ILIPOISHIA:
Nilitafuta
sehemu nzuri, upande wa nyuma kabisa wa shamba hilo kubwa, nikajificha na
kuanza kupanga namna ya kwenda kutimiza azma yangu. Ilikuwa ni lazima nimuokoe Saima
kwa gharama yoyote, hasa ukizingatia kwamba ndani ya tumbo lake, alikuwa na
kiumbe, mwanangu mtarajiwa, ambaye angekuja kuyabadilisha kabisa maisha yangu
na kunifanya na mimi nianze kuitwa baba.
SASA
ENDELEA...
Nikiwa bado palepale mafichoni,
usingizi ukikizonga kichwa changu kutokana na ukweli kwamba sikuwa nimelala
hata kidogo usiku kucha, nilisikia muungurumo wa pikipiki zaidi ya moja kutokea
upande wa nyuma wa shamba kubwa.
Nilijiweka sawa, ‘chuma’ changu
nikakikamata vizuri mkononi kwa ajili ya chochote kwani japokuwa nilikuwa
sehemu ambayo naujua isingekuwa rahisi kwa mtu yeyote kuniona, nilikuwa
nafahamu vizuri jinsi Mute anavyoendesha shughuli zake. Alikuwa na intelijensia
ya hali ya juu pengine kuliko hata vyombo vingi vya usalama.
Nikiri kwamba japokuwa ni kweli
nilikuwa na matatizo makubwa na Mute, lakini ni yeye ndiye aliyenifundisha kila
kitu nilichokuwa nakifanya. Nikiwa kwake, ndiko nilikojifunza kutumia bunduki,
mbinu za mapigano ya mwilini au kwa kitaalamu ‘martial arts’, kutumia silaha
nyingine mbalimbali na sehemu muhimu unazotakiwa kuwa nazo makini unapotaka
kupigana na mtu, iwe ni silaha au kwa mikono.
Unajua tofauti kubwa kati ya raia wa
kawaida na askari aliyepitia mafunzo, ni kwamba raia wa kawaida unaweza kuwa
unajua kwamba ukimpiga ngumi usoni adui yako, utampasua na kumtoa damu au
kumng’oa meno lakini hutaweza kuzuia asiendelee kupambana na wewe lakini askari
anajua kabisa akikupiga sehemu gani, unaweza kudondoka na kupoteza fahamu papo
hapo, au pengine kufa kabisa.
Sikuwa askari lakini kwa mafunzo
niliyoyapata bila hiyari yangu nikiwa chini ya mikono ya Mute, nilikuwa na
ujuzi pengine kuliko hata askari wenye mafunzo ya kawaida na pengine hiyo ndiyo
sababu iliyofanya niwe tishio kwa watu waliokuwa wananijua.
Licha ya yote hayo, bado kuna kosa
kubwa sana alikuwa amelifanya Mute kwenye maisha yangu, kwa sababu kwanza mbinu
zilizotumika mpaka nikawa mfuasi wake, hazikuwa sahihi, unajua kazi hizi za
hatari bora mtu aamue mwenyewe kuwa mtu mbaya lakini siyo kuingizwa ukiwa hujui
chochote na ndiyo maana chuki yangu kwake ilikuwa kubwa mno kiasi cha kujiapiza
kwamba siku nikikutana naye, lazima nitautoa uhai wake, tena kwa mikono yangu
mwenyewe.
Kule upande wa nyuma wa shamba lile
nilikokuwepo, kulikuwa na njia ndogo ambayo nakumbuka kabla mimi na Mute
hatujaingia kwenye haya matatizo makubwa, tulikuwa tukiitumia kuingia na kutoka
mle shambani hasa kwenye ‘misheni’ maalum ambazo zinatakiwa kufanyika kwa usiri
mkubwa.
Muungurumo ulizidi kusogea, na mimi
nikawa najaribu kunyanyua shingo yangu kutoka pale kwenye maficho yangu,
kujaribu kutazama ni nini kilichokuwa kinaendelea.
Nikashtuka kuona pikipiki kubwa tatu
zikija kwa kasi kubwa, na kati ya hizo, ya kwanza ilikuwa na watu wawili, nyingine
ilikuwa na watu wawili na nyingine ilikuwa na watu watatu.
Kwa jinsi nilivyokuwa naujua utendaji
kazi wa vijana wa Mute, nilijua pale lazima kuna mtu ametoka kutekwa au kuna
jambo lisilo la kawaida limetokea kwa sababu pia kulikuwa na sheria nyingine
inayoagiza kwamba mnapoenda kwenye kazi, lazima pikipiki moja ibebe watu
wawili, dereva na abiria ambaye kimsingi ndiye aliyekuwa akikaa na silaha ili
likitokea la kutokea, dereva yeye kazi yake iwe ni kukimbia na yule abiria wa
nyuma kazi yake iwe ni kujihami.
Ilikuwa ni makosa pikipiki kuwa na
dereva peke yake au kuwa na zaidi ya watu wawili kwa hiyo nikajua lazima kuna
jambo. Kama muda ule ndiyo walikuwa wakiwasili pale Kibaha, maana yake ni
kwamba walikuwa wamefanya tukio usiku wa manane na eneo la mbali lililowalazimu
kutembea umbali mrefu ili kuwahi kuukwepa mkono wa kisheria.
Basi macho yangu yote niliyaelekeza
kwenye ile pikipiki iliyokuwa na watu watatu kwa sababu kwa hesabu zangu,
nilijua kwamba lazima pikipiki zote zilikuwa na watu wawili kama ilivyo
kawaida, sasa huyu mtu wa tatu ni nani? Nikawa natafuta majibu.
Nilipoitazama ile pikipiki vizuri,
niligundua kwamba yule mtu wa tatu, alikuwa mwanamke na kwa jinsi ilivyoonesha,
ni kama alikuwa ameteswa kwa muda mrefu kwani hata kukaa mwenyewe hakuweza,
badala yake mtu aliyekuwa nyuma yake ndiyo akawa amemshikilia. Kwa maana hiyo
ni kwamba alikuwa amekalishwa katikati, mbele dereva na nyuma mtu mwingine.
Pia nguo zake zilikuwa zimelowa kwa
damu na wakati nazidi kukazia macho, moyo wangu ulinilipuka mno baada ya
kugundua kwamba blauzi aliyokuwa amevaa, japokuwa ilikuwa imelowa damu, ilikuwa
ikifanana sana na blauzi ya kipenzi cha moyo wangu, Saima.
Kumbukumbu zangu zilinionesha kwamba
ndiyo aliyokuwa amevaa siku ya mwisho wakati anatekwa na kuchukuliwa kwa nguvu
kutoka kule nyumbani, kabla ya baadaye nyumba yenyewe kuchomwa moto.
“No! Haiwezekani, haiwezekani,”
nilisema huku nikitetemeka kuliko kawaida. Nilijisikia uchungu usiomithilika
ndani ya moyo wangu, kwa nini wamfanyie vile Saima wangu?
Amewakosea nini mpaka wamteke na
kumtesa kiasi kile? Kama shida ya Mute ilikuwa ni mimi, kwa nini asinichukue na
kwenda kunifanya chochote anachokitaka? Kwa nini wamfanye vile Saima, tena
akiwa na ujauzito wangu?
Wamasai wana kitu kinaitwa mori! Yaani
kijana wa Kimasai akipandisha mori, anaweza hata kupambana na simba na akamuua
kwa mikono yake.
Basi na mimi japokuwa sikuwa Mmasai,
nilijikuta nikipandwa na mori, mapigo ya moyo yakawa yananienda mbio kuliko
kawaida, mwili nikahisi ukiwa na nguvu za ajabu, hofu yote ikaniisha na
nikajiapiza kwamba ama zangu, ama zao! Nife mimi, au wafe wao wote lakini
siwezi kukubali kumuona Saima wangu katika hali ile.
Japokuwa pale nilipokuwa nimekaa
palikuwa ni juu kidogo, kwenye tawi la mti mkubwa, nilijirusha mpaka chini na
cha ajabu hata sikufikiria mara mbili nitadondokea sehemu gani, kwa bahati
nzuri pale chini palikuwa pameliwa matuta ya viazi, kwa hiyo ikawa ahueni
kwangu.
Kishindo cha kuruka kwangu,
kiliwashtua wale vijana wa Mute, nikamuona mmoja akiwapa ishara wenzake, wale
waliokuwa wamembeba Saima wakazidi kuongeza kasi huku wale wengine wakigeuza
pikipiki zao na kutazama kule nilikokuwepo, ambako ndiko kishindo kilipotokea.
Nilitambua kwamba malengo yao ni
kuhakikisha misheni ya kumuingiza Saima ndani ya lile shamba inafanikiwa na
ndiyo maana wale wengine waliongeza mwendo na sasa wakawa wamekaribia kwenye
geti dogo la nyuma, huku wale wengine wakijiandaa kukabiliana na chochote
kilichokuwa kinataka kuvuruga misheni yao.
Kwa sababu tayari nilishajua lengo
lao, na mimi niliamua kupiga hatua moja zaidi kichwani mwangu, na kuhakikisha
nazuia Saima asiingizwe mle ndani. Kwa kawaida, bunduki ikiwa na risasi, ili
ufyatue risasi ni lazima kwanza uzivute risasi kwenye chemba kisha ndiyo uvute
‘trigger’ ili kuruhusu risasi itoke.
Na kisheria, kama bunduki haitumiki,
risasi hazitakiwi kukaa kwenye chemba kwa sababu ni hatari sana, zinaweza
kukulipukia hata wewe mwenyewe kwa bahati mbaya endapo ukigusa ‘trigger’ hata
kwa bahati mbaya.
Kama umewahi kufuatilia kwa makini,
hata kwenye filamu za mapigano, kabla mtu hajafyatua risasi, ni lazima kwanza
aikoki bunduki au bastola yake, kile kitendo cha kukoki ndiyo kinachozivuta
risasi kutoka kwenye ‘magazini’ na kuziingiza kwenye chemba.
Ni kitendo ambacho kinachukua sekunde
kadhaa tu, lakini kwa akili ya mtu kama mimi, ninapokuwa na ‘bomba’ mkononi,
sekunde moja pekee ilikuwa inatosha kufanya tukio la kushangaza. Maana yangu ni
kwamba, wakati mimi nilishaikoki bunduki yangu na kuzijaza risasi kwenye
chemba, wale wafuasi wa Mute bado walikuwa hawajafanya hivyo kwa sababu
nilikuwa ni kama nimewashtukiza.
Kwa hiyo ule muda wa sekunde kadhaa za
kushuka kwenye pikipiki, kuweka sawa bunduki zao na kuzikoki, ulitosha
kunifanya niwe nimeshawatangulia mbele hatua kadhaa, kwa hiyo nilichokifanya,
nilimlenga yule dereva aliyekuwa anaongeza mwendo kuelekea kwenye lile geti
dogo.
Nadhani nilichokifanya hawakukitegemea
kabisa kutokana na jinsi nilivyoweza kufanya ‘timing’ sahihi ya muda, basi yule
mwenzao alipiga yowe kwa nguvu, pikipiki ikayumba na kupoteza mwelekeo,
wakadondoka kama mzigo. Nilijua lazima Saima naye anaweza kuumia lakini ilikuwa
ni bora nusu shari kuliko shari kamili.
Kilichofuatia baada ya hapo, ilikuwa
ni mvua ya risasi, mitutu zaidi ya minne ilielekezwa kwangu, kila mmoja akawa
ananifyatulia risasi. Wasichokijua wengi ni kwamba vita ya kurushiana risasi
siyo sawa na kupigana ngumi, kwamba wewe unarusha na mwenzako anarusha kwa
wakati huohuo! Ilikuwa ni lazima kutumia akili, mwenzako akiwa anakushambulia
wewe unaji-cover kwenye eneo ambalo risasi haziwezi kukupata, kisha na yeye
akizubaa kidogo na wewe unashambulia kwani pale unakuwa umeushika uhai wako
mkononi, akifanya uzembe kidogo tu, basi unakuponyoka.
Sasa sijui ni kwa sababu ya ‘kupaniki’
au nini, wale wafuasi wa Mute ambao nilikuwa naamini kwamba nao wanazo mbinu
kama nilizonazo mimi, walikuwa wakishambulia tu bila ku-take cover.
Kwa hiyo nilichokifanya kabla risasi
ya kwanza haijafyatuliwa, niliwahi kuruka na kulala chini, nyuma ya matofali
ambayo ilionesha yalisalia wakati wa ujenzi wa ukuta, kwa hiyo risasi zote
zilikuwa zikiishia kwenye matofali hayo, wakawa wananishambulia huku
wakinisogelea ‘kibwegebwege’, nikaona huo ndiyo muda wa kukamilisha kile
kilichonifanya nifunge safari mpaka eneo hilo.
Ghafla niliinuka huku ‘bomba’ likiwa
mkononi, kidole kikiwa kwenye ‘trigger’, nikazichekesha kwa mtindo wa kufagia
kutoka kushoto kwenda kulia lakini ghafla nilihisi kitu kikipenya kwenye mwili
wangu, damu zikaruka kama bomba lililopasuka, ghafla nikaanza kuhisi kama kizunguzungu.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu
kwenye Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment