ILIPOISHIA:
“Tulia jamal, mbona una haraka,
nimesema leo ndiyo leo na watu wote watatujua sisi ni akina nani. Shenaiza na
Firyaal, naomba mkaze mioyo yenu maana kinachoenda kutokea kwa baba yenu siyo
kizuri lakini lazima tufanye hivi,” alisema Junaitha, akawasha gari, tukaondoka
huku ile difenda ikitufuata kwa nyuma.
SASA ENDELEA...
Msafara uliendelea na safari mpaka
tulipofika Kurasini, tukakata kushoto na kuiacha barabara ya lami, nikaikumbuka
vizuri njia hiyo kwani ndiyo tuliyopita siku ile tulipoenda nyumbani kwa akina Shenaiza.
Tulipoingia kwenye barabara hiyo, ile
difenda iliyokuwa nyuma, ilituwashia taa, nikamuona Junaitha akipunguza mwendo
na kupaki pembeni, ile difenda nayo ikapunguza mwendo na kusimama. Yule askari
aliyekuwa na nyotanyota begani akamsogelea Junaitha.
“Kumbe mlikuwa mnamaanisha huyu mzee
Loris?”
“Ndiyo, kwani maelezo yote si
yanajitosheleza afande?”
“Ni hatari sana kwa kweli, hata
sidhani kama itawezekana.”
“Kwani mheshimiwa, wananchi
wanapoletamalalamiko kwenu, tena mazito kama haya, wakiwa na ushahidi wa kila
kitu, ni nani anayeweza kuwasaidia kama siyo jeshi la polisi?”
“Wewe ni nani unayeuliza maswali ya
namna hiyo? Isitoshe sizungumzi na wewe, naongea na huyu mama aliyeleta
taarifa.”
“Naitwa Richard Bukos, ni mwandishi wa
habari kutoka Kitengo Maalum cha Oparesheni Fichua Maovu (OFM),” majibu yale ya
yule mwandishi wa habari ambaye tulikuwa naye ndani ya lile gari, Toyota
Alphard, yalimshtua mno yule askari. Ni kama hakutegemea kama kulikuwa na
mwandishi wa habari mle ndani, tena akiwa na vitendea kazi vyote.
“Kwa nini mmekuja na waandishi wa
habari?” alimgeukia Junaitha na kumuuliza swali hilo, akionesha kutofurahishwa
kabisa na uwepo wa Bukos eneo lile.
“Kwani kuna tatizo gani afande?
Tunataka Watanzania wote wajue kinachoendelea,” alijibu kwa kujiamini,
nikamuona akigeuka na kurudi kule kwa wenzake bila kuzungumza kitu. Shenaiza
alinigeukia, tukatazamana kisha wote tukageuka na kumtazama Bukos kisha
tukageukia kule kwenye ile difenda. Tukamuona yule askari akijadiliana na wenzake,
wakiwa ni kama wanalaumiana kitu.
Muda mfupi baadaye, tulimuona akitoa
simu ya upepo (Radio Call), akaibonyeza na kuanza kuzungumza na watu wa upande
wa pili. Mpaka muda huo sikuwa nimeelewa ni nini hasa kilichomfanya aonekane
kusitasita.
“Kwani kuna nini kinaendelea?”
“Inaonekana wanamjua huyu mzee,”
alisema Junaitha, yule askari akawa anazungumza na simu huku akisogea pale
kwenye gari. Alipomaliza kuzungumza, alimgeukia Junaitha.
“Huku ni kama mmetuleta uwanja wa
vita, hatuwezi kuingia kichwakichwa, hata nyie humo ndani ya gari, itabidi
gariligeuzwe na kwenda kupaki kule barabarani, mbali kabisa, tunaenda kuuwasha
moto ambao haitakuwa rahisi kuuzima, umenielewa?” alisema askari huyo,
sautikutoka kwenye simu yake ya upepo ikawa inasikika, askari wengine wakipeana
maelekezo.
Imebidi niombe msaada kutoka makao
makuu, kuna wenzetu wanakuja ila nakuonya siku nyingine lazima uwe unatoa
taarifa ambazo zimekamilika. Wewe mwandishi wa habari itabidi ukae mstari wa
mbele kabisa wa mapambano, si unajifanya unajua kufuatilia matukio magumu?”
alisema huku akigeuka na kuondoka.
Kwa muda wote huo, Firyaal na Shenaiza
ambao walikuwa wamekumbatiana, walikuwa kimya kabisa, Raya na Shamila nao
walikuwa kimya, wakitazama kila kilichokuwa kinaendelea.
“Wasitake kututisha bwana, wanataka
tukasimame barabarani ili iweje? Watakuwa wanataka kutuchezea mchezo mchafu
hawa.”
“Hapana, alichokisema ni kweli, kule
ndani kwetu kuna walinzi wengi wenye bunduki wanamlinda baba na kama amerudi
ulinzi huwa unaongezwa zaidi, kuna kamera kila sehemu,” alisema Shenaiza na
kuungwa mkono na mdogo wake, Firyaal.
Yule askari ambaye alikuwa amesogea
pembeni, alianza kumuonesha ishara Junaitha kwamba ageuze gari, kufuatia
maelezo yale ya Shenaiza na Firyaal, ilibidi tugeuze tu, tukaanza kurudi kule tulikotoka
ambapo tulilipita lile gari la polisi ambalo lilikuwa limewasha taa za mbele na
za juu.
Wale askari waliokuwa ndani ya gari
hilo, wote walishashuka na kutawanyika eneo lile na kadiri muda ulivyokuwa
unazidi kusonga mbele, ndivyo eneo lote lilivyokuwa linaonekana kama uwanja wa
vita.
Junaitha aliendesha gari mpaka
barabarani, akatafuta sehemu nzuri nakupaki, yule askari akawa anatembea kwa
kasi kutufuata.
“Kuna yeyote anayeifahamu vizuri ngome
ya Loris na mazingira yake ya ndani?”
“Ndiyo, tuko na binti yake mdogo, yeye
anaweza kuwa msaada mkubwa kuwaongoza,” alisema Junaitha akimuonesha Firyaal.
“Basi itabidi tuongozane naye,”
alisema, mapigo ya moyo wangu yakanilipuka paah! Yaani wao wenyewe walishasema
kwamba pale ni uwanja wa vita halafu safari hii wanataka eti Firyaal ndiyo
awaongoze. Wao wamevaa nguo maalum za kuzuia risasi (bullet proof) lakini
Firyaal yeye amevaa blauzi tu!
“Haiwezekani.”
“Haiwezekani nini?”
“Haiwezekani Firyaal ndiyo awaongoze,
bora hata mimi ndiyo niwaongoze.”
“Kwani wewe unayafahamu mazingira ya
mle ndani?”
“Hapana, nitamuuliza akinielekeza na
mimi nitawaelekeza.”
“Mbona unataka kuleta mzaha kwenye
mambo ‘serious’ we kijana, hebu usiingilie kazi yetu,” alisema yule askarikwa
sauti yenye mamlaka, nikageuka na kumtazama Firyaal, tukawa tunatazamana. Sijui
kwa nini roho yangu ilikuwa ikinienda mbio kiasi hicho, nilishahisikwamba kuna
jambo baya linaenda kutokea mbele yetu.
“Junaitha, do something!” (Junaitha,
fanya chochote) nilimwambia Junaithan, akanigeukia na kunitazama.
“Kwani wasiwasi wako ni nini Jamal.”
“Vita haina macho, wanaweza kumpiga
risasi Firyaal.”
“Siku zote huwa nakufundisha namna ya
kuishinda hofu ndani ya moyo wako, kwa nini ufikirie mabaya tu?”
“Kama wasiwasi wako ni huo,
tutamvalisha ‘bullet proof’ na kofia ngumu ya chuma, atakuwa salama,” alisema
yule askari, akageuka na kuondoka zake.
“Usiwe na wasiwasi Jamal, nitakuwa
sawa. Ni lazima tushirikiane nao ili kukomesha ushetani anaoufanya baba,”
alisema Firyaal kwa kujiamini, nikakosa cha kujibu. Ukimya ulitawala mle ndani
ya gari, kila mmoja akawa anawaza lake.
Muda mfupi baadaye, tulizinduliwa na
ving’ora vya magari manne ya polisi yaliyokuwa yanakuja kwa kasi kubwa, yote
yakiwa yamewasha taa za mbele, ndani yake kukiwa na askari wengi wenye silaha.
Yote yakaiacha barabara ya lami na
kuingia kwenye barabara ya vumbikwa kasi kubwa, yakaenda kusimama jirani na
lile la kwanza na hata kabla hayajasimama, askari wote tayari walikuwa
wameshashuka kwa kuruka. Ungeweza kufananisha kila kitunafilamu ya mapigano.
Yule askari aliyekuwa akizungumzana
sisi mara kwa mara, alianza kutoa maelezo, akawapanga katika makundi mawili,
kila mmoja akiwa na bunduki mkononi, akawa anawaelekeza nini cha kufanya na
baada ya kilammoja kujipanga kwenye sehemu yake, alitufuata pale kwenye gari,
tulipokuwa tumekaa, tukishuhudia kila kitu kilichokuwa kinaendelea.
Mkononi alikuwa ameshika koti maalum
la kuzuia risasi na kofia ngumu ya polisi kama alivyokuwa ametuahidi, mapigo ya
moyo wangu yakawa yanazidi kunienda mbio. Cha ajabu, Firyaal yeye uso wake
ulikuwa umejawa na tabasamu pana, akasogea mpaka pale kwenye gari na kutuambia
kuwa muda wa kazi umewadia.
“Wewe mpigapicha itabidi ukae kwa
mbali maana hatuna vifaa vya kutosha vya kukukinga na risasi, binti njoo
nikuelekeze namna ya kuvaa,” alisema akimuoneshea Firyaal, harakaharaka
akashuka kwenye gari, ikabidi na mimi nishuke.
“Dont worry Jamal, each and everything
is going to be okay!” (Usiwe na wasiwasi Jamal, kila kitu kitakuwa sawa)
alisema Firyaal na kunisogelea, akanikumbatia na kunibusu mdomoni huku kila mtu
akishuhudia. Sikujali, nilikuwa nampenda sana Firyaal na sikuwa tayari kuona
jambo lolote baya linamtokea, hasa kabla ya mimi na yeye kukutana na kumaliza
kile tulichokuwa tayari tumekianza.
No comments:
Post a Comment