasiowajua, kila anayemuona anahisi ni polisi au mpelelezi.
Kwa sababu mara kwa mara nilikuwa
nakuja eneo hilo na wenzangu wakati nikiwa mwanachama kamili, nilikuwa nazijua
njia nyepesi za kutoroka, hasa polisi wanapokuja kwa lengo al kufanya ukaguzi,
niliamua kutumia njia hizohizo kuingilia kwa sababu nilikuwana uhakika pale
getini nisingeruhusiwa kuingia.
Basi nilizunguka upande wa pili na
kukwea juu ya mti uliokuwa jirani na fensi, nikatambaa na kujivuta juu kwa juu
mpaka nilipopanda juu kabisa ya fensi, nikatafuta sehemu nzuri ya kurukia,
nikadondokea ndani kimyakimya bila mtu yeyote kujua.
Unaweza kushangaa huu umahiri wa
kuparamia kuta za watu, taha ndefu kiasi gani bila kushtukiwa na mtu yeyote
nimeupata wapi? Katika kipindi chote nilichokuwa nafanya kazi za uhalifu, mimi
ndiyo nilikuwa nategemewa zaidi kwenye masuala ya kuruka fensi na kwenda
kufungua mageti kwa ndani.
Mara nyingi ili majambazi waingie
ndani kwa urahisi, lazima mmoja atangulie ndani kupitia ukuta na akiingia,
anaenda kufungua geti kwa ndani ili wote waliopo nje waingie na huko ndiko
nilikopata ujuzi huo.
“Kumbe wakati napanda kwenye ule mti,
mmoja kati ya walinzi wa eneo hilo, alikuwa ameshaniona na akawa anasubiri aone
mwisho wangu. Nikiwa pale chini, nilishtukia bomba la baridi likinigusa
shingoni, likifuatiwa na sauti ya ‘tulia hivyohivyo kwa usalama wako)’, nikajua
nimepatikana.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Gazeti la Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment