ILIPOISHIA:
“Jamal! Jamal! Amka, kuna tatizo,” sauti
ya Junaitha ndiyo iliyonizindua kutoka kwenye usingizi fofofo, nikakurupuka
nikiwa na shauku kubwa ya kutaka kujua kumetokea nini tena.
SASA ENDELEA...
“Kuna nini tena?”
“Huyu mshenzi anataka kunizidi nguvu,
amka ukanisaidie,” alisema Junaitha, huku kijasho chembamba kikimtoka.
Harakaharaka nikakurupuka na kuvaa bukta na fulana, nikaongozana na Junaitha
ambaye tayari alishatoka na kuanza kukimbilia kule kwenye chumba chake cha
siri.
Tulipokaribia nilisikia sauti za kutisha
mno, yule mwanamke tuliyemteka akawa ananguruma kama mnyama wa porini huku
akikwangua mlango wa chuma kwa kucha zake ngumu, akitaka kutoka.
“Nisikilize! Jamal nisikilize,” alisema
Junaitha ambaye alikwama ghafla pale mlangoni.
“Tukifungua mlango atatuzidi, inabidi
tuingie kwa kutumia nguvu zetu tukapambane naye hukohuko ndani, amenitia meno,
si unaona,” alisema Junaitha huku akinionesha alama ya meno mkononi mwake, huku
damu nyeusi zikichuruzika.
Kumbe zile kelele ziliwashtua Raya, Firyaal
na Shamila ambao kwa muda mrefu walikuwa wamelala fofofo kutokana na uchovu,
nao wakawa wanakuja kwa kujikokota, kila mmoja akionesha kuwa na hofu kubwa
ndani ya moyo wake.
“Msije, nyie ishieni hapohapo,” alisema
Junaitha kwa sauti ya juu, wote wakafunga breki na kuanza kututazama.
“Inabidi tupeane migongo na kuunganisha
mikono ili tuingie kwa urahisi, haya sogea,” alisema. Bila kupoteza muda
nilifanya kama alivyoniambia, tukashikana mikono kwa nguvu, mkono wake wa kulia
ukaushika wangu wa kushoto na wangu ukamshika yeye kwa namna ya kubadilishana,
kushoto na kulia.
Alinielekeza tufumbe macho, tulipofumbua
tayari tulikuwa ndani ya chumba hicho cha siri ambacho sikuwahi kuingia hata
siku moja, yule mwanamke akawa anaendelea kusumbua pale mlangoni bila kujua
kwamba tayari tulikuwa nyuma yake.
“Kumbe ana kamba nyingine pale shingoni,
inabidi ufanye kama tulivyofanya kule porini, kaikate kwa nguvu, usijali hata
akikuumiza dawa ipo, ishinde hofu,” alisema Junaitha, nikawa namsogelea kwa
kunyata, mara nikakanyaga kitu chini kilichofanya niteleze na akuanguka kama
mzigo, puuh!
Kishindo cha kuanguka kwangu kilimshtua
yule mwanamke ambaye sasa macho yake yalikuwa yamebadilika na kuwa ya kung’aa
kama mnyama mkali wa porini anavyong’aa gizani.
Nilipotupia macho haraka kwenye kitu
kilichofanya niteleze, nilishtuka mno baada ya kugundua kuwa ilikuwa ni mifupa
ya fuvu la mtoto mdogo.
“Ishinde hofu, kamilisha kazi kwanza
mengine baadaye,” alisema Junaitha, nilipogeuka kumtazama yule mwanamke, bado
alikuwa amenikazia macho huku akiendelea kunitazama kwa ukali, udenda mwingi
ukitoka na meno yake makali yakionekana.
Kwa ujasiri wa hali ya juu nilisimama,
yule mwanamke naye akakaa mkao wa kutaka kushambuliana na mimi, tukawa
tunatazamana. Kiukweli alikuwa akitisha sana lakini sauti ile ilisikika tena
ndani ya moyo wangu kwamba natakiwa kuishinda hofu.
Kwa kasi ya ajabu nilimrukia yule
mwanamke, kutokana na uzito wangu nikamzidi nguvu na kudondoka naye mpaka
chini, akapiga kelele kwa nguvu zaidi kisha akanikamata mkono wa kushoto na
kuning’ata kwa nguvu.
Kwa jinsi meno yake yalivyokuwa makali,
nilihisi kama mkono wangu unakatika lakini nikapiga moyo konde na kumkamata
shingoni, nikafanikiwa kukamata kamba nyingine ngumu na kuivuta kwa nguvu zangu
zote, ikakatika na kumfanya yule mwanamke wa ajabu aishiwe nguvu, akadondoka
kama mzigo na macho yake yakabadilika na kurudi kwenye hali ya kawaida.
“Unaniuaaa! Jamal unaniuaaa,” alisema
huku akilitaja jina langu, nikashangaa sana amelifahamu vipi jina langu?” kabla
sijajibu chochote, Junaitha alimrukia pale chini na kumkaba shingoni, akaanza
kumzibua makofikwa hasira.
“Safari hii ukirudia tena nakuchinja kwa
mikono yangu,” alisema Junaitha, tukasaidiana kumfunga tena kamba na safari
hii, tulimfunga mikono kwa nyuma na kuunganisha na miguu, akawa analia kwa
uchungu huku akisema tumsamehe kwani na yeye ana familia hivyo hayupo tayari
kufa.
“Leo utasema kila kitu, wewe si
unajifanya mshenzi,” alisema Junaitha na kabla ya yote, akamtaka kwanza
mwanamke huyo amtibu jeraha alilomng’ata mkononi pamoja na lile alilokuwa
amenijeruhi mimi kwenye mkono wangu wa kushoto.
Kama ilivyokuwa mwanzo, mwanamke huyo
alitoa ulimi wake mrefu uliokuwa na mabakamabaka na kumlamba kwenye lile
jereha, mvuke kama moshi ukatoka kisha taratibu likaanza kujifunga.
Na mimi nikasogea ambapo alifanya
hivyohivyo lakini cha ajabu, mwanamke huyo alinitazama kwa namna ambayo
sikuielewa, ni kama aliyekuwa anataka nitafute upenyo wa kuzungumza naye tukiwa
wawili tu.
Kwa muda wote huo bado sikuwa nimepata
nafasi ya kukichunguza vizuri kile chumba, ni mpaka jeraha langu lilipoanza
kupunguza maumivu ndipo nilipopata akili ya kutaka kutazama vizuri kwanza lile
fuvu lililosababisha nijikwae, kuteleza na kuanguka na vitu vingine vilivyokuwa
ndani ya chumba hicho.
Cha ajabu, Junaitha aliniwahi na
kuniziba macho, nikamsikia akitamka maneno fulani kisha kufumba na kufumbua,
tukajikuta tumetoka nje ya chumba hicho kimazingara, tukaangukia palepale
tulipokuwa tumekaa awali tukijadiliana namna ya kuingia.
“Vipi mbona sielewi?”
“Usiwe na haraka Jamal, naomba uniamini
kwanza hayo mengine yote utayajua, tumalize kwanza kazi yetu,” alisema Junaitha
kwa sauti ya chini, akiwa ni kama hataki akina Raya, Shamila na Firyaal ambao
bado walikuwa wamesimama palepale, wasikie.
“Lakini...”
“Lakini nini Jamal? Unanipenda
hunipendi?”
“Nakupenda.”
“Basi naomba unisikilize
ninachokwambia,” alisema kwa sauti ya kunong’ona, nikawa sina ujanja.
Nilimsikia yule mwanamke kule ndani ya chumba cha siri akiangua kicheko kwa
sauti ya juu. Sikuelewa kwa nini amecheka kiasi hicho, nikabaki na viulizo
vingi ndani ya kichwa changu.
Baada ya kukubaliana na Junaitha,
niligeuka na kuanza kurudi kule sebuleni, akina Raya, Shamila na Firyaal
wakatukimbilia kwa pamoja na kunikumbatia mimi na Junaitha.
“Mpo salama jamani?”
“Tupo salama wala msijali, niliwaambia hii
kazi ni nzito sana, vipi yaani nyie ndiyo mnaamka saa hizi?” alisema Junaitha,
nikawaona kila mmoja akikosa cha kujibu.
“Sasa muacheni Jamal akapumzike, nyie
njooni huku kuna dawa niwape maana inatakiwa mrudiwe na nguvu zenu, bado kuna
kazi kubwa, si mnaona purukushani iliyopo?”
“Yule kule aliyekuwa ananguruma kama
mnyama ni nani?” Firyaal aliuliza swali, nikawaona wenzake wote wakitingisha vichwa,
kuunga mkono swali hilo.
“Ni stori ndefu kidogo, ngoja
nitawaeleza lakini njooni kwanza huku niwape dawa,” alisema.
Je, nini kitafuatia? Usikose next issue.
No comments:
Post a Comment