ILIPOISHIA:
Alikuwa
hanielewi kwa nini nimebadilika ghafla, nimekuwa na mambo mengi ya ajabuajabu,
sioneshi kumhitaji tena kama siku za mwanzo na wala sijali hisia zake. Ukweli
ni kwamba nilikuwa namlinda na ndiyo maana ilikuwa lazima nifanye hivyo na njia
pekee, ilikuwa ni kumshawishi naye ajiunge nasi, kazi ambayo isingekuwa nyepesi
lakini nilishajipanga kumkabili.
SASA ENDELEA...
“Rahma!” nilimuita msichana huyo baada
ya kukutana naye koridoni, mimi nikitoka bafuni kuoga na yeye akitoka chumbani
kwake. Tofauti na siku zote ambazo alikuwa akinichangamkia sana anaponiona,
wakati mwingine hata akinifuata chumbani kwangu, siku hiyo Rahma alikuwa
tofauti kabisa, alipooza na alionesha kutotaka kuzungumza chochote na mimi.
“Rahma si nakuita jamani,” nilisema
baada ya kumuona amenipa mgongo, akitembea haraka kuelekea sebuleni. Licha ya
kutamka maneno hayo, bado hakutaka kusimama, ikabidi nitumia nguvu kumshika
mkono na kumgeuza.
“Samahani nina mazungumzo na wewe,
naomba unisikilize tafadhali,” nilimwambia kwa upole, akanitazama usoni, macho
yake na yangu yakagongana, nikashtuka kumuona akilia.
“Unalia nini Rahma?” nilimuuliza lakini
hakunijibu kitu zaidi ya kuendelea kunitazama kwa huzuni. Ilibidi nianze
kumbembeleza lakini kwa kuwa tulikuwa tumesimama koridoni, niliona haiwezi kuwa
picha nzuri kwani mtu yeyote angetuona tukibembelezana hapo angeweza
kutufikiria vibaya.
“Naomba tutoke tukanywe japo soda pale
dukani, nina mazungumzo ya muhimu sana na wewe,” nilimwambia Rahma, akatingisha
kichwa bila kunijibu chochote kisha akarudi chumbani kwake.
Ilibidi na mimi nirudi chumbani kwangu,
nikachukua nauli iliyokuwa imebaki siku nilipoenda Mlandizi na kuitia mfukoni,
nikajiweka vizuri na kutoka nje. Nilizugazuga pale nje, nilipoona hakuna
anayenifuatilia, nilifungua geti kubwa na kutoka nje. Ile kutoka tu, madereva
Bajaj na bodaboda waliokuwa wanapaki pale nje, waliacha kila walichokuwa
wanakifanya na kuanza kunitazama.
Kibaya ni kwamba upande ule waliokuwa
wakipaki, kwa mbele kidogo ndiyo kulikuwa na duka ambalo nilipanga tukae pale
na Rahma kwa sababu kulikuwa na viti upande wa nyuma, kwa hiyo ilikuwa ni
lazima niwapite palepale walipopaki.
Nimewahi kusikia matukio kadhaa ya
madereva hao wa Bajaj na bodaboda kushirikiana kufanya uhalifu, hasa pale
inapoonekana mmoja wao ameonewa, nikajua lazima watakuwa wamenipania kwa jinsi
nilivyomsulubu mwenzao. Hata hivyo, kwa sababu nilikuwa na nguvu za giza, tena
za kutosha kabisa, sikuogopa chochote, ndiyo kwanza nikawa napiga mluzi huku
nikielekea kule walikokuwa.
Cha ajabu, nilishangaa kuona kila mmoja
akikimbilia kwenye chombo chake na kukiwasha, wakaanza kuondoka mmoja baada ya
mwingine wakikimbia kwa kasi, sekunde chache baadaye eneo lote likawa tupu.
Hakukuwa na mashaka kwamba walikuwa
wakinikimbia mimi, kwa sababu hata kama wanawahi abiria, wasingeweza kuondoka
wote kwa mkupuo, tena kwa kasi kubwa wengine wakinusurika kugongana wao kwa
wao.
Sikuelewa nini kimetokea mpaka wawe
wananiogopa kiasi hicho lakini sikuwajali maana na mimi nilikuwa na majanga
yangu mengi kichwani. Nilienda mpaka pale dukani, nikamsalimia muuza duka
ambaye aliponiona tu, alishtuka sana, akaitikia kwa woga.
“Naomba Fanta,” nilisema huku nikimeza
mate kwani mara ya mwisho kunywa soda, ilikuwa ni siku ile tuliposafiri kuja
jijini Dar es Salaam.”
“Hatuuzi soda hapa!” alisema yule
muuzaji, kauli ambayo nilishindwa kuielewa ina maana gani. Juu ya meza kulikuwa
na chupa tupu za soda kuonesha kwambamuda si mrefu kuna watu walikuwa wakinywa
soda, na mara kadhaa nilipita pale na kuona watu wakipata vinywaji, kwa nini
aniambie kwamba hawauzi soda?
Nikiwa bado nimeduwaa, nikishindwa
nimuulizeje, mara Rahma aliwasili, kumbe hatukuwa tumeachana umbali mrefu,
akamsalimia yule muuzaji. Alimuita kwa jina lake na ilionesha wanafahamiana.
“Kumbe anaitwa Vero,” nilijisemea
moyoni, alikuwa mwanamke ambaye kwa kumkadiria alionesha kuwa bado mdogo lakini
mwenye uso uliokomaa na kupoteza nuru kama walivyo wanawake wengi wa vijijini
kama kule kwetu Chunya.
“Huyu ni kaka yangu, unamjua? Anaitwa
Togo,” Rahma alisema huku akinishika begani, nikamuona yule mwanamke akijaribu
kuvaa tabasamu la uongo usoni.
“Tuletee soda, Togo unakunywa nini?”
alisema Rahma, yule mwanamke akawa anababaika, kama anayeshindwa ajibu nini
maana mimi aliniambia hawauzi soda. Rahma alinishika mkono huku akionesha
kabisa kwamba anailazimisha furaha, tukaenda mpaka kwenye viti na kukaa, tukawa
tunatazamana huku tukisubiri yule mwanamke aje atuhutubie.
“Unataka kuniambia nini?” alisema Rahma
huku akikwepesha macho yake pembeni.
“Rahma! Najua unanifikiria vibaya sana kwa
sasa, najua unaona kama nakufanyia makusudi kwa sababu sikupendi lakini ukweli
ni kwamba ni matatizo makubwa sana na badala ya kunichukia, unatakiwa unionee
huruma mwenzio,” nilianza kumbembeleza Rahma.
Kama nilivyosema awali, sikuw anajua
mambo ya mapenzi kwa hiyo hata kubembeleza kwangu, nilikuwa naungaunga tu
ilimradi Rahma anielewe. Niliendelea kushuka mistari kwa kuzunguka, nikamwambia
kuna jambo zito ambalo halijui nataka kumweleza.
Maneno yangu yalimbadilisha kabisa
Rahma, akawa ananitazama kwa shauku huku ile huzuni aliyokuwa nayo, ikiyeyuka
ghafla. Ili kumuweka sawa, ilibidi nibadilishe mada kwanza, nikamuuliza vipi
yule muuzaji mbona haleti hizo soda?
“Una kiu? Ngoja nimfuate,” alisema huku
akiinuka lakini alipofika pale dukani, yule mhudumu alikataa katakata kutoka,
akampa Rahma funguo ya friji na kutaka ajihudumie mwenyewe. Rahma aliichukua,
akaniuliza nakunywa soda gani, akatoambili pamoja na yake, akaja mpaka pale
tulipokuwa tumekaa, akazifungua zote na kurudisha funguo kwa mwenyewe.
“Kwa nini amekataa kuja kutuhudumia
mwenyewe?”
“Hata mimi nashangaa! Achana naye tuendelee
na yetu,” alisema Rahma, nikapiga funda moja kisha nikaendelea kuzungumza.
Lengo langu lilikuwa ni kumpasulia ukweli kwamba baba yake alikuwa mwanachama
wa jamii ya siri, vilevile baba yangu na mimi pia wameniingiza bila ridhaa
yangu.
Niliona hiyo ndiyo gia nzuri ya
kumuingia kwa sababu kama ningesema mimi mwenyewe ndiye niliyetaka kujiunga,
angenishangaa sana na pengine nisingeweza kumshawishi. Nilianza kwa kumdadisi
kwa kina kuhusu baba yake, nikitafuta sehemu ya kuanzia.
“Mbona unaniuliza kama una kitu unataka
kuniambia? Tatizo langu wala halimhusu baba, ni mimi na wewe.”
“Ni stori ndefu Rahma ila naomba
unielewe nitakachokwambia,” nilisema, nikashusha pumzi ndefu na kuamua liwalo
na liwe. Nilitaka kwenda moja kwa moja, kwamba baba yake na baba yangu walikuwa
wachawi. Cha ajabu, kila nilipotaka kusema hivyo, mdomo ulikuwa mzito, nikawa
naumauma maneno, hali iliyosababisha anikazie macho.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment