Saa saba na
dakika zake mchana, tumbo la Ashrafu lilikuwa likiunguruma kwa kusakamwa na
njaa kali, aliamua kutoka ofisini kwao ndani ya Jengo la Al- Haramain, Mtaa wa
Shaurimoyo jijini Dar na kuamua kushuka kwa kuzikanyaga ngazi moja baada ya
nyingine.
Kazi yake ya
ufundi wa kompyuta na vifaa vya kielektroniki ilimfanya kuwa kijana maarufu sana
na hii ilitokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao kwenye kazi yake kiasi cha
makampuni mengi kugombea kumwajiri lakini mwenyewe akawa hataki.
Kwake aliona
ni bora ajiajiri lakini kama kuna kampuni inahitaji huduma yake, inamfuata na
wanafikia makubaliano kisha kazi inafanyika.
Baada ya
kushuka ngazi kwa tabu hatimaye alijisogeza taratibu hadi mgahawani ambapo
palijulikana kwa jina maarufu la Kwa Makofia.
Hapo
alikutana na umati mkubwa hivyo kushindwa kabisa kuagiza chakula alichokuwa
akihitaji hivyo aliamua kuhamia kwenye mgahawa wa jirani yake, kabla hajachukua
uamuzi wa kuondoka Kwa Makofia, macho yake yalikutana na kitu kilichomfanya ashtuke
kidogo.
Mrembo
matata mwenye mvuto wa kipekee, mweupe aliyepanda juu, mwenye macho kama
anasikia usingizi, alikuwa amekaa kama anayesubiria huduma!
“Dah, huyu
ni mtu wa kawaida au ni malaika ameshuka kupunga upepo duniani?” Ashrafu
alijikuta akiropoka ingawa ni kwa sauti ndogo na ya chini kabisa na hakuna
aliyemsikia hata kwa herufi moja.
“Nafanyaje
jamani kuhusu huyu msichana mzuri hivi? Naanzaje kumuacha tena amekaa mwenyewe
katika mazingira kama haya? Sasa sijui yuko na mwenzake na ametoka kidogo tu au
yuko mwenyewe na mbona leo nimekosa kabisa ujasiri ambao nimekuwa nao kwa siku
zote?” Ashrafu alijiwazia moyoni huku akiondoka eneo hilo na kujisogeza kwenye
mgahawa wa jirani na hapo.
Alifika na
kuagiza chakula ambapo alichagua moja ya viti vilivyokuwemo ndani na kukaa huku
mawazo yake yakibaki kwa msichana aliyekutana naye pale Kwa Makofia.
Katika hali
ya kushangaza, wakati anawaza juu ya mwanamke huyo, alishangaa kumuona msichana
yule akiingia mgahawani hapo na kukaa kwenye moja ya viti na kisha kuagiza
chakula.
Ni hapo
ndipo Ashrafu alishindwa kuvumilia na kuamua kutumia ujasiri wake wa asili
ambao humuwezesha kumvaa mtu yeyote kwa wakati wowote na kumwambia chochote kwa
mazingira yoyote.
“Dada,
samahani kidogo,” Ashrafu aliita kwa nidhamu zote na kuonesha heshima ambayo
hata yeye mwenyewe aliishangaa imetoka wapi.
“Mimi…?” Msichana
wa watu aliitika kwa mshangao na macho ya kuuliza kama ni yeye aliyekuwa
akiitwa.
“Yeah…” Ashrafu
aliitikia na kumpa ishara ya mkono msichana yule ambaye alionesha kusita...akatingisha
bega lake kuonesha kukataa wito wake.
“Samahani
nakuomba au ni vibaya kukuita? Kataa neno usikatae wito,” Ashrafu alichombeza.
“Samahani
kaka! Samahani lakini, mimi kwa watu ambao siwafahamu siwezi hata
kuwasogelea...” alisema yule msichana na kuagiza chakula.
Ashrafu
alishusha pumzi chini...lile tumbo lake lililokuwa likiunguruma safari hii
aliona limezidi mara mbili yake.
“Hata mimi
nikuombe samahani! Naomba nikae hapo karibu na wewe!” Ashrafu alirusha karata
nyingine tena huku akimtolea jicho la aibu.
Yule
msichana alikubaliana na Ashrafu, ilikuwa furaha kubwa kwake kama siyo ushindi
kutokana na mazungumzo ambayo alipanga kuyaendesha kwa muda ambao watakuwa
wanasubiri chakula, aliamini kabisa hadi zoezi la kula linamalizika, atakuwa
ameshaibuka kidedea.
“Siwezi
kumkosa huyu mtoto, kwanza anaonekana laini na mwepesi kama maharage ya Mbeya,”
Ashrafu aliwaza huku akimtazama usoni msichana yule.
“Samahani
tena kwa usumbufu…”
“Bila
samahani kaka…”
“Naitwa Ashrafu
kwa kirefu, sijui wewe mrembo unaitwa nani?”
“Kwa nini
unaniita mrembo jamani?” Aliuliza yule msichana huku akijiangalia kiunoni hadi
miguuni.
“Si kama
hivi ulivyo mzuri na mrembo au huoni?”
“Aaah,
kawaida bwana na huwa sipendi kabisa mtu akiniita mrembo…”
“Okey,
samahani kwa hilo.”
“Wala
usijali.
“Unaitwa
nani?”
“Naitwa Nancy,
ni mwenyeji wa Morogoro eneo la Kilombero.”
Ashrafu
aliendelea kumtolea macho na masikio akiwa haamini kama maneno yale yanatoka
kwa yule msichana.
“Mi mwenyewe
mkazi wa Morogoro!”
“Weee!
Sehemu gani?” Nancy alishangaa, alionekana kubadilika sura na kuwa ya tabasamu
mara baada ya kuambiwa kuwa wanatoka mkoa mmoja kumbe ulikuwa uongo wa Ashrafu
ili kumnasa.
“Mi natokea
Morogoro mjini kabisa eneo moja hivi linaitwa Kihonda, unapajua?”
“Ndiyo, sasa
mara nyingi huwa nafikia kwa Shangazi sehemu moja inaitwa Mji Mpya nakaa siku
mbili tatu ndiyo naelekea Kilombero.”
Wakati
wanaendelea na mazungumzo ya kufahamiana, mhudumu alileta vyakula kulingana na
maagizo ya kila mmoja wao, ambapo kwa pamoja waliamua kutumia meza moja kula.
“Hujaniambia
lakini kuhusu kazi yako,” Nancy alianza kuchokoza.
“Ah, mi
mzugaji tu mjini hapa, nabangaiza ilimradi siku ziende. Nakaa mtaa wa tatu
kutoka hapa,” Ashrafu alidanganya kwa mara nyingine hali iliyomfanya Nancy
ashtuke.
“Mh!
Hongera, kama kweli unafanya kazi hizo na unaonekana mtanashati hivyo!”
“Asante sana
na wewe je?”
“Mimi nafanya
kazi katika kampuni ya kuuza vifaa vya solar kutoka China, pale karibu na ‘round
about’ alimuelekeza Ashrafu kwa kumnyooshea mkono.
“Naishi
Mikocheni, niko mwenyewe na maisha yanasonga kwa kweli,” alisema Nancy huku
akimtazama Ashrafu kwa macho yaliyojaa aibu za kikekike.
Kwa
ilivyoonesha, Nancy alikuwa mzungumzaji sana maana ndani ya muda mfupi tu,
alishayatawala mazungumzo na mbinu kali alizozitumia Ashrafu, zilimfanya
ajikute akimzoea haraka utafikiri wamefahamiana miaka kadhaa iliyopita.
Walimaliza
kula. Nancy akamwambia alikuwa na safari ya kuelekea Posta kufuatilia hundi ya
malipo kwenye kampuni moja waliyofanya nayo biashara.
“Okey, basi nakuomba
tubadilishane mawasiliano ili tuendelee kuwa karibu zaidi,” Ashrafu alitupa
ndoano kimtego kwa Nancy.
“Namba za
simu tena? Hapana huwa sitoi namba za simu, utanisamehe kwa hilo,” Nancy alisema
huku akiinuka, akachukua mkoba wake mdogo na kuanza kutembea kimadaha, akaenda
mpaka kaunta na kulipa bili yake, akamgeukia Ashrafu ambaye bado alikuwa amekaa
palepale akiendelea kuusifu uumbaji wa Maulana kwa kiumbe yule.
Alimpungia
mkono kichokozi huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akatoka
zake na kumuacha Ashrafu akiwa bado ameganda palepale kama barafu.
“Ndege mjanja
hunasa kwenye tundu bovu,” alijisemea huku tabasamu hafifu likichanua kwenye
uso wake, akashusha pumzi ndefu na kuinuka kuelekea kaunta kulipa.
Je, nini kitafuata?
Usikose kufuatilia next issue.
No comments:
Post a Comment