ILIPOISHIA:
Ni kama fahamu zake zilikuwa zimemrejea
kwani alishtuka sana kuniona ndani ya chumba chake, akageuka huku na kule huku
akijaribu kujitoa kwenye mikono yangu kwa hofu kubwa.
“Togoo! Umeingiaje humu?” aliniuliza kwa
sauti ya juu, nikasikia mlango wa chumba cha pili ukifunguliwa kuashiria kwamba
kuna mtu alikuwa amesikia na sasa anatoka.
SASA ENDELEA...
“Nimekwisha!” nilijisema huku nikigeuka
huku na kule, sikumuona baba wala baba yale Rahma, Sadoki akanibadilikia na
kunishika kwa nguvu ii nisipate nafasi ya kukimbia.
Akili za haraka, zilinituma kutumia
nguvu zangu kujiokoa na kwa kuwa nilikuwa na ile kinga yangu ya hirizi mkononi,
nilipiga mguu wa kushoto chini huku nikiwa nimevibana vidole gumba na vile vya
mwisho. Hii ni mbinu niliyofundishwa ya kutaka kupotea kwenye macho ya watu,
yaani unakuwepo sehemu hiyohiyo lakini huonekani.
Nilipofanya hivyo, nilishtukia nikiwa
mwepesi kama upepo, Sadoki akabaki ameduwaa kwani japokuwa alikuwa amenishika,
alishtukia nikiyeyuka mikononi mwake, giza nene likatanda chumba kizima.
Mara mlango ulianza kugongwa kwa nguvu,
Sadoki akaenda kuufungua maana alikuwa amefunga kwa komeo kwa ndani, mama yake
Sadoki akaingia mbiombio akiwa ameshika kibatari.
“Una nini Sadoki?”
“Mama! Nimemuona Togo kwa macho yangu,
hata sijui ameingiaje humu ndani wakati milango ilikuwa imefungwa.”
“Togo huyu rafiki yako? Wewe utakuwa
unaota, Togo ataingiaje humu wakati milango yote imefungwa? Halafu mbona watu
wenyewe hawapo hapa kijijini na hakuna anayejua walikohamia?” mama yake Sadoki
alisema huku akionesha kumshangaa mwanaye.
“Kweli mama, nimemuona kwa macho yangu!”
“Kwanza umemuonaje wakati hukuwa
umewasha kibatari? Acha kutushtua wenzako kwa sababu ya ndoto zako,” alisema
mama yake Sadoki huku akimulika huku na kule kwa kibatari. Japokuwa nilikuwa
mlemle ndani, hakuna aliyeniona, mwanamke huyo akawa anamtuliza mwanaye na
kumwambia kwa kuwa wanalindwa na Mungu hakuna jambo lolote baya linaloweza
kuwapata.
Japokuwa mama yake Sadoki aliamini
kwamba mwanaye alikuwa ndotoni, mwenyewe aliendelea kushikilia msimamo wake na
alipoona mama yake hamuamini, aliamua kunyamaza lakini mara kwa mara alikuwa
akigeuka huku na kule, akionesha kuwa na hofu kubwa ndani ya moyo wake.
“Haya sogea huku tusali,” alisema mama
yake Sadoki, akamshika mwanaye mikono, wote wakafumba macho. Kabla hata
hawajaanza kusali, nilishtukia nikivutwa kwa nguvu kuelekea nje, kutazama
vizuri kumbe walikuwa ni baba na baba yake Rahma, tukadondokea kwenye majani
pembeni ya nyumba ya akina Sadoki, wote wakiwa wanahema kwa nguvu.
“Mpumbavu sana wewe,” alisema baba huku
akinizabua kibao kwa nguvu, nikashangaa kwa nini ananipiga kwa sababu sikuwa
nimefanya kosa lolote.
“Kwa nini hukumgeuza kinyumenyume kama
wewe?” alisema baba kwa ukali, ni hapo ndipo nilipolitambua kosa langu. Wakati
nikitoka na Sadoki, mimi ndiye niliyetanguliza mgongo lakini yeye alikuwa
ameelekea nilipo mimi kwa sababu nilikuwa nimemshika mikono nikimvuta,
hakutanguliza mgongo.
“Lakini hukuniambia hivyo baba,”
nilisema huku nikiugulia maumivu makali ya kibao cha baba. Muda huo tayari
walishaanza kusali, wakawa wanakemea na kutaja jina la Mungu kwa nguvu.
Ukweli ambao wengi hawaujui, ambao hata
mimi mwenyewe nilikuwa siujui, hakuna sumu mbaya kwa jamii ya watu wa nguvu za
giza, kama mtu anayesali na kumuamini Mungu kwa moyo wake wote, bila kujali ni
wa dini gani.
Hapa nazungumzia wale watu ambao kweli
wanafuatisha amri za Mungu, yaani kama ni Mkristo, awe anafuatisha yale yote
aliyoagizwa na dini yake na kama ni Muislam vivyo hivyo.
Watu wa namna hii, huwa hawagusiki
kabisa maana hata pale baba aliniambia kama wasingetumia nguvu za ziada kuingia
na kunivuta kwa nguvu, maombi ya Sadoki na mama yake yangenidhuru vibaya sana
na hata wao hawajui nini kingenipata.
Ila kitu ambacho nilikuja kujifunza
baadaye, ambacho ningependa watu wengine wajue, kinga waliyonayo watu
wanaomuamini Mungu, haiwahusu wale wanaosali kinafiki, kwamba ukifika kwenye
nyumba za ibada unajifanya wewe ni mwema sana lakini kumbe ni mwizi, mwongo,
mwasherati au unashinda kwa waganga wa kienyeji.
Ilibidi tuondoke haraka pale nyumbani
kwa akina Sadoki kwa sababu sasa palikuwa hapakaliki tena kutokana na maombi
yaliyokuwa yanaendelea ndani, njia nzima baba akawa ananilaumu kwa uzembe nilioufanya.
Kwa bahati nzuri baba Rahma alinitetea kwamba ni kwa sababu sikuwa najua.
Kiukweli lawama za baba zilikuwa ni
uonevu wa hali ya juu, maelezo aliyokuwa ananipa, alikuwa ananielekeza vitu
nusunusu, sasa kwa mfano hapo kwa akina Sadoki, mimi ningejuaje kama natakiwa
kumgeuza Sadoki pia atoke kinyumenyume huku nikiwa nimemshikilia bila kupewa
maelekezo?
“Sisi tunakusaidia wewe mwenyewe kwa
sababu ya upumbavu ulioufanya, kwani sisi ndiyo tulikutuma uende kwenye msiba
ambao wewe mwenyewe ndiye uliyeusababisha? Utajuana mwenyewe na Mkuu, we fanya
masihara utaona mwisho wake,” alisema baba.
Tayari tulishakaribia pale kwenye uwanja
wa shule ya msingi niliyosoma ambapo ndipo tulipofikia.
“Sasa mzee mwenzangu, tukiendelea
kufanya mambo kwa hasira, kweli tutampoteza huyu kijana, hapa kinachotakiwa ni
kuhakikisha tunamaliza kwanza suala la Mkuu na Togo na kama unavyoona huku
ndiyo tayari tumeshakwama na muda unayoyoma,” alisema baba yake Rahma.
Mwanzo nilikuwa nalichukulia suala hilo
kama jepesi lakini kwa jinsi mazungumzo hayo yalivyokuwa, niligundua kwamba
kweli nipo kwenye hatari kubwa kwa sababu ya makosa niliyokuwa nimeyafanya bila
kujua.
“Hivi si kuna yule mtu aliyepoteza
maisha kwenye ile ajali ya bodaboda aliyoisababisha huyu mwendawazimu?” baba
aliuliza. Baba yake Rahma akamjibu kwa kutingisha kichwa, nikiwa na shauku
kubwa ya kutaka kusikia baba atasema nini.
“Taarifa zinaonesha kwamba amezikwa
jioni ya leo, ila sijui amezikwa wapi, kama tukifanikiwa kujua, tunaweza
kumtumia kama mbadala wa Sadoki ili tulimalize hili tatizo la huyu
mwendawazimu,” alisema baba huku akiendelea kunishutumu.
Sikuelewa anamaanisha nini na hata kama
tungelijua kaburi lake tungefanya nini.
“Twendeni Mlandizi, tutajua hukohuko
tukifika, si unalikumbuka eneo la ajali?” baba aliniuliza, nikatingisha kichwa
kwa sababu ilikuwa ni palepale kwenye nyumba iliyokuwa na msiba ndipo hiyo
ajali nyingine ilipotokea. Yaani baba alivyokuwa akizungumza, utafikiri kutoka
Chunya mpaka Mlandizi ni karibu sana.
Kukukumbusha tu, hapa aliyekuwa
anazungumziwa aliyekuwa ni yule dereva wa bodaboda ambaye wakati nikiwa
nakimbia kuokoa maisha yangu baada ya wale wazee kunishtukia pale kwenye msiba,
nilimgonga wakati nikivuta barabara, yeye akiwa kwenye bodaboda iliyokuwa
kwenye kasi kubwa. Pale alipodondoka hakuweza hata kuomba maji, alipoteza
maisha palepale na sikuwa najua mpaka nilipokuja kuambiwa na akina baba ambao
hata sijui wao walijuaje.
Basi tulienda mpaka pale chini ya ule
mti, tukakuta kuna watu wengine wengi wakiwa wanafanya mambo ambayo hata
sikuyaelewa lakini yalionesha kuhusiana na nguvu za giza.
Tukakaa na kuweka duara kama
tulivyofanya kule Kunduchi wakati tukitaka kuondoka, nikaambiwa nifumbe macho
na nisifumbue mpaka nitakapoambiwa, lakini baba akanisisitiza kwamba natakiwa
kuwa nalifikiria eneo lile ajali ilipotokea.
Kweli nilifanya hivyo, wao wakafanya
tena mambo yao kama kule Kunduchi na muda mfupi baadaye, upepo mkali ulianza
kuvuma, sikuelewa tena kilichoendelea mpaka nilipokuja kuzinduliwa na baba
aliyekuwa akinitingisha kwa nguvu.
Yaani kilichokuwa kinatokea, inakuwa
kama nimepitiwa na usingizi mzito wa ghafla, kisha nikizinduliwa najikuta nipo
kwenye mazingira mengine tofauti kabisa. Nilishtukia nikiwa nimelala pembeni ya
barabara ya lami, baba aliponiamsha, nikawa nashangaashangaa, nikageuka huku na
kule kama ninayejaribu kuvuta kumbukumbu.
Sikuyaamini macho yangu kugundua kwamba
tulikuwa Mlandizi, tena jirani kabisa na pale ile ajali ilipotokea.
Nilipotazama upande wa pili wa barabara, niliwaona watu wengi wakiwa wamekaa na
kuuzunguka moto, pale kwenye ile nyumba iliyokuwa na msiba wa kwanza wa yule
mtoto, moyo ukashtuka sana nikikumbuka kilichotokea.
“Mbona umeshtuka,” baba aliniuliza.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
Hawa Lufingo
No comments:
Post a Comment