ILIPOISHIA:
Sikuyaamini macho yangu kugundua kwamba
tulikuwa Mlandizi, tena jirani kabisa na pale ile ajali ilipotokea.
Nilipotazama upande wa pili wa barabara, niliwaona watu wengi wakiwa wamekaa na
kuuzunguka moto, pale kwenye ile nyumba iliyokuwa na msiba wa kwanza wa yule
mtoto, moyo ukashtuka sana nikikumbuka kilichotokea.
“Mbona umeshtuka,” baba aliniuliza.
SASA ENDELEA...
Sikumjibu zaidi ya kumuonesha kidole
kwenye ile nyumba ambapo bado watu walikuwa wakiendelea kuota moto huku
wakipiga stori za hapa na pale msibani. Baba wala hakuhangaika hata kugeuka,
akanitaka kuelekeza akili zangu kwenye jambo lililotupeleka pale kwani muda
ulikuwa umetutupa mkono.
Ilionesha baba alikuwa anaelewa kila
kitu kilichokuwa kikiendelea, nikawa najiuliza ameyajuaje yote hayo? Kiukweli
sikupata jibu, baba Rahma naye wala hakujishughulisha na chochote na wale watu
kama baba.
“Onesha aliangukia wapi? Unatupotezea
muda,” alisema baba, nikawa najaribu kuvuta kumbukumbu, nikawa natembea pembeni
ya barabara kuelekea pale yule dereva wa bodaboda alipodondokea, wakawa
wananifuata kwa nyuma.
“Nadhani ni hapa.”
“Unadhani? Kwani huna uhakika?”
“Nilipomgonga aliyumbayumba kwa mita
kadhaa, akaja kudondokea hapa, sina uhakika kwa sababu mimi nilikuwa nimesimama
kule mbali.
“Hebu nenda ulipokuwa umesimama,”
alisema baba. Ilionesha hakuwa akitaka majibu ya kubahatisha, nikageuka na
kutazama tena kule msibani. Bado moyo wangu ulikuwa na hofu, nikiamini wale
wazee wanaweza kuwa miongoni mwa watu waliokesha pale msibani halafu nikayazua mengine
tena.
Nilirudi kwa hofu mpaka pale
nilipokatiza barabara nikiwa spidi kali kama kiberenge, nikasimama na
kuwageukia akina baba. Niliweza kupata ramani halisi, nikatembea harakaharaka
kuelekea mpaka pale nilipokuwa nimewaacha.
“Ni hapa,” nilisema huku nikioneshea
kidole katikati ya barabara. Ni kweli nilipatia kwa sababu bado palikuwa na
alama za damu na vioo vya ile bodaboda, baba akainama pale katikati ya lami
kisha akawa ni kama anaokota vitu fulani hivi.
Baada ya hapo alikuja upande wa pili
tulipokuwa tumesimama, akawa anatazama chini kisha akainua uso na kunitazama:
“Walipomtoa pale katikati ya barabara
walimlaza hapa,” alisema huku akionesha, ni kweli pale pembeni napo palikuwa na
alama za damu nyingi zilizokaukia, kwa kutumia mikono miwili, alizoa udongo
uliokaukia damu, kisha akapiga magoti na kuuinua juu, akazungumza maneno fulani
kama anayenuiza jambo kisha akausogeza ule udongo puani kwake, akaunusa kisha
akapiga chafya mfululizo.
Hakusema chochote baada ya hapo zaidi ya
kuinuka na kuanza kutembea kwa haraka kuelekea upande wa kusini, kama
anayetafuta kitu, baba yake Rahma alinipa ishara kwamba tumfuate, akawa
anatembea kwa kasi huku akiongea maneno ambayo sikuwa nayaelewa.
Alivuka barabara, na sisi tukawa
tunamfuata, akawa anazidi kuongeza kasi kiasi kwamba nililazimika kuwa nakimbia
ili kwenda nao sawa. Bahati nzuri ni kwamba tulikuwa tukielekea upande tofauti
kabisa na kule kulikokuwa na msiba.
Ilifika mahali akachepuka na kuingia
vichakani, safari hii akaanza kutimua mbio, sote tukawa tunakimbia kumfuata.
Japokuwa ilikuwa ni usiku, tulikimbia vichakani kwa muda mrefu sana, baadaye
tukatokezea kwenye makaburi mengi, baba akawa anazunguka huku na kule na mwisho
aliishia kwenye kaburi moja lililoonesha kuwa jipya.
“Amezikwa hapa,” alisema baba huku
akigeuka huku na kule, nikawa natetemeka kwa hofu, sikujua nini kinachoenda
kutokea.
“Simama kwa kule,” alisema baba huku
akinielekeza kusimama upande uliokuwa na msalaba ambapo kimsingi ndiyo
kichwani. Nilifanya hivyo, baba yake Rahma akasimama upande wa miguuni na baba
akasimama katikati, juu ya kaburi.
Baada ya kusimama hapo, aligeuka huku na
kule kama anayetafuta kitu kisha akashuka kutoka pale juu ya kaburi na
kunifuata, akawa ananiongelea sikioni.
“Huyu amezikwa leo, katika sheria za
jamii yetu, anaruhusiwa kutolewa kafara kwa hiyo tutamchukua huyu badala ya
Sadoki, kule tutarudi siku nyingine kwa sababu kuna mambo hayakwenda sawa kwa
sababu yako, sasa ukifanya ujinga tena na hapa, hakuna wa kumlaumu,” alisema
baba.
Hofu ikazidi kuongezeka kwenye moyo
wangu. Kama nilivyoeleza, hakuna sehemu niliyokuwa naiogopa kama makaburini,
nikawa nahisi kama mwili na akili vinatengana. Kibaya zaidi ilikuwa ni usiku na
nimeshawahi kusikia kwamba makaburini nyakati za usiku kunakuwa na mambo mengi
sana ya ajabu, sikuelewa baba anavyosema tunamchukua yule dereva bodaboda
aliyefariki kwenye ajali, alimaanisha nini.
Ninavyojua mimi, huwezi kufukua kaburi
na kutoa maiti kwa sababu kwanza siyo kazi nyepesi lakini pia, lazima watu
watakuona ukiwa unalifukua kwa sababu makaburi mengi huwa yanakuwa na ulinzi,
na kama si hivyo, mizimu mibaya iliyopo makaburini lazima itakudhuru tu.
Sikuelewa malengo ya baba ni nini lakini kama mwenyewe alivyokuwa anasisitiza
kwamba lengo ni kunisaidia mimi, ilibidi nitulie kuona mwisho wake.
Baada ya kuzungumza na mimi, alimfuata
baba yake Rahma, wakawa wanajadiliana jambo pale, wakazungumza kwa zaidi ya
dakika mbili kwa sauti ya chini kiasi kwamba sikuwa nikisikia walichokuwa
wanakisema.
Baada ya hapo, baba yake Rahma
alinifuata na kuniambia natakiwa kuvua nguo zote na kukaa juu ya kaburi kwa
sababu kazi iliyokuwa inaenda kufanyika, si ya kitoto. Nilishtuka, yaani nivue
nguo halafu nikae juu ya kaburi? Mapigo ya moyo yakaanza kunienda mbio tena.
Ni kama baba yake Rahma alinielewa jinsi
nilivyokuwa na hofu, akaniambia sitakiwi kuwa na hofu yoyote kwa sababu kwenye
jamii yao, kukaa bila nguo ni kitu cha kawaida kabisa, isitoshe wao ni baba
zangu ambao wananijua tangu nikiwa mtoto mchanga, kwa hiyo lazima nifanye
walichoniambia.
Ilibidi nikubaliane naye maana baba
alikuwa akisisitiza kwamba muda unakwenda. Nikasogea pembeni na kuvua nguo
zote, nikajiziba sehemu ya mbele kwa mikono yangu na kupanda kwenye tuta la
lile kaburi, nikawa natetemeka mno.
Baada ya kukaa juu ya tuta la kaburi,
nikiwa nimeupa msalaba mgongo kama nilivyoelekezwa, baba na baba Rahma, mmoja
akiwa amesimama upande wa kichwani na mwingine upande wa miguuni, walianza
kuimba nyimbo za kutisha kwa kupokezana, akiimba baba, baba yake Rahma
anaitikia, wakaendelea hivyo kwa dakika kadhaa kisha wakaanza kulizunguka lile
kaburi, kutoka kulia kwenda kushoto.
Walifanya hivyo kwa dakika kadhaa, baadaye
baba akaniambia nisimame. Nilifanya hivyo huku nikijiziba kwa soni,
akanielekeza kuelekea upande ule wa kichwani niliokuwa nimesimama awali, kisha
akaniambia niwe makini kutazama anachokifanya.
Milio ya bundi na ndege wengine wa
usiku, iliendelea kusikika na kufanya hali iwe ya kutisha mno pale makaburini.
Baba alionesha kwa ishara kwamba natakiwa kupiga makofi na kupiga mguu wangu wa
kushoto chini kwa nguvu, na vyote vifanyike kwa wakati mmoja.
Alinihesabia kwa alama za vidole kisha
akaniruhusu, nikapiga makofi kwa nguvu na wakati huohuo nikapiga kishindo cha
nguvu. Alinionesha kwa ishara kwamba natakiwa kufanya hivyo mara tatu, nikarudia
mara ya pili, kisha nikafanya kwa mara ya tatu.
Kilichotokea baada ya kufanya hivyo kwa
mara ya tatu, kilinifanya nihisi kama mwili wangu unakufa ganzi kwa hofu,
sijawahi kushikwa na hofu kama niliyoipata siku hiyo na kama baba asingeniwahi,
huenda ningedondoka kama mzigo chini maana mwili wote uliisha nguvu.
Japokuwa ilikuwa ni usiku, tena nikiwa
sina nguo na kulikuwa na baridi kali, nilihisi kijasho chembamba kikinitoka,
ama kweli duniani kuna mambo na ukishangaa ya Musa, utayaona ya Firauni.
Je, nini kilitokea? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment