ILIPOISHIA:
Nilikimbia na kujaribu kuruka ukuta
lakini kabla sijaruka, nikasikia wale askari wakifungua milango na kuruka
kwenye gari lao kwa kasi kubwa, mmoja kati yao akatoa amri ya kunitaka nisimame
na kuinua mikono juu, jambo ambalo niliona kama haliwezekani.
SASA ENDELEA...
Yaani nisalimu amri kirahisi namna
hiyo? Nijivalishe mwenyewe kitanzi kwenye shingo yangu? Lilikuwa ni jambo
lisilowezekana kwa hiyo ilikuwa ni lazima nifanye kitu, tena haraka
iwezekanavyo.
Pale nilipokuwa nimesimama, karibu na
ukuta, kulikuwa na mtaro, ile inayochimbwa kandokando ya barabara. Kwa sababu
maeneo mengi ya Masaki na Mikocheni yana kama asili ya majimaji, mitaro mingi
iliyochimbwa ni mirefu na ina maji.
Kwa kasi ya kimbunga, nilijirusha
kwenye mtaro, nikasikia risasi kadhaa zikipita mita chache kutoka pale nilipo,
nikaangukia ndani ya mtaro. Kwa jinsi nilivyochukua uamuzi huo kwa kasi kubwa,
nadhani hata polisi wenyewe hawakutegemea.
Katika medani za kivita, adui
anapokuwa sehemu ambayo yupo chini kuliko wewe, kama kwenye shimo au handaki na
ana silaha ya moto, huwa ni hatari sana kwa wewe uliyesimama juu ya ardhi kwa
sababu yeye anaweza kukupiga risasi lakini wewe huwezi.
Wale polisi walilitambua hilo kwa
sababu nadhani huwa wanafundishwa, kwa hiyo walichokifanya, ilikuwa ni kukimbia
haraka kurudi nyuma ili kutafuta sehemu ya kujikinga na mashambulizi ya wazi ya
risasi.
Nilikuwa na uwezo wa kufanya chochote
lakini sikuona sababu ya msingi ya kuingia kwenye matatizo na polisi kwa muda
huo, kwa hiyo nilichokifanya, nilifyatua risasi moja hewani ili kuwatisha
wasije kichwakichwa kisha nikautumia muda huo kutambaa kwa kasi kama nyoka
kwenye ule mtaro.
Nilifanikiwa kuibukia mita kadhaa
mbele na kwa sababu wao waliamini lazima nitakuwa palepale niliporukia,
waliendelea kufyatua risasi huku wakisogea, safari hii wakiwa makini zaidi.
Nikatoka kwenye mtaro na kukimbia huku nikiwa nimeinama, nikatokezea kwenye
ukuta wa jengo lingine ambalo linatumika kama ‘godauni’ la kuhifadhia mizigo,
nikaruka ukuta mrefu na kuangukia kwa ndani.
Niliona ni afadhali kupambana na
walinzi wa godauni hilo kuliko kupambana na polisi ambao kila mmoja alikuwa na
silaha.
Kama nilivyoeleza awali, uzembe uleule
wa walinzi, ambao sijui kwa wakati huo walikuwa wapi, pengine nao walijificha
baada ya kusikia milio ya risasi, uliniwezesha kukatiza eneo lote la godauni
bila kuonwa, nikaenda kuruka ukuta wa upande wa pili na kutokea mtaa wa pili,
nikawa nakimbia huku mwili wangu wote ukiwa umelowa kwa maji machafu ya ule
mtaro.
Nilikimbia kwa tahadhari kubwa huku
nikiendelea kusikia milio ya risasi kule nilikotoka, nadhani polisi bado
walikuwa wakijiaminisha kwamba nipo palepale niliporukia. Baada ya dakika
kadhaa, nilitokezea kwenye Barabara ya Cocacola, ile inayotokea Mwenge kwenda
Mikocheni.
Nilijua kabisa kwamba nikiwa nakimbia
pembeni ya barabara ni rahisi kuonekana, kwa hiyo nikavuka na kuingia upande wa
pili wenye viwanda na magodauni mengi, ambao kwa wakati huo ulikuwa kimya
kabisa.
Nilikimbia kwa umbali mrefu huku
nikimuomba Mungu wasishtukie nilikokimbilia, lengo langu likiwa ni kufanya kila
kinachowezekana kufika Kibaha usiku huohuo. Baada ya kukimbia kwa umbali mrefu,
niliona mwanga wa bodaboda ikija kwa kasi mbele yangu, nikajua hiyo ndiyo
nafasi yangu ya kujiokoa.
Nilijitokeza na kusimama katikati ya
barabara na kuinua bunduki juu huku mkono mmoja nikimuamuru dereva wa bodaboda
kusimama. Nilipoona anaongeza mwendo, niliikamata bunduki vizuri na
kumnyooshea, nikiwa tayari kufanya lolote kumsimamisha kama atakaidi
ninachokitaka.
Akiwa ni kama hakutegemea alichokuwa
anakiona mbele yake, dereva alifunga breki za ghafla, akaruka kwenye bodaboda
na kuiacha ianguke, akaanza kukimbia kurudi kule alikotoka huku akiwa ameinua
mikono juu, nadhani aliogopa zaidi baada ya kugundua kwamba nilikuwa na
bunduki.
Sikutaka kushughulika naye,
harakaharaka niliifuata ile bodaboda ambayo bado ilikuwa inanguruma pale chini
huku taa zikiwa zimewaka, nikaiinua na kuhakikisha kama ipo salama, nikapanda
na kuiondoa kwa kasi kubwa huku bunduki yako nikiwa nimeivaa begani.
Niliendesha kwa kasi kubwa mno, kwenye
matuta nikawa nainuka bila kupunguza mwendo na kuyafukia kama ‘nimesimama’,
muda mfupi baadaye nikawa tayari nimeshafika Afrikana.
Nilikunja kona kushoto, nikawa narudi
upande wa mjini kwa sababu awali nilikuwa kwenye ile Barabara ya Old Bagamoyo,
ile inayopita kule kwenye Ofisi za Times FM.
Nilirudi mpaka njia panda ya...
nikakata kona na kuingia upande wa kulia, nikawa nakimbia kwa kasi kubwa kwenye
barabara ya kuelekea Mbezi, ambayo kipindi hocho bado ilikuwa haijawekwa lami
kama ilivyo sasa hivi. Kwa wanaoijua barabara hii, inaenda kukutana na Morogoro
Road eneo la Mbezi Mwisho.
Basi nilikamua kwelikweli, sikuwa na
uhakika kama mafuta yaliyomo kwenye bodaboda hiyo yatatosha kunifikisha
ninakoenda kwa sababu pale yule dereva alipoitupa na kukimbia, mafuta
yalimwagikia barabarani.
Baada ya kama dakika ishirini hivi,
tayari nilikuwa nimeshafika Mbezi, nikaingia kwenye barabara ya lami na
kuendelea kukimbia kwa kasi kubwa, mpaka ikafika mahali nikawa nahisi bodaboda
inaweza kulipuka. Sikuwa dereva mzuri wa bodaboda lakini nilikuwa na uelewa wa
kutosha wa namna ya kuendesha na kwa sababu usiku huo hakukuwa na magari mengi
barabarani, basi sikupata sana shida.
Baada ya kukimbia kwa muda mrefu,
hatimaye niliwasili Kibaha Maili Moja, nikapita na mbele kidogo, nilikunja
upande wa kulia kwenye viwanda, nikanyoosha na barabara na kuanza kupandisha
kuelekea Machinjio ya Zamani, wenyeji wa Bagamoyo watakuwa wanakufahamu vizuri.
Ni nje kabisa ya Mji wa Kibaha.
Muda ulikuwa umeyoyoma sana na kwa
mbali nikaanza kuona kama ule mwanga wa alfajiri umeanza kulifukuzia mbali giza
totoro la usiku. Niliendelea kusonga mbele, nikipita kwa kasi kwenye barabara
yenye mchanga mwingi na kusababisha muda mwingine pikipiki iwe inaniyumbisha
kwa nguvu.
Mpaka nafika Machinjioni, tayari
kulikuwa kumeshaanza kupambazuka na nikajua fika kwamba sitaweza kuikamilisha
kazi hiyo kwa siku hiyo, kwa sababu muda mzuri ulikuwa ni usiku wa giza totoro.
Kwa kuwa nilikuwa nalifahamu vizuri
shamba nilikoelekezwa kwamba Saima ndiko alikopelekwa, nilitafuta sehemu ya
kuificha pikipiki, nikaiingiza ndanindani kabisa kwenye mashamba ya mikorosho
na kuipaki, nikashuka na kukaa chini kwa sababu upepo uliosababishwa na spidi
kubwa niliyokuwa naendeshea pikipiki hiyo, ulisababisha kifua changu kiwe ni
kama kinataka kupasuka.
Tayari mapambazuko yalishawadia kwa
hiyo nilichokifanya, ilikuwa ni kuhakikisha hakuna mtu anayeweza kuiona
pikipiki hiyo, nikaanza kutembea kwa miguu kuelekea kwenye shamba kubwa lenye
zaidi ya ekari hamsini, ambalo ndiko yalikokuwa maficho niliyoelekezwa kwamba
Saima atakuwa amefichwa akiteswa.
Mmiliki wa shamba hilo kubwa, alikuwa
ni mfanyabiashara mkubwa, Mutesigwa au maarufu kama Bosi Mute, ambaye naweza
kukiri kwamba licha ya awali kuwa msaada mkubwa kwangu wakati nafika mjini kwa
mara ya kwanza, sasa alikuwa ndiyo adui yangu mkubwa na nilishajiapiza kwamba
popote nitakapopata bahati ya kukutana naye kwenye kumi na nane zangu, lazima
nimuue, tena kwa mikono yangu mwenyewe.
Kwa nje lilikuwa linaonekana kama ni
shamba, likiwa limezungushiwa uzio mrefu wa matofali na nyaya lakini kwa ndani,
ilikuwa ni kama kambi ya waasi.
Mipango yote michafu ilikuwa
ikifanyikia ndani ya shamba hilo, mali nyingi za wizi, yakiwemo magari,
yalikuwa yakifichwa ndani ya shamba hilo na kwa sababu Mutesigwa alikuwa anajua
namna ya kula na wakubwa, hakuna mtu yeyote aliyekuwa anaweza kulisogelea
shamba lake.
Miongoni mwa makosa makubwa
aliyoyafanya, ilikuwa ni kuanza kuniandama, akiamini sina cha kumfanya.
Nilishamtumikia kwa kipindi kirefu, kwa hiyo nilikuwa namjua kuliko mtu
mwingine yeyote na siyo kumjua yeye tu, bali mpaka familia yake na watu wote
aliokuwa akishirikiana nao. Kwa kuwa yeye alikuwa amenianza, nilijiapiza
kummaliza kwa sababu wahenga wanasema akuanzaye mmalize.
Maisha yangu na kila nilichokuwa
nakipitia, ilikuwa ni kwa sababu yake, yeye ndiye aliyenibadilisha kutoka kuwa
kijana mzuri, mpole na mstaarabu mpaka kuja kuwa mnyama na sasa silaha
aliyoitengeneza, ilikuwa inarudi kumuangamiza yeye mwenyewe.
Nilitafuta sehemu nzuri, upande wa
nyuma kabisa wa shamba hilo kubwa, nikajificha na kuanza kupanga namna ya
kwenda kutimiza azma yangu. Ilikuwa ni lazima nimuokoe Saima kwa gharama
yoyote, hasa ukizingatia kwamba ndani ya tumbo lake, alikuwa na kiumbe,
mwanangu mtarajiwa, ambaye angekuja kuyabadilisha kabisa maisha yangu na
kunifanya na mimi nianze kuitwa baba.
Je, nini kitafuatia? Usikose Ijumaa
kwenye Championi Ijumaa.
No comments:
Post a Comment