ILIPOISHIA:
Kazi iliyokuwa imesalia, ilikuwa ni
kuvunja lile godauni kuangalia ndani kulikuwa na nini? Nilikuwa na shauku kubwa
ya kujua kilichokuwemo mle ndani kwani kwa jinsi nilivyosikia stori za mzee
huyo na mazingira ya ile ngome yake aliyokuwa akiishi, achilia mbali ulinzi wa
hali ya juu, ilionesha ana mambo mengi sana maovu.
SASA ENDELEA...
Askari waliokuwa na silaha,
walilizunguka godauni lote na wengine waliokuwa na vifaa maalum vya kuvunjia
mageti, walisogelea geti hilo na kuseti mitambo yao, tayari kwa kazi. Kwa muda
wote huo, yule mwandishi wa habari alikuwa bize kuhakikisha hakosi picha hata
moja.
Alikuwa akichakarika kisawasawa, akawa
anapiga picha za mnato na za video, kwa ajili ya kuwajuza wananchi juu ya
kilichokuwa kinaendelea. Wakati askari hao wakijiandaa kuvunja godauni hilo,
milio ya ving’ora vya magari mengi ya polisi vilisikika.
Kwa kuwa nilikuwa mwepesi, niliweza
kupaa juu na kutazama upande wa kule barabarani, nikashtuka kuona magari mengi
ya polisi, yakiwa naaskari wengi wenye silaha, yakija kwa kasi eneo lile.
Nadhani awali Junaitha alipowapelekea taarifa juu ya oparesheni hiyo, walidhani
ni tukio dogo tu lakini kilichotokea, kiliwafanya walipe tukio hilo uzito wa
juu.
Binafsi hata sikuona umuhimu wa wao
kufika muda huo kwa sababu tayari jeshi la mtu mmoja nilikuwa nimesafisha njia.
Wale askari waliendelea na kazi yao na muda mfupi baadaye, walifanikiwa kuvunja
geti hilo.
Katika hali ambayo hakuna
aliyeitegemea, milio ya risasi ilianza kusikika upya kutokea ndani ya lile
godauni, ikabidi haraka sana niingie mstari wa mbele, nilipigwa na butwaa kwa
nilichokikuta mle ndani.
Ilikuwa ni himaya nyingine
inayojitegemea kabisa, mlangoni upande wa ndani kulikuwa na walinzi karibu
saba, kila mmoja akiwa na bunduki mkononi. Pia kulikuwa na eneo maalum la mapokezi
ambapo kulikuwa na wasichana kadhaa waliovalia magauni mekundu yenye
mchanganyiko wa rangi nyeupe. Kila kitu kilionekana kuwa rasmi sana kwa sababu
hata wale askari walikuwa na sare kabisa.
Baada ya eneo lile la mapokezi,
kulikuwa na geti jingine na ofisi ndogondogo zilizokuwa na vifaa vya kisasa
kabisa. Taa zote za ndani ya godauni hilo zilikuwa na mwanga mkali kiasi kwamba
ukiwa ndani humo, isingekuwa rahisi kutambua kama ni mchana au usiku.
Kwa kasi kubwa niliingia na kuanza
kuwaangusha wale walinzi, mmoja baada ya mwingine, nikawa nawavunja shingo kwa
kasi kubwa, hali iliyowapa nguvu wale askari ya kusonga mbele, wakafanikiwa
kuingia ndani lakini wale waliokuwa wa kwanza kuingia, walionesha kupigwa na
mshangao kwa sababu hawakujuani nani aliyekuwa akiwasaidia kuwaangusha maadui
zao, tena bila kuwa na majeraha yoyote ya risasi.
Wakafanikiwa kuwaweka chini ya ulinzi
wale wasichana wote na kuwatoa nje. Wakati wakiwatoa nje, wale wengine walikuwa
wakihangaika kuvunja lile geti la ndani na hatimaye, walifanikiwa.
Nilikuwa mstari wa mbele kuhakikisha
nakuwa wa kwanza kuona kila kilichokuwa kikitokea. Nilishtushwa sana na
nilichokiona, kwani kulikuwa na ngazi zilizokuwa zikielekea upande wa chini ya
ardhi, ambako kulikuwa na jengo kubwa mithili ya hospitali, likiwa na vitanda
zaidi ya mia moja, kila kimoja kikiwa na mgonjwa juu yake.
Kulikuwa pia na idadi kubwa ya watu
waliokuwa wamevalia kama madaktari, waliokuwa wakiendelea na kazi lakini
ghafla, kila mmoja aliacha baada ya kuona wakivamiwa na polisi.
Kumbe lile eneo lote ambali kwa juu
lilikuwana nyumba na bustani nzuri, chini lilikuwa na handaki hilo kubwa,
ambalo hata sikujua niliite hospitali au maabara. Upande wa kaskazini, kulikuwa
na maandishi makubwa meusi yaliyokuwa yakisomeka ‘Black Heart’.
Ni hapo ndipo nilipopata picha halisi
ya kile kilichokuwa kikiitwa Black Heart. Yale maelezo niliyoyapata kwamba
shirika hilo ambalo kwa nje lilikuwa likijitangaza kwamba linasaidia maskini na
watu wasiojiweza, kwenda kuwalipia gharama za masomo na matibabu nje ya nchi,
kilikuwa kitu kingine tofauti kabisa.
Japokuwa nilishaambiwa kwamba lilikuwa
likihusika na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na viungo vya binadamu,
nilikuwa siamini mpaka siku hiyo ambapo kwa macho yangu, nilishuhudia kila
kitu. Katika kila kitanda, kulikuwa na mtu aliyelala ambapo wote walionesha
kutokuwa na fahamu.
Walikuwepo wengine ambao tayari
walikuwa wameshafanyiwa upasuaji wa kutolewa viungo mbalimbali vya miili yao,
ambavyo vilihifadhiwa kitaalamu kwenye majokofu makubwa yaliyokuwa mwisho
kabisa mwa jengo hilo refu.
Niliwaona askari waliokuwa
wameshasambaa kila kona, wakipatwa na kigugumizi cha nini cha kufanya. Amri
iliyotoka, ilikuwa ni kuwakamata madaktari wote na kuwatoa nje, huku mipango ya
namna ya kuwanusuru wale watu ambao wote walikuwa kwenye usingizi wa kifo,
wengine wakiwa wamefungwa mashine za kuwasaidia kupumua, ilianza kufanyika.
Lilikuwa ni tukio la kusisimua mno,
nilimuona hata yule mwandishi wa habari tuliyeongozana naye, Richard Bukos
akitetemeka kwa hofu. Jengo lote lilikuwa likinukia umauti.
“Inatakiwa usimamie hatua kwa hatua,
usikubali mtu yeyote akatibua hii oparesheni, kuwa makini na hao wanaoingia
sasa hivi,” alisema Junaitha, sauti ambayo ilisikika vizuri kwenye masikio
yangu.
“Vipi huko hospitalini? Sitaki kufa
tena wala sikati Firyaal apatwe na tatizo lolote,” nilimwambiaJunaitha ambaye
alinitoa wasiwasi, akaniambia nifanye kazi yangu na yeye nimuachie afanye kazi
yangu. Kumbuka kwamba kwa kipindi chote hiki, mimi kwa maana ya mwili wangu
unaoonekana, na Firyaal, tulikuwa tumepelekwa Hospitali ya Muhimbili baada ya
kupigwa risasi kwenye yale mashambulizi.
Nilikuwa na shauku kubwa ya kutaka
kufika mwenyewe na kuona jinsi hali ilivyokuwa ikiendelea lakini sikuweza kwa
sababu nilikuwa na jambo muhimu sana la kulisimamia kwa wakati huo. Kweli wale
madaktari wote walitolewa chini ya ulinzi mkali na kwenda kuunganishwa na wale
wenzao waliokamatwa awali.
Mle ndani kukabaki wale wagonjwa tu
waliokuwa wamelala, wakiwa hawaelewi chochote kilichokuwa kinaendelea. Ilibidi
na mimi nitoke nje kuangalia kilichokuwa kinaendelea, askariwalikuwa
wameongezeka zaidi ya mara nne ya wale waliokuwepo awali, tena kila mmoja akiwa
na silaha.
Miongoni mwao, nilimuona askari
mwingine ambaye alikuwa na nyota nyingi kuliko yule wa kwanza tuliyekuja naye,
nikahisi lazima atakuwa na cheo kikubwa zaidi ya yule wa mwanzo, nikawa makini
kumfuatilia kila alichokuwa anakifanya.
Nilimsikia akitoa amri ya yule kamanda
tuliyefika naye awali aende naye wakazungumze pembeni. Kwa kuwa sikuwa
naonekana, na mimi nilisogea pembeni, nikamuona akimpigia saluti na kunifanya
niamini kweli kwamba alikuwa na cheo cha juu zaidi yake.
“Nani aliyetoa amri ya kuja kuvamia
hapa wakati uongozi wa juu haujui?” nilimsikia akimuuliza, nikapigwa na butwa
mno kwani sikutegemea kama anaweza kumuuliza swali kama lile.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
mwendelezo lini tena mpendwa
ReplyDeleteThis comment has been removed by the author.
ReplyDeletemwendelezo mkuu
ReplyDelete