ILIPOISHIA:
Naamua kuendelea kujilaza, vishindo
vinazidi kusogea na sasa vinasikika mita chache tu kutoka pale nilipojilaza,
naamua kuushinda usingizi na kuyafumbua macho yangu, napigwa na butwaa na
ninachokiona mbele ya macho yangu.
SASA ENDELEA...
“Iqram! Ni wewe au naota? Ooh Mungu
wangu,” msichana mrembo mwenye mchanganyiko wa damu kama chotara wa Kizungu na
Kiafrika, anashuka kutoka kwenye mgongo wa farasi mkubwa mweupe aliyekuwa
amesimama mita chache kutoka pale nilipokuwa nimejilaza.
Kumbe vile vishindo vilikuwa ni vya farasi
huyo mkubwa lakini mzuri, kwa wale wenye mazoea ya kwenda ufukweni, hasa
nyakati za jioni watakuwa mashahidi kwamba mara chache unaweza kukutana na mtu
au watu waliopanda farasi, wanaokimbia nao ufukweni wakipunga upepo wa bahari.
Sikuwa nimezoea kuwaona farasi kwa karibu,
nikawa namshangaa huku nikijiuliza maswali mengi ndani ya kichwa changu kuhusu
mnyama huyo. Ni kama nilisahau kabisa uwepo wa msichana huyo mrembo.
“Iqram! Iqram!” alisema, safari hii
akiwa ameshateremka kwenye yule farasi, akanisogelea na kuniinamia pale chini.
Nilimtazama, macho yake na yangu yakakutana, sura yake haikuwa ngeni kabisa
machoni mwangu ingawa sikuweza kabisa kukumbuka nilimuona wapi.
Kingine kilichonishangaza, ni kwamba
aliniita jina ambalo mara kwa mara ndilo nililokuwa nikiamini kwamba ndiyo jina
langu halisi ingawa watu wote, hata wazazi wangu walikuwa wakikataa kwamba hilo
siyo jina langu.
Kwa mujibu wa mtu ambaye alikuwa akisema
kwamba ndiye mama yangu mzazi, nilipozaliwa nilipewa jina la Davis na watu wote
wanaonifahamu walikuwa wakinijua kwa jina hilo.
Mara kwa mara nilikuwa nikiingia kwenye
ugomvi mkubwa na ‘wazazi’ wangu, nikiwaambia kwamba mimi jina langu siyo Davis,
naitwa Iqram na hilo ndiyo jina nililopewa nilipozaliwa, hiyo ikawa miongoni
mwa sababu za wao kuamini kwamba huenda kweli nilikuwa na matatizo ya akili.
“Umeniitaje?”
“Swali gani hilo, kwani wewe jina lako
siyo Iqram? Mbona upo huku? Kwa nini una hali hiyo Iqram? Nini kimekusibu
jamani?” alisema yule msichana huku akishindwa kuzizuia hisia zake, machozi
yakawa yanamtoka kwa uchungu.
“Samahani, unaweza kunikumbusha wewe ni
nani?” nilimuuliza swali lililomfanya ashtuke, akanitazama vizuri huku
akijifuta machozi yake. Sijui kwa nini alishtuka kiasi hicho baada ya mimi
kumuuliza swali.
“Akili yako imepatwa na tatizo gani
Iqram?”
“Mbona sina tatizo lolote? Watu wote
wananiita Davis, wewe umejuaje kama mimi naitwa Iqram?” nilimuuliza swali
lingine, nadhani kwa jinsi nilivyokuwa nikiongea na yeye alianza kupatwa na
wasiwasi kama akili yangu ipo sawa maana hakunijibu zaidi ya kunitazama kwa
macho yake mazuri ambayo sasa yalikuwa yamebadilika rangi na kuwa mekundu.
“Mbona hunijibu?”
“Upo ‘siriasi’ na hayo maswali yako?
Umenisahau au hunijui? Iqram, unajua ni kwa kiasi gani nimehangaika kukutafuta?
Yaani kwanza hata siamini kama ni wewe, tafadhali naomba usinifanyie hivyo,”
alisema huku akianza tena kulia.
Katika hali ambayo sikuitegemea, bila
kujali hali yangu niliyokuwa nayo, aliniinamia pale chini na kunibusu,
nikashtuka kidogo, machozi yake ya moto yakawa yananidondokea mwilini, harufu
ya pafyumu yake ikapenya kwenye pua zangu na kunifanya nishtuke zaidi.
Ilikuwa ni harufu ya pafyumu ambayo
nilikuwa naijua ingawa sikukumbuka nimewahi kukutana nayo wapi. Tofauti kabisa
na watu wote niliokuwa nikikutana nao nikiwa kwenye hali hiyo, msichana huyo
mrembo hakuonesha kuwa na hata chembe ya kinyaa juu yangu.
“Umepatwa na nini Iqram?” aliendelea kusema
huku akilia, mara kwa mara akinibusu, nikawa namtazama usoni huku nikiendelea
kujiuliza maswali yaliyokosa majibu. Msichanahuyu mrembo ni nani? Amelijuaje
jina langu la Iqram? Kwa nini ameguswa sana na hali aliyonikuta nayo?
Nilijiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu.
Nilitamani kuendelea kumuuliza lakini
niliogopa kuendelea kuonekana mwendawazimu, isitoshe msichana mwenyewe alionesha
kuguswa sana na hali yangu na kadiri nilivyokuwa nikizidi kuzungumza naye,
ilionesha kama ndivyo alivyokuwa akizidi kuumia kwa hiyo nilichoamua ilikuwa ni
kuendelea kujiuliza maswali kimyakimya.
“Baba na mama watafurahi sana wakikuona,
wamehangaika sana juu yangu chanzo cha yote ikiwa ni wewe, namshukuru Mungu kwa
kunileta huku ufukweni jioni hii,” alisema huku akinishika mkono.
“Twende nyumbani kwetu, leo itakuwa ni
siku ya kipekee sana,” alisema huku akiinuka akiwa bado ameushikilia mkono
wangu. Bado sikuwa naelewa kinachoendelea, nikajikuta nimesimama lakini maumivu
makali ya miguu yalinifanya nirudi tena pale chini.
Miguu ilikuwa ikiuma sana, pia nilikuwa
na majeraha mengi ya kukanyaga vitu vyenye ncha kali na vipande vya chupa,
ukichanganya na yale maumivu ya kutembea kwa miguu umbali mrefu kila siku,
nilikuwa kama mlemavu wa miguu.
“Vipi tena? Miguu inakuuma? Hebu
nione...” alisema huku akiinama na kuitazama miguu yangu.
“Mungu wangu! Mbona upo hivi?” alisema
huku akijiziba mdomo kwa kiganja chake cha mkono kuonesha ni kwa kiasi gani
alikuwa ameshtuka kutokana na miguu yangu ilivyokuwa.
“Ok, nataka unishikilie nikupandishe
kwenye farasi, tukifika nyumbani kwetu daktari wa familia yetu atakusaidia na
nakuhakikishia utapona na kuwa sawa,” alisema, mimi bado nikawa namtazama
usoni, akili zangu zikiwa zinawaza mambo mengine tofauti kabisa.
Kuna wakati kama nilikuwa nakaribia
kumkumbuka hivi lakini kumbukumbu zikawa zinapotea, ilinibidi nikubaliane naye,
kweli akaninyanyua tena. Hakuwa na nguvu za kuweza kunimudu lakini na mimi
nikawa najitahidi, akanipandisha kwenye mgongo wa yule farasi mkubwa ambaye
bado alikuwa amesimama palepale, na yeye akapanda na kukaa nyuma yangu, nikawa
nalisikia joto la mwili wake na kunifanya nijihisi kama nimefufuka kutoka
katika wafu.
Tayari kigiza kilishaanza kuingia,
akamgeuza yule farasi, akazichezesha hatamu zake na kuanza kukimbia, huku
kigiza kikizidi kuingia.
***
MIAKA 11 ILIYOPITA
Vwawa, Mbozi
Ilikuwa ni Jumatatu kama zilivyo
Jumatatu nyingine zote, niliamshwa usingizi na sauti ya mama yangu aliyekuwa
akinisisitiza kuwahi kuamka ili nisichelewe shuleni. Huo ndiyo uliokuwa
utaratibu wa kila siku, mama yangu alikuwa akipenda sana niwahi shuleni na
alikuwa akinisisitiza kwamba elimu ndiyo kitu pekee kitakachokuja kunifanya
niweze kuyamudu maisha yangu, hata kipindi ambacho wao watakuwa wameshaondoka
kwenye uso wa hii dunia.
Baada ya kumaliza kujiandaa, nilitoka
haraka na kuchukua baiskeli yangu ndogo, ambayo mama alininunulia baada ya
kufanya maajabu kwenye mtihani wa darasa la nne, kipindi hicho nikiwa bado
mdogo kabisa ambapo niliibuka na kuwa mshindi wa kwanza kwa mkoa mzima wa
Mbeya.
Mama alifurahishwa sana na heshima
niliyokuwa nimemletea, kama zawadi ndiyo akaenda kuninunulia baiskeli hiyo. Kwa
kipindi hicho, mtoto, tena mwanafunzi kumiliki baiskeli ndogo ya kisasa, wengi
wanapenda kuziita ‘sport’, ilikuwa ni lazima utoke kwenye familia inayojimudu
kisawasawa kiuchumi.
Basi nilipanda kweye baiskeli yangu,
begi langu la daftari likiwa mgongoni, safari ya kuelekea shule ikaanza huku
nikiwa na furaha kama kawaida yangu. Miongoni mwa sifa za kipekee nilizokuwa
nazo, ni kwamba muda wote nilikuwa napenda sana kufurahi na hiyo ilisababisha
niwe na marafiki wengi sana, kuanzia wanafunzi wenzangu mpaka walimu.
Ilikuwa ni nadra sana kunikuta nimenuna,
muda wote tabasamu pana lilikuwa limechanua kwenye uso wangu. Nadhani hiyo
ilichangiwa pia na aina ya maisha tuliyokuwa tukiishi, familia yetu ilikuwa na
amani na upendo mkubwa sana. Kila nilichokuwa nakihitaji nilikuwa nikikipata
kwa wakati, kwa hiyo kitu kitwacho shida kwangu ulikuwa ni msamiati mgeni.
Ili kufika shuleni nilikokuwa nasoma,
Mwenge Primary School, ilikuwa ni lazima uvuke barabara kubwa ya lami ya
Mbeya-Tunduma. Kwa wale waliowahi kuitumia barabara hii, watakuwa wanaelewa
vizuri kwani ni miongoni mwa barabara kubwa zinazounganisha nchi moja na
nyingine.
Ni barabara hii ndiyo iliyokuwa
ikiziunganisha Tanzania na Zambia, kwa hiyo muda wote ilikuwa ‘bize’ sana,
magari ya kila aina yalikuwa yakipita, tena kwa kasi kubwa, mengine yakielekea
upande wa Tunduma na mengine upande wa Mbeya.
Basi nikiwa na baiskeli yangu,
nilipofika njiani, nilikutana na rafiki yangu mmoja kipenzi, Mungu aipumzishe
roho yake mahali pema peponi. Jina lake alikuwa akiitwa Wilson, alikuwa rafiki
yangu kipenzi sana kiasi kwamba darasani tulikuwa tukikaa dawati moja.
Japokuwa baiskeli yangu haikuwa na
sehemu ya kumpakiza mtu, nilipomuona Wilson nilisimama ili apande kwa nyuma,
yaani kwenye tairi la nyuma kuna ‘msumari’ mmoja mrefu unaotoa sapoti ya tairi kuzunguka, kwa hiyo
kama baiskeli haina kiti cha nyuma, mtu anaweza kusimama kwenye msumari huu,
kwa kuacha upenyo mdogo katikati ya miguu kuruhusu tairi lizunguke, halafu
anakuwa amesimama na kumshikilia dereva mabegani kisha safari inaendelea.
Kwa waliopitia maisha ya ‘utundu’ kama
mimi wanaweza kuwa wananielewa vizuri
ninaposema hivi, basi hivyo ndivyo ilivyotokea, nilimpakia Wilson na
safari ya kuelekea shule ikaendelea, huku tukipiga stori za hapa na pale,
tukicheka na kufurahi kama kawaida yetu.
Dakika chache baadaye, tayari tulikuwa
tumewasili eneo maarufu ambapo barabara ya vumbi inakatisha kwenye barabara kuu
ya Mbeya-Tunduma. Ni jirani kabisa na kituo kikuu cha polisi cha Vwawa.
Siku zote ninapovuka barabara huwa nipo
makini sana lakini sijui nini kilitokea siku hiyo, tukiwa tunaendelea kupiga
stori, akili zikiwa hazipo kabisa kwamba sasa tunavuka kwenye barabara kubwa ya
lami, tena yenye shughuli kibao, nilishtukia honi kali za lori zikipigwa,
zikifuatiwa na kelele za vyuma vya breki kusuguana na matairi, sambamba na
matairi kusuguana na lami, kikasikika kishindo kikubwa kisha giza nene
likatanda kwenye upeo wa macho yangu. Sikuelewa tena kilichoendelea.
Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu
kwenye Championi Jumatatu.
No comments:
Post a Comment