ILIPOISHIA:
“Dont worry Jamal, each and everything
is going to be okay!” (Usiwe na wasiwasi Jamal, kila kitu kitakuwa sawa)
alisema Firyaal na kunisogelea, akanikumbatia na kunibusu mdomoni huku kila mtu
akishuhudia. Sikujali, nilikuwa nampenda sana Firyaal na sikuwa tayari kuona
jambo lolote baya linamtokea, hasa kabla ya mimi na yeye kukutana na kumaliza
kile tulichokuwa tayari tumekianza.
SASA ENDELEA...
“Inabidi ubaki usaidiane na hawa
askari, bado kuna kazi kubwa mbele yetu. Nakukumbusha tu kwamba huonekani na
mtu yeyote kwa hiyo utakuwa na nafasi ya kuyafanya hata yale ambayo watu wa
kawaida hawayawezi, ni lazima Loris akamatwe, umepigwa risasi na Firyaal naye
amepigwa risasi, haiwezekani iwe ni kwa ajili ya kazi bure,” alisema Junaitha,
sauti ambayo ilipenya vilivyo masikioni mwangu, akawa ni kama amezidi
kuniongezea hasira.
Wale askari walipoingia, wengine
ilibidi wabaki nje, wakatawanyika kule ndani kwa tahadhari kubwa na muda mfupi
baaddaye, mvua nyingine ya risasi ikaanza kumwagika.
Nilishindwa kuelewa ni kwa sababu gani
nyumba hiyo ilikuwa ikilindwa kiasi hicho, nikasikia sauti ya Junaitha masikioni
mwangu akinielekeza kusonga mbele haraka mpaka pale walipokuwepo walinzi
wengine waliokuwa wakifyatua risasi kwa kasi.
Nilipiga hatua mbili tu, bila
kuonekana na mtu nikawa tayari nimeshafika kwenye geti la pili ambalo nalo
lilikuwa na vyumba viwili vya walinzi kama kule mwanzo lakini tofauti yao, hawa
hawakuwa ghorofani, vyumba vyao vilikuwa vya chini.
Kwenye chumba cha kwanza kilichokuwa
upande wa kusini, kulikuwana walinzi wawili ambao tofauti na wale wa nje, hawa
walikuwa wamevalia sare maalum, kwa kasi ya ajabu nikawashika vichwa na
kuwagonganisha kwa nguvu, wote wakadondoka chini kama mizigo.
Nikainama na kushika shingo ya wa
kwanza, nikaigeuza kwa kasi, sauti ya mfupa ukiteguka ikasikika, nikamfuata na
yule wa pili, naye nikafanya hivyohivyo! Nikasikia sauti ya Junaitha
ikinipongeza na kunielekeza kuelekea upande wa pili ambapo bado risasi zilikuwa
zikiendelea kumiminwa.
Nilipoingiatu, kwa mbali nilishuhudia
askari wengine wawili wakipigwa risasi na kudondoka chini, kwa jazba nikamshika
wa kwanza na kumrushia ukutani na bunduki yake, kwa kuwa alikuwa ameshika
sehemu ya kufyatulia risasi ‘trigger’, risasi kadhaa zilimiminika kwenye kifua
cha mwenzake, nikammalizia kwa kuvunja shingo yake, eneo lote likawa kimya.
Sikuwa mimi ambaye najijua, roho ya
mauti ilikuwa imenijaa kiasi kwamba kupoteza uhai wa mtu niliona kuwa kitu
chepesi mno. Mpaka muda huo nilikuwa nimeshawanyonga walinzi kadhaa lakini bado
nilikuwa na hamu ya kuendelea kuua tena na tena.
Nikawaona askari wengine wakiburuza
miili ya wenzao na kuisogeza pembeni huku wengine wakija kwa kasi kubwa. Kwa
muda wote huo hakuna aliyekuwa anajua kwamba mimi ndiyo nilikuwa mstari wa
mbele, nikiwasafishia njia, wakawa wanaendelea kukimbilia ndani huku wakifyatua
risasi.
Wakafika kwenye geti la pili na
kulivunja, wakaingia ndani. Wakati wao wanahangaika kufungua geti, mimi
nilikimbia na kuingia mpaka ndani kabisa, nikapigwa na butwaa kwa jinsi jengo
hilo lilivyokuwa limejengwa.
Japokuwa kwa nje lilikuwa linaonekana
kama jengo la kawaida tu, ndani ilikuwa ni zaidi ya ngome. Kulikuwana nyumba
karibu saba, tena zote za kifahari, zikiwa zimejengwa kwa mtindo wa kuzunguka
na kutengeneza kama duara hivi, huku kila moja ikiwa imezungukwa na mandhari
nzuri sana.
Upande wa Magharibi kulikuwa kama na
godauni hivi likiwa limezungushiwa nyaya za umeme, huku mlangoni kukiwa na
walinzi wawili wenye bunduki ambao nao waliposikia ile mvua ya risasi, walikaa
mkao wa kujihami.
Kwa hesabu za harakaharaka, mle ndani
kulikuwa na zaidi ya watu kumi na mbili na miongoni mwao, walikuwepo wanawake
watatu ambao kwa kuwatazama tu walikuwa wakifanana sana na Firyaal na Shenaiza,
kuanzia rangi ya ngozi zao na watoto wa kiume wawili ambao hata bila kuuliza
niligundua kwamba walikuwa ni wadogo zao Firyaal na Shenaiza.
Lakini pia kulikuwa na wanaume wengine
kama wanne hivi, wenye miili mikubwa wakiwa na bunduki mikononi, nadhani ndiyo
walikuwa walinzi wa mwisho wa familia hiyo. Wakiwa katika hali ya taharuki, walishtukia
askari wengi wakiwavamia, wakiwa na silaha na yule kiongozi akasikika akitoa
amri kwamba wote wasalimu amri vinginevyo watawapiga risasi.
Kwa jinsi askari walivyokuwa
wamefanikiwa kuingia mpaka ndani kabisa, wale walinzi walijikuta wakikosa cha
kufanya zaidi ya kusalimu amri, wakainua mikono juu huku wakitupa bunduki zao,
wale wanawake nikawaona wote wakiwakimbilia watoto wao na kuwakumbatia,
wakajikunyata chini huku wakipiga kelele.
Kwa kuwa askari wote walikuwa na
mafunzo ya kazi zao, hawakushughulika sana na wale wanawake na watoto,
wakawaweka chini ya ulinzi wale walinzi wote waliokuwa wameinua mikono juu,
wote wakafungwa pingu na kulazwa chini.
Bado nilikuwa na shauku ya kutaka
kujua mle ndani ya lile godauni lililokuwa likilindwa vikali mlikuwa na nini?
Wakati hayo yakiendelea, tulishtushwa ghafla na mlio mkali wa gari lililoonesha
kwamba linaondoka kwa kasi kubwa.
Kwa kasi ya ajabu nilianza kukimbia
kuelekea kule muungurumo huo ulikokuwa unatokea, baadhi ya askari nao wakafanya
hivyo.
Kumbe ile ngome ilikuwa na mlango
mwingine wa dharura upande wa nyuma ambako nako kulikuwa na walinzi kadhaa
wenye silaha, nikamuona mwanaume mwenye asili ya kiasi, mweupe, mnene, mrefu na
mwenye nywele zenye mvi kiasi, akiwa katikati ya mabaunsa wanne, kila mmoja akiwa
na bunduki, wakiwa ndani ya gari dogo lakini la kifahari ambalo nyuma lilikuwa
wazi, Jeep.
“Mungu wangu,” nilijisemea kwa sababu
kwa kumtazama tu, nilijua lazima huyo ndiyo baba yao akina Firyaal na Shenaiza
na hapo alikuwa akijaribu kutoroka. Tayari geti lilikuwa limefunguliwa na
zilihitajika sekunde chache tu kwa ile kasi yao, wawe tayari wameshatoka nje,
jambo ambalo sikuwa tayari kuona likitokea.
Kwa uwezo wa nguvu za kipekee
nilizokuwa nazo, niliwahi getini bila kuonekana na mtu yeyote, ndani ya hizo
sekunde chache tu na mimi nikalifunga lile geti haraka. Kwa kasi waliyokuwa
nayo, dereva alikanyaga breki lakini gari liliserereka na kwenda kulibamiza
geti, ukuta wa juu ukabomoka na tofali kubwa likadondokea mbele ya gari hilo,
likatua kwenye kichwa cha dereva na kumpasua.
Ungeweza kufananisha kila kitu na movi
ya kusisimua ya mapigano, tayari askari nao walishafika na kulizingira lile
gari ambalo bado lilikuwa likiendelea kunguruma, huku damu nyingi zikimwagika
kutoka kwenye kichwa cha dereva.
Kwa jinsi kila kitu kilivyotokea kwa
kasi kubwa, hata wale walinzi wa Loris walishindwa cha kufanya, wakazitupa
silaha zao na kujisalimisha, wakawekwa chini ya ulinzi na kufungwa pingu, wote
wakalazwa chini isipokuwa Loris ambaye ilibidi askari wawili wenye miili
mikubwa wamshike huku na kule, akiwa amefungwa pingu kwani naye hakuwa mtu wa
mchezomchezo.
Japokuwa alionesha kuwa umri umeenda,
lakini alikuwa na mwili mkubwa wa mazoezi, mikono yake ikiwa na misuli kuonesha
kwamba siyo mtu ambaye unaweza kumdhibiti kwa urahisi.
Wale walinzi wengine walirudishwa na
kwenda kuchanganywa na wale wenzao, Loris akapelekwa moja kwa moja kwenye gari
la polisi chini ya ulinzi mkali, akakalishwa chini.
Kazi iliyokuwa imesalia, ilikuwa ni
kuvunja lile godauni kuangalia ndani kulikuwa na nini? Nilikuwa na shauku kubwa
ya kujua kilichokuwemo mle ndani kwani kwa jinsi nilivyosikia stori za mzee
huyo na mazingira ya ile ngome yake aliyokuwa akiishi, achilia mbali ulinzi wa
hali ya juu, ilionesha ana mambo mengi sana maovu.
No comments:
Post a Comment